Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam imewataka wanafunzi wote wa UDSM watakapofungua chuo rasmi Jumatatu, Juni Mosi, kuhakikisha wanavaa barakoa (mask) muda wote wanapokuwa darasani na viunga vya chuo.
Mbali na hilo, wanachuo hao pia wametakiwa kuhakikisha wanapowasili chuoni ni lazima watumie vitakasa.
"Kila mwanafunzi utakapowasili chuoni utakutana na vitakasa mikono vya aina mbili vya kukanyaga kwa miguu na vya automatic ukiweka mikono inatoa sabuni na maji. Kila mwanafunzi atatakiwa kunawa mikono kila anapotoka sehemu moja kwenda nyingine,hususani anapoingia darasani na kutoka nje. Kumbuka vitakasa mikono vitawekwa maeneo yote ya kuingilia na kutoka madarasani na sehemu zote za mikusanyiko." ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya kwa wanafunzi.
Aidha kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kikao kilichoshirikisha uongozi wa serikali ya wanachuo na Wizara ya Elimu, jana Jumanne, Mei 26 kikao hicho kimeafiki pia kupunguza muda wa masomo kutoka wiki 15 na saa 45 za awali hadi wiki 12 na saa 36 ili kukamilisha muhula wa pili baada ya muda mwingi kupotea baada ya janga la Corona kutangazwa.
Taarifa hiyo pia imesema, baadhi ya shule, taasisi na Ndaki zitapangiwa vipindi kwenye madarasa yaliyopo katika sehemu zao ili kuondoa uwezekano wa watu kukusanyika.
Mitihani ya kumaliza muhula inatarajiwa kuanza rasmi Agosti hadi Agosti 28 huku wanafunzi wote wakitakiwa kuipakua ratiba hiyo ya masomo kaunzia leo, Jumatano kupitia tovuti ya chuo.
Kwa upande wa vyuo vya ualimu, taarifa hiyo imesema kutakuwa na mabadiliko ya mafunzo ya vitendo ambayo itaanza rasmi Agosti 31 na kuhitimisha Oktoba 9 ambapo itakuwa ni pungufu ya wiki mbili na awali.
Kwa upande wa wanafunzi wa Kimataifa wanakaribishwa kuendelea na masomo lakini kwa wale ambao nchi zao hazitawaruhusu kutokana na 'Lockdown' watatakiwa kuandika barua ya kuahirisha muhula na kuja kusoma mwaka unaofuata wa masomo 2020/2021.