Misongamano yenye ulazima itatakiwa kufuata masharti yote ya kiafya.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imepiga marufuku misongamano yote isiyokuwa ya lazima ikiwa ni moja ya hatua za kukabiliana na kuongezeka kwa kasi kwa maambukizi ya wimbi la tatu la ugonjwa virusi vya corona (Uviko-19).
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ameeleza katika taarifa kwa umma kuwa kuna baadhi ya maeneo mwitikio wa kufuata miongozo ya kujikinga na Uviko-19 umekuwa mdogo kiasi cha kuchangia kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
“Ili kuimarisha zaidi kasi ya kupambana na kudhibiti maambukizi ya Uviko-19 natamka kuwa kuanzia leo Julai 22, 2021 nimekataza shughuli zote za msongamano yote isiyokuwa ya lazima na ile yenye ulazima tahadhari ya kutosha ichukuliwe bila kuathiri shughuli za kiuchumi na kitaifa,” amesema Dk Gwajima katika taarifa hiyo iliyotolewa Alhamis.
Katika utekelezaji wa marufuku hiyo, Dk Gwajima ameelekeza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuweka utaratibu mzuri kwa wale wanaoomba vibali vya shughuli zenye ulazima.
Maambukizi ya Uviko-19 nchini Tanzania yamezidi kuongezeka katika siku za hivi karibuni tangu Serikali ianze kutoa takwimu Juni 28 mwaka huu. Kwa zaidi ya mwaka mmoja Tanzania ilikuwa haitoi takwimu za Uviko-19 na mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa Mei 2020 ambapo kulikuwa na wagonjwa 509 na vifo 21.
“Hali hii imeendelea kuchangia kuongezeka kwa maambukizi na hatimaye kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa waliolazwa ambapo hadi kufikia 21 Julai 2021 katika vituo vya huduma za afya kote nchini kulikuwa na wagonjwa 682 waliokuwa wanaugua maradhi ya Uviko-19,” amesema Dk Gwajima akieleza namna watu wasiotii miongozo ya kujikinga na ugonjwa huo walivyochangia kuongezeka kwa wagonjwa.
Kwa takwimu hizo mpya za wizara ya afya, ndani ya wiki mbili zaidi ya wagonjwa wapya 274 wameripotiwa katika vituo vya kutolea huduma nchini kutoka 408 waliorekodiwa Julai 8, 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 67.
Iwapo hesabu hiyo itapigwa hadi Juni 28 alipotangaza Rais Samia Suluhu Hassan uwepo wa wagonjwa zaidi ya 100 wanaougua Uviko-19, kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo yameongezeka zaidi ya mara sita ndani ya mwezi mmoja.
Wimbi la tatu la Uviko-19 limeendelea kuyatesa mataifa mbalimbali ulimwenguni na kuangamiza maisha ya watu wengi.
Hadi kufikia leo Saa 1:30 jioni, watu zaidi 160,000 barani Afrika walikuwa wamepoteza maisha kutokana na maradhi hayo kwa mujibu wa Kituo cha Kuzuia na Kupambana na Magonjwa Afrika (Africa CDC).
Ili kuendelea kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo, Dk Gwajima amewataka Watanzania kutekeleza afua za kujikinga ikiwemo kuhakikisha vyombo vya moto havibebi abiria wengi kiasi cha kuleta msongamano mkubwa na watu kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono