Kutafsiri ni kueleza katika lugha lengwa kuhusu jambo ambalo limeelezwa katika lugha chanzi huku usawa wa kisemantiki na kimtindo ukihifadhiwa. Lengo la tafsiri ni kugeuza taarifa asilia ikiwa katika lugha moja ili iwe katika lugha tofauti huku yaliyomo katika ujumbe huo yakihifadhiwa pamoja na wajibu wa kimatumizi wa taarifa asilia.
Tafsiri huchangia pakubwa maendeleo ya elimu katika mataifa. Wanafalsafa wa kimapokeo Wagiriki, kwa mfano, walitafsiri elimu, ujuzi na mawazo waliyopata huko Afrika kaskazini, haswa Misri, na wakayatumia kuendeleza nchi ya Ugiriki. Wasomi walitafsiri mawazo ya Wagiriki kama vile Plato, Aristotle na Socrates ili kujenga nchi zao katika Nyanja kama vile elimu, siasa, dini na utabibu. Maandishi matakatifu yalitafsiriwa kutoka kwenye Kigiriki na Kihebrania na filosofia kutafsiriwa kutoka kwenye Kiarabu, Kigiriki na Kihebrania.
Wananchi wa lugha za kigeni wanaweza kutumia mbinu ya tafsiri kujifunza lugha mpya. Mazoezi ya kutafsiri humpa mtu nafasi ya kudadisi vipengele vya kiisimu vya lugha husika ili aweze kutoa tafsiri bora. Vipengele kama vile msamiati, sintaksia na mnyambuliko wa vitenzi humpa mtu ujuzi wa kuifahamu lugha barabara.
Tafsiri huweza pia kuinua uchumi wa kitaifa. Katika afisi, benki, viwandani, madukani na nyanja za ndege, tafsiri hutumiwa wakati mwingi ili biashara zifanikiwe. Tafsiri inaweza pia kuwaajiri wananchi wengi katika sekta za utalii, uchukuzi wa kimataifa na makanisani. Ajira hii huimarisha hali ya maisha na kupunguza ufukara.
Wataalamu wa tafsiri watahitajika kila wakati. Baadhi ya mambo na shughuli ambazo hazingefua dafu bila wataalamu wa tafsiri ni kama vile: mazungumzo ya Baraza la Umoja wa Mataifa, ‘glasnost’ ama ‘perestroika’, Tafrija za Filamu za Cannes, Matuzo ya Nobel, maendeleo ya kiutabibu, sayansi na uhandisi, sheria za kimataifa, Michezo ya Olimpiki; mswahili hangesoma ‘Shamba la Wanyama’ na ‘Visa vya Oliver Twist’. Kwa hivyo, tafsiri hujenga uhusiano mwema wa kimataifa ambao huleta maendeleo katika mataifa yote husika.
Kwenye ulimwengu unaobadilika kwa kasi sana ambamo fahamu za binadamu zinapanuka pakubwa, upashaji wa habari umeanza kutegemea zaidi tafsiri ya kina. Kwa mfano, uvumbuzi na ukuaji wa tarakilishi tarakilishi umehitaji tafsiri ambazo husaidia mataifa yanayonunua vifaa hivi. TUKI, kwa mfano, inashirikiana na Microsoft kuandaa mtandao wa lugha ya Kiswahili.
Taaluma ya tafsiri inapoimarishwa katika taifa lenye wingi-lugha haswa lugha za kimakabila, lugha rasmi na lugha za kitaifa, wananchi hukomaa kisiasa na kuchangia kikamilifu katika mijadala ya kitaifa inayowahusu moja kwa moja. Mfano mzuri ni hapa nchini Kenya ambapo vyombo vya habari hutafsiri habari muhimu na kuzipasha kwa umma wote. Magazeti ya Taifa Leo na Taifa Jumapili hutekeleza jukumu hili barabara pamoja na mashirika kama vile KBC, KTN, NTV. Tafsiri hizi huwawezesha wananchi kutoa mawazo yao ya kibinafsi kuhusu mijadala yenye mtazamo wazi.
Historia ya tafsiri ni historia ya uvumbuzi wa kifasihi ambapo istilahi mpya huibuka , aina mpya za Fasihi hugunduliwa kama ilivyo katika mashairi huru ya Kiswahili. Mifano ya kazi za kifasihi ambazo zimetafsiriwa na kufaidi Fasihi ya Kiswahili ni kama vile riwaya ya Chinua Achebe, ‘Shujaa Okonkwo’ na ‘Wimbo wa Lawino’ (Okot p’Bitek). Tafsiri hizi zimetajirisha Fasihi ya Kiswahili ambacho ni lugha ya taifa nchini Kenya.
Tafsiri ni taaluma yenye umuhimu mkubwa sana katika mataifa yote yenye nia na ari ya kujiendeleza na kushindana na mataifa mengine yaliyofikia upeo wa maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa.