Monday

LEKSIKOGRAFIA NININI?

0 comments
Katika kulijibu swali hili tutaanza na kutoa fasili mbalimbali kwa mujibu wa wataalamu.Kidahizo kwa mujibu wa TUKI (2001) ni neno  linaloingizwa katika kamusi ili lifafanuliwe kwa kupatiwa maelezo yanayohusu taarifa za kisarufi, maana, matumizi, etimolojia, semi mbalimbali za lugha nakadhalika.
BAKIZA (2010) Kidahizo ni neno  linalochapishwa kwa hati zilizokoza, na pengine kutiwa rangi, kwenye kamusi ambalo taarifa zake zinafafanuliwa.
Kutokana na fasili hizi tunaweza kusema kuwa kidahizo ni umbo la msingi linaloingizwa katika kamusi ambamo maumbo mengine yanatokana nalo.
Leksikografia kwa mujibu wa Mdee (2010) akimnukuu Wiegand (1984) ni kazi ya kisayansi ya kutunga kamusi.
Wikipedia wameifasili  leksikografia kuwa ni kazi ya kisayansi na kisanaa ya kutunga kamusi inayojumuisha uorodheshaji wa msamiati wa lugha inayotungiwa kamusi pamoja na maelezo ya kufafanua neon lililoorodheshwa kadri ya watumiaji wa kamusi iliyotungwa.
Kutokana na fasili hizi tunaona kuwa leksikografia ni taaluma ya kisayansi  inayohusiana na utungaji wa kamusi.
Watunzi wa kamusi ya Kiingereza tangu Robert Cawdrey (1604) hadi Murray (1882-1928) walibuni kanuni tofauti za uteuzi wa vidahizo na kuziingiza katika kamusi ambazo ni kama zifuatazo:
 Kanuni ya maneno magumu.
Kanuni ya maneno yote ya lugha.
Kanuni ya msamiati wa fani mbalimbali.
Kanuni  ya msamiati wa lahaja.
Kanuni ya kihistoria.
Pia katika uteuzi wa vidahizo kuna taarifa za kileksikografia ambazo huingizwa katika kamusi  na kuipa kamusi hiyo maudhui yaliyokusudiwa.Taarifa za kileksikografia  katika kamusi huingizwa katika kitomeo.Kitomeo hujengwa na kidahizo pamoja na taarifa mbalimbali ambazo zinazotolewa kukifafanua kidahizo.Hivyo kila kitomeo hupatiwa taarifa hizo japokuwa taarifa hizo hutofautiana kulingana na kategoria ya kidahizo.
Kidahizo katika   kamusi za Kiingereza kilipitia hatua tafauti mpaka kinapoonekana leo na kuingizwa taarifa za kileksikografia kulingana na kanuni ya mtunzi wa kamusi husika;
Kwa upande wa kanuni ya maneno maneno magumu ,Watunzi wa kamusi ambao walitumia kanuni hii walikuwa na lengo la kuwasaidia wazungumzaji wa Kiingereza kuelewa maneno mageni yaliyoingia katika  lugha yao ambayo hawakujua maana zake. Kamusi hizo zilikuwa na maneno magumu tu yaliyotoholewa kutoka katika lugha za Kiebrania, Kigiriki, Kilatini na Kifaransa.
Muanzilishi wa kanuni ya maneno magumu ni Mwalimu Robert Cawdrey (1604) ambaye kamusi yake iliitwa  A Table of Alphabetical na ilikuwa na vidahizo 3000.Cawdrey ndie aliyeweka msingi wa kamusi  za Kiingereza kwa kuyaondoa maneno yaliyoorodheshwa na Faharasa  na kuyaweka katika mfumo wa kamusi (Siemens 1994).Vilevile alibadilisha tahajia kutoka katika lugha za kigeni na kuzipa tahajia ya lugha ya Kiingereza.
Kamusi nyengine za maneno magumu zilizotunngwa wakati huo ni;
John Bullokar (1616), An English Expositor: Teaching the interpretation of the hardest words used in our language.
Henry Cockeram (1623) The English Dictionarie: or An Interpreter of hard English Words.
Thomas Blount (1656) Glossographic: or A Dictionary Interprettting all such Hard Words.