Wasilisho lililoandaliwa kwa ajili ya Maadhimisho ya BAKITA, Dodoma, 19-20/1/2021
M.M. Mulokozi
Profesa Mstaafu, TATAKI, Chuo Kikuu Dar es Salaam
Ikisiri
Ubepari ni mfumo wa uchumi wa soko. Katika mfumo huo, kitabu ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine kama sembe, nguo, kalamu, gari, n.k. Mwandishi wa kitabu ni mfanyakazi katika “kiwanda” cha kuzalisha bidhaa hiyo kama alivyo mwendesha mashine ya kufuma nguo katika kiwanda cha kutengeneza nguo. Kiwanda aghalabu huwa na mmiliki. Katika mfumo wa ujamaa, kwa kawaida mmiliki ni dola; katika mfumo, wa ubepari, kwa kawaida mmliki ni bepari (ambaye siku hizi anaitwa mwekezaji au mfanyabiashara binafsi). Mfanyakazi (mzalishaji) huajiriwa kwa ujira maalum ili azalishe bidhaa kiwandani, na hulipwa sehemu ndogo ya fedha zinazotokana na bidhaa aliyoizalisha; sehemu kubwa zaidi hubakia mikononi mwa mwajiri/mmiliki wa kiwanda. Katika tasnia ya uchapishaji wa vitabu, mchapishaji ndiye mmiliki wa “kiwanda” na “mwajiri” wa Mwandishi; huamua bidhaa gani izalishwe, lini, na kwa idadi gani, na humlipa mwandishi kiasi fulani (mrabaha) cha mapato yanayotokana na mauzo ya bidhaa hiyo (kitabu chake). Je, ni kwa kiasi gani “