Monday

Rombo Kuanzisha Mnada Wa Mifugo

0 comments










HALMASHAURI ya Wilaya ya Rombo inapanga kufungua mnada wa mifugo katika kitongoji cha Munga, kijiji cha Shimbi Mashariki, kwa lengo la kuzuia wizi wa mifugo na kuongeza mapato ya serikali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo,  Godwin Chacha alisema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao cha ujirani mwema kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Rombo, Khamis Maigwa na kuwakutanisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Taveta nchini Kenya ikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Joseph Maina.

Akizungumza katika kikao hicho, Chacha alisema ili kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Kenya,  Halmashauri ya Rombo ipo mbioni kufufua mnada wa mifugo wa Munga ili kudhibiti wizi wa mifugo ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya watu na kuharibu sifa za ujirani mwema.

"Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakinunua mifugo maeneo ya mpakani na kuja kuiuza Tanzania, wakati mwingine tumekuwa tukipata taarifa kuwa mifugo hiyo imeibiwa Kenya na kuja kuuzwa Tanzania jambo ambalo limekuwa likiharibu uhusiano mzuri kati ya nchi hizi mbili. Sasa tutafungua mnada huo," alisema Chacha.

Alisema kufunguliwa kwa mnada huo kutaondoa changamoto zote za mifugo kuuzwa kwa kupitishwa kwenye njia za panya na wafanyabiashara sasa watafika katika mnada huo kwani watanunua sehemu maalumu  hivyo kuwanufaisha wafugaji, wafanyabiasha, halmashauri na serikali kwa ujumla.

Alisema serikali itahakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mifugo wa ndani na nje ya nchi ili wafanye shughuli hiyo bila shaka.

"Mnada huo utatengewa maeneo ya kufanya uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati vya kufanya uchakataji wa nyama na kuuza maeneo mengine ndani na nje ya wilaya ya Rombo na utakuwa na manufaa makubwa kwani bei ya mifugo itakuwa nzuri kwa wafugaji na wafanyabiasha," alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Gilbert Tarimo alisema kuna mwamko mkubwa wa biashara ya mifugo na kwamba halmashauri na serikali kwa zitaingiza mapato mengi  kutokana na ushuru utakaokusanywa katika mnada huo.

Ofisa Mifugo na Uvuvi wa wilaya hiyo, Emanuele Sindiyo alisema wafanyabiasha wengi kwa sasa hulazimika kwenda mpakani kununua mifugo na kwamba biashara hiyo hufanyika katika njia zisizo rasmi.

Mkuu wa Wilaya ya Taveta, Maina alieleza kufurahishwa na hatua ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kufungua mnada wa mifugo kwani utachochea kasi ya maendeleo ya wananchi hususani wafanyabiasha na wafugaji.

Alisema uwapo wa mnada huo utasaidia kupunguza mifugo kuzurura ovyo na kula mazao ya wakulima na kuwapongeza askari wa usalama kwa kukomesha wizi wa mifugo.

Kikao hicho pia kiliwakutanisha wenyeviti wa vijiji vinavyopakana na nchi ya Kenya, maofisa watendaji wa kata, madiwani, wakuu wa idara za maliasili na mifugo kutoka pande zote mbili, lengo likiwa ni kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili

No comments:

Post a Comment