Dhana ya “isimu” imefasiliwa na wataalamu mbalimbali miongoni mwa wataalamu hawa ni;
Massamba (2004) anasema, “isimu ni taaluma ya ufafanuzi, uchambuzi na uchanganuzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi.”
Naye Hartman (1972) anasema “isimu ni eneo maalumu la mtalaa ambalo lengo lake huwa ni kuchunguza lugha. Wanaisimu huzichunguza lugha zikiwa ni nyenzo muhimu za mawasiliano ya mwanadamu.
Besha (1994) anasema“isimu ni taaluma ambayo huchunguza na kuweka bayana kanuni ambazo ndizo msingi wa kila lugha.
Hivyo kundi linafasili isimu kuwa ni taaluma inayohusika na ufafanuzi, uchambuzi na uchanganuzi wa lugha kwa kutumia mbinu za kisayansi. Mbinu hizo zaweza kuwa ni uchunguzi uliodhibitiwa, uundaji wa mabunio, uchanganuzi, ujumlishi/jumuishi, utabiri, majaribio na uthibitishaji pamoja na urekebishaji au ukataaji wa mabunio.
Baada ya kufasili isimu kutokana na wataalamu mbalimbali hivyo kuna umuhimu wa kufasili jamii kuwa;
Jamii ni mkusanyiko wa watu wanaoishi kwa pamoja katika eneo moja la kijiografia wakiunganishwa na historia yao na wakitambuliwa kwa utamaduni wao, lugha, mila na desturi.
Kwa mujibu wa Msanjila na wenzake (2011) wanasema “isimujamii ni taaluma inayo shughulika na matumizi ya lugha katika jamii.”
King’ei (2010) anasema “isimujamii ni taaluma inayo eleza uhusiano wa karibu uliyopo kati ya matumizi ya lugha na maisha ya jamii. Pia anaendelea kueleza kuwa kwanza lugha ni zao la jamii, nanikipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii, pili lugha hutumiwa na jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha kuwezesha wanajamii kuwasiliana.Isimujamii hueleza na kufafanua mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.
Hivyo basi isimujamii ni taaluma mojawapo ya isimu inayo chunguza namna lugha inavyo tumika katika jamii na uhusiano wake baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti, aina mbalimbali za lugha na mazingira yake na uhusiano wa lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia. Bila kuwepo kwa jamii hakuna lugha na bila kuwepo lugha hakuna jamii hivyo lugha na jamii hukamilishana ili kukidhi haja za mawasiliano.
Isimujamii ni taaluma iliyo pana kiasi kwamba uhusiana na taaluma nyingine za isimu, uhusiano huo ni kama ifuatavyo;
Isimujamii na isimu sosiolojia, sosiolojia ni taaluma inayoshughulikia uchunguzi na uchanganuzi wa matabaka na makundi ya watu katika jamii, mfano wa makundi hayo ni matabaka ya wenye kipato cha juu na wenye kipato cha chini, matabaka ya wafanya biashara na wakulima, matabaka ya watawala na watawaliwa. Uhusiano uliopo baina ya isimujamii na isimu sosiolojia ni kuwa katika jamii kuna matabaka mbalimbali na kila tabaka lina namna tofauti tofauti ya kutumia lugha kulingana na mazingira, mfano tabaka la wafanyakazi wana lugha wanayotumia tofauti na tabaka la wakulima, tabaka la wasomi nao wana lugha yao, pia wazee na vijana wana lugha yao. Hivyo basi mwanaisimu jamii kuyafahamu matabaka yaliyo katika jamii yake na jinsi lugha inavyotumika katika matabaka hayo.
Isimujamii na isimu anthropolojia, anthropolojia ni taalamu inayojihusisha na kuangalia mila na desturi za jamii fulani na jinsi zinavyotumika katika maisha yao ya kila siku. Uhusiano wa isimujamii na isimu anthropolojia ni kuwa matumizi ya lugha katika jamii huendana na mila na desturi ya jamii husika hivyo lugha hutofautiana kutoka katika jamii moja hadi nyingine. Mwanaisimujamii ajue mila na desturi zilizomo katika jamii ili kutumia lugha ambayo hujitokeza katika msamiati wa lugha husika. Mfano katika jamii yenye utamaduni wa tohara na ukeketaji, kuna msamiati wa kurejelea kwa yule aliye tahiriwa na yule ambaye bado hajapitia hatua hiyo. Hali hii huwa ni tofauti na jamii ambazo hazina utamaduni huo kama vile jamii ya wakurya mvulana ambaye hajatahiriwa huitwa “umurisia” na Yule ambaye ametahiriwa huitwa “umumura.” Hivyo baadhi ya maeneo lugha inapotumika katika mazingira fulani huonekana ya kawaida ilhali katika mazingira mengine huonekana kama ukiukaji wa utamaduni wa jamii husika.
