Monday

KEN WALIBORA, HATUONEI FAHARI LUGHA YETU ASHIRAFU YA KISWAHILI, SI KATIKA UHAI SI KATIKA MAUTI

0 comments




 Na KEN WALIBORA
Kwa Ufupi :
Wiki hii nimekwenda kufanya ziara katika maziara ya Wazungu Zanzibar
Muhimu ni kwamba niliazimia kujua kumbukumbu za watu hawa makaburini zimeandikwa kwa lugha gani
Nimekuta Kijerumani na Kiingereza katika makaburi Zanzibar
WIKI hii nimekwenda kufanya ziara katika maziara ya Wazungu Zanzibar. Labda hilo litakushangaza kidogo kama unaelewa maana ya maziara. Maziara ni makaburi. Kwa kifupi nilikwenda kuzuru makaburini eneo la Zanzibar Mjini Magharibi.
Huku makaburini sikuwa nimekwenda kutoa heshima zangu kwa jamaa zangu waliokufa, hapana. Sina jamaa zangu hapa Zanzibar, walio hai au wafu. Marafiki ninao na pia “ndugu wa kiroho” kama unanielewa.


Rafiki yangu mmoja Mzanzibari alinishangaza majuzi yale kwa kunifikiria miye kuwa nduguye Rais wa Liberia, George Weah.
Rafiki yangu kaniambia kwamba yeye hucheza muziki na aliwahi kuzuru Dubai kutumbuiza hotelini alikofikia George Weah. Kwa hiyo kaniambia mimi na George Weah shilingi kwa nyingine.
Basi nini kilichonipeleka makaburini wiki hii? Si tu kwamba nilitaka kuona kumbukumbu ya Wazungu waliozuru na kufia Zanzibar tu. (Nami nimezuru Zanzibar tu wala kamwe sina nia ya kufia Zanzibar).
Si tu kwamba nilitaka kujua walitoka nchi gani na walikufa wakiwa na wastani wa miaka mingapi, hapana.
Muhimu ni kwamba niliazimia kujua kumbukumbu za watu hawa makaburini zimeandikwa kwa lugha gani. Ndiyo maana nimeifanya ziara yangu makaburini kiini cha makala yangu leo.
Nini nilichogundua? Niligundua kwamba wengi walikufa wakiwa bado vijana sana, umri usiozidi miaka thelathini na wakazikwa katika makaburi haya mapema katika karne ya 20.
Labda homa ndiyo iliyowaangamiza, nami sijui nini kitakachonimaliza hapa Zanzibar au kokote nitakakofia. Ila kwangu nasisitiza kwamba nilishangaa kuona kwamba Wajerumani walikuwa na maziara yao kando, pekee yao. Nani alisema hata katika mauti kuna ubaguzi? Wamezikwa katika maziara yao kando na wengine na kumbukizi zao kwenye makaburi zimeandikwa kwa Kijerumani. Nao Waingereza nao wamezikwa katika makaburi yao, kando na wengine. Wao vile vile wameandikiwa kumbukizi zao kwa Kiingereza. Sijui kama unanielewa? Yaani nasema nimekuta Kijerumani na Kiingereza katika makaburi Zanzibar! Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba katika uhai na kifo, Wajerumani wanapenda Kijerumani chao na Waingereza wanapenda Kiingereza chao.
Nikakumbuka makala moja ya kitaaluma iliyoandikwa na Dkt Musa Hans wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Katika makala hiyo, Hans anasema kwamba zipo shule Tanzania zimeweka sheria kwamba wanafunzi wasizungumze Kiswahili.
Nikakumbuke sheria kama hizo kwingi katika shule ambazo hupita nikiwahamasisha wanafunzi nchini Kenya ambapo ilani husema: “This is an English-speaking zone.”
Nikambuka makaburi ya Langata ambako nimewazika jamaa na marafiki kwa miaka na mikaka. Sijawahi kuona kumbukizi za Kiswahili maziarani humo: kila kitu katika Kiingereza. Nikafahamu kwamba katika uhai na kifo, hatuonei fahari lugha zetu.
Basi nikifia huku Zanzibar wanizike huku, lugha gani itatumika kuandika kumbukizi zangu za tarehe ya kuzaliwa na kufa? Je, Wataandika Kichina, Kilingala, au Kimaasai? Je, Kiswahili kitaendelea kuzikwa katika kaburi la sahau hadi lini?