Justin M.K. Mallya
1. Utangulizi
Popote pale duniani mwandishi wa kitabu anapoketi chini kuandika anategemea vitu vitatu: kwanza, kitabu chake kitoke vizuri na haraka iwezekanavyo; pili, kisomwe na watu wengi iwezekanavyo; na tatu, apate chochote kutokana na jasho lake. Hivi vikikosekana lazima mwandishi yeyote yule alalamike. Na mtu wa kwanza kumlalamikia au kumlaumu ni mchapishaji.
Katika Tanzania ni waandishi wachache wenye bahati ya kupata mambo yote hayo matatu. Kwa hiyo malalamiko na lawama kwa wachapishaji ni nyingi. Nia ya makala haya ni kuangalia malalamiko au lawama hizi; na jinsi mengi ya malalamiko yanavyotokana na matatizo waliyo nayo wachapishaji wenyewe.
Si nia yangu kuwatakasa wachapishaji - wengi tuna madhambi yetu dhidi ya waandishi, na hii lazima tukiri. Lakini naamini kuwa kulaumiana kwingi kunatokana na waandishi kutofahamu yanayotokea katika dunia ya uchapishaji nchini, na matatizo yake; na kwamba haya yakiwekwa wazi kwa waandishi kutakuwa na uelewano mzuri zaidi kati yao na wachapishaji katika kufanya kazi pamoja na kufanikisha usambazaji wa 'neno'.
Tutaanza kwa kuangalia malalamiko ya waandishi kwa ujumla kabla ya kuangalia yanatokanaje na matatizo ya uchapishaji nchini.
2. Malalamiko ya Waandishi
Kama nilivyotaja mwanzoni, mwandishi ana mategemeo makuu matatu wakati anapoandika kitabu:
(a) Kitabu kitoke katika ubora wa maudhui na fani, na haraka iwezekanavyo. Katika uchapishaji hapa tuko katika hatua muhimu za uhariri na utayarishaji wa mswada kwa uchapaji, na mwandishi hutegemea msaada wa kiuhariri kutoka kwa mchapishaji pamoja na kusukumwa kwa kitabu chake katika mitambo ya uchapaji.
(b) Kitabu kisambazwe na kusomwa na watu wengi iwezekanavyo. Mwandishi hutegemea usambazaji mzuri na uuzaji wa nguvu (aggressive marketing) kutoka kwa mchapishaji.
(c) Mapato ya fedha kutokana na jasho lake. Kwa wachapishaji hapa tunaongelea juu ya swala la kifedha(finance).
2.1 Utayarishaji na Uchapaji
2.1.1 Tathmini ya Miswada
Kabla ya mchapishaji yeyote kuukubali muswada, lazima autathmini kuona kama unafaa kuchapishwa. Kazi hii hufanywa aidha na wahariri wake au na wasomaji - wataalamu wengine kutoka nje ya shirika.
Malalamiko mengi ya waandishi hapa ni kuhusu muda unaotumika. Wakati mwingine mwandishi huweza kukaa mwaka mzima bila kupata ripoti hata moja! Ukichukulia kwamba kwa kawaida hutakiwa ripoti zaidi ya moja kabla mchapishaji hajaamua kuukubali au kuukata muswada, unaweza kuelewa ni kwa nini waandishi hulalamika kuhusu muda mrefu unaotumika katika kutathmini miswada yao.
Afadhali basi hata baada ya muda wote huo mrefu ripoti zingekuja za muswada kukubaliwa. Lakini mara nyingi ama zinahitaji muswada ufanyiwe marekebisho au zinaukataa moja kwa moja! Hakuna kinachoudhi mwandishi kama kurudia tena kazi ambayo alifikiri alikwisha kuimaliza mwaka mmoja uliopita. Kinachokatisha tamaa zaidi ni kule kukataliwa kwa muswada na hivyo nguvu za mtu kupotea bure. Kwa wanataaluma ambao kupanda kwao vyeo hutegemea vitabu walivyoandika, hii ina maana maisha yao ya kikazi yanapata pigo. Na lawama dhidi ya wasomaji 'wabaya' na wachapishaji huzidi.
2.1.2 Uhariri
Katika nchi nyingi zilizoendelea, malalamishi juu ya wahariri hutokana na jinsi wanavyoondoa na kubadili mambo mengi katika muswada, au kusisitiza waandishi wabadilishe mpangilio au mtazamo wao wa mambo. Katika Tanzania hali hii haijazuka sana ama kwa sababu kazi ya uhariri haijaendelea kufikia kiwango hicho cha kuhariri, au kwa kuwa waandishi wanachukulia maamuzi ya wahariri kama neno la mwisho. Tutaongea zaidi kuhusu hili baadaye.
2.1.3 Uchapaji .
Hata baada ya muswada kukubalika, huweza kuchukua muda wa mwake mmoja mpaka miwili hadi kitabu kitoke. Katika hali kama hii, waandishi wengi hudai - na ni kweli kabisa - kuwa yaliyomo kwenye kitabu yanakuwa yameshachachuka. Na mbaya zaidi ni kwamba ubora wa kitabu katika uchapaji hauwi wa kuridhisha.
2.2 Usambawji
2.2.1 Uuviji na Utangawji
Hakuna kimuumizacho mwandishi kama kuona kitabu chake - ambacho wakati wa kuandika kwenye mawazo yake alikuwa anaona watu wanakikimbilia na kupigania kukinunua - hakinunuliwi na kusomwa. Lawama nyingi hapa huenda kwa wachapishaji: kwamba hawauzi vitabu kwa juhudi, na wala hawavitangazi. Waandishi wengi hutembelea maduka ya vitabu wenyewe na kuuza vitabu vyao, na pale wanapofanikiwa kuuza vitabu kwa wingi hii huzidi kuwathibitishia hoja yao kuwa wachapishaji hawasambazi vitabu vyao kama inavyotakikana.
2.3 Mapato
2.3.1 Malipo ya Mrabaha na Maelezo ya Mauza
Malalamiko ya waandishi hapa ni kwamba hawapati malipo yao ya mrabaha, na kwa wakati uliokubalika. Mara nyingi hawapati maelezo kuhusu kitabu kilitoka lini, nakala zilizochapwa, na mauzo katika kipindi kilichowekwa katika mkataba. Wakati mwingine chapa ya piii na nyingine hutolewa na mwandishi hajulishwi - waandishi wengi hudai kwamba chapa kama hizi hufanywa kwa siri kwa madhumuni ya kuwaibia!
2.3.2 Malipo Kidogo
Wachapishaji wengi nchini hutoa asilimia 10 - 15 ya mauzo halisi kama mrabaha. Waandishi wengi hudai kwamba huu ni unyonyaji wa wazi kwani mchapishaji hubaki na donge nono zaidi. Ukichukulia idadi ndogo ya vitabu vinavyouzwa pamoja na asilimia ndogo ya mrabaha wanayopata, wengi huzidi kudai kwamba malipo kwa uandishi ni kidogo kiasi cha kutompa mtu motisha wa kuandika.
2.4 Picha ya Jumla
Ukichukulia malalamiko yote haya, picha ya jumla inayopatikana ni ya mchapishaji aliyeshiba anayemwangalia kwa dharau mwandishi anayelalamika huku kakondeana! Lakini, je, ni kweli kwamba wachapishaji Tanzania ni watu wanene walioshiba?
3. Malalamiko ya Waandishi na Matatizo ya Uchapishaji
3.1 Utayarishaji na Uchapaji
3.1.1 Tathmini ya Miswada
Ili kuhakikisha kuwa anachapisha kazi bora kufuatana na sera ya kampuni yake, kila mchapishaji lazima aitathmini miswada anayopokea. Kampuni haiwezi kuajiri wahariri ambao ni wataalamu katika kila nyanja inazozishughulikia. Kwa hiyo miswada mingi lazima itathminiwe nje na wasomaji wenye utaalatnu unaohusika. Hawa hutoa ripoli ambazo humsaidia mchapishaji kuamua aidha:
(a) kuukubali muswada kama ulivyo;
(b) kuukubali muswada ikiwa marekebisho machache yatafanyika;
(c) kuukataa muswada lakini kupendekeza kuwa uandikwe upya na kurejeshwa tena kwenye kampuni; au
(d) kuukataa muswada kabisa, na kushauri mwandishi afikirie tena mradi mwingine, au aupeleke muswada kwa wachapishaji wengine.
Kwa hiyo basi ripoti za wasomaji - wataalamu huwa na manufaa, mosi kwa mchapishaji katika kumsaidia kufanya uamuzi; na pili, kwa mwandishi kwa kumsaidia kuandika muswada bora zaidi. Wachapishaji wengi hupeleka ripoti moja kwa moja kwa waandishi. Sisi katika Dar es Salaam University Press (DUP) humwandikia mwandishi yale tunayoona kuwa ni ya manufaa tu kutoka kwenye ripoti tunazopokea.
Tatizo kubwa hapa ni kwamba wasomajiwataalamu wengi tunaowategemea ama ni wanataaluma au wakuza mitaala ambao wana kazi nyingine nyingi - za kufundisha, kufanya utafiti, kuandika, n.k. Ni hawa ndio hukaa na miswada kwa muda mrefu bila kuleta ripoti. Wengine huweza kukaa na muswada hata kwa zaidi ya miezi sita na baadaye kuurudisha bila ya ripoti.
Tatizo hili huwa kubwa zaidi ukizingatia kuwa wasomajiwataalamu ni wachache, na kazi wanayofanya ni kama ya kujitolea kwani wanachopewa ni ahsante tu, na siyo malipo halisi kwa kazi wanayofanya. Ukizingatia pia kuwa waandishi wengi nchini ni wachanga na wanahitaji ripoti nzuri iwezekanavyo iwasaidie kuendeleza kazi yao, kinachobaki kwa wachapishaji ni kuwabembeleza na kuwasukumasukuma wasomaji - wataalamu hawa wachache walete ripoti kila wachelewapo kufanya hivyo.
Si rahisi kuthibitisha kuwa ripoti nyingi za wasomaji - wataalamu ni za upendeleo. Kwa kawaida wachapishaji hutafuta ripoti zaidi ya moja. Ni vigumu basi, kupata ripoti kutoka kwa watu wawili tofauti zenye upendeleo na upande mmoja. Katika DUP mhariri hupitia muswada kabla'ya kuupeleka kwa msomaji - mtaalamu pamoja na vidokezo vya mambo ambavyo angependa huyo msomaji ayaangalie. Mara tu ripoti inapopokelewa, mhariri yuleyule huipitia na kuchuja mambo yanayoonekana wazi ni ya uperideleo au yanayotokana na mtizamo tofauti wa msomajimtaalamu, na kumpelekea mwandishi yale tu anayoona ni ya msingi.
3.1.2 Uhariri
Kwa kawaida kazi za mhariri wa mchapishaji ni tano:
1. Kubuni miradi. Kutokana na mahitaji ya soko na maendeleo katika nyanja fulani za vitabu, mhariri anaweza kuwaendea waandishi ambao anajua wanaweza kuandika kuhusu mada fulani na kuwapa mawazo juu ya kitabu au vitabu ambavyo anafikiri vinaweza kuandikwa katika nyanja hizo; Huduma hii haijaendelezwa sana hapa nchini. Pale inapotolewa hufanywa na wakuu wa makampuni ya uchapishaji. Ni wazi kuwa hawa ni wachache na wana kazi nyingi kuweza kuifanya kazi hii kwa ukamilifu kama inavyotakikana.
2. Tathmini ya miswada. Wahariri wanaweza kuitathmini miswada wenyewe, au wakaipitia na kushauri wasomaji - wataalamu wanaoweza kuitathmini. Kutokana na uchache wao pamoja na msongamano wa kazi nyingine, wahariri pia huweza kusababisha ucheleweshaji wa miswada.
3. Uhariri wa Undani (Substantive editing). Hii inahusika na kukata au kuongeza mambo mengi katika muswada, kupanga upya mtiririko wa muswada, na kuhakikisha kuwa mambo yameelezwa katika lugha wazi na fasaha. Ni kama kuandika kitabu upya. Katika nchi yenye waandishi wengi wachanga, hii ni huduma muhimu sana. Sina hakika kama hii inafanyika kama inavyotakikana hapa nchini.
