Bibi Titi Mohamed

Historia ya Bibi titi mohamed
-mwanamke shujaa na mwanaharakati wa ukombozi wa Tanganyika

BIBI Titi Mohammed alizaliwa juni mwaka 1926 ,Dar es salaam, katika harakati zake za kuwakomboa wanawake ,Bibi Titi alikaririwa siku moja akisema; " Dhumuni langu kubwa ni kuhakikisha naamsha akili za wanawake waliolala na kubadilisha fikra na mitazamo yao na kuwaaminisha kwamba Uhuru wa Tanganyika utapatikana kama wanawake watajitambua".

Kumbukumbu pekee tulinayo ya Mwanaharakati huyu katika taifa letu ni mtaa na Barabara ya Bibi Titi iliyopo Dar es salaam, Kihistoria Bibi Titi Mohammed aliingia katika siasa kwa kushawishiwa na Schneider Plantan ,akapewa kadi namba 16 ,na mumewe bwana Boi Selemani alipewa kadi namba 15.( Bibi Titi Mohammed aliolewa akiwa na umri wa miaka 13) Alikuwa muasisi wa Umoja wa wanawake Tanganyika (UWT) uliokuja kuundwa rasmi Mwaka 1963, wakati wa harakati za kupigania Uhuru alisimamia vikundi vya muziki kama vile " Lelemama " na mara zote alitangulia kuongea na umati mkubwa wa watu Kabla hata ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hajaongea na watanganyika.

Bibi Titi alikuwa na Maneno makali dhidi ya ukoloni na alikuwa ana nguvu kubwa ya kushawishi .Akiwa na miaka 16 tu alikuwa mmoja kati ya wanawake wachache walioaminiwa katika kuongoza mapambano dhidi ya udhalimu waliokuwa wakifanyiwa watanganyika.

Mwaka 1955 ,Nyerere na Bibi Titi walifanya mkutano mkubwa huko Tabora ,Hii ni kutokana na mualiko walioupata toka kwa watu wa huko ,Ikumbukwe kuwa Tabora ya wakati huo ilikuwa na hamasa kubwa Katika kudai Uhuru. Hivyo mualiko ulitoka kwenye kamati ya wazee kama Hassan Mohamed Ikunji, Hamisi Khalfani ,Swedi Mambosasa, Germano Pacha ,Juma Mrisho ,Shaaban Mohamed Silabu ,Bilali Rehani ,Waikela ,Mohamed Mataka wakati ule akiwa muadhim wa Masjid Nur-msikiti wa Wamanyema pale Tabora.

Kuna mikutano mingi ya harakati za Uhuru aliyoongoza Bibi Titi Mohammed mfano ni ule wa Mombasa alioshirikiana na Tom Mboya wa Kenya, katika ukumbi wa Tononoka. Kiujumla Mkutano Mkuu wa kwanza Tabora ulifungua njia kukubalika kwa TANU baadaye kulifanyika Azimio la Tabora, Azimio hilo liliongozwa na Mwl Nyerere na wengine kama Sheikh Suleiman Takadir ,Mzee Jumbe Tambaza ,Juma Selemani na Bibi Titi. Hivyo Bibi Titi alikuwa mmoja wa waasisi wa Azimio la Tabora.
Baada ya Uhuru mwaka 1961 Bibi Titi alichaguliwa kuwa Mbunge bila kupingwa na kiongozi wa Wilaya mbili ,Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Mufindi na baadae alichaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa wanawake Tanganyika(UWT) na baadae Waziri, halikuwa jambo la kushtua kwani alistahili.

Mwaka 1963 Inaelezwa kulitokea kutoelewana kati ya Bibi Titi na Mwl Nyerere wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU uliofanyika Ukumbi wa Karimjee Dar es salaam. Hapo walitupiana maneno makali kabisa ,Inaelezwa kuwa kati ya mambo mengine mengi sababu zilikuwa ni Halmashauri Kuu ya TANU kulivunja Baraza la wazee wa TANU ,ambao kwa hakika walisaidia wakati wa harakati za Uhuru.

Hilo lilipingwa na Bibi Titi, jambo jingine linaelezwa na Mohamed Said katika kitabu chake kuwa Uamuzi wa Bibi Titi kutetea jumuiya ya EAMWS ambapo Mwalimu Nyerere alipinga hilo kwani aliona ni hatari kuchanganya dini na siasa. Bado pamekuwa na Ugumu kupata chanzo cha mgogoro wao huo kwani wengi wanaelezea mkutano huo ulikuwa ni nafasi ya kuonesha tofauti zao waziwazi.

Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965 ,Bibi Titi na Tewa Said Tewa (Rais wa jumuiya ya EAMWS) wakapoteza vitu vyao ndani ya TANU na Serikalini pia. Mwaka 1968 ,Bibi Titi pamoja na Waziri wa ulinzi Mh. Michael Kamaliza walikamatwa na kuhusishwa na matukio ya uhaini, Mahakamani wakakutwa na hatia ,wakahukumiwa kwenda jela kifungo cha maisha. Baada ya miaka miwili mwaka 1972 waliachiwa huru kwa msamaha wa Rais aliporudi uraiani Bibi Titi alitengwa na jamii ikiwemo mme wake, Boi Selemani, Pamoja na rafiki zake aliowapigania.

Walikuwa na urafiki na Mwl Nyerere kama zamani pamoja na kurudi toka jela( itakuwa hapakuwa na ugomvi mkubwa kati yao kama ilivyotiwa chumvi) .Bado aliendelea kukana kuhusika na tukio lile la uhaini. Alirudi nyumbani kwake na kuendelea na maisha yake ya kawaida huko maeneo ya Temeke ,Inaelezwa kwamba alipoteza kumbukumbu nyingi za harakati za Uhuru kama vile picha na taarifa nyingi za vikao ,baadaye alihamia upanga.

Alianza kuumwa, Bibi Titi alikaa kimya na kuendelea na matibabu yake ya moyo baada ya kupelekwa na Serikali ya Tanzania katika hospitali ya Net Care huko, Johannesburg, Afrika Kusini. Alifariki dunia akiwa hapo hospitalini akipata matibabu Novemba 5 mwaka 2000( mwaka mmoja baada ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere)
Mungu iweke roho yake mahala pema peponi.Amina.