Jadili kwa kina kazi na Changamoto za Nadharia ya Mofofonolojia katika kuchanganua Sauti za Lugha.
Na, Ester Amos Mwakisitu
Ikisiri
Makala hii imenuia kueleza kazi na changamoto za nadhari ya mofofonolojia kama zilivyoelezewa na Massamba(2012).Katika kulijibu swali hili tutaligawa katika sehemu kuu nne. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao utakuwa na fasili na dhana mbalimbali za mofofonolojia na historia ya kuibuka kwa nadharia hiyo . Sehemu ya pili ni kiini cha swali ambapo tutaeleza kazi za nadharia ya mofofonolojia yaani sababu zilizopelekea kuibuka kwa nadharia hii. Sehemu ya tatu tutajadili changamoto za nadharia ya mofofonolojia ambazo zilipelekea kushindwa kwa nadharia hii na kusababisha kuibuka kwa nadharia ya fonolojia zalishi.Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Utangulizi
Massamba (2012) anaeleza kuwa nadharia ya mofofonolojia iliasisiwa mnamo mwezi Oktoba 1929 na mwanazuoni Price Nikolaj Trubetzkoy katika mkutano mkuu wa wanafilolojia wa Ki-Slavu. Trubetzkoy alilitumia neno hili kwa maana ya tawi la isimu ambalo kwa mujibu ya maelezo yake lingeshughulikia matumizi ya mofolojia katika kufafanua tofauti fulani za kifonolojia ambazo isingewezekana kuzieleza kwa kutumia data za kifonetiki peke yake. The New Oxford American Dictionary (2010) imefafanua mofofonolojia kuwa tawi la isimu linalojishughulisha na uwakilishi wa kifonolojia wa mofimu. Kwa maneno mengine ni kuwa tawi hili la isimu linahusika na kudhihirisha uhusiano wa kiutegemezi uliopo baina ya fonolojia na mofolojia. Kwa ujumla mofofonolojia ni kiwango cha kiisimu kinachojishughulisha na uhusiano wa kifonolojia na jinsi kinavyohusiana moja kwa moja na mofolojia. Nadharia ya mofofonolojia iliibuka kutokana na matatizo yaliyoibuka katika kuchanganua baadhi ya vipengele vya kifonolojia ambavyo vilihitaji maelezo zaidi kuliko yale ya kifonolojia.
Kazi za Nadharia ya Mofofonolojia
Massamba (2012) anaeleza kuwa, mofofonolojia ina kazi kuu tatu, miongoni mwa kazi hizo ni kuchunguza miundo ya mofimu katika lugha, kuchunguza mabadiliko ya sauti yanayotokea baada ya sauti mbili kuungana na mwisho ni kuchunguza ubadilishanaji wa sauti ambao unauamilifu kimofolojia.
2.1.1 Kuchunguza Miundo ya Mofimu katika Lugha
Nadharia ya mofofonolojia ilikuwa na kazi ya kuchunguza miundo ya mofimu katika Lugha kwa kuangalia mofimu zilizounda neno.
Mfano
Umbo la ndani Umbo la Nje
i. /Mu+ana/ [Mwana]
ii. /Mu+anafunzi/ [Mwanafunzi]
iii. /Mu+izi/ [Mwizi]
Katika mifano hiyo hapo juu, mofimu ‘mu’ ambayo imeanza mwanzoni mwa neno inawakilisha umbo la ndani la sauti.
2.1.2 Kuchunguza Mabadiliko ya Sauti yanayotokea baada ya Sauti mbili kuungana
Aidha mofofonolojia huweza kuchunguza mabadiliko ya sauti mbili tofauti kuungana na kuunda sauti nyingine katika lugha. Massamba (2011) anaeleza kuwa katika lugha ya Kiswahili na nyingine za kibantu irabu ya juu ‘i’ inapoungana na irabu ya chini ‘a’ hupelekea kuzaliwa kwa irabu nyingine ambayo haikuwepo hapo awali ambayo ni sauti ‘e’. Tuchunguze mifano ifuatayo kuthibitisha hilo dai
Mfano
Umbo la ndani Umbo la nje
i. /Ma+ino/ [Meno]
ii. /Wa+ingi/ [Wengi]
iii. /Pa+ingine/ [Pengine]
iv. /Wa+ingine/ [Wengine]
/a/ + /i/ [e] / K - K
Katika mifano hiyo hapo juu muungano wa irabu ama sauti /a/ na /i/ na kuunda sauti [e] inaleta athari katika maumbo ya maneno husika. Hakika hili lisingeweza kuzungumziwa bila kuhusisha nadharia ya mofofonolojia.