4. Uhariri wa maandishi (copy-editing). Hii huhusu hasa kumalizia muswada na kuhakikisha kuwa hauna makosa ya taipu, sarufi, matumizi ya maneno, tofauti za mtindo k.m. katika kuunga maneno, marejeo, n.k. Huu ni msaada ambao waandishi wanashukuru kuupata kwani unahusu mambo madogomadogo lakini ambayo ni muhimu katika kufanya kitabu kisomeke kwa urahisi na kueleweka. Hapa hakuna malalamiko mengi kutoka kwa waandishi.
5. Kutayarisha mswada kwa uchapaji. Hapa mhariri huchambua na kumwonyesha mcbapaji sehemu kadhaa za muswada na namna anavyotaka zionekane katika maandishi kutokana na umuhimu wake.
Msaada mwingi kwa waandishi wachanga unahitajika sana katika uhariri. Kati ya huduma muhimu ambazo waandishi wanazikosa hapa nchini ni hii ya uhariri, hasa katika vipengee 1 na 3. Hii inatokana na ukweli kwamba ni wahariri wachache ambao wanaweza kuzifanya kazi hizo. Hakuna watu wengi wanaotambua umuhimu wa kazi hizi, sanasana kazi ya uhariri inaeleweka kuwa ni kutathmini miswada, kusahihisha makosa ya taipu, kunyoosha makosa ya lugha hapa na pale, kutayarisha muswada kwenda kwa mchapaji, na kusoma prufu tu. Marupurupu ya wahariri yanapotengenezwa kutokana na mtizamo finyu kama huu yanakuwa sio ya kuvutia, na matokeo yake ni wale ambao wangeweza kuwa wahariri wazuri kuikimbia kazi hii. Hata makampuni ya uchapaji hapa nchini hayaonekani kama yanajali hali hii ya mambo - angalia TPH, EAPL, DUP, na utakuta hali ni ileile ya wahariri kukimbia kila kukicha.
3.1.3 Uchapaji
Matatizo ya uchapaji hapa nchini yanatokana na sababu tatu muhimu. Kwanza, kuna wachapaji wachache wa vitabu kulingana na mahitaji ya huduma hizi. Pili, wachapaji wana matatizo ya vipuli na mali ghafi. Tatu, wana uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kuchapa, na ujuzi wa kutunza na kutengeneza mitambo yao.
Kutokana na sababu hizi wengi hupendelea kuchapa madaftari na makaratasi mengine ya kuandikia, na mafomu ya kutumia maofisini kuliko kuchapa vitabu. Hii ni kwa sababu kuchapa madaftari, mafomu ya maofisi ni, n.k., huhitaji ujuzi mdogo sana, ni rahisi, na unaingiza pesa nyingi na za haraka ukilinganisha na kuchapa vitabu. Mchapaji kwa vyovyote vile atapendelea kuviringa plate moja kwenye mashine yake na kuchapa madaftari 100,000 kuliko kutumia plale8 kuchapa vitabu 5000. vya kurasa 128 tu. Sababu hizi ndizo zinazofanya vitabu visote kwenye foleni ya kuchapwa hata kwa miaka miwili!
3.2 Usambazaji
3.2.1. Uuzaji wa Vitabu ni Nini
Lengo la mwisho la uuzaji wa vitabu ni kufikisha vitabu kwa wasomaji. Kwa mchapishaji hii inahusisha mambo matatu muhimu: kwanza, kutambua soko lako ni la akina nani; pili, liko wapi; na tatu, unawezaje kulifikia. Kufahamu soko lake ni la kina nani kunamsaidia pia mchapishaji kupanga atauzaje vitabu vyake, na kuamua. achapishe vingapi.
Ukiondoa soko la shule na la vitabu vya kitaaluma, vitabu vingi nchini hulengwa kwa wasomaji wa kawaida. Hili ni soko la kijumla sana na hufikiwa kwa kutumia maduka ya vitabu.
