FONETIKI AU UTAMKWAJI WA SAUTI-FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU FONETIKI AU UTAMKWAJI WA SAUTI-FONIMU ZA KISWAHILI SANIFU MWIZA PETER - 02:36  3.2.1 Maana Ya Fonetiki Fonetiki ni taaluma inayojishughulisha na jinsi sauti yo yote inavyotolewa au inavyopatikana. Hii ni sayansi huru ambayo inatumia nadharia za sayansi halisi kama vile fizikia, uhandisi, baiolojia, nk. na kufaidi matokeo ya kiutafiti ya taaluma hizi. Mathalani, ili mwanafonetiki aelewe jinsi ala za sauti zinavyofanya kazi wakati wa utolewaji wa sauti, atafaidika na maelezo ya kibaiolojia kuhusu namna mfumo wa mwili wa mwanadamu unavyofanya kazi. Mgulu, (2001:48) anadai: ‘ ... fonetiki ni moja tu, lakini fonolojia zipo nyingi kama lugha zenyewe zilivyo nyingi. Kwa mfano, hatuna fonetiki ya Kiingereza au fonetiki ya Kiswhili. Fonetiki ni fonetiki tu. Kwa upande mwingine, tuna fonolojia za lugha mbalimbali ambazo hutofautiana. Tunazo, kwa mfano, fonolojia ya Kiswahili, fonolojia ya Kiingereza, fonolojia ya Kifaransa, fonolojia ya Kinyamwezi, fonolojia ya Kindendeule, nk. Tunapozungumzia upatikanaji wa sauti za lugha za binadamu, tunafafanua jinsi sauti za lugha husika zinavyotamkwa katika bomba la sauti la mwanadamu. (Tazama Jedwali 3.5). Tunazibainisha ala, hususani alasogezi na alapahala husika katika kuitamka sauti husika. Alasogezi ni ile ala ambayo inaweza kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. Alapahala au Ala-tuli ni ile ala ambayo haiwezi kujimudu wakati wa utamkwaji wa sauti husika. (Tazama Kielelezo 3.1). Ni alasogezi ambayo hujisogeza kwenye alapahala husika wakati wa utamkwaji wa sauti husika (Nchimbi, 1979). 3.2.2 Utamkwaji wa Sauti-Fonimu za Kiswahili Ieleweke kwamba hewa itokayo kwenye chemba ya mapafu ambayo sisi sote twaitumia kwa kupumua ili tuishi, ndiyo hiyo hiyo itumikayo katika utamkwaji wa sauti za lugha za binadamu. Hewa hiyo itapitishwa kwenye chemba zilizomo katika bomba la sauti kwa mujibu wa sauti inayotarajiwa kutamkwa hadi nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo au chemba ya pua Hewa hiyo ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate ku Lakini hewa hiyo, isipopitia chemba ya pua, ikapitia chemba ya midomo tu hadi nje, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-sing’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. (Tazama Kielelezo 3.4). Tutaanza kufafanua utamkwaji wa sauti-fonimu-irabu za Kiswahili, ukifuatiwa na ufafanuzi wa utamkwaji wa sauti-fonimu-konsoni za Kiswahili. Ufafanuzi utafanywa kwa kuzingatia vigezo vin’ne, navyo ni: (a) utamkwaji ki-alapahala, (b) utamkwaji ki-sampuli, (c) utamkwaji ki-ughuna, (d) utamkwaji ki-ung’ong’o na, (e) msimamo wa midomo hususani kuhusu utamkwaji wa fonimu-irabu. 3.2.3 Utamkwaji wa Fonimu-Irabu-Mama za Lugha za Binadamu Irabu-mama katika lugha zote za binadamu ni /i a u/ ambazo utamkwaji wake katika bomba la sauti unajitokeza kwenye alapahala ya burutio-gumu/kaakaa-gumu ikishirikiana na alasogezi ya ulimi-kati ki-alasogezi-pahala kama ilivyo kwenye Kielelezo 3.5. Katika Kielelezo 3.5 alasogezi-pahala za irabu, irabu-mama /I/ inajidhihirisha kuwa ni ya juu-mbele wakati irabu-mama /U/ ni ya juu-nyuma. Irabu-mama /A/ ni ya chini-kati. Vigezo vya kufafanulia matamshi ya irabu ni kama ifuwatavyo: (i) Kwa Mujibu wa Alapahala:ni burutio-gumu; ama sehemu ya mbele, ama sehemu ya kati, ama sehemu ya nyuma ya burutio-gumu. (ii) Kwa Mujibu wa Alasogezi: ni ulimi; ama sehemu ya mbele (ulimi-mbele), ama sehemu ya kati (ulimi-kati), ama sehemu ya nyuma ya ulimi (ulimi-nyuma). (iii) Kwa Mujibu wa Midomo: ni ama midomo-tandazi au midomo-futuzi. (iv) Kwa Mujibu wa Mpenyo: ni ama mpenyo-mwembamba, ama mpenyo-mwembamba-kiasi, ama mpenyo-mpana. (v) Kwa Mujibu wa Kidaka-Tonge: ni ama irabu-ng’ong’o ama irabu-sing’ong’o (vi) Kwa Mujibu wa Nyuzi za Sauti/Glota: ni ama irabu-ghuna ama irabu-sighuna. 