Kwa Mukhtasari
Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto.
Sehemu ya Tano A
UTANGULIZI
SUALA la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya ovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike. (Sasa endelea sehemu ya tano)
SEHEMU YA TANO
Sakina: Wewe mjinga kweli! Kosa umefanya wewe bado unatishia kutoroka, ondoka ukafie huko…
Mwanawima: (Kimya, analia kwa kwikwi.)
Sakina: Tena futa kabisa hayo mawazo kichwani mwako,
Mwanawima: (Kimya.)
Sakina: Unajua adhabu ya kuua? Unajua dhambi ya kuua wewe?
Subiri kesho asubuhi nitakuja hapo nyumbani, sawa!
Mwanawima: Sawa dada ila naomba sana unisitiri, usimwambie mtu.
Sakina: Usijali wewe fanya mambo yako kama kawaida, sawa?
Mwanawima: Sawa, asante (Anakata simu na kujifuta machozi.)
(Asubuhi na mapema Sakina anaingia nyumbani na kuwakuta wazazi wote wapo nyumbani, anawaza atatokaje na Mwanawima.)
Baba Mwanawima:Vipi mbona leo umekuja asubuhi yote hii.
Mama Mwanawima:Kwema huko?
Sakina: (Anadanganya) Kwema tu, kuna tatizo kidogo limetokea jana usiku hata sijalala.
Mama Mwanawima: Nini tena!
Sakina:Jana homa ilipanda sana usiku, nilivuja jasho usiku mzima, nimeona niwahi hospitali.
Mwinyikheri:Huyo mumeo hayupo?
Sakina:Wiki ya pili hii sasa ametoka na hizo meli zao za
mizigo.
.
Mama Mwanawima:Sasa huyu leo ni siku ya skuli itakuwaje?
Baba Mwanawima:Hapo hakuna njia nyingine waache tu waende
wote.
Sakina: (Anaingia chumbani kwa Mwanawima) Jiandae tuwahi.
Mwanawimaa: Sawa.
Sakina:(Ananong’ona) Hapa hamna namna tumwambie tu mama.
(Anakaa kitandani na kuinamisha kichwa chini.)
Mama Mwanawima:(Muda kidogo mama naye anaingia) Ukiweza umpime na huyo mdogo wako maana naye kila kukicha analalamika kichwa kinamuuma.
Sakina: Mama hapa ngoja tukueleze ukweli, funga kwanza mlango huyo mzee asije akatusikia.
Mama Mwanawima: ( Anafunga mlango haraka) Kwani vipi, mbona siwaelewi! Kuna nini?
Sakina: Mama mwanao haumwi na kichwa wala homa, mwanao ni mjamzito (Ananong’ona.)
Mama Mwanawima: Nini? Unasemaje? (Kwa sauti ya chini huku akimsogelea Mwanawima.)
Sakina: Taratibu mama, mwache kwanza haya mambo ni yetu sisi wanawake, naomba baba asiyasikie.
Mama Mwanawima: Hapana, hapana! Huyu ngedere amevuka mipaka, kwenye familia yangu hakuna huu uchafu (Anazidi kumsogelea Mwanawima kitandani. Anataka kumpiga kofi Sakina anamshika mkono).
Sakina: Mama achaa, utaibua mengine, baba yupo akisikia itakuwaje?
Mama Sakina:Kwa nini unataka unigombanishe na baba yako? Wewe unadhani akisikia haya mimi nitabaki salama? (Anainamisha kichwa chini.)
Sakina: Basi mama naomba utupe ruhusa yako tukaitoe hii mimba, tulitaka tukaitoe bila kukutaarifu lakini nafsi imetusuta, wewe ndio mama yetu.
Mama Mwanawima:Hii ni aibu mtaani, umekosa michezo yote ukaona huo ndio mzuri sio?
Sakina: Samahani mama, kutoa mimba ni zoezi gumu, hatuwezi kukamilisha pasipo moyo wako kuridhia.
Mama Mwanawima: Sawa nendeni, mimi sina hata cha kusema, ameshanivua nguo huyu…
(Wanaondoka. Wakiwa njiani Sakina anaanza kumsema na kumuonya Mwanawima.)
Sakina: Umefanya vibaya mdogo wangu, mimi pamoja na mapepe yote niliyokuwa nayo sijawahi kufanya uchafu huu.
Mwanawima: Ni sawa dada ila najuta, nakiri sitarudia nisamehe.
Sakina: Usiniombe mimi msamaha, rudi kwa Mola wako ufanye toba, uombe msamaha kwa Allah. Hapa unaenda kutoa mimba na hii ni dhambi ya kuua.
Mwanawima: (Anajifuta machozi) Sina jinsi dada, pia mimi naumia, naumia dada (Anazidi kulia.)
Sakina:Hii ni aibu kwani kwenye familia yetu hakuna hii laana. Huyo aliyekupa hii mimba unamjua?
wanawima: Ndio dada, ni dereva wa daladala.
Sakina: Kwa hiyo ulijiona mjanja kuwa na dereva! Muone!
Mwanawima: (Anajifuta tena machozi yaliyoambatana na kamasi nyembamba.)
Sakina: Hebu nipe hizo namba zake nimpigie.
Mwanawima: (Anaingiza mkono mfukoni na kutoa karatasi zenye namba za simu na kumpa dada yake.) Hii hapa!
Sakina: (Anapokea kwa dharau na kuanza kupiga) Haloooo! Halooo! Habari yako?
Dereva:Safi tu, nani mwenzangu?
Sakina:Mimi rafiki yake Mwanawima, vipi uko wapi?
Dereva:Anhaaa! Mimi nipo Kagera, naelekea Uganda na sidhani kama nitarudi huko.
Sakina:Uganda! (Anashikwa na kigugumizi kwa hasira.)
Dereva: Ndio! Tulipata ajali Juzi, gari letu liligonga mtu akafa hapo hapo. Imenibidi kuondoka ili kukwepa kitanzi. Msalimie sana mrembo wangu panapo majaliwa tutaonana.
Sakina: (Anakunja uso kwa dharau) Mrembo gani? Looh! Mtu mzima unakosa haya! Unajua kuwa umempa mimba. mdogo wangu?
Dereva:(Anashtuka) Nini? Mmekosa kazi za kufanya enhee (Anakata simu.)
Sakina: Halooo! Haloo! (Anaangalia anakuta simu imekata, anapiga tena, inaita bila kupokelewa.)Si unaona anakata simu! Hii ndio tabia ya wanaume watakupenda wakiwa na shida zao ila ikifika kwenye ujauzito unabaki unatangatanga na mzigo wako.
(Walifika hospitali majira ya saa tano, wakaenda mapokezi na kuelekezwa waende kwa daktari, wanaingia wanamkuta daktari Twalib ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka… ameweka mashine za kupimia mapigo ya moyo shingoni.)
Sakina:Daktari samahani tuna shida.
Daktari:Shida zenu hapa ndio zimefika, enhee niambie ni shida gani?
Sakina: Mdogo wangu amepata ujauzito daktari na bado anasoma, isitoshe nyumbani wazazi ni wakali mno tusadie daktari.
Daktari Twalib:Msaada gani mnataka!
Sakina: Tunaomba utusaidie tuitoe hii mimba daktari.
Daktari Twalib:Hebu panda kitandani. (Anamlaza Mwanawima na kumpima).
Mwanawima: Tusaidie daktari naona aibu, ni fedheha nitaonekana mhuni.
Daktari Twalib:Kwa imani ya dini na mila zetu za Kiafrika kutoa mimba ni dhambi, tena dhambi kubwa sana! Labda iwe kwa dharura maalumu kama kuokoa maisha ya mama mjamzito.
Sakina:Ni kweli daktari wote tunajua hilo…
Daktari Twalib:Ahaaa, kumbe mnajua eee, lakini pia kwa sheria za nchi yetu kutoa mimba ni kosa la jinai. Adhabu yake ni kifungo cha miaka mingi jela.
Sakina:Ni kweli daktari lakini tunaomba utusaidie. Daktari! (Anamuonesha hela kiasi cha shilingi maelfu ya fedha.
Daktari Twalib:Nataka mtambue kuwa hamna uwezo wa kunilipa, tena siku nyingine msirudie kunionesha visenti vyenu vya sambusa, mnaweza kunilipa mimi!
Sakina:Samahani daktari tusamehe kwa hilo, ila tunaomba utusaidie.
Daktari Twaib:Hamuwezi kunilipa hata kidogo.
Sakina:Ni kweli daktari tusaidie kwa leo tu please! Wazazi wetu ni wakali, baba hataturuhusu tuendelee kukaa pale.
Daktari Twalib:Wazazi wenu ni wakali eee! Ni wakali kuliko Mungusio? Ni wakali kuliko Serikali? Haahaa! Acheni kuropoka. Kama ni kuchukia basi Mungu amechukia ulivyozini. Pia, atachukia zaidi kama mtafanya hiki mnachotaka kufanya… Mimi hela yenu naipenda sana lakini sio kwa kufanya mauaji. Mwanawima, kumbuka kuwa kuna changamoto nyingi endapo utatoa mimba. Unaweza poteza maisha lakini pia unaweza usizae tena katika maisha yako.
Sakina: Unasikia! (Anamwangalia Mwanawima) Chagua kusuka au kunyoa…
Daktari Twalib: Mimi nakushauri uachane na haya mawazo, nenda kaongee na wazazi wako, kawapigie magoti uwaombe msamaha, pia uwe karibu na Mungu wako.
Mwanawima: Mimi siwezi. (Analia kwa kwikwi) Mimi siwezi dada.