Tuesday

SIMBA YA KIMAFIA YAREJEA

0 comments

SIMBA YA KIMAFIA YAREJEA


NA ZAITUNI KIBWANA
UNAIKUMBUKA Simba ile iliyokuwa ikisifika kwa umafia, hasa linapokuja suala zima la usajili wa wachezaji? Kama jibu ni ndio au hapana, usikonde. Kwa wasiofahamu, klabu hiyo kwa sasa si ya kuchezea tena kama ilivyokuwa kwa misimu michache iliyopita.
Unajua ni kwanini? Baada ya Simba kudorora ndani ya misimu mitano iliyopita, safari hii imeibuka kwa kishindo na kuwa tishio katika suala zima la usajili wa wachezaji ambapo hadi sasa, imefanikiwa kuwanasa nyota kadhaa wakiwamo kipa mahiri, Aishi Manula, beki wa kulia ,Shomari Kapombe na mshambuliaji wa kati, John Bocco, wote kutoka Azam.
Mbali na hao, Simba inamrejesha nyota wake Mganda, Emmanuel Okwi, huku pia ikiwa katika mkakati wa chini kwa chini kuwasainisha kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima na mshambuliaji wa watani wao hao wa jadi, Donald Ngoma.
Wakati Manula, Kapombe na Bocco wakiwa tayari wameshamwaga wino Msimbazi, Niyonzima anatarajiwa kumaliza mchezo muda wowote kuanzia jana jioni kwani kuna kiongozi wa Simba yupo nchini Rwanda kumalizana na nyota huyo.
Kwa upande wa Ngoma, imeelezwa kuwa Mzimbabwe huyo naye yupo mbioni kutua Msimbazi tayari kukinukisha msimu ujao akiwa na jezi za rangi nyekundu na nyeupe.
Ukiachana na hao, wapo wachezaji nyota kadhaa wanaowindwa na Simba ambapo kutokana na jeuri yao kifedha safari hii, inaonekana wazi hawawezi kushindwa katika vita ya usajili.
Imeelezwa kuwa klabu hiyo kwa sasa haina shida ya fedha tena kwani mwanachama wao maarufu, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameahidi kutoa kiasi chochote cha fedha kwa mchezaji anayetakiwa na timu hiyo, ikiwamo kuwabakiza wale wanaowahitaji waliopo kikosini kwa sasa kama Jonas Mkude, Ibrahim Ajib na wengineo.
Juu ya Kapombe, beki huyo aliyetua Azam akitokea Msimbazi, amesaini mkataba wa miaka miwili jana, japo alikuwa kwenye mazungumzo na klabu yake ya kuongezwa mkataba mpya, kabla ya Simba kufanya umafia wao dakika za mwisho.
Imeelezwa kuwa Azam walimtengea Kapombe Sh milioni 20, lakini Simba wakawazidi ujanja kwa kutoa Sh milioni 35.
Meneja wa Kapombe ambaye hakutaka kutajwa jina lake  alisema: “Kwa hali ya kawaida, mtu anakupa milioni 20 mezani, halafu mwingine anakupa zaidi ya milioni 30, sasa unakataa zipi hapo? Azam wajilaumu wenyewe kwa kumkosa Kapombe si kwa kosa letu.”

No comments:

Post a Comment