Thursday

Mwanafunzi Chuo Kikuu Anyongwa na Mpenziwe Kisa Mapenzi

0 comments


​​​​​​​MWANAFUNZI wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Iringa, Petronel Mwanisawa (22) amefariki dunia kwa kunyongwa na mpenzi wake huku chanzo kikisemekana kuwa ni wivu wa mapenzi.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba hadi sasa wanamshikilia mtuhumiwa, Prudence Patrick (21), ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho.

 

Akizungumza na chombo kimoja cha habari, Kamanda Bwire amesema tukio hilo limetokea Juni 1, mwaka huu maeneo ya Kihesa, kwamba siku hiyo ya tukio marehemu hakurudi nyumbani kwao na haikuwa kawaida yake, hivyo wazazi wake waliingiwa na wasiwasi na kuanza kumtafuta.

 

“Marehemu alikuwa anaishi na wazazi wake, na huyu mtuhumiwa yeye alikuwa amepanga. Kwa hiyo siku ya tukio alitoka kwenda chuo, lakini mpaka usiku akawa hajarudi, ndipo wazazi walianza kupata wasiwasi, wakampigia simu rafiki yake lakini hawakufanikiwa.

 

“Kwa hiyo jana ndo tukampata, na hiyo ni baada ya mtuhumiwa mwenyewe kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa mzazi wa marehemu akisema alikuwa na Petronel na kwamba amefariki. Baada ya hapo hakupatikana tena,” amesimulia Kamanda Bwire.

 

Amesema baada ya wazazi kupata taarifa hizo waliripoti kituo cha polisi, ndipo askari walikwenda katika nyumba ya mtuhumiwa na kuukuta mwili wa marehemu.

 

Kamanda Bwire amesema kuwa, kwa sasa Jeshi la Polisi mkoani Iringa linamshikilia Prudence Patrick (21) Mwanafunzi wa chuo kikuu hicho cha Iringa anayedaiwa kuhusika na mauaji hayo, ambaye amekamatwa katika kituo kikuu cha mabasi cha Iringa akiwa anatoroka baada ya mauaji hayo kuelekea nyumbani kwao Bukoba mkoani Kagera.

 

“Mtuhumiwa tulimkamata njia ya kuelekea Dodoma alipokuwa akijaribu kutoroka na upelelezi wa tukio hilo unaendelea. Prudence alikuwa akimtuhumu Petronel kuwa na uhusiano na Mwanaume mwingine ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambaye pia anadaiwa kumpa ujauzito.” amesema Kamanda Bwire.

 

Kamanda Bwire amesema kuwa mara baada ya mwili huo kuagwa, utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajili ya mazishi. Kamanda Bwire amesema mara baada ya kufanya mauaji hayo, Prudence anadaiwa kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa Mama wa Marehemu na kumtaarifu kuhusu tukio hilo.

No comments:

Post a Comment