Isimujamii na isimu saikolojia, saikolojia ni taaluma ambayo hushughulika na michakato ya kiakili, uzalisha wa matamshi katika kujifunza lugha na tabia za watu katika jamii. Taaluma hii ina husiana na isimujsmii kuwa mwanaisimujamii hutumia saikolojia kuchunguza matumizi ya lugha miongoni mwa wanajamii. Saikolojia humwezesha kutafiti na kueleza michakato ya ubongo katika kujifunza lugha na umri ambao watoto hujifunza lugha.Pia mwanaisimujamii huchunguza na kutoa ufafanuzi kwa nini watu hutofautiana kitabia hivyo ufafanuzi huo huzingatia vipengele mbalimbali kama vile mazingira watokayo watu hao,historia za familia zao na hulka asili za wahusika kutokana na lugha anayotumia mzungumzaji ni rahisi kwa mwana isimu saikolojia kutambua mzungumzaji ni wa rika gani aidha ni mtoto mdogo au ni mtu mzima.
Isimujamii na isimu historia, uhusiano uliopo kati ya taaluma hizi ni kuwa mwanaisimu jamii huweza kuchunguza lugha za wazungumzaji na kupata taarifa za ziada zinazohusu jamii husika. Lugha inayotumiwa na jamii huweza kutoa taarifa fulani kuhusiana na msamiati wa lugha hiyo pamoja na ukale wa msamiati kama ulivyokuwa ukitumika. Hivyo basi mwanaisimujamii huchunguza na kutambua mabadiliko yaliyotokea na yanayoendelea kutokea katika lugha kwa mfano katika lugha ya Kiswahili neno oa lilikuwa lola wakati fulani wa nyuma.
Isimujamii na isimu miundo, isimu muundo fasili yake ni kuwa Massamba na wenzake(2001) wanasema isimu muundo ni utanzu wa sarufi unaojishughulisha na uchanganuzi wa mpangilio wa maneno katika sentensi na uhusiano wa vipashio vyake. Isimujamii huhusiana na isimu muundo katika kuonesha au kuboresha mpangilio wa vipashio vya lugha katika sentensi ili kujenga upatanisho wa lugha wenye mantiki. Pia isimujamii humsaidi mwanaisujamii kuzingatia kanuni na sheria ambazo hufuatwa katika mfuatano unaokubalika na wenye kuleta maana inayoeleweka na kila lugha huwa na utaratibu wake maalumu wa kupanga vipashio katika tungo. Kwa mfano sentensi inaweza kuwa “kula kijiko kwa wali” muundo wa sentensi ni mzuri lakini hauna maana, hivyo muundo ungekuwa “kula wali kwa kijiko.”
Isimujamii na isimu maana, isimu maana ni taaluma inayochunguza maana katika lugha. Hivyo taaluma hii ina uhusiano wa moja kwa moja kati ya isimujamii na isimu maana kutokana kwamba kila lugha yoyote ile inakuwa na maneno ambayo yana maana inayotokana na lugha katika jamii husika,mwanaisimujamii anapaswa kufahamu maana mbalimbali za maneno jinsi yanavyotumika katika jamii.mfano katika jamii inayotumia lugha ya Kindali mwanaisimu aweze kujua maana zinazopatikana katika lugha hiyo. Kwa hiyo uhusiano kati ya isimujamii na isimu maana huendana katika matumizi ya lugha katika jamii fulani.
Isimujamii na jiografia, jiografia ni eneo lililotenganishwa kwa mipaka ya jamii ya eneo fulani linakuwa na namna tofauti ya utumiaji wa lugha kulingana na mipaka yao. Mwanaisimujamii hanabudi kuelewa jiografia ya eneo fulani ili kutambua mipaka ya wazungumzaji wa lugha ingawa ni vigumu kutambua mipaka ya jamii kama si mhusika wa lugha hiyo au jamii hiyo, hivyo hulazimika kutumia lugha kulingana na eneo fulani mfano eneo la wahaya hutumia kihaya kutokana na eneo husika.
Kwa ujumla isimujamii ina mawanda mapana na mawanda finyu ambayo huchunguza uhusiano na tofauti za wazungumzaji wa lugha. Isimujamii pia hutofautiana na taaluma nyingine katika maana na vipengele vingine lakini lugha na jamii ni dhana mbili ambazo huwezi kuzitenganisha. Hivyo isimujamii na taaluma nyingine humsaidia mwanaisimujamii anapokuwa anachunguza matumizi ya lugha katika jamii.