Epuka kuelezea wasifu wako kwani tayari wameshausoma.
Elezea mafanikio yako na jinsi unaweza kuwa na mchango utakapoajiriwa.
Usisahau kuongelea shauku yako juu ya kazi hiyo.


Dar es Salaam. Kama ni mtafuta ajira ambaye umewahi kupata bahati ya kuitwa kwenye usaili, bila shaka swali hili sio geni.  Ni swali la “wewe ni nani” ambalo mwajiri anauliza ili kufahamu taaluma, ujuzi na uzoefu wako.
Amini ninapokuambia kuwa, wala hahitaji kujua kabila na mkoa uliozaliwa. Anahitaji madini ya kung’amuliwa mchango ambao unaweza kuwa nao kwenye kazi unayoomba.
Hivi ndivyo vitu unavyotakiwa kujibu swali hilo:

Ongelea ujuzi na mafanikio yanayoendana na kazi unayoomba
Ni wazi kuwa hauwezi kufika kwenye swali hili ukiwa haujataja jina lako lakini kama ndiyo swali ulilolipata mara baada ya kuingia mlangoni, ni muhimu ukaanza na utambulisho ambao ni majina yako na elimu yako au cheo.
Tovuti ya masuala ya ajira, Resume Now imeeleza kuwa, ni muhimu kueleza historia yako kikazi na mambo uliyokuwa unajishughulisha nayo kabla ya kufika kwenye chumba hicho au eneo ulilofika.
Kama hauna, usijali. Unaweza kujitambulisha na kuelezea sifa ambazo zinaweza kukuongezea maksi kwa wanaokuhoji.
Ni muhimu kumsoma anayekuuliza maswali usoni kujua kama ni muda wa wewe kumaliza jibu lako au kama anahitaji kujua zaidi.
Usiwe mwenye stress. Tabasamu, jiamini na jieleze kimkakati. Picha| Mary Ellen Foundation.

Usiyafanye kuwa mazungumzo ya kuhusu wewe
Ni kweli umeulizwa swali linalokuhusu lakini swali hilo pia linahitaji kuambatana na maelezo ya namna gani utakuwa wa msaada kwenye kampuni ambayo unaomba kazi.
Kwa mujibu wa Programu ya masuala ya uongozi kwa wanawake ya She Lead, inashauriwa ujibu swali hili kwa ufupi lakin usisahau kuongelea mchango utakaoutoa kwenye kampuni hiyo endapo utaajiriwa.
Tovuti ya The Muse imetoa kanuni fupi ya kujibu swali hili ambayo ni “sasa + kale + yajayo”. Zungumzia unachokifanya kwa sasa na mafanikio uliyonayo, ongelea ya kale kwa kueleza wapi ulifanya kazi zamani na katika cheo gani na mwisho unachotarajia, kwanini unahitaji kazi hiyo na kwanini wewe na si wengine.

Usisahau shauku yako kwenye kazi hiyo
Kutaka kupata kazi ili upate mshahara ni jambo moja lakini kufanya kazi kwa sasabu ni kazi unayoipenda na unaiweza kuifanya hata ukishtushwa saa 10 za usiku ni jambo lingine.
Waajiri wanafahamu kuwa taaluma pekee haitoshi kukupatia nafasi ambayo unaiomba. Ni pamoja na ujuzi, uzoefu na shauku uliyonayo juu ya kazi hiyo.
Ni imani kuwa kama kazi una shauku nayo, mwajiri hatolazimika kutumia nguvu kukuelekeza na wewe kuifanya kwa weledi. 
Licha ya kutupia utaalamu wako, usisahau kuweka shauku yako na kazi hiyo ina maana gani kwako.
Mfano: “Ninaweza kufanya kazi nyingi. Kutengeneza magari, kuchezea programu za kompyuta na hata kujenga lakini ninapokaa na kufanya kazi ya utangazaji, huwa najiona kana kwamba ndilo kusudi la mimi kuwepo duniani. Maneno huja yenyewe na hata sielewi ni jinsi gani huwa nahamishia hisia kwenye ukurasa. Uandishi wa habari ni jambo ambalo ninafahamu kuwa nimeumbwa kufanya.”
Hakikisha muonenkano wa mara ya kwanza (first impression) unavutia. ni kupitia lugha, mavazi na unavyojibeba. Picha| Adobe Stock.

Usielezee wasifu (CV) wako
Baadhi huanza kutiririka yale yaliyopo kwenye wasifu wao bila kujua kuwa kabla ya wewe kuingia kwenye chumba hicho cha usaili, unaowakuta humo wameshapitia wasifu wako na wanachopima ni kingine.
The Muse inaeleza kuwa, kupata nafasi ya usaili ni nafasi ya waajiri kutaka kukujua zaidi na siyo uwaeleze kile ambacho tayari wanakijua.

Natumaini siku ukipata barua pepe ya kuitwa kwenda katika usaili, utapiga pamba zako safi, kiatu chako murua na utaingia katika chumba cha usaili kwa kujiamini na utaondoka chumba hicho jina lako likiwa limeandikwa kwenye karatasi ya mteule.