JESHI la Polisi mkoani Geita limewafikisha mahakamani watu watatu kutoka wilayani Nyang’hwale mkoani Geita kwa tuhuma za mauaji ya mwanafunzi wa chekechea aitwaye Dorcus Dotto, mwenye umri wa miaka saba.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Kamishina Msaidizi (ACP), Henry Mwaibambe ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari mjini Geita ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa mauaji hayo Juni 12 mwaka huu.
Amewataja watuhumiwa hao ni Sita Bujiku Msabila (52), ambaye ni mganga wa tiba asilia pamoja na Mathias Shilole (26) na Lucy Ndelema (75) ambao ni wakulima, wote ni wakazi wa kijiji cha Kilimani, Kata ya Ibambila wilayani Nyang’hwale.
“Siku ya Juni 12 mwaka huu majira ya mchana, Dorcus akiwa na mwenzake aitwaye Malemi Musa Adrian (miaka mitano), wanachunga mbuzi na dama alinyakuliwa na watuhumiwa Sita Bujiku Msabila na mwenzie Mathias Shilole.
“Kisha walimficha sehemu isiyojulikana na baadaye kumbaka, kumlawiti na kumvunja shingo yake baada ya kumuua waliuficha mwili wa marehemu kwenye shimo dogo lenye kina cha futi tatu.