3.2.4 Utamkwaji wa Fonimu-Irabu //i e a o u/ Fonimu-irabu za kiswahili sanifu ni /i e a o u/. Fonimu-irabu-mbele za kiswahili sanifu ni /a e i/ na fonimu-irabu-nyuma ni /a o u/. Fonimu-irabu na nusu-irabu-mbele /a e i j/. Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-mbele / a e i /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-mbele. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [e] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i]. Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [i] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi , basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [j] hudhihirika, yaani [a e i j]. Aidha, midomo hubakia tandazi (Nchimbi,1979). Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Utamkwaji wa Fonimu-Irabu na Nusu-Irabu-Nyuma /a o u w/:Wakati wa utamkwaji wa fonimu-irabu-nyuma / a o u /, alasogezi ya ulimi-kati hujikweza kuelekea kwenye alapahala ya burutio-gumu-nyuma. Mpenyo unaofanyizwa kati ya alasogezi ya ulimi-kati na alapahala yake ya burutio-gumu-mbele ni mpana wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [a], ni mpana kidogo wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [o] na ni mwembamba wakati wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u]. Aidha, alasogezi ya mdomo-chini na alapahala ya mdomo-juu hujifutua, na kwa hiyo, kufanyiza mpenyo aina ya mviringo. Mpenyo huu wa matamshi ya sauti-endelezi ya irabu [u] unapofanyizwa kuwa mwembamba zaidi, basi matamshi ya sauti-endelezi ya nusu-irabu [w] hudhihirika, yaani [a o u w], na midomo hubakia futuzi. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Kielelezo 3.7: Alasogezi-Pahala za Irabu na Nusu-Irabu za Burutio-Gumu-Nyuma na Midomo-Futuzi [o u w] Tija itokanayo na mfumo wa matamshi ya sauti-irabu za kiswahili sanifu: maelezo yanayotokana na (a) utamkwaji wa fonimu-irabu za burutio-gumu-mbele [a e i] na nusu-irabu [j] na (b) utamkwaji wa fonimu-irabu za burutio-gumu-nyuma [ o u] na nusu-irabu [w], yanatuwezesha kufanyiza (i) Jedwali ya mfumo wa matamshi ya irabu za kiswahili sanifu [i e a o u], (ii) Tarapezi ya mfumo wa irabu za kiswahili sanifu [i e a o u], na (iii) Jedwali la mfumo wa matamshi ya nusu-irabu/konsoni za kiswahili sanifu [j w], kama ilivyo katika Jedwali 3.6. Jedwali 3.6: Jedwali ya Mfumo wa Matamshi ya Irabu za Kiswahili Sanifu [i e a o u] ALAPAHALA YA KITAMKWA Burutio-gumu Mbele. Burutio-Gumu Kati. Burutio-Gumu Nyuma MPENYO i u UNG’ONG’O Mwembamba (Juu) Sing’ong’o Mpana Kiasi (Kati) e o Mpana (Chini) a Ulimi-kati mbele Midomo-tandazi/sifutuzi Ulimi-kati nyuma Midomo-futuzi/sitandazi ALASOGEZI YA KITAMKWA Kielelezo 3.8: Tarapezi ya Mfumo wa Irabu za Kiswahili Sanifu [i e a o u] Jedwali 3.7: Jedwali ya Mfumo wa Matamshi ya Nusu-Irabu/Konsoni za Kiswahili Sanifu [j w] MSIMAMO WA MIDOMO ALAPAHALA YA KITAMKWA UGHUNA BURUTIO-GUMU BURUTIO-LAINI Midomo tandazi J Ghuna Midomo futuzi w Ulimi-Kati Ulimi Nyuma ALASOGEZI ZOEZI 1. Zitaje chemba (cavities) zinazolijenga bomba la sauti la mwanadamu. 2. Zitaje alasogezi (articulators) zilizomo katika bomba la sauti la mwanadamu. 3. Zitaje alapahala (places of articulation) zilizomo katika bomba la sauti la mwanadamu. 4. (a) Tofautisha matamshi ya irabu-mbele na irabu-nyuma. (b) Eleza tofauti kati ya matamshi ya irabu [i] na nusu-irabu [j], au irabu [u] na nusu-irabu [w]. 5. Eleza tofauti kati ya alasogezi na alapahala. 3.2.5 Utamkwaji wa Sauti-Fonimu-Konsoni za Kiswahili Sanifu Utamkaji wa fonimu-konsonanti za Kiswahili utafafanuliwa kwa mujibu wa vigezo vinne: utamkaji ki-alapahala, utamkaji ki-sampuli, utamkaji ki-ughuna, na utamkaji ki-ung’ong’o. (i) Utamkwaji wa Sauti-Fonimu-Konsoni za Kiswahili Ki-Alasogezi-Pahala Fonimu-konsoni zote ishirini na tisa (29) za Kiswahili sanifu hudhihirishwa kimatamshi kwa kutumia alapahala saba (7) ambazo nazo huhusishwa moja kwa moja na alasogezi husika zilizomo katika bomba la sauti (Nchimbi, 1979), kama ifuatavyo: Utamkwaji wa Vimidomo [p, b]: Wakati wa matamshi ya sauti za midomoni [p, b], alasogezi ya mdomo-chini hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka, kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. (Tazama Kielelezo 3.8). Utamkwaji wa Vimdomochini-Menojuu [f v]: Wakati wa matamshi ya vimdomochini-menojuu [f] na [v], alasogezi husika ambayo ni mdomo-chini, hujikweza na, ama kujibandika kwenye alapahala ya meno-juu, au hujisogeza na kuacha nafasi finyu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni hujipenyeza kwa taabu kadiri unavyopitishwa katikati ya nafasi finyu inayofanyizwa kwa mdomo-chini na meno-juu, au kati ya jino na jino wakati mkondo huo unapoelekezwa n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomoni. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Utamkwaji wa Viulimincha-Menojuu [θ ð]: Wakati wa matamshi ya viulimincha-menojuu [θ] na [ð], alasogezi ya ulimi-ncha hujisogeza kwenye alapahala ya meno-juu na kuacha nafasi finyu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni hujipenyeza kwa taabu kadiri unavyopitishwa katikati ya nafasi finyu inayofanyizwa kwa ulimi-ncha na meno-juu wakati mkondo huo unapoelekezwa nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomoni. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Utamkwaji wa viulimincha-ufizijuu [t d s z ]: Alasogezi ya ulimi-ncha na alapahala ya ufizi-juu ndizo zinazotumika wakati wa matamshi ya viulimincha-ufizijuu. [t d s z r l]. Utamkwaji wa [t d]: Alasogezi ya ulimi-ncha inajikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu; mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika ndii... kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Kwa mantiki hii, viulimincha-ufizijuu vinavyotamkwa ni [t d ]. Utamkwaji wa [s z]: Wakati alasogezi ya ulimi-ncha inapojisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya ufizi-juu, mkondo wa hewa utokao mapafuni hupata nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [s z ]. Utamkwaji wa Viulimikati-Burutiogumu [c ɟ ʃ j]: Utamkwaji wa [c ɟ] Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [c ɟ], alasogezi ya ulimi-kati, hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya Bomba la Sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [c ɟ]. Utamkwaji wa [ʃ j]: Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [ʃ j ]; alasogezi ya ulimi-kati hujisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya burutiogumu. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [ʃ j]. Utamkwaji wa Viuliminyuma-Burutiolaini [k g Ɣ]: Wakati wa matamshi ya viulimikati-burutiogumu [k g], alasogezi ya ulimi-nyuma, hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu-nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [k g], Tazama Kielelezo 3.15. Unapojitokeza wakati wa matamshi ya [Ɣ], alasogezi ya ulimi-nyuma hujisogeza kiasi cha kuacha nafasi finyu kati yake na alapahala ya ukuta wa marakaraka au ncha ya kidaka-tonge. Nafasi hii itaruhusu mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Midomo hubakia tandazi itamkwapo sauti [Ɣ] Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [Ɣ] Utamkwaji wa Kiglota [h]: Wakati wa matamshi ya kiglota [h], alasogezi ya ulimi hubakia chini kiasi cha kuacha nafasi kubwa kati yake na alapahala ya burutio. Mkondo wa hewa kutoka mapafuni unapopita katika chemba ya koromeo, nyuzi sauti zilizomo katika chemba hiyo ama hurindima na ikapatikana sauti [ h ], au hazirindimi na kupatikana sauti [h]. Aidha , mkondo huu wa hewa kutoka mapafuni hupitishwa moja kwa moja katika chemba ya kinywa bila kizuizi mpaka n’nje ya kinywa. Kwa mantiki hii, nyuzi sauti zinaweza kueleweka kama alasogezi ya matamshi ya sauti [h] ya fonimu /h/. Midomo hubakia tandazi itamkwapo sauti [h]. Na alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o [h] (ii) Utamkaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Sampuli Utamkwaji wa sauti ki-sampuli unabainisha kati ya sauti-endelezi na sauti-sendelezi. Utamkaji wa sauti ki-sampuli ni ule unaosababishwa na alasogezi ya ulimi na mdomo-chini inaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika. Ulimi au mdomo-chini unaponyanyuka kuelekea kwenye alapahala husika, husababisha matamshi ya sampuli za sauti zifuatazo: Sauti-sendelezi-konsoni ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husika hujikweza na kujibandika kwenye alapahala husika; ambayo kwa [p b ] ni mdomo-juu, kwa [t d] ni ufizi-juu, kwa [c ɟ ] ni burutio-gumu-mbele na kwa [k g N] ni burutio-gumu- nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii utamkaji wa sauti-konsonanti-katizi hauendelezeki. Mifano ya sauti-konsonanti-katizi katika Kiswahili ni [p b  t d c ɟ k g ]. Sauti-endelezi-konsoni-madende ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Kuzuiliwa kwa mkondo huu wa hewa ni kwa muda mfupi sana. Kwa mantiki hii, alasogezi ya ulimi-ncha huonekana ikiyumbishwa kana kwamba inajigongagonga kwenye matuta ya alapahala ya ufizi-juu. Aidha, utamkaji wa sauti hii huwa katizi unaoendelezeka kwa vigongo, yaani, kimadende. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Hisia ya sauti inayosikika ni sauti-sing’ong’o. Mfano wa sauti-konsonanti-madende-endelezi ni [r]. Sauti-Endelezi-Konsoni-Kwama Kwamizi ambayo wakati wa utamkwaji wake, alasogezi husika hujikweza na kuunda mpenyo mwembamba sana kwenye alapahala husika, kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo hupita, lakini kwa hukwamizwa kwamizwa, unapoelekea n’nje ya Bomba la Sauti. Matokeo yake ni matamshi ya sauti-konsonanti-endelezi kwama kwamizi, kama vile: [f v θ ð s ʃ [Ɣ] h] Sauti-endelezi-konsonanti-tambazi ambayo wakati wa utamkaji wake, alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu, kiasi kwamba sehemu ya mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi hapo kwenye alapahala ya ufizi-juu ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti, na sehemu iliyobakia ya mkondo huo wa hewa huchepukia pembezoni mwa ulimi na hatimaye kuelekea n’nje ya bomba la sauti. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua. Kwa mantiki hiyo, hisia za n’nje zinazosikika ni za aina ya sauti-endelezi sing’ong’o ambapo hewa yake inatambaa. Mfano wa hii sauti-konsonanti-tambazi ni [l]. 3.2.6 Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ughuna 3.2.6.1 Utangulizi Utamkwaji wa sauti ki-ughuna unabainisha kati ya sauti-ghuna ambayo husababisha nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye chemba ya koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani: [KO: ], na sauti-sighuna ambayo haisababishi nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, na kwa hivyo, hisia inayojitokeza si ya mawimbi-mawimbi, yaani: [KO:___________]. Aidha, hisia za sauti-sighuna hazijitokezi kwenye Chemba ya Pua [PU:____________], wala kwenye chemba ya kinywa [KI:__________] wala kwenye Hisi N’nje [NJE:________]. Tazama kwa mintarafu ya Kielelezo 3.19. Kielelezo 3.19: Utamkwaji Wa Sauti-Ghuna Na Sauti-Sighuna, Kwa Mfano, Katika Neno “Sasa” Kwenye Mingogramu (Mingo) Ufasili wa Mingo hii ya Neno “Sasa”: (a) Sauti [s]: (i) ni sauti sighuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO: ___________] (ii) ni