Monday

MATATIZO YA TAFSIRI CHANGAMOTO ZA TAFSIRI

0 comments


CHANGAMOTO ZA KITAMADUNI KATI YA LUGHA CHANZI NA LUGHA LENGWA
Makala hii inasehemu kuu tatu; sehemu ya kwanza ni fasili ya tafsiri, utamaduni na vipengele vya kiisimu ambavyo vinaleta changamoto katika mchakato wa kutafsiri. Sehemu ya pili ni vipengele vya kiutamaduni vinavyosababisha changamoto katika shughuli ya kutafsiri. Sehemu ya tatu ni hitimisho.
Wataalamu mbalimbali wanaeleza tafsiri kama ifuatavyo;
Newmark (1988) na Mwansoko na wenzake (2006) wanaelekena sana katika fasili zao ambapo wanaeleza kuwa; tafsiri ni zoezi la kuhawilisha mawazo au maneno ya lugha chanzi kwenda lugha lengwa. Kwa upande wa Nida na Taber  (1969) wanatofautiana kidogo na mawazo ya wataalamu wenzake kwa kutueleza kuwa; kutafsiri hujumuisha kuzalisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asilia vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi kimaana na kimtindo.
Kutokana fasili za wataalamu hawa tunaweza kutoa maana ya tafsiri kuwa; ni uhawilishaji wa mawazo yaleyale yaliyoandikwa katika matini chanzi kuyapeleka katika matini lengwa.
Pia maana ya utamaduni imefasiliwa na wataalamu kama ifuatavyo;
Newmark (1988) anaeleza kuwa; utamaduni ni mkusanyiko wa mila na desturi zote za jamii inayotumia lugha mahususi kama njia yake ya mawasiliano.
Ruhumbika (1978:261) anatofautiana na mawazo ya Newmark kueleza utamaduni kwa kupinga kwamba utamaduni wa binadamu si mila na desturi zake na mambo ya yake tu. Bali utamaduni ni jumla ya juhudi zote za jamii fulani katika kila kipengele cha maisha, katika umma wake, katika filosofia zake za maisha, mfumo wa sheria zake, mbinu zake za ulinzi na usalama wa nchi, taratibu za kuelimisha raia zake, taratibu zake za mgawanyo wa kazi za uzalishaji mali na mifumo ya ugawaji wa matunda ya kazi hizo na juhudi za kuiwezesha jamii isonge mbele.
Kwa upande wa tofauti za kiisimu ambazo ni changamoto katika shughuli ya kutafsiri hujidhihirisha katika vipengele vikuu vinne yaani maumbo sauti, maumbo ya maneno, miundo ya sentensi pamoja na maana.
Baada ya kueleza fasili ya tafsiri  na utamaduni pamoja na kuainisha  vipengele vya kiisimu ambavyo ni changamoto katika tafsiri. Tuangalie sehemu ya pili ambayo ni tofauti za kiutamaduni ni changamoto kwa wafasiri wote katika shughuli nzima ya tafsiri.
Vipengele vya kiutamaduni vinavyosababisha changamoto hizo zimebainishwa na wataalamu kama ifuatavyo;
Nida (1964) akinukuliwa na Mwansoko na wenzake (2006:31) na Newmark (1988:95) visawe vya utamaduni wamevibainisha katika makundi matano yaani; ekolojia, violwa, mila na desturi, siasa na dini. Licha ya wataalamu hawa kubainisha katika makundi matano kwa ujumla tumeweza kubaini kwamba kipengele cha kisiasa kinajitegemea hakiwezi kuingizwa katika utamaduni na kipengele cha dini nacho kinaingia katika kipengele cha mila na desturi. Hivyo kutokana na mawazo haya vipengele vya kiutamaduni tumevibainisha katika makundi manne yaani; ekolojia, violwa na mila na desturi pamoja na semi kwa mujibu wa mawazo yetu Tukianza kueleza kipengele kimoja hadi kingine namna vilivyo na changamoto katika tafsiri kwa mfasiri au wafasiri.