3.2.2 Matatizo ya Wauza Vitabu
Kama ilivyo kwa wachapishaji, wauza vitabu sio watu wanene - hakuna mtu mwenye fedha nyingi anayeweza kuziingiza katika duka la vitabu: ataziweka kwenye biashara ambayo ina uhakika wa kuleta mapato ya harakaharaka na faida kubwa. Wauza vitabu wengi basi ni watu wenye mtaji kidogo. Ukichukulia kuwa wachapishaji wengi hudai malipo kwanza kabla ya kuwapelekea vitabu, hii ina maana kuwa mtaji huo mdogo huzidi kufungwa zaidi katika mali. Hii ina maana kuwa muuza vitabu atanunua tu vile vitabu ambavyo ana uhakika vitauzwa harakaharaka na kurudisha mtaji wake. Vitabu vinavyouzwa haraka ni vya shule, na mara chache riwaya za msisimko. Kwa maneno mengine kama vitabu vyako haviingii katika makundi haya, mwuza vitabu hawezi kununua zaidi ya vitabu kumi kwa wakati mmoja.
Popote pale duniani biashara kubwa ya vitabu iko katika vitabu'vya kiada na ziada vya shule na vyuo. Sera ya serikali kuifanya biashara hii imilikiwe na TES na maduka machache 'yaliyoteuliwa' imeua maduka mengi ya vitabu, na kuyafanya mengine yaanze kuuza vitu vingine pembeni. Watu wengi hununua vitabu baada ya kuviona na angalao kuvipitia juujuu kidogo, na hili hufanyika mtu anapokuwa amefuata kitabu maalumu cha shule au kitu kingine muhimu dukani. Kuyazuia maduka kuuza vitabu vya shule hakuwanyimi tu wenye maduka hayo biashara na pesa ambazo wangeweza kutumia kununua na kuweka vitabu vingine, bali pia huwanyima wasomaji fursa ya kuona na kununua vitabu vingine.
Kipunguzo wanachopewa wauza vitabu ni asilimia 20 hadi 25 ya bei ya kitabu. Ukilinganisha na wanachopewa wengine katika nchi zilizoendelea - kati ya asilimia 35 mpaka 50 - kiasi hiki ni kidogo sana kuwawezesha wauza vitabu kulipia gharama zao na kupata faida kidogo, hasa ukizingatia pia kuwa idadi ya vitabu wanavyouza ni ndogo. Kwa hiyo wengi wanapandisha bei ya vitabu kuwa ya juu zaidi kuliko ile waliyoiweka wachapishaji.
Matokeo ya matatizo yote haya ni kwamba njia kuu ya kuvifikisha vitabu kwa wasomaji inakuwa imezibwa. Hata uuze kwa nguvu gani na utangaze namna gani, mafanikio ya juhudi zako yataathiriwa na matatizo haya ya wauza vitabu.
3.2.3 Utangazaji (Promotion)
Baada ya kujua soko la vitabu na njia ya kulifikia, mchapishaji lazima: kwanza, awafahamishe na kuamsha ari ya wasomaji ili waende madukani kununua vitabu vyake; na pili, ahakikishe kuwa vitabu viko madukani kukidhi mahitaji haya ya wasomaji. Kuna njia tatu za kutangazia vitabu kwa wasomaji:
mosi, vyombo vya habari; pili, majarida na machapisho ya kila muda ya mapitio ya vitabu; na tatu, maonyesho. Kwa maduka njia zitumikazo ni kuwapelekea nakala mpya ya kila chapisho jipya, katalogi, na kutumia wauzaji wa mchapishaji au wakala wake kutembelea maduka.
