Teknolojia hiyo inajulikana kama “liquid screen protector” hutumika kufunika kioo cha simu kisichubuke au kuharibika haraka.- Wafanyabiashara, watumiaji wasema haiwezi kukinga kioo cha simu kisivunjike ikianguka.
- Wachambuzi wa teknolojia wasema matumizi sahihi ya teknolojia hiyo yatapunguza changamoto zinazojitokeza sasa.
Dar es Salaam. Ni saa 4:00 asubuhi wakati jua likiwaka mithiri ya moto wa kifuu, kituo cha daladala cha Makumbusho jijini Dar es Salaam kama kawaida yake kimeshamiri watu na sauti za honi za magari na vipaza sauti vya matangazo ya bidhaa za wafanya biashara wa eneo hilo.
Unaweza kuchanganyikiwa! Wakati magari yakiingia na kutoka kituoni hapo, sauti za vipaza za wafanyabiashara zinakuita usogee karibu kwaajili ya kupata bidhaa mbalimbali ikiwemo simu na vifaa vingine vya kielektroniki.
“Ofa ofa ofa, tunabandika “protector za liquid” zinazotumia mitambo ya kisasa, pia tunabandika “protector za 10D na 3D”…,” ni sauti ya kipaza sauti cha Juma Salehe ambaye amekaa kwenye kibanda chake akijibu meseji zake za simu yake iliyojaa nyufa huku akisubiria kuwahudumia wateja wanaopita mbele ya kibanda chake.
“Liquid screen protectors” ni aina ya technolojia mpya ya kisasa ya kulinda kioo cha simu yako kisipasuke au kupata michubuko wakati wa kuitumia.
Teknolojia hiyo iko kwenye mfumo wa maji maji ambapo maji hayo hupakwa kwenye kioo cha simu na kuachwa ikauke ili kulinda simu yako.
Faida ya kutumia aina hiyo ya kifuniko cha kioo cha simu ni kuwa huifanya simu yako kuwa na muonekano mzuri na kuepusha simu kuchakaa au kukwaruza hasa sehemu ya kioo.
Salehe ameuambia mtandao .huu kuwa kipaza sauti hicho kimekuwa nyenzo ya kuvutia wateja kuulizia teknolojia hiyo ambapo wateja 10 wanaofika katika kibanda hicho, wawili huwekewa kifuniko hicho ambacho hushikamana na kioo cha simu.
“Wanavutiwa na teknolojia mpya hasa ikizingatiwa kuwa simu yako haitapata “scratch” (imechubuka) na hautopata tabu ya kubadilisha mara kwa mwara kwa sababu inakaa muda mrefu,” amesema Salehe.
Teknolojia hiyo imewavutia watu wengi ikiwemo Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kampasi ya Dar es Salaam (TUDARCo), Joyce Julius ambaye amekuwa akitumia karatasi za plastiki kufunika kioo cha simu lakini zimekuwa hazidumu na kulazimika kutoboa mfuko kununua kila mara.
“Nimechoka. Kariakoo hamna nimezunguka hadi basi. Nikiangalia mtandaoni siamini kama zinaweza kunifikia najidunduliza nikaweke,” amesema Joyce, anayetafuta Sh15,000 kukamilisha zoezi lake.

Lakini unahitaji kujua zaidi
Huenda Joyce hafahamu kuwa wapo ambao wanajutia furaha ambayo walikuwa nayo hapo mwanzo kutumia teknolojia hiyo baada ya kukumbana na changamoto mbalimbali.
Mfanyabiashara wa simu katika kituo cha Makumbusho, Samira Yusuph amewataka watu wajiridhishe kwanza kabla ya kutumia teknolojia hiyo ili kuepuka madhara yanayoweza kuharibu simu zao.
Cheyo anasema moja ya mapungufu ya teknolojia hiyo ni kuwa haizuii kioo cha simu kuvunjika ikiwa itaanguka chini.
“Nimelipia Sh30,000 mimi kuweka huo “upuuzi”. Siku nimedondosha simu yangu, kwa mbwembwe na imani naokota kukuta kioo kimepasuka. Kwenda kwa fundi, Loh! Hadi kioo cha simu kimepasuka,” anasema Samira kwa uchungu baada ya simu yake ya Samsung S6 Edge iliyopasuka mbele na nyuma.
Hata hivyo, mfanyabiashara mwingine wa simu kituoni hapo, Benedict Bisanga amesema hayo yote yanatokea kwa sababu wapo baadhi ya wanyabiashara wanachakachua teknolojia hiyo ili kujinufaisha wenyewe.
“Hii teknolojia ni nzuri lakini wanachokosea hapa kwetu, wanachakachua,” amesema Bisanga na kuongeza kuwa anawafahamu watu watatu waliotumia teknolojia hiyo kwa kujiamini lakini baadaye hupata maumivu kwa simu zao kuharibika.
Muuzaji wa duka la vifaa vya simu lililopo Makumbusho, Spesioza Buhongwa amesema mbali na simu kuvunjika, baadhi ya simu zilizowekewa teknolojia hiyo zimekuwa zikipata matatizo ya kuharibika kwa spika na kioo cha simu yenyewe.
“Wapo wanaokosea kuiweka. Wanaweka hadi kwenye spika za simu wakati aitakiwi kufika huko,” anasisitiza muuzaji huyo.
Zaidi, amesema wapo ambao huweka protector za kawaida baada ya kuweka protector za liquid kwani hawana imani nayo.
“Wengine wanaweka kwaajili ya ile kuepusha simu zao zisi “scratch” (kuchubuka) lakini ukumuuliza kwanini kafanya hivyo anasema haziamini kwa asilimia 100,” amesisitiza Spesioza.
Kutokana na mapungufu ya teknolojia hiyo, baadhi ya wadau wa teknolojia wameshauri watu watumie karatasi za plastiki kufunika vioo vyao ambavyo ni imara na vinaweza kuilinda simu hata ikianguka.
Natumaini sasa unaweza kufanya maamuzi sahihi ni teknolojia gani inakufaa kwa ajili ya kufunika kioo cha simu yako.