Ni filamu inayohusu marafiki wawili wenye ndoto za kushinda mashindano ya kimataifa.- Changamoto ni kwamba, watashindaje huku hawajui kuimba?
- Kama una uwalakini na ndoto zako, huenda filamu hii ikakuamshia uthubutu.
Dar es Salaam. “Tangu tukiwa wadogo, tumekuwa na ndoto moja tu,” Sigrit Ericksdóttir (Rachel McAdams) anasema na Lars Erickssong (Will Ferrell) anajibu “Kushinda mashindano ya muziki ya Euro Vision.”
Wawili hao ambao ni marafiki wa dhati tangu utotoni, wana ndoto ya kuwa wanamuziki mashuhuri wakiiwakilisha nchi ya Ice Land katika mashindano hayo makubwa katika bara la Ulaya kupitia bendi yao isiyofahamika iitwayo “Fire Saga”.
Lakini wanawezaje kufikia ndoto zao iwapo Iceland ambayo wanatarajia kuiwakilisha, inawaona kama majokeri, wazee, wapitwa na wakati na wasio na swaga?
Tuache utani. Kwakweli, hata wewe huenda ungeomba kurudishiwa pesa yako endapo ungehudhuria baadhi ya matamasha yao.

Hata hivyo, wawili hao hawakuweza kuchaguliwa kuingia katika mashindano ya ndoto zao kwani walikuwa wakichuana na mwana dada Katiana Lindsdóttir (Demi Lovato) aliyeimba kiasi cha kufikirisha kama koo lake limeumbwa kwa nyama kama yalivyo ya watu wengine.
Unaweza kusema ni bahati ya mtende kwani Lars na Sigrit wanabaki tumaini lisilo na upinzani kwa Iceland baada ya washindani wengine wote kufa baada ya boti waliyokuwa wakifanyia sherehe ya pongezi kulipuka na kuwabakiza wao tu.
“Fire Saga itaiwakilisha Iceland kwenye mashindano ya Euro Vision mwaka huu. Siwapendi, hawafai kabisa, ni wazee, wanatia kinyaa lakini hatuna namna,” ni majadiliano ya kamati ya nchini humo yanayoendelea huku Fire Saga wakiwa hapo hapo.
Je, hali itakuwaje endapo umempa mtu asiyejua kuimba kipaza sauti aimbe mbele ya shindano linalohudhuriwa na watu 180 milioni, likiwaniwa na nchi 42, huku wanamuziki zaidi ya 100 wakichuana na dunia nzima ikitazama kwa runinga?
Vichekesho, huba, kuanguka na kusimama tena, ni kati ya safari utakayoipitia ukiitazama filamu ya Eurovision Song Contest: The Story of Fire Saga huku nyota Will Ferrell maarufu kupitia filamu za Get hard, The Other guys na Zoolander akiwa tayari kumalizana na mbavu zako.
Tazama filamu hii inayofuka moshi kupitia mtandao wa Netflix endapo tu, umelipia kifurushi chako.
Kama Netflix siyo fungu lako, bado unaweza kufurahia filamu za “Action” watoa huduma wengine kama DStv ambapo leo saa 8:40 mchana, Tom Cruise atakonga nyoyo kupitia filamu ya “Top Gun” huku filamu zingine kama “Ralph Breaks the Internet”, Snow White and the Seven Dwarfs pia zikitarajiwa leo
.
.