Afisa habari wa Yanga Dismas Ten ametoa ufafanuzi kuhusu maendeleo ya afya ya kiungo wao Thabani Kamusoko ambaye ilielezwa amepona majeraha na anatarajiwa kuonekana uwanjani wakati wowote lakini hakuonekana uwanjani katika mechi mbili zilizopita na hakusafiri na timu kwenda Seychelles kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika.
“Hakuna taarifa iliyotoka kwamba anaweza kuanza kucheza, taarifa iliyotoka ni Kamusoko kupona majeraha. Mchezaji akitoka kwenye majeraha hawezi kuanza kucheza mechi za ushindani moja kwa moja, anaanza kufanya mazoezi taratibu hadi awe kwenye kiwango cha asilimia 100 cha utimamu wa mwili ili aweze kupambana”-Dismas Ten.
“Anaweza akapona leo kesho akachezeshwa mechi akaumia tena, kwa hiyo Kamusoko alipewa muda, daktari amerejea kwa hiyo atamfanyia uchunguzi ili kuthibitisha kama tayari anaweza kurejea uwanjani kwa ajili ya mechi.”
“Daktari amerudi kutoka Seychelles kwa hiyo atafanya vipimo kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa wamesalia kwa sababu za majeraha nadhani taarifa yake itatolewa muda wowote.”
“Wachezaji waliokuwepo walikuwa wanaendelea na matibabu na walikuwa wanaendelea vizuri kwa maana wanaweza kurejea uwanjani wakati wowote lakini ni vyema kusubiri taarifa ya daktari yeye ndio anaweza kuamua nani na nani watakuwa tayari kwa mchezo wa FA na mchezo wa ligi Mtwara.”