Friday

FAHAMU JINSI YA KUJIKINGA NA UGONJWA WA HOMA YA DENGUE

0 comments


Ugonjwa wa dengue umerejea nchini baada ya wagonjwa 11 kugundulika jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka Wizara ya Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto zinaeleza kuwa homa ya ugonjwa huo imendulika baada ya wagonjwa kadhaa waliokuwa na dalili zake kupimwa na kuthibitishwa.

Kutokana na hilo, ili kuudhibiti, serikali imeanza karantini ya kuzuia kuenea kwake kwa kuweka vituo vya uchunguzi wa awali na tiba katika mikoa ya Dar es Salaam na Tanga.

Wagonjwa hao waligundulika katika Hospitali ya Ocean Road.


HOMA YA DENGUE NI NINI?
Ugonjwa huu ni moja ya maradhi yanayosababishwa na virusi aina ya Dengue vinavyoenezwa na mbu. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 50 huugua ugonjwa huu kila mwaka duniani huku watu wengi katika nchi 112 duniani wakiwa kwenye hatari ya kupata maambukizo. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO ugonjwa huu unaenezwa zaidi na mbu kuliko magonjwa mengine ya virusi.

 Homa ya dengue pia hujulikana kama breakbone fever, na maradhi hayo yamepewa jina hilo kwa sababu wahanga wa ugonjwa huu mara nyingi hujikunja kutokana na maumivu makali ya viungo na misuli.

Homa ya dengue huenezwa na mbu wa jamii ya Aedes hasa aina ya Aedes Aegypti. Aina hii ya mbu hupatikana kwa wingi katika maeneo yote ya kitropiki ikiwemo nchi yetu Tanzania hasa mikoa ya Pwani

Kuna aina 5 ya virusi vya dengue vinavyosabisha maradhi hayo. Maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mwanadamu kung'atwa na mbu wa Aedes aliye na virusi vya dengue. Mbu huambukiza virusi hivyo pale anapomg'ata mtu kwa kuingiza vijidudu hivyo kwenye damu, na kwa ajili hiyo ugonjwa huu hauwezi kuenezwa moja kwa moja toka kwa mtu hadi kwa mtu mwingine.

Kwa kuwa kuna aina kadhaa za virusi vinavyosababisha homa ya dengue, pale mtu anapoambukizwa virusi vya aina moja ya ugonjwa huo, mwili wake hujenga kinga ya maisha kwa aina hiyo ya virusi, lakini anaweza kuambukizwa homa ya dengui kutokana na virusi vya aina nyingine. Miongoni mwa sababu zinazopelekea maambukizo ya maradhi hayo, ni wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kusambazwa ugonjwa huo na mbu. Pia watu wanaoishi katika makazi duni wapo kwenye hatari ya kuathiriwa zaidi na homa ya dengue kwa sababu ya kuishi katika mazingira yenye takataka nyingi na madimbwi ya maji machafu ambako mbu huzaliana.

Dalili za homa ya dengue
Baada ya mtu kuambukizwa ugonjwa huu dalili hujitokeza baada ya siku 4 hadi 6 na huweza kudumu hadi siku 10.

Mgonjwa huhisi homa kali inayoweza kufikia nyuzi joto 41,
 kutetemeka na hupata maumivu makali ya mgongo na viungo.
Homa hudumu kwa siku 2-7 na homa inayodumu zaidi ya siku 10 huenda ikawa haisababishwi na dengue.
Dalili nyingine zinazoambatana na homa hiyo ni maumivu ya kichwa, maumivu ndani au nyuma ya macho, maumivu ya viungo, kichefuchefu na kutapika, vipele, uchovu, kukosa hamu ya kula, maumivu ya koo, kuvuja damu isiyo nyingi katika pua na fizi na kuvimba mitoki.

Baadhi ya wakati dalili za homa ya dengue si kali sana na zinaweza kukosewa na kuonekana kama mafua au maambukizo ya virusi vingine. Baadhi ya wagonjwa wanaopatwa na homa hii huweza kupata madhara zaidi kama vile homa inayoandamana na kuvuja sana damu, tatizo linalotokea kwa nadra ambapo mgonjwa  huwa na dalili zifuatazo, homa kali sana, kuharibika mishipa ya damu, kutokwa damu puani na kwenye fizi, ini kuwa kubwa na kushindwa kufanya kazi mfumo wa kupumua.

Dalili hizi zinaweza kuendelea na kusababisha damu kutoka kwa kiasi kikubwa, kupata shock na kifo. Hali hiyo huitwa kitaalamu DSS yaani Dengue Shock Syndrome. Watu wenye mfumo wa kinga ya mwili ulio dhaifu pamoja na wale waliopatwa na maambukizo ya ugonjwa huu kwa mara ya pili au wale wanaougua mara kwa mara na Homa ya Dengue wako katika hatari kubwa ya kupatwa na shock ya aina hiyo.

Uchunguzi na matibabu
Baada ya dalili kujitokeza chunguzi hufanyika kwa lengo la kubaini virusi vya dengue kwenye mwili. Vipimo kwa kawaida hufanywa kwenye maabara kwa kutegemea dalili za mgonjwa na uchunguzi wa mwili na hasa katika maeneo ambayo ugonjwa huo hushuhudiwa sana.

Homa ya dengue huthibitishwa kwa kipimo cha PCR kinachotumika kutambua virusi vya ugonjwa huo.  Kipimo hicho kinaweza kuonekana negativu mwanzoni mwa maambukizo ya maradhi hayo. Hata hivyo vipimo vingine hutumika ili kujua iwapo mgonjwa ana maradhi mengine au la.

 MATIBABU
Hakuna dawa ya kutibu homa ya dengue na mara nyingi ugonjwa huu hukoma wenyewe bila matibabu yoyote.

Mgonjwa anashauriwa kunywa maji ya kutosha, kupumzika na kutumia dawa za kutuliza maumivu na kushusha homa kama paracetamol. Pia mgonjwa wa homa ya dengue anapaswa kujiepusha kunywa dawa kama vile asprin ambazo huzidisha kuvuja damu.

Wagonjwa wanaopata tatizo la kuvuja damu wanahitaji uangalizi wa karibu hospitalini. Iwapo utaugua ugonjwa huo na kujihisi vibaya baada ya masaa 24 tangu homa kushuka, unapaswa kwenda haraka hospitali ili uchunguzwe iwapo ugonjwa huo umesababisha madhara mwilini.

 Epuka dawa jamii ya aspirini kama aspirini,diclopar,diclofenac,maana huweza kusababisha damu iendelee kutoka 
JINSI YA KUJIKINGA 
Hakuna kinga ya homa ya dengue na njia pekee ya kujikinga na ugonjwa huo ni kuzuia kuenea virusi vya maradhi hayo kwa kupambana na mbu. Watu wanashauriwa kujilinda wasipatwe na maambukizo ya ugonjwa huo kwa kujizuia wasing'atwe na mbu wanaoeneza ugonjwa huo kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Pia kuweka mazingira katika hali ya usafi na kutoishi kwenye mazingira yanayosaidia mbu kuzaliana kama madimbwi ya maji, vichaka, maeneo ya mabondeni na yenye majani marefu na malundo ya takataka.

Zifuatazo ni njia tunazoweza kuchukua ili kuzuia mbu, ambao kama tulivyosema ndio wanaosambaza na kueneza virusi vya homa ya dengue.

 Kwanza kabisa ni kujizuia kung'atwa na mbu kwa njia mbalimbali kama vile kuvaa nguo za kuzuia mbu wasitung'ate  kama vile mashati ya mikono mirefu na suruali pamoja na nguo ndefu zinazofunika mwili na kuzuia kung'atwa na mbu.

Pia kuzuia mbu wasiingie katika nyumba zetu kwa kuweka nyavu kwenye madirisha, na kuwa na tabia ya kufunga madirisha ya nyumba mapema kabla ya kuingia giza.

Kutumia vyandarua katika vitanda wakati wa kulala kila inapowezekana. Ni vizuri zaidi kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua mbu.

 Tunaweza pia kujipaka dawa za kufukuza mbu au kutumia na kufukiza dawa za kufukuza mbu majumbani ambazo hupatikana kwa wingi katika maduka mbalimbali.

Dawa za kujipaka za kufukuza mbu ni salama kwa watoto na mama wajawazito, lakini tunashauriwa kuwa waangalifu na kuhakikisha kwamba dawa hiyo haigusi macho na midomo.

Njia nyingine ya kuwaepuka mbu ni kuwa na tabia ya kusafisha mazingira yanayotuzunguka, kwa kukata majani marefu, kufukia vidimbwi vya maji vinavyowavutia mbu kuzaana kwa wingi, kutia dawa za kuulia mbu kwenye mashimo ya vyoo, maji yaliyosimama na kadhalika.

tukumbuke kuwa, kinga daima ni bora kuliko tiba, hivyo tujitahidi kutong'atwa na mbu ili tusipatwe na homa hatari ya  Dengue.