Mwandishi Wa makala
Miss Happylight J.@masshele
Kwa mujibu wa BAKITA (2015), utandawazi ni mfumo wa mawasiliano rahisi unaoziwezesha nchi nyingi duniani kuwasiliana na kushirikiana katika masuala ya biashara, siasa na teknolojia kwa njia ya mtandao uliounganishwa kwenye kompyuta, aipadi au simu.
Utandawazi umechangiwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Matumizi ya simu za viganjani, kompyuta, mitandao ya kijamii yamechangia sana katika kukuza muingilianao baina ya jamii.
Katika kipindi hiki cha maingiliano ya jamii. Lugha ya Kiswahili inatumika katika nyanja mbalimbali. Yafuatayo ni baadhi ya maeneo ambapo lugha ya Kiswahili inatumika.
Lugha ya Kiswahili inatumika katika vyombo vya habari. Katika vyombo vya habari lugha ya kiswahili inatumika kwa namna mbalimbali. Kwanza kama lugha ya kutolea habari ambapo vipo vyombo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania vinavyotoa habari kwa kutumia lugha ya Kiswahili.
Kwa mfano Tanzania yapo magazeti, redio na vituo vya televisheni zaidi ya 100 vinavyotoa matangazo kwa lugha ya Kiswahili. Mtesigwa (2004), anasema zipo idhaa zaidi ya 30 nje ya Tanzania zinazotoa habari kwa Kiswahili. Baadhi ya idhaa hizo ni Deustchwelle ya ujerumani, Sauti ya Amerika (VOA), BBC, Redio Japan, Redio Saudi Arabia, Redio China. Vilevile vipo vipindi vya lugha ya Kiswahili vinavyojadili maendeleo na mada mbalimbali za Kiswahili.
Matumizi ya Kiswahili katika idhaa hizi yanadhihirisha kukua kwa lugha ya Kiswahili kimatumizi ambako kumechangiwa sana na utandawazi.
Lugha ya Kiswahili inatumika katika mitandao ya intaneti.
BAKITA (2004), wanasema katika mtandao wa intaneti Kiswahili kinatumika kwa namna tatu. Kiswahili kama lugha ya mawasiliano baina ya watumia mtandao, pili ni lugha ya kuwasilishia taarifa ndani ya mtandao, na tatu Kiswahili ni mada ya taarifa zinazotumwa mtandaoni.
Tungaraza (2013), akielezea matumizi ya Kiswahili katika intaneti anataja jitihada za Microsoft katika kutengeneza scanner ORC ambayo ilikua maalumu kwa ajili ya kutambua lugha za kiafrika na mojawapo ya lugha zilizoteuliwa mwaka 2011 ni Kiswahili. Hivyo ni wazi kuwa lugha ya Kiswahili ni lugha ya kimtandao na inazidi kuenea kwa njia ya mitandao ya kijamii
Kiswahili inatumika katika mawasiliano.
Lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha kuu Saba zinayotumika sana duniani. Lugha hii inatumika ndani na nje ya Afrika. Nchi za Afrika Kama Kenya, Kongo, Afrika ya kusini, Sudan, Somalia na Ghana ni baadhi ya nchi zinazotumia Kiswahili kwa mawasiliano rasmi na yasio rasmi.
Wakati huo nchi za Marekani, China na Ujerumani zikiwa miongoni mwa nchi za nje ya Afrika ambazo zinatumia Kiswahili katika mawasiliano.
Mathalani Tungaraza (2013), anataja ibada za Kiswahili zinazofanywa na wazungumzaji wa Kiswahili nchini Marekani na kuongeza kuwa vipo vyama vya watumia Kiswahili nchini humo.
Lugha ya Kiswahili inatumika katika taaluma. Kiswahili inatumika Kama lugha ya kufundishia lakini pia Kama somo katika taasisi za elimu ndani na nje ya Tanzania. Nchi Kama Afrika ya kusini na Rwanda in miongoni mwa nchi zinazotumia lugha ya Kiswahili kufundishia katika baadhi ya shule. Vilevile vipo vyuo vingi duniani kote vinavyofundisha lugha hii.
Kwa mfano Marekani zipo taasisi zisizopungua 100 zinazofundisha lugha ya Kiswahili. Baadhi ya vyuo vinavyofundisha Kiswahili ni Bayreuth, Kolon, Berlin, Hamburg na Humbolt.
Lugha ya Kiswahili inatumika katika biashara. Katika shughuli za kibiashara lugha ya Kiswahili inatumika katika kutambulisha bidhaa na kuwaunganisha wanunuaji na wauzaji bidhaa.
Kwa mfano katika maonyesho ya biashara ya Sabasaba ambayo huunganisha watu wa mataifa mbalimbali Kiswahili hutumiwa na wauzaji katika kutambulisha bidhaa zao. Vilevile zipo bidhaa mbalimbali ambazo zina majina ya lugha ya kiswahili na hata maelezo ya matumizi yake yameandikwa kiswahili. Kwa mfano sabuni ya Zoazoa.
Faukwa na hayo wapo watu wa mataifa mengine kama India, Waarabu, Wachina ambao wanatumia lugha ya Kiswahili katika kuwasiliana na wateja wao.
Kwa kuhitimisha, pamoja na kupiga hatua kubwa kimaendeleo, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika kipindi cha utandawazi yanakumbana na changamoto kadhaa. Baadhi ya changamoto hizo ni uchache wa machapisho kama kamusi na vitabu vya Kiswahili, kasumba ya kutoithamini lugha ya Kiswahili, uhaba wa visawe pamoja na ushindani kutoka lugha nyingine kama vile kichina na kiingereza.
MAREJELEO
BAKITA (2004). Kiswahili na Utandawazi. Dar es Salaam. BAKITA.
BAKITA (2015). Kamusi kuu ya Kiswahili. Nairobi. Longhorn Publishers.
Kihore, Y.M. & Chuwa,A.R. (2004). Kiswahili katika Karne ya 21. Dar es Salaam. TUKI.
Massamba D.P.B (ed) (2013). Jarida la Kiswahili: Juzuu ya 76. Dar es Salaam. TUKI.