MKAZI wa Kijiji cha Kapanga wilayani Tanganyika, Heleni Nyankole maarufu Beberu (36), anayedaiwa kuwa kinara wa kufanya mauaji ya kukodiwa ndani ya Mkoa wa Katavi na nje ya mkoa huo, ameuawa kwa kupigwa risasi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 11, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ally Hamad Makame, amesema mtuhumiwa huyo aliuawa usiku wa kuamkia jana Jumapili Julai 10, 2022, wakati akipambana na polisi.
Kamanda Makame amesema kuwa, Beberu anadaiwa kukodiwa kufanya mauaji ndani ya Mkoa wa Katavi na nje ya mkoa huo, alikuwa anatafutwa na polisi kwa muda mrefu kwa tuhuma hizo pamoja na za kukata mapanga watu maeneo tofauti.
Amesema Juni 28, 2022 usiku katika Kijiji cha Bukombe, mtuhumiwa huyo anadaiwa kumuua mkazi wa Kijiji cha Bukombe Tanganyika, Mandalu Ndulu (36) kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni.
Kamanda Makame amesema kuwa Beberu alikodiwa na watu wawili wakazi wa Kijiji cha Luhita-Bujombe kwa makubaliano ya kumlipa Sh 800,000, ili amuue Ndulu.
Amesema polisi baada ya kupata taarifa za tukio hilo, waliwakamata watuhumiwa hao wawili baada ya kuwahoji walikiri kumkodi mtuhumiwa huyo, ambapo walimpa kiasi cha shilingi 300,000 ikiwa ni malipo ya awali kisha kutekeleza mauaji hayo.
"Tulianza msako mkali Julai 7,2022 usiku, tulimkuta mtuhumiwa huyo wa mauaji Kijiji cha Lwega wilayani Tanganyika akiwa amelala ndani ya nyumba yake, polisi walipomuamuru kujisalimisha alikaidi," alisema ACP Makame na kuongeza:
"Alipanda juu ya dari, kisha kutoboa paa la nyumba iliyoezekwa kwa nyasi kwa kutumia panga, akiwa juu alijaribu kushuka, ghafla alishuka akiwa na kipande cha nondo kwa lengo la kumjeruhi askari.”
Kamanda Makame amesema kuwa askari walifyatua risasi hewani ili kumuonya, lakini alikaidi na kuendelea kuwafuata.
“Walifyatua nyingine ikamjeruhi tumboni, alipoteza maisha wakati anakimbizwa kituo cha afya,” ameeleza.
Imeandaliwa na Swaum Katambo, Katavi .