Sunday

Mage: Wananiita Maiti Inayotembea

0 comments


SIKU zote kuna usemi usemao; ‘kabla hujafa hujaumbika!’ Ndivyo ilivyo kwa Mage Masalu (32), mkazi wa Magu jijini Mwanza.

 

Maskini Mage; tumbo lake limevimba mno kutokana na maradhi ambayo mpaka sasa hayajajulikana kwa sababu hakuwahi kwenda hospitali maalum kwa ajili ya kupata matibabu zaidi.

 

Badala yake, alikuwa akitibiwa kwa njia ya miti shamba pekee ambayo ndiyo imemuongezea ugonjwa zaidi.

Gazeti la IJUMAA kupitia ukurasa wake huu wa kuwapa sauti watu wenye taabu mbalimbali za kimaisha, limemfikia Mage.

 

Katika mahojiano na Gazeti la IJUMAA, Mage anasema kuwa, ugonjwa huo ulimuanza mwaka 2014.

Anasema kuwa, alianza kusikia kama vichomi kwenye kitovu, akajua ni kitu cha kawaida na tatizo hilo lingeisha, lakini haikuwa hivyo kwani tumbo lilianza kujaa taratibu.

 

Baadhi ya ndugu zake na mumewe kabla ya kutengana, walimpeleka kwa mganga wakidhani alikuwa amefanyiwa mambo ya Kiswahili (ushirikina) hivyo akaanza kutumia dawa za miti shamba.

 

“Nilianza kusikia vichomi vikali kwenye kitovu, nikajua labda ni kawaida tu au labda nataka kuingia kwenye siku zangu, lakini kila wakati vilianza kunichoma mno. Baadaye nikagundua kuwa tumbo langu linaanza kuvimba taratibu ndipo walipoanza kunipeleka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kupata dawa, labda kutakuwa na mtu amenifanyia kitu kibaya,” anasema Mage.

 

Anaendelea kusema kuwa, tumbo liliendelea kuvimba, kiasi ambacho mumewe alianza kumletea visa na zaidi akamletea hawara ndani ya nyumba na kulala naye.

Anasema mama yake mzazi aliumizwa na kitendo hicho ndipo akaenda nyumbani kwa mtoto wake huyo na kumtukana mumewe.

 

Anasema wakati huo yeye alikuwa hayupo kwa sababu aliondoka kwa muda kumpisha mumewe na hawara maana aliumizwa mno na kitendo alichokuwa akifanya mumewe.

 

“Niliamua kuwaachia nafasi kidogo, nikaenda Sengerema kwa wifi yangu, lakini nyuma, mama yangu alishikwa na hasira, akaenda kwa mume wangu na kumtukana sana ndipo mume wangu akamwambia wifi yangu anirudishe nyumbani na niliporudi, akaniambia niondoke na mama yangu na tangu siku hiyo akawa ameniacha kabisa,” anasema Mage.

 

Anasema kuwa, wakati anaondoka, aliondoka na watoto wake wadogo wawili, akawa anakaa nao kwa shida mno na kuna kipindi aliwahi kulala nao kwenye choo cha baa kwa sababu walikuwa wakitafuta chakula huku yeye akiwa na hali mbaya.

 

Anasema mwishoni mwa mwaka jana, mumewe huyo aliwachukua watoto wake wote na mpaka sasa hajawarudisha huku yeye yupo katika hali mbaya ya ugonjwa.

 

“Yaani mwaka jana alikuja kuwachukua watoto baada ya kuambiwa wanateseka na njaa na hadi leo sijawaona kabisa, maana kwa sasa hivi tumbo langu limejaa sana hata kutembea ni shida kwa sababu nimepata msaada wa dada Flora Lauwo ndiye amenisaidia, nimeanza kupatiwa matibabu na kama mume wangu anasoma habari hii, basi namuomba tafadhali aniletee watoto wangu japo niwaone kidogo tu,” anamalizia kusema Mage.

 

Kama umeguswa na habari hii na unataka kumchangia Mage chochote ulichobarikiwa na Mungu, basi unaweza kumtumia kupitia namba; 0759 665 555.

IMEANDALIWA NA IMELDA MTEMA

Chanzo : Gazeti la ijumaa

No comments:

Post a Comment