Vyombo vya habari hutumika kwa nadra sana na wachapishaji hapa nchini kutangazia vitabu. Majarida yahusikayo na machapisho ni kama hakuna kabisa, na machache yenye mapitio ya vitabu ni ya kitaaluma, na yanawafikia wachache tu. Maonyesho yanafanyika mara chache nayo huonwa na wachache tu walio kwenye miji mikubwa. Katalogi, pale ambapo hutolewa, nazo ni za msimu. Wachapishaji wenye wakala (watu binafsi) ni wachache sana, na si kawaida kuwakuta wauzaji wa wachapishaji wakitembelea maduka - hasa huko bara - mara kwa mara katika fitihada ya kuuza vitabu. Hapa inaweza kuonekana kuwa lawama za waandishi kuwa wachapishaji hawatangazi au kuuza vitabu vyao kwa nguvu ni za kweli. Lakini yote hii lazima iwe na sababu kwani hakuna mchapishaji ambaye hangependa kuuza vitabu vyake - la sivyo asingevichapisha!
Wachapishaji wengi, sio Tanzania tu, wanaanrini kuwa kitabu kama hakiuziki hata kama ukikitangaza namna gani hakiwezi kuuzwa na kurudisha gharama za utangazaji. Hakuna maana kutumia Sh. 20,000 kutangazia vitabu, na baadaye ukauza vitabu vya Sh. 40,000 kama una bahati! Hakuna faida kumtuma mfanya kazi wako mikoani kuuza vitabu akatumia Sh. 20,000 na kukuletea maagizo ya Sh. 100,000. Wengi wanaamini kuwa kutangaza vitabu kunaongeza mauzo ya vitabu ambavyo tayari vinauzika; hakuuzi vitabu visivyouzika.
Na vitabu vingi vinavyouzika nchini ni vya shule. Kutokana na uhaba wa vitabu vya kiada na rejea mashuleni, kitabu kikisha kukubalika na Wizara ya Elimu wachapishaji wengi nchini hawaoni tena haja ya kukitangaza zaidi: wanaamini watu wenyewe watakitafuta TES au madukani.
Kuhusu katalogi, ni kwamba hakuna mchapishaji hapa nchini ambaye anatoa vitabu vipya vya kutosha kumfanya agharamie kuchapisha katalogi kila mwaka. Labda baada ya kuundwa kwa PATA (Publishers Association of Tanzania) mipango inaweza kufanywa kutoa katalogi ya jumla ya wachapishaji wote nchini.
3.3 Mapato
3.3.1 Matatizo ya Kifedha ya Wachapishaji
Biashara ya uchapishaji ni ya watu wembamba - hutamkuta mtu mnene katika kazi hii. Sababu zake ni kwamba ni biashara isiyokuwa na uhakika, na inachukua sio chini ya miaka mitatu kabla hujaanza kuona matunda yake. Kwa muda wote huo huna budi kuzika fedha ndani yake, na kwa sababu hakuna benki inayokubali kukopesha pesa biashara isiyo na uhakika, basi hata mtaji wa kuiendeleza biashara unakuwa mdogo. Ndiyo sababu ukitoa mashirika ya serikali na ya kigeni, ni makampuni machache sana ya watu binafsi yameweza kuishi kwa zaidi ya miaka mitano. Na watu wengi binafsi wanaoingia katika kazi hii ni wale wenye mtaji kidogo ambao hauwezi kuingizwa katika biashara nyingine zenye faida zaidi.
Uchapishaji kokote duniani umekua na kuendelea kwa kutegemea soko la shule ambalo ndilo kubwa na lenye uhakika. Jinsi sera ya serikali ya kuandaa, kuchapisha, na kusambaza vitabu vya kiada inavyoathiri wachapishaji wa binafsi ni suala lililo nje ya makala haya. Napenda nigusie tu sera hiyo inavyoathiri hata mashirika ya umma ya uchapishaji.
Kila kukicha utasikia wananchi na Wizara ya Elimu ikilalamika kuwa hakuna vitabu vya kutosha mashuleni. Lakini ni rahisi kusema kuna mahitaji makubwa ya vitabu kuliko kutenga fedha za kutosha kununulia vitabu hivyo kama vikiwepo. Kinachotokea ni kama ifuatavyo:
A. Taasisi ya Ukuzaji Mitaala itaandaa muswada wa kitabu cha kiada na kuupitisha kwa Wizara ambayo itakiidhinisha. Muswada utapatiwa mchapishaji.
B. Mchapishaji, akiwa na hakika kuwa kitabu kitanunuliwa, anatumia karibu mtaji wake wote na kukitoa kitabu haraka iwezekanavyo na kukipeleka Wizarani.
