Tuesday

Jinsi sifa yakini zinavyoathiri uundaji wa mtindo katika lugha.

0 comments



Mwandishi. ELIZABETH   P.
UDSM/BAED 2019 

Makala  hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu, utangulizi ambapo inaelezea maana ya  dhana muhimu za  kama vile mtindo kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, kazi za kifasihi na kazi zisizo za kifasihi. Sehemu ya pili ni kiini ambayo imeelezea jinsi sifa yakini zinavyoathiri uundaji wa mtindo katika lugha, na sehemu ya mwisho ni hitimisho ambayo inaelezea muhtasari wa yale yaliyojadiliwa. 

Kwa kuanza na dhana ya mtindo,maana ya mtindo imejadiliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo; 

Senkoro (1982) anaeleza kuwa mtindo katika kazi za fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi hiyo na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huanisha kanuni au kaida zilizofuatwa za kimapokeo au za kipekee.


Wamitila (2003) anaeleaza kuwa mtindo ni ujumla wa mbinu au sifa zinazomuezesha mwandishi kuwasilisha ujumbe wake, huelezea mwandishi anavyounda kazi yake.
Samweli (2015) anaeleza kuwa mtido ni upangaji wa fani na maudhui kwa namna ambayo inampambanua msanii mmoja na mwingine.


Hivyo basi, mtindo ni ule upekee alionao mtunzi wa kazi ya fasihi katika kuipa kazi yake sura fulani kifani na kimaudhui. Mtunzi mwingine hawezi kufanya hivyo hata kama kitu kinachoongelewa ni kilekile, kwani watunzi wengi wa kazi za kifasihi watatofautiana katika kuwasilisha maudhui yao kwa hadhira.


Kazi za kifasihi ni zile kazi ambazo zina usanaa ndani yake yaani zinatumia lugha ya kifasihi zaidi. Kwa mfano; riwaya, tamthiliya na ushairi na kazi zisizo za kifasihi ni zile kazi ambazo hazina usanaa ndani yake yaani hazitumii lugha ya kifasihi mfano; magazeti, risala, hotuba, taarifa za habari nakadhalika. 

Uundaji wa mitindo  katika lugha huweza kuathiriwa na sababu mbalimbali ambazo ni sababu au sifa dhahania zinazotokana na hali ya kiuchumi, wasikilizaji, hali ya kijamii, rika pamoja na kisaikolojia. Lakini pia sababu nyingine ni sababu au sifa yakini ambazo ndizo hujenga au kuunda mitindo mbalimbali katika lugha.

Katika makala hili tutajikita zaidi kuelezea sifa yakini jinsi zinavyoathiri mitindo katika lugha.


Zifuatazo ni sifa yakini na jinsi zinavyoathiri uundaji wa mitindo mbalimbali katika lugha;

Namna ya utekelezaji wa mawasiliano, kuna namna mbili za utekelezaji wa mawasiliano namna ya mazungumzo na namna ya maaandishi. 


Utofauti baina ya mazungumzo na maandishi unatokana na matumizi maalumu ya kiisimu ambayo  katika mawasiliano ya kimaandishi lazima yatendeke. Kwa upande wa maandishi humlazimisha mtu kuchagua msamiati, sentensi na mpangilio wa sentensi unaostahili ili kufikia lengo lililokusudiwa, kwa upande wa mazungumzo ambayo yanaweza kuwa monolojia au daiyolojia huruhusu matumizi ya mbinu zingine zisizo za kiisimu kama vile mazingira na matumizi ya ishara. 

Kwa mfano tamthiliya ya Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe ya Edwin Semzaba, jinsi ilivyoigizwa ni tofauti na jinsi ilivyoandikwa kwani  hutofautiana katika kipengele cha matumizi ya lugha mfano; tanakali sauti, misemo, methali, mbinu nyingine za kisanaa pamoja na vipengele arudhi vya lugha. 

Hivyo ni dhahili kuwa jinsi ya utekelezaji wa mawasiliano huathiri moja kwa moja uundaji wa mtindo katika lugha.


Vifaa vitumikavyo katika mawasiliano, kuna vifaa mbalimbali vitumikavyo katika mawasiliano miongoni mwa vifaa hivyo ni kama vile barua, redio, televisheni. Kifaa kinachotumika kufikisha ujumbe huathiri mtindo wa lugha ya mzungumzaji au mwandishi wa kazi hiyo. Kwa mfano kiongozi akialikwa kwenye kipindi cha redio au kwenye televisheni juu ya jambo la kijamii, mazungumzo yake yatatofautiana sana  na mazungumzo anayozungumza kwa kutumia simu kuzungumza na familiya yake, ndugu zake au rika moja, kwani mazungumzo ya kutumia simu yanakuwa mafupi na yanatumia lugha ya mkato, tafsida na misimu ambapo wazungumzaji



 wanaufafano kihistoria. Hivyo vifaa vinavyotumika katika mawasiliano huathiri moja kwa moja mtindo.Vifaa ndivyo huteua mtindo yaani mtindo gani unatakiwa kutumika kulingana na kifaa hicho cha mawasiliano.


