Sunday

Desperados”: filamu mahususi kwa wanaoteswa na mapenzi

0 comments


Safari inaanza ya mabinti hao watatu kusafiri kwenda Mexico kumtafuta Jared na kuhakikisha haisomi barua ile. Picha|Mtandao.

  • Inamuhusu mwanadada Wesley ambaye anaanza safari ya kumtafuta mwenzi wake wa maisha.
  • Safari hiyo inaishia  katika majuto baada ya kutuma ujumbe wa kumtukana mpenzi wake bila kujua yaliyomsibu.
  • Wesley na marafiki zake, wanafungasha virago kumtafuta Jared ili wahakikishe hasomi ujumbe huo.

Dar es Salaam. Ukisikia “majuto ni mjukuu” ndiyo hivi. Binti Wesley Darya (Nasim Pedrad) ambaye umri wake unazidi kwenda ana shauku ya kupata mtu wa kumuoa na hivyo anajikuta katika safari ya kutafuta mwenza wake wa maisha. 
“Unaonekana kama binti mzuri sana lakini kwangu mimi wakati bado siyo sahihi,” ni maneno anayoambiwa na mmoja wa wadau anaokutana nao katika safari hiyo.
Maneno hayo yanampelekea kuchanganyikiwa na kujikuta kwenye ajali ambayo baada ya kuamka, anakutana na sura ya Jared (Robbie Amell).
“Ulikuwa wapi maisha yangu yote?”.Ni swali analojiuliza Wesley ambaye anajikuta anamdondokea Jared kimahaba.
“Unafahamu nini kuhusu mwanaume huyo? Marafiki zake wanamhoji kwa taharuki kwani binti huyo hisia zake zipo juu ya mawingu.
“Anataka watoto, anamiliki shuka aina ya “Duvet” ninahitaji nini zaidi? Anawajibu na kuwaacha kwenye mshangao.
Hata penzi linaponoga na wawili hao kupeana mahaba moto moto, Jared anatoweka kwa siku tano mfululizo. 
Wesley ambaye hajibiwi meseji wala kupokelewa simu, anajikuta kwenye mpasuko wa moyo huku akidhani kuwa huenda Jared ametoweka baada ya kuupata “utamu” wa Wesley.
Simanzi na manung’uniko, yanampelekea binti huyo kushirikiana na marafiki zake kuandika barua pepe ndefu ikiwa na matusi yenye thamani ya mamilioni na kuituma kwa Jared.

    Lahaula!, Jared anapiga simu na kumwambia kuwa yupo Mexico na amehusika kwenye ajali ya gari hivyo amekuwa hospitalini kwa muda wote ambao alikuwa kimya.
    “Jared akisoma barua pepe ile, maisha yangu yamekwisha,” Wesley anawaambia marafiki zake.
    Safari inaanza ya mabinti hao watatu kusafiri kwenda Mexico kumtafuta Jared na kuhakikisha haisomi barua ile. 
    Vimbwenga vya kuvunja mbavu vimejaa kwenye filamu hii inayojulikana kama “Desperados” ambayo huenda inagusa maisha ya wanawake wengi waliowahi kujihisi wamesalitiwa au kuachwa kwenye “Chorus” ya mahusiano yao.
    Itazame filamu hii kupitia mtandao wa Netflix endapo tu, umelipia kifurushi chako?

    No comments:

    Post a Comment