2.1.3 Kuchunguza Ubadilidhanaji wa Sauti ambao unauamilifu Kimofolojia.
Massamba 2012 anaeleza kuwa mabadiliko ya sauti yanayotokea katika baadhi ya maneno baada ya sauti Fulani kufuatiwa na kiambishi cha unominishaji (i). Mofofonolojia imeonyesha mabadiliko ya sauti ya kifonolojia na umbo la neno kimofolojia.
Mfano
i. Jenga - mjenzi
ii. Penda - mpenzi
iii. Fuata - fuasi
/g/ [z]/ - i (ya unominishaji)
Katika mfano wa data yetu hapo juu kinominishi ‘i’ kimebadili umbo la neno kutoka kitenzi kuwa nomino. Hivyo mofofonemiki imeonyesha uhusiano wa kifonolojia na mofolojia.
2.1.4 Kuchunguza Athari za mfuatano wa Sauti mbili zinazofanana
Mgullu (2010) anasema kuwa irabu hudondoshwa zaidi zinazofanana huwa zinavutana. Hii ni kuonesha kuwa yapo mabadiliko yanapotokea iwapo irabu mbili zinazofanaana zinapokaribiana, mathalani maneno kama vile
Mfano
Umbo la ndani Umbo la Nje
i. /Wa+anafunzi/ [Wanafunzi]
ii. /Wa+alimu/ [Walimu]
/a/ [Ø]/ - I = /a/
Katika data yetu hapo juu, mabadiliko ya kuachwa kwa irabu iliyokuwa awali hayawezi kuzungumzwa kifonolojia pekee kwa kuwa yanaathiri umbo la neno zima.
Changamoto za Nadharia ya Mofofonolojia
Nadharia hii inakumbwa na changamoto kadhaa katika uchambuzi na uchanganuzi wa sauti za lugha, miongoni mwa changamoto hizo ni kama ifuatavyo;
3.1.1 Kuwa na viwango vitatu vya Uchanganuzi
Nadharia hii ilikuwa na viwango vitatu vya uchanganuzi ambavyo ni mofofonemiki, fonemiki na fonetiki. Aidha kipashio cha msingi cha mofofonemiki ni mofofonimu, pia kipashio cha fonemiki ni fonimu na kipashio cha fonetiki ni foni. Viwango hivi kwa kiasi kikubwa vinahusiana.
Mfano
Mofofonemiki fonemiki fonetiki
Mu+ana Mu+ana [Mwana]
Hivyo waliona hakuna haja ya kuwa na viwango vitatu vya uchanganuzi kwani mofofonemiki na fonemiki vinahusiana.
3.1.2 Kuwa na Umbo Kiini ambalo ni Dhahania
Massamba (2012) anaeleza kuwa umbo kiini ni umbo lichukuliwalo kama kiwakilishi cha kila mofimu (kama sehemu maanifu ya sarufi). Umbo kiini lilikuwa na udhahania hii ni kutokana na kukosekana kwa misingi yoyote ya Kiisimu ambayo imetumika.
Mfano
fuaTa – fuaSi
katika maneno hayo {T} na {S} ndizo fonimu kuu katika maneno fuaTa na fuaSi lakini ukichunguza zaidi utaona kuwa hakuna sifa za msingi ambazo zimejengwa katika ubainishaji wa fonimu kuu.
3.1.3 Hakukuwa na utumiaji wa Sheria na Kanuni bali walitumia maelezo tu
Nadharia hii ilikuwa inatumia maelezo kwa kiasi kikubwa katika uchanganuzi wa sauti za lugha. Nadharia hii ilikuwa haitumi sheria wala kanuni katika uchanganuaji wa sauti.
Mfano
Penda – Mpenzi
/d/ [z] / - i (ya unominishaji)
Hitimisho
Aidha mapungufu ya nadharia hii imechochea kuibuka kwa nadharia nyingine ili kuja kukidhi hayo mapungufu yaliyojitokeza katika nadharia hii.
Marejeleo
Mgullu,R.S(1999). Mtalaa wa Isimu: Fonetiki, Fonoloji na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publisher.
Massamba,D.P.B (2011) Maendeleo Katika Nadharia ya Fonolojia. Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili.
Massamba,D.P.B (2012) Misingi ya Fonolojia. Dar es Salaam: TUKI.
The New Oxford American Dictionary (2010), Oxford University Press. New York.