sauti sing’ong’o kwa kuwa nyuzi sauti/glota hazioneshi ishara ya kutetemeka/mawimbi-mawimbi kwenye msitari wa chemba ya pua, yaani: [PU:_______]. (b) Sauti [a]: ni sauti ghuna kwa kuwa nyuzi sauti/glota zinaonesha ishara ya kutetemeka/mawimbi- mawimbi kwenye msitari wa chemba ya koromeo, yaani: [KO: ] Utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi za Kiswahili sanifu: Katika Kiswahili sanifu, sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi zinazojitokeza ni [a], [e], [i], [o], [u], [v], [ð], [z], [r], [l], [j], [Ɣ]. Sauti-ghuna hizi ndizo zinazosababisha nyuzi za sauti/glota zilizomo kwenye chemba ya koromeo zitetemeke, yaani hisia ya kwenye Chemba ya Koromeo [KO] huwa ya mawimbi-mawimbi, yaani: [KO: ]. Kumbuka kwamba wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna, alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejikweza na kujibandika kwenye ukuta wa marakaraka, kitendo ambacho hakiruhusu hewa kupenya hadi kwenye chemba ya pua wakati wa utamkwaji wa sauti-ghuna-sing’ong’o-endelezi. (iv) Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Ung’ong’o Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka n’nje ya bomba la sauti. Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [m]: Wakati wa matamshi ya sauti ya midomoni [m], alasogezi ya mdomo-chini hujikweza na kujibandika ndii... kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [m] hudhihirishwa na ikadhihirika. Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [n]: Alasogezi ya ulimi-ncha na alapahala ya ufizi-juu ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimincha-ufizijuu [n] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi. Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimincha-ufizijuu [n], alasogezi ya ulimi-ncha hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [n] hudhihirishwa na ikadhihirika. Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [ɲ]: Alasogezi ya ulimi-kati na alapahala ya burutio-gumu(kaakaa-gumu) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ɲ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi. Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ɲ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ɲ], hudhihirishwa na ikadhihirika. Utamkwaji wa Sauti-Konsoni-Ghuna-Ng’ong’o-Endelezi [ŋ]: Alasogezi ya ulimi-kati na alapahala ya burutio-laini(kaakaa-laini) ndizo ala zinazotumika wakati wa matamshi ya kiulimi-kati [ŋ] ambayo ni sauti-konsoni-ghuna-ng’ong’o-endelezi. Wakati wa matamshi ya sauti ya kiulimi-kati [ŋ], alasogezi ya ulimi-kati hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutio-gumu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao mapafuni haupati nafasi ya kupenya kuelekea n’nje ya bomba la sauti kwa kupitia chemba ya midomo. Lakini wakati huo huo, alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua; sauti-ghuna-ng’ong’o-endelezi [ŋ], hudhihirishwa na ikadhihirika. Katika mfumo wa sauti-irabu za Kiswahili Sanifu [a e i o u ], tunagundua kwamba apana sauti-irabu-ng’ong’o hata moja baina yao, zote ni sauti-irabu-sing’ong’o. Lakini katika mazungumzo ya kimtindo, aghalabu hizi sauti-irabu-sing’ong’o huweza kung’ong’oishwa na msikilizaji akapata hisia ya sauti-irabu-ng’ong’o, kama hivi: [a e i o u ], yaani wakati wa utamkwaji wa kila irabu kivyake, hewa itokayo mapafuni lazima itoke n’nje sambamba kwa kupitia chemba ya midomo na tundu za pua, kama Kielelezo 3.25 kinavyoushereheshea. Hewa hiyo inayotoka mapafuni, ikipitia chemba ya pua tu au chemba ya pua na chemba ya midomo bila kusitishwa, basi hisia za sauti itakayotamkwa zitakuwa za sauti-ng’ong’o-endelezi [a], [e], [o], [m], [ŋ], nk., yaani, sauti za ming’ung’uto. Alasogezi ya kidaka-tonge huwa imejishusha kutoka kwenye ukuta wa marakaraka (paroi pharangale) ili hewa hiyo ipate kupita na kutoka nje ya bomba la sauti, bila kusitishwa! (v) Utamkwaji wa Sauti za Fonimu za Kiswahili Ki-Mang’ong’o Utamkwaji wa Mang’ong’o ya Kiswahili Sanifu [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng] au [] Utamkwaji wa sauti za fonimu za Kiswahili ki-mang’ong’o, ni utamkwaji wa sauti-fonimu-mang’ong’o [mb] au [], [nd] au [], [nj] au [], [ng] au []. Huu ni utamkwaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi, yaani utamkwaji wa MANG’ONG’O kama kielelezo3.26 kinavyotushereheshea: Kila sauti-fonimu-mang’ong’o ni sauti-ghuna, ughuna ambao hujidhihirisha kwenye msitari wa chemba ya koromeo [KO: ] na hususani kwenye msitari wa chemba ya pua [PU: ] kama ilivyo katika utamkaji wa sauti-fonimu-ng’ong’o za kawaida [m n ɲ ŋ], Kivyake, kila sauti-fonimu-mang’ong’o hutamkwa kama ifuatavyo: (a) Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [mb] au [] Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [mb] au [] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo: · alasogezi ya mdomo-chini inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya mdomo-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika: · alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua. · mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya mdomo-chini hujibandua kutoka kwenye alapahala ya mdomo-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. (b) Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [nd] au [] Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nd] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo: · alasogezi ya ulimi-ncha inapojikweza na kujibandika ndii kwnye alapahala ya ufizi-juu kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya Bomba la Sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika: · alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua. · mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-ncha hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ufizi-juu na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. (c) Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi [nj] au [] Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [nj] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo: · alasogezi ya ulimi-kati inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti. Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika: · alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua. · mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-kati hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-mbele na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. (d) Utamkwaji wa Sauti-Ng’ong’o-Sendelezi , [ng] au [] Utamkaji wa sauti-ng’ong’o-sendelezi [] hudhihirishwa katika hatua zifuatazo: · alasogezi ya ulimi-nyuma inapojikweza na kujibandika kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma kiasi kwamba mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo haupati nafasi ya kutoka n’nje ya bomba la sauti, (angalia Kielelezo 3.27). Wakati kitendo cha hapo juu kinatendeka, kitendo kifuatacho hufanyika: · alasogezi ya kidaka-tonge hujibandua kutoka kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka na kuacha nafasi wazi kwa mkondo wa hewa utokao kwenye chemba ya koromeo kupenyeza mpaka kwenye chemba ya pua. · mrindimo-ng’ong’o unapoanza kujidhihirisha kwenye nyufa za chemba ya pua, alasogezi ya ulimi-nyuma hujibandua kutoka kwenye alapahala ya burutiogumu-nyuma na alasogezi ya kidaka-tonge hujikweza na kujibandika kwenye alapahala ya ukuta wa marakaraka; vitendo vyote hivi vitatu hutendeka wakati mmoja. Jedwali 3.7 (a): Mfumo wa Matamshi ya Konsoni za Kiswahili Sanifu Alasogezi Alapahala Alasogezi-Pahala Kitamkwa/Sauti Mdomo-chini mdomo-juu Midomo [p], [], [b], [m], [w] Mdomo-chini meno-juu mdomochini-menojuu [f], [v] Ulimi-ncha meno-juu ulimincha-menojuu [θ], [ð] Ulimi-ncha Fizi-juu ulimincha- fizijuu [t], [], [d], [n], [s], [z], [r], [l] Ulimi-kati Burutio-gumu(kaakaa-gumu) ulimikati-burutiogumu [c], [], [ ɟ], [ɲ], [ʃ], [j]. Ulimi-nyuma Burutio-laini(kaakaa-laini) uliminyuma- burutiolaini [k], [], [g], [ŋ], [Ɣ], [w] nyuzi-sauti (nyuzi-glota) Glota Glota [h]. 3.2.7 Uhusiano Baina ya Fonetiki na Fonolojia Sauti-fonimu-irabu na konsoni zilivyojipanga katika mfumo wa kifonetiki/matamshi ambao unasababisha kuwako tofauti ya maana katika jozi milinganuo finyu za lugha ya Kiswahili ndio unaotuonesha uhusiano baina ya fonetiki na fonolojia. Upo uhusiano wa karibu sana kati ya taaluma ya fonetiki na taaluma ya fonolojia. Sifa-bainifu za kifonolojia asili yake iko kwenye sifa-bainifu za kifonetiki. Kwa mfano, (a) sauti [p] inatofautiana na sauti [b] kwa sifa ya kifonetiki ya u-ghuna; kwamba [p] ni [ - ghuna] wakati sauti [b] ni [+ ghuna]; (b) sauti [b] inatofautiana na sauti [k] kwa sifa mbili za kifonetiki: (i) sifa ya ki-ghuna, kwamba sauti [k] ni [ - ghuna] wakati sauti [b] ni [+ ghuna]; (ii) sifa ya ki-alasogezipahala, kwamba sauti [b] ni ki-midomo wakati sauti [k] ni ki-uliminyuma-burutiolaini. Sifa hizi za kifonetiki/matamshi ndizo zinasababisha maana ya neno ibadilike, kwani badala ya neno kutamkwa [paka] linatamkwa [baka]; au [bata] linatamkwa [kata]; nk. Kwa mantiki hii, sifa-bainifu za kifonetiki ndizo zinazosababisha kuwako kwa sifa-bainifu za kifonolojia. Na tunazibaini fonimu (ambacho ndicho kipashio cha fonolojia) kwazo. Kwa mfano: (a) pata ~ peta ~ pita ~ pota ~ puta; Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe (commutation), tunadiriki kudai kwamba sauti [a], [e], [i], [o], na [u] ni fonimu /a/, /e/, /i/, /o/, /u/ katika Kiswahili. (b) yeye ~ wewe; yote ~ wote Kwa mbinu ya nitowe-nikutowe, tunadiriki kudai kwamba sauti nusu-irabu [j] na [w] ni fonimu /j/ na /w/ katika Kiswahili. (c) pawa ~ bawa ~ tawa ~ dawa ~ chawa ~ jawa ~ kawa ~ gawa. Kwa mbinu ya nitoe-nikutoe, tunadiriki kudai kwamba sauti sauti [p], [b], [t], [d], [c], [ɟ], [k], [g] ni fonimu /p/, /b/, /t/, /d/, /c/, /ɟ/, /k/, /g/ katika Kiswahili. Hii ndiyo mbinu kongwe ya kiisimu ambayo inatumiwa na wanaisimu katika utafiti wa fonimu za lugha yo yote ya binadamu. Na ndiyo mbinu iliyotumiwa kuzigundua fonimu za lugha, kama vile fonimu za Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, nk. ambazo tunajifunza katika vyuo vyetu. MAREJELEO Maganga (1997), OSW 102: Historia ya Kiswahili. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Masebo, J. A. Nyengwine, N. (2002), Nadharia ya Lugha ya Kiswahili, Kidato cha 5 na 6. Aroplus Industries Ltd: Dar es Salaam. Nkwera, Fr. F. V. (2003), Sarufi, Fasihi na Uandishi wa Vitabu, Sekondari na Vyuo. Creative Prints Ltd: Dar es Salaam. jiunge nasi bofya hapa ku-install application yetu swahiliform ili usisumbuke kuingia kwenye website yetu Share on Facebook Share on Twitter Share on Google Plus About mwiza peter  mwiza peter ni mwalimu ambaye alipata taaluma hii chuo cha ualimu morogoro(motco) kwa sasa nipo morogoro nimiongoni mwa vijana ambao lengo langu nikukufanya wewe kupata elimu kuhusu somo la kiswahili na kuongeza ufahuru wa somo hili. tupo morogoro kihonda magorofani Tanzania.karibu mwaa tunawapenda wote.elimu ni ukombozi wa maisha chukua hatua RELATED POSTS BLOGGER COMMENT 0 comments:  Chapisho Jipya Taarifa za zamani Nyumbani JUMLA YA MARA ILIYOTAZAMWA  375030 HABARI MPYA  RSS Feed Widget   TWITTER  MATANGAZO  BLOG RAFIKI EMT BLOG habari jackiline blog shoe designer blog DESIGNED/ADMIN BY  Copyright © 2015 Swahili form Created By Sora Templates and My Blogger Themes