Ekolojia; suala la tabia za kijiografia kwa kawaida zinaweza kutofautiana kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine. Hivyo kwa mfasiri ni ugumu sana kupata visawe mwafaka kwa maneno husika. Mfano lugha ya Kiswahili huzungumzwa zaidi katika nchi za joto hususani za Afrika Mashariki ambapo tunabainisha misimu minne ya mwaka yaani kiangazi, vuli, masika na kipupwe. Lakini Kiingereza huzungumzwa nchi za baridi hususani Uingereza wao hubainisha misimu minne pia ya mwaka summer, autumn, winter na spring. Lakini kwa waingereza;
         Summer ni kiangazi (lakini joto la kiangazi ni kali zaidi ya lile la
        Summer wanalolifahamu Waswahili)
         Winter-kipupwe (lakini baridi ya winter kwa Waingereza ni kali
         zaidi ya ile ya baridi ya kipupwe wanayoifahamu Waswahili)
Pia kuna michezo ambayo hufanyika sehemu zenye baridi ambayo kwa kawaida haiwezi kufanyika  nchi za joto kama hizi za Afrika Mashariki. Kwa mfano;
Skate-sketi (mchezo wa kusketi).
Ski-skii (mchezo wa kuskii).
Hivyo kwa mfasiri itamwia vigumu sana kupata visawe sahihi hususani anapofasiri matini ya kiingereza kuzipeleka Kiswahili. Kwa sababu vipindi kama hivyo hatuna na michezo hiyo haipo kwa hiyo kupata kisawe mwafaka kwa neno husika ni vigumu.
Violwa; kuhususha suala la uvumbuzi wa kisayansi na teknolojia kuingizwa katika nchi zetu zinazoendelea. Uvumbuzi na ubunifu huu umeathiri sana utamaduni wa lugha yetu ya Kiswahili na kusababisha wafasiri kushindwa kupata visawe mwafaka kwa baadhi ya maneno katika lugha ya Kiswahili. Badala yake kinachofanyika ni kutohoa maneno hayo kutoka katika lugha ya Kiingereza kwa kuyafanyia tu marekebisho ya kisarufi yanapoingizwa katika lugha yetu yaani ya kimatamshi na kimaumbo. Kwa mfano;
Kiingereza            Kiswahili
Radio                    redio
Chemical               chemikali
Telefax                  telefaksi,
Digital                  digitali
Software              softiwea
Hardware          hadiwea           
Mila na desturi; tofauti hizi inaweza kujidhihirisha kupitia ulaji, vinywaji, mavazi na imani (dini) baina ya utamaduni wa jamii moja na jamii nyingine. Hivyo basi tofauti hizo ni changamoto kubwa sana kwa mfasiri au kwa wafasiri wakati wa kutafsiri. Tukianza na;
Ulaji; utamaduni wa Waswahili wanamilo mikuu mitatu tu yaani kifungua kinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni. Lakini Waingereza wao wanamilo mikuu mitano yaani breakfast, lunch, high tea, dinner na supper. Kwa hiyo kwa mfasiri wa Kiswahili high tea ambayo ni chai nzito kwa kawaida ambayo hunywewa 11-12 jioni itampa ugumu kuifasiri. Kwani katika utamaduni wetu wa Waswahili hatuna chai ambayo watu wanakunywa wakati huu. Hata supper mlo wa usiku kwa kawaida mwepesi pia itamwia vigumu sana kwa wafasiri kupata visawe kwa sababu katika utamaduni wetu hatuna chakula ambacho huwa kinaliwa wakati huu.
Pia hata Wafaransa wanamlo ambao huliwa kabla ya “Lunch” uitwao “Appacative” mlo huu kwa utamaduni wa Waswahili haupo hivyo kwa mfasiri ni vigumu sana kupata kisawe chake kitakachofanyika ni kutumia mbinu ya ufafanuzi kuwafanya hadhira lengwa kuelewa nini kinachomaanishwa.
Hata upande wa matini za Kiswahili ambapo mfasiri anapofasiri matini ya Kiswahili kuipeleka katika lugha ya Kiingereza atashindwa kufasiri maneno ya vyakula kama vile; ugali na kande kwa sababu katika utamaduni wa Waingereza hakuna vyakula hivi atakachofanya mfasiri ni kutumia mbinu ya kuhawilisha maneno kama yalivyo kuyapeleka katika lugha lengwa au kutumia mbinu ya ufafanuzi.
Vinywaji; kwa upande wa vinywaji baridi vinavyonywewa katika utamaduni wa Waingereza vimekosa visawe katika utamaduni wetu wa Waswahili. Kwa hiyo kwa wafasiri ni changamoto kinachofanyika yanatoholewa na kufanyiwa mabadiliko ya kisarufi hususani ya kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano;  Cognac-konyagi, Whisky-wiski, Beer -bia  .
Pia kwa matini ya Kiswahili kuipeleka Kiingereza kuna baadhi ya vinywaji vinavyopatikana katika utamaduni wa Waswahili lakini utamaduni wa Waingereza havipo.
 Kwa mfano;      Ulanzi ,Mbege, Chibuku, Gongo
Kwa hiyo upande wa mfasiri ni vigumu sana kupata visawe kwa maneno haya. Mfasiri anakichofanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha kama yalivyo kuyapeleka katika matini lengwa.
Mavazi; upande wa mavazi ni changamoto vilevile kwa wafasiri wote hususani pale unapokutana na mavazi ambayo asilia yake ni utamaduni fulani mfano yale ya Waingereza ambayo yanatengenezwa katika nchi yao. Suala hili linajidhihirisha katika jamii zetu za Waswahili mavazi mengi yanatoka nchi za Magharibi. Kinachofanyika yanatoholewa na kuyafanyia mbadiliko kidogo ya kisarufi ambayo kama vile ya  kimatamshi na kimaumbo.
Kwa mfano;   Skirts-sketi, Jeans-jinsi, Pullovers-pulova
Pia kwa mavazi ambayo kwa asili hutengenezwa katika nchi zetu vigumu sana kupata visawe yakitumika katika matini za Kiswahili wakati wa kutafsiri, kwa sababu nguo hizi zipo tu katika utamaduni wetu wa Waswahili. Utamaduni wa nchi za wenzetu hazivaliwe na hazitengenezwi. Kwa hiyo wafasiri wanachokifanya ni kuyahawilisha kama yalivyo wakati wa kutafsiri au ktumia mbinu ya ufafanuzi kuwafanya hadhira lengwa kujua nini kinachomaanishwa.
 Kwa mfano;   Khanga,  Kiko, Kitenge
Dini; kwa wafasiri masuala ya dini pia ni changamoto kubwa sana, kwani baadhi ya maneno mfano yatumiwayo katika utamaduni wa Waingereza yanayotaja nyama kama vile nyama nguruwe
Pork-nyama ya nguruwe.
Harm-paja la nguruwe lililokolea chumvi na kukaushwa katika moshi.
Bacon-nyama ya nguruwe iliyotiwa chumvi au kutengenezwa
           isioze.
Ni vigumu sana kupata visawe vyake katika lugha ya Kiswahili kutokana na kwamba utamaduni wa Waswahili kuathiriwa kwa kiasi fulani utamaduni wa lugha  ya kiarabu ambayo waamini wake wengi ni waislamu. Wafasiri wanachokifanya ni kutumia mbinu ya kuyahawilisha maneno haya kama yalivyo na kuyapeleka katika matini lengwa.
Kwa mfano; Kadhi, Hijabu, Nikabu., Sheikh.
Semi ni tungo au kauli fupifipu za kisanaa zenye lugha ya mafumbo ambazo hukusudia kuleta mafunzo kwa jamii husika. Semi ni moja ya kipengele kigumu katika kufanya kazi ya kutafsiri. Hii ni kutokana na tofauti kati ya utamaduni wa jamii moja na nyingine. Semi hizi zinaweza zikatumika katika jamii moja na jamii nyingine zisitumike semi hizo. Kwa hiyo hujidhihirisha katika vipengele vyake. Kwa mfano;
Methali –     Ndondondo si chururu, chururu si ndondondo.
Nahau      –Mkono mrefu (mchoyo),  –Zunguka mbuyu (toa rushwa), -Amevaa miwani (amelewa)
Misimu –   Amejaa upepo (amekasirika), –Amenitoa upepo ( nimempa fedha)
Vitendawili- Kuku wangu anataga mibani (nanasi),  –Popo mbili zavuka mto (macho)
Misemo –   Mtu ni afya (kuzingatia usafi),  –Maji ni uhai (kulinda vyanzo vya maji).
Metheli za kiingereza kama vile
Advance is least heeded when most needed. Maana yake when the problem is serious people often don’t follow the advice given.
-All cats are grey in the dark. Maana yake people are undistinguished until they have made a name.
-A bad tree does not yield good apples. Maana yake a bad parent does not raise good children.
Hivyo basi wafasiri wengi wanachokifanya ni kutafuta semi ambazo huwa zinakaribiana na zile za lugha lengwa kwa lengo la kufikisha ujumbe uliokusudiwa  kwa hadhira lengwa hali ambayo inaweza kupotosha maana halisi ya semi husika ya matini chanzi ambayo inafungamana na utamaduni husika.