C. Wizara itaiandikia TES barua inunue vitabu na kusambaza. TES inasema itachukua kwa mkopo na kumlipa mchapishaji baadaye. Mchapishaji akikubali atasubiri mwaka mmoja mpaka miwili kabla ya kulipwa. Kama tayari TES inalo deni lake lingine na/au mchapishaji anadaiwa na mchapaji kabla ya kupewa vitabu, mchapishaji anakataa kuuza vitabu kwa mkopo. Anakwama navyo: hawezi kuwauzia TES kwa sababu hawana pesa; na hawezi kuuzia wananchi kupitia maduka ya vitabu kwa sababu sera ya Serikali hairuhusu.
D. TES inadai haina pesa kwa sababu maafisa elimu wa wilaya wana madeni ambayo hawajalipa. Nao maofisa wanasema hawawezi kulipa kwa sababu hawakupata fedha zakutosha kutoka wizarani. Wizara nayo haikuweza kutoa pesa za kutosha kwa sababu ya 'hali halisi'.
E. 'Hali halisi' kwa mchapishaji ni kwamba aidha anakopesha vitabu na kubaki ameishiwa, au anabaki na vitabu na huku ameishiwa. Matokeo ni kwamba shughuli za kutoa vitabu vingine zinakwama. Na wakati huohuo majukwaani maneno yanazidi: waandishi andikeni vitabu vya kiada, na wachapishaji chapisheni - tuna njaa kubwa ya vitabu mashuleni!
Labda mikanganyiko na hali kama hii ndiyo inafanya wachapishaji wengi washindwe kuwalipa waandishi mirabaha yao kila baada ya kipindi kilichokubaliwa? Lakini hii haimzuii mchapishaji kumpa mwandishi maelezo kuhusu machapisho na mauzo ya kitabu chake kwa wakati uliotakiwa.
3.3.2 Mahesabu Ya Gharama ya Uchapishaji
Kwa wastani mahesabu ya wachapishaji wengi nchini katika kuweka bei ya kitabu ni kama ifuatavyo:
Uchapaji (kuseti, karatasi, kuchapa na kujalidi)
|
30.00%
|
Kipunguzo (maduka - 20%, wakala - 10%)
|
30.00%
|
Gharama za Mchapishaji (uhariri, uzalishaji, uuzaji na usambazaji, uhasibu na utawala)
|
20.00%
|
Mrabaha (kwa bei ya kitabu)
|
10.00%
|
Faida (kabla ya kodi)
|
10.00%
|
Jumla
|
100.00%
|
Kutokana na mahesabu hayo hapo juu itaonekana wazi si kweli wachapishaji wanawadhulumu waandishi kwa kuwapa asilimia kidogo kama mrabaha. Ukweli unaweza kuwa kinyume chake kabisa. Mathalani, katika chapisho la vitabu 5000, mchapishaji lazima auze angalao vitabu 4000 ndio awe amerudisha gharama zake za kukitoa kitabu. Hii ina maana haanzi kupata faida kabla hajauza nakala 4000. Lakini mpaka aziuze zote hizo mwandishi anaendelea kupata mrabaha wake. Wachapishaji wengine hutoa malipo ya awali ya mrabaha kwa waandishi. Itokeapo kwamba mauzo ya kitabu hayakuweza kurudisha fedha zilizotolewa awali mwandishi hadaiwi - mchapishaji huhesabu hii kama mojawapo ya hasara zake. Kwa hivyo katika kipengele hiki kama mwandishi atamlaumu mchapishaji atakuwa anamwonea bure.
Hapa inaweza kudaiwa: kwa nini basi asilimia ya mrabaha isiongezwe? Lakini kuongeza asilimia ya mrabaha ni kuongeza pia bei ya kitabu, na athari yake inajulikana - wasomaji kutoweza kuvinunua.
Kila mchapishaji ana namna yake ya kufanya mahesabu ya bei ya kitabu. Hata hivyo wote hutumia gharama za uchapaji kama ndio factor ya kufanyia mahesabu ya bei. Kwa mfano sisi katika DUP hutumia fomula ya
, ambapo:
b = bei ya kitabu
u = gharama za uchapaji
a = asilimia ya gharama za uzalishaji katika bei ya kitabu.
Kwa mfano tukichukua kwamba gharama za uchapaji wa kitabu ni Sh. 45.00, na hii ni asilimia 30 ya bei ya kitabu, basi bei ya kitabu itakuwa:
Ukiongeza mrabaha kufikia tuseme asilimia 15, ina maana kupunguza asilimia ya gharama za uzalishaji kuwa 25. Hapa bei ya kitabu itapanda na kuwa:
Kama nilivyosema hapo mwanzoni athari za kuongezeka kwa bei ya vitabu ni watu kutomudu kununua kitabu, na hii haimsaidii yeyote: si mwandishi wala mchapishaji.
4. Hitimisho
Kama nilivyosema mwanzoni, nia yangu haikuwa kuwakosha au kuwatakasa wachapishaji - nia ilikuwa ni kuwaelimisha waandishi kuhusu misingi ya migogoro yao na wachapishaji: kwamba mengi ya malalamiko yao yanatokana na matatizo ya uchapishaji nchini, na kwamba kwa kuyafahamu tutaunga nguvu ili kwa pamoja tupingane nayo.
Kwa mfano, kwa kutumia PATA Na UWAVITA tunaweza kuifanya serikali iifikirie upya sera yake ya uandaaji, uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya shule na vyuo. Tunaweza kuiomba serikali iondoe kodi ya mauzo ya karatasi - ni ajabu kwamba vitabu vinavyotoka nje havilipiwi kodi, lakini karatasi za kuvichapia nchini zinalipiwa tena maradufu! Kwa pamoja tunaweza kuungana na wachapaji na kudai wapatiwe mitambo, mali ghafi na vipuli ili wawe na uwezo wa kuchapa vitabu kwa wingi zaidi, na kwa ubora zaidi.
Lakini lazima tukubali kuwa nasi wachapishaji na wachapaji lazimatuziweke nyumba zetu sawa - kuna mambo yanayotokea kwa sababu ya uzembe, nayo hayahitaji mali ghafi wala fedha za kigeni kuyaweka sawa - ni sisi wenyewe.
Hata hivyo lazima tukiri kwamba iwapo vitabu vitaendelea kuandikwa kwa kutegemea mapato angalao kidogo, na vitaendelea kuchapishwa kibiashara, lazima kutaendelea kuwako mgogoro kati ya waandishi na wachapishaji. Lakini ninaamini kuna mengi ya kuwaunganisha waandishi na wachapishaji kuliko ya kuwatenga. Kama vile ambavyo mchapishaji hawezi kuwako bila ya mwandishi, mwandishi naye hawezi kuwako bila ya huduma za wachapishaji. Kuna mifano ya waandishi ambao kutokana na kutoridhika kwao na huduma za wachapishaji, walianzisha kampuni zao za uchapishaji. Mwishowe walijikuta ama wanafanya shughuli zilezile za wachapishaji wenyewe, au wanafanya baadhi na baadhi nyingine wanawapa wachapishaji wenye ujuzi wa shughuli hizo wawafanyie. Kwani itambulike kuwa kuchapisha ni zaidi ya kuandika na kuchapa: ni pamoja na kuhariri, kusambaza, na kuratibu shughuli zote hizi. Na waandishi na wachapishaji lazima wawepo kwa pamoja ili kuzifanikisha.
Marejeo
Altbach, P.G. and Rathgeber, Eva Marie (1980) Publishing in the Third World - Trend Report and Bibliography. Praeger, New York.
Bgoya, Walter (1986) Books and Reading in Tanzania. UNESCO, Paris.
Dessaur, J.P. (1981) Books Publishing: What It Is, What It Does. R.R. Bowker Company, New York.
Smith, D.C. (1979) The Economics of Book Pubtishing in Developing Countries. UNESCO, Paris.
Zell, H.M. (compiler) (1984) Publishing and Book Development in Africa: A Bibliography. UNESCO, Paris.