Shuhudia vipigo vya mbwa koko huku ukiona jinsi mabinti hawa wanavyotoa visago kwa minjeba iliyojishibia. Picha| Mandatory.
- Imesheheni visa na mikasa ya kuchekesha huku ikikufundisha namna ya kuepukana na msongo wa mawazo baada ya mahusiano kuvunjika.
- Utapata somo pia kuhusu ushirikiano
- Zipo filamu nyingine kama The After Math zitakazokufaa wakati huu wa msimu wa mahaba.
Dar es Salaam. Foleni za barabarani, mlundikano wa kazi, jua kali, kelele za magari ya kubebea wagonjwa na ving’ora vya viongozi mashuhuli huenda vikawa vimekuandama wiki nzima kiasi cha kuichosha akili yako.
Wakati ukiwa na kila sababu ya kutafuta sehemu kwa ajili ya kutafakari maisha yako, mtandao huu unakuletea uchambuzi wa filamu mpya ambayo itaonyeshwa wiki hii.
Filamu hii siyo tu atakuondolewa upweke na msongo wa mawazo bali utakuacha na kicheko ambacho kitakusahaulisha matatizo yako yote.Ni filamu ya “Birds of Prey”.
Harleen Quinze (Margot Robbie) ambaye ameachana na mpenzi wake “Joker” anaugulia maumivu ya kuachika.
Baada ya kufukuzwa nyumbani alipokuwa akiishi na Joker, anaishi na Doc ambapo anaendelea kuugulia maumivu ya kuachika kwake.
Kujifungia ndani na kula vyakula vya kila aina kunaisha pale anapoamua kubadili mtazamo wa maisha yake kwa kutafuta furaha iliyo potea.
Hapo ndipo anaungana na wasichana wenzake wanne wote wanawindwa kuuwawa lakini kauli ya Quinze ya “tufanye kazi pamoja” inawashangaza wasichana hao ambao wanajikuta wakikubali kutokana na kila mmoja anaugulia maumivu yake.
Helena Bertinelli, Black Canary, Renee Montoya, Cassandra Cain na Cassandra Cain wanaunda kundi kupambana dhidi ya Roman Sionis / Black Mask (Ewan McGregor) ambaye anawawinda kama paka awindavyo panya.
Shuhudia vipigo vya mbwa koko huku ukiona jinsi mabinti hawa wanavyotoa visago kwa minjeba iliyojishibia kwenye filamu iliyoongozwa na Cathy Yan aliyetumia kibunda cha Sh224.3 bilioni chini ya kampuni ya Warner Bros ya nchini Marekani.
Bado utamu haujaisha
Hata hivyo, katika mwezi huu wa mahaba, kama umepanga kufurahia muda wako na umpendaye, zipo filamu mahususi kwaajili yenu ambazo zitawafundisha masomo mbalimbali na kuongeza ufahamu wa mahusiano yenu.
Kama hilo ni fungu lako, unaweza kuangalia filamu ya “Berlin I Love You” ambayo ni filamu itakayokufundisha kuwa mapenzi siyo safari ya barabara safi. Kuna kugombana na hata kurudiana baada ya ugomvi uliohisi umelimaliza penzi lako.
Pia, unaweza kupakua filamu ya The After Math ambayo itakuonyesha sababu ya wewe kumuweka mpenzi wako kwanza kabla ya majukumu yako.
Ndiyo mkono lazima uende kinywani lakini pia, lazima uwe na uhakika kuwa uliye naye kama mwenzi wa maisha, anakupenda kweli kweli.
Unapata shida ya kutofautisha ulimwengu wa uhalisia na ulimwengu wa kimapenzi? Filamu ya Falling In Love itakufungulia njia ya ufahamu.
Angalizo! Usije kunilaumu kuwa mapenzi yako yameharibiwa na makala hii, chonde chonde, ya kuambiwa changanya na yako. Tukutane ijumaa ijayo.

0 Comments