Monday

Google kuwalinda wanaofuatiliwa na wapenzi wao mtandaoni

0 comments

  • Inafanya mabadiliko ya sera yake kuzuia matangazo ya programu zinazofuatilia watu mtandaoni bila ridhaa yao. 
  • Yasema kila mtu ana uhuru wa kutumia intaneti bila kuingiliwa. 
  • Huenda ikawasaidia watu waliopo kwenye mahusiano kufurahia haki ya faragha mtandaoni. 

Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu ambao wanaogopa kufanya vitu kwa uhuru ukiwa mtandaoni kwa sababu tu unahofia kuna watu wanakufuatilia au wanaingilia mawasiliano yako, sasa ondoa shaka hiyo. 
Kampuni ya teknolojia ya Google imetangaza kuiboresha sera yake ya matangazo ili kudhibiti matangazo yote ya programu za bidhaa na huduma ambazo zinahimiza kuwafuatilia watu mtandaoni bila ridhaa yao.
Kampuni hiyo inayotoa huduma ya watu kutafuta vitu mtandaoni, imesema kila mtu ana haki ya faragha kwa anayoyafanya mtandaoni bila kuingiliwa na mtu yoyote. 
Imesema miongoni mwa matangazo ya bidhaa na huduma hizo zitakazozuiliwa ni pamoja programu zinazotumika na watu waliopo kwenye mahusiano ya kimapenzi (intimate partner surveillance).
Pia matangazo ya programu zinazotumika kudukua na kufuatilia meseji, mawasiliano ya simu, historia kivinjari kwenye simu au kompyuta, eneo alilopo mtu na vifaa kama kamera maalum na vifaa vya kurekodi ambavyo vinalenga kufuatilia watu mtandaoni. 
“Sera hii itatumika duniani kote na tutaanza kutekeleza maboresho ya sera Agosti 11, 2020,” imeeleza taarifa ya Google iliyotolewa hivi karibuni.

Google imesema tabia hizo za watu kuwafuatilia wenzao wanayofanya mtandaoni siyo nzuri na zinatakiwa kudhibitiwa ili watu wafurahie haki zao za kutumia intaneti kwa shughuli mbalimbali. 
“Ukiukaji wa sera hii utasababisha akaunti yako kusimamishwa mara moja bila kupewa onyo la awali,” imeeleza Google.
Hata hivyo, mabadiliko hayo ya sera ya matangazo hayatahusu huduma za uchunguzi binafsi na bidhaa na huduma za zilizosanifiwa kwa ajili ya wazazi kuwafuatilia watoto wao wakiwa mtandaoni. 
Rehema John ambaye ni mtumiaji wa simu janja ameiambia  mtandao huu kuwa mabadiliko hayo ya Google yatasaidia watu ambao wako kwenye mahusiano ambao wamekuwa wakikosa uhuru kwa sababu tu ya kuhofia wenza wao wanafuatilia. 
“Hata kama niko na mpenzi bado ni uhuru wangu wa kufanya mambo yangu bila kuingiliwa au kufuatiliwa na mtu hata kama ni mpenzi wangu nikiwa mtandaoni,” amesema Rehema ambaye mkazi wa Jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment