Inawahusu watahiniwa wa kidato cha nne wanaotarajia kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.- Watakiwa kuingia katika mfumo wa selform.tamisemi.go.tz ili kufanya mabadiliko.
- Serikali yaanzisha tahasusi mpya tano za PMC, KFC, BPF, PGE na KEC.
Dar es Salaam. Kama wewe ni muhitimu wa kidato cha nne mwaka 2020 na una mpango wa kubadilisha tahasusi (combination) uliyochagua kusoma utakapojiunga kidato cha tano au chuo cha elimu ya ufundi mwaka huu, dirisha limefunguliwa kwa ajili yako.
Serikali imetangaza utaratibu mpya kwa wahitimu wa kidato cha nne mwaka 2020 kubadilisha tahasusi za kidato cha tano na kozi za vyuo vya elimu ya ufundi kwa njia ya mtandao kwenye mfumo wa kieletroniki wa uchaguzi wa kidato cha tano na vyuo mwaka 2021.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo amesema kuwa lengo la kufanya mabadiliko ya tahasusi na kozi ni kuwawezesha wanafunzi kubadilisha machaguo yao kulingana na ufaulu wao kwenye matokeo ya mtihani wa idato cha nne waliofanya mwaka jana.
“Baadhi ya wanafunzi hawakujaza kwa uhakika tahasusi au kozi kutokana na kutokuwa na uhakika wa ufaulu katika masomo waliyachagua, hivyo kwa sasa wanafahamu masomo waliyofaulu vizuri na wanaweza kuchagua tahasusi au fani za kusomea,” Jafo amewaambia wanahabari leo Machi 29, 2021 jijini Dodoma.
Jafo, ambaye ni Mbunge wa Kisarawe, amesema kuwa Serikali imetoa fursa hiyo ili kuwawezesha wanafunzi kusoma fani au tahasusi itakayowandaa kuwa na utaalam katika maisha yao ya baadaye.
Wanafunzi wanaotaka kufanya mabadiliko ya kozi au tahasusi wanatakiwa kuingia kwenye mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi unaopatikana katika anuani ya selform.tamisemi.go.tz.
Dirisha hilo la kufanya mabadiliko limefunguliwa leo Machi 29, 2021 na litakuwa wazi hadi Aprili 11 mwaka huu.
Ikumbukwe kuwa wahitimu hao ambao wana sifa kufanya mabadiliko ni wale ambao walifanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) mapema mwaka huu.
Serikali yaanzisha tahususi mpya
Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, Serikali imeanzisha tahasusi mpya tano kwa ajili ya wanafunzi wanaoingia kidato cha tano mwaka huu ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa wataalam wanaohitajika katika soko la ajira.
Waziri Jafo amezitaja tahasusi hizo kuwa ni Physics, Mathematics na Computer Studies (PMC), Kiswahili, French, Chinese (KFC), Kiswahili, English na Chinese (KEC), Physical Education, biology na Fine Art (PBF) na Physical Education, Geography, Economics (PGE).
Tahasusi ya PMC itatolewa katika Shule ya Sekondari ya wasichana ya Dodoma na Shule ya Sekondari ya wavulana ya Iyunga.
KFC na KEC itatolewa katika Shule ya Sekondari ya wasichana Morogoro na ya wavulana Usagara na tahasusi ya PBF na PGE itatolewa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Makambako, Shule ya Sekondari ya wavulana Kibiti na Sekondari ya Mpwapwa ambayo ni ya mchanganyiko.
"Nchi yetu ilikosa kuwa na wataalam wa michezo kutokana na kutokuwepo na tahasusi maalum,hivyo hili ni jambo jipya ambalo mwanzo halikuwepo," amesisitiza Waziri Jafo.