Kwa ujumla suala la kufasiri semi ni changamoto kubwa kwani semi nyingi hufungamanishwa na utamaduni wa jamii husika. Hivyo ni vizuri kufanya utafiti wa kina kwa wafasiri wote kabla ya kufanya tafsiri kwa hadhira chanzi kwa lengo la kuepukana changamoto hizi kwa kiasi fulani.
Changamoto hizi namna zitakavyoepukwa na wafasiri katika shughuli nzima ya kutafsiri kama ifuatavyo;
Suala la msingi kwa mfasiri ni lazima afahamu fika utamaduni wa lugha lengwa; hii itamsaidia mfasiri au wafasiri kufanya kazi za kutafsiri kwa ufanisi. Sululisho hili ni kwa mujibu wa maoni ya Mwansoko na wenzake (2006:36). Kwa maelezo ya wataalamu hawa mfasiri itamlazimu kutafiti kiundani sana utamaduni wa lugha ambayo anashughulikia.
Mfasiri anapaswa awe na umulisi wa lugha chanzi na lugha lengwa; ili anapokosa visawe mwafaka aweze kutumia mbinu ya ufafanuzi ili kuweka wazi wazo lililopo katika matini chanzi anapolitafsiri katika matini lengwa kwa lengo la kumfanya mteja au hadhira lengwa waelewe nini kinachomaanishwa.
Wataalamu wamejaribu kupendekeza mbinu kadha za kuepukana na changamoto za kiutamaduni wakati wa kutafsiri kwa mfasiri kama vile;
Matumizi ya tafsiri huru; mfasiri awe na ubunifu wa kuunda visawe vipya vinavyokubalika na lugha lengwa, hii itamsaidia mfasiri kupata visawe vinavyoendana na lugha chanzi wakati wa kufanya kazi yake ya kutafsiri kwa matini ambayo anaishughulikia.
Kukopa maneno; ni mbinu nzuri zaidi kwa mfasiri wakati wa kukabiliana na vipengele vya kiutamaduni vya matini chanzi kwa kutumia visawe vinavyokaribiana au kufanana na vile vya matini lengwa ambavyo vinafahamika na wasomaji wa matini lengwa. Kwa kuzingatia sheria na kanuni za lugha lengwa kwa dhana zisizofahamika. Ukopaji huu upo wa aina mbili yaani wa moja kwa moja (uhawilishaji) yaani ambao unafanyika pasipo kubadili umbo lolote la neno la lugha chanzi.
 Kwa mfano;
 kiingereza   (data)       
Kiswahili   (data)
Kiswahili      (ugali )      
Kiingereza   (ugali)
Ukopaji wa kubadilisha umbo la matamshi na umbo la neno (utohoaji); ukopaji ambao kuna mabadiliko kidogo ya kisarufi kwenye maneno ambayo yamekopwa kutoka lugha chanzi au lugha nyingine ambako neno hilo limekopwa kama vile  ya kimatamshi na kimaumbo.
 Kwa mfano;
Kiingereza        (Account, Photo)
Kiswahili          (akaunti,  Foto)
Matumizi ya tanbihi; mfasiri anatakiwa kutoa maelezo ya ufafanuzi wa kina zaidi kuhusu zile dhana ngumu ambazo zinakuwa vigumu kueleweka na hadhira lengwa au mteja, wakati aisomapo matini husika kila mwishoni mwa kila ukurasa. Pamoja na faharasa mwishoni mwa kazi yake ya tafsiri.
Hitimisho; mfasiri hana budi kuzingatia kwa makini kipengele cha utamaduni pindi afanyapo kazi ya kufasiri ili asiweze kuhuisha maana iliyomaanishwa katika matini chanzi. Wakati anafanyapo kazi ya kuifasiri matini ambazo zinafungamanishwa na utamaduni wa jamii fulani.
MAREJEO
Mwansoko, H. J. M. na wenzake, (2006) Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1988) A Textbook of Translaton. London: Prentice Hall.
Nida, A. E. na C. R Taber, (1969) The Theory and Practice of Translation. London: Prentice Hall.
 Ruhumbika, G. (1978) “Tafsiri za Kigeni katika Ukuzaji wa Fasihi ya Kiswahili” Makala kwenye Semina za Kimataifa ya Waandishi wa Kiswahili Dar es Salaam. Dar es Salaam: TUKI.

No comments:

Post a Comment