Tanzu za mawasiliano kama vile nyimbo, ushairi, hadithi, barua, risala na hotuba. Mtindo wa lugha unaathiriwa sana na namna jinsi mawasiliano yanavyowasilishwa kwa hadhira. Kwa mfano; mtunzi au mzungumzaji anatumia mtindo fulani wa lugha kutokana na tanzu fulani ya mawasiliano anayoitumia. Kwa mfano katika barua za kiofisi mwandishi anatumia mtindo wa lugha ya moja kwa moja isiyokuwa na misemo wala methali. Lakini katika kazi za za fasihi kama vile ushairi.Mtindo wa lugha inayotumika katika ushairi huambatana na lugha za taswira, methali, nahau na misemo ili kumvutia msomaji au msikilizaji wa kazi ya fasihi. Hivyo utanzu wa mawasiliano unaotumika huathiri uundaji wa mtindo katika lugha kwani mwandishi au mzungumzaji hutakiwa kutumia lugha kulingana na utanzu atakao utumia katika kuwasiliana.  


   
Shughuli za kijamii ,shughuli inayotendeka katika jamii wakati huo inaathiri mtindo wa lugha utakaotumika katika muktadha huo. Mfano katika shughuli za kijamii kama vile; siasa, dini  na msiba mitindo ya lugha inayotumika katika shughuli hizi hutofautiana katika shughuli moja na nyingine. Kwa mfano, mtindo wa lugha inayotumika katika shughuli za siasa huwa ni lugha ambayo ina ushawishi mkubwa lakini mtindo wa lugha inayotumika msibani huwa ni lugha ya kuwaliwaza na kuwatiamoyo wafiwa juu ya  kupotelewa na mwenzao katika familia. 

Licha ya kuwa sifa yakini huathiri uundaji wa mtindo katika lugha villevile kuna sifa za kidhahania ambazo pia zina leta athari katika uteuzi wa mtindo katika lugha kama ifuatavyo;


Mazingira ya wazungumzaji au waandishi, mtindo wa lugha unateuliwa kulingana na mazingira ya sehemu ambapo mazungumzo hayo yanafanyika. Kwa mfano mazungumzo ya darasani baina ya mwalimu na mwanafunzi yatakuwa tofauti sana na mazungumzo ya mwanafunzi na mwalimu wanapokuwa nje ya eneo la darasa au nje ya eneo la shule au chuo. Vile mwandishi anateua mtindo wa lugha kulingana na mazingira ya hadhira yake.
 Kwa mfano mwandishi anaandika kuhusu usafiri wa daladala basi mtindo wa lugha ambao utatumika utagusa muktadha wa daladala.Kwahiyo muktadha pia huweza huathiri uundaji wa mtindo katika lugha.


Uhusiano baina ya wahusika kiumri, tabaka na hata hali ya kiuchumi. Mwandishi au mzungumzaji anateua mtindo wa lugha kulingana na hadhira yake. Kwa mfano; mzungumzaji anapozungumza na kijana mwenzake atatumia mtindo wa lugha ambayo inaweza  kuwa yenye utani mwingi, dhihaka au kejeli tofauti na anapokuwa anazungumza na mtu aliyemzidi umri au watoto wa umri chini yake .Vile vile mwandishi anafuata rika au umri wa hadhira anayoiandikia kazi yake kama ni watoto atatumia lugha za kuchekesha na kufurahisha. Kwahiyo uhusiano baina ya wazungumzaji au huweza kuteua au kuathiri uundaji wa mtindo katika lugha kwani mzungumzaji wa lugha hutakiwa kuendana na hadhira yake ili kuwasilisha dhamira yake.


Kwa jumla uundaji wa mitindo katika lugha huathiriwa na sifa yakini ambazo ni kama vile nyenzo za mawasiliano, njia za kutekeleza mawasiliano, kazi au shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na aina ya mazungumzo lakini pia uundaji wa mitindo katika lugha huathiriwa na sifa dhahania yaani zitokanazo na hali ya kiuchumi na kisaikolojia.Hivyo ni muhimu kuzingatia sifa hizi zote wakati wa uundaji wa mitindo katika lugha.


                                                      




                                                        MAREJELEO
Mwansoko H.J.M (1991), Mtindo ya Kiswahili Sanifu: Dar es salaam, Dar es salaam University 
                               press.
Samweli M. (2015), Umahiri katika Fasihi ya Kiswahili, Mwongozo kwa Mwanafunzi na    
                  Mwalimu wa Fasihi Simulizi na Andishi: Dar es salaam. Meveli publishers.
Senkoro F.E.M.K (1982), Fasihi: Dar es salaam: press & publicity centre.
Wamitila K.W (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi: Nairobi: Focus publishers

masshele.blogspot.com

No comments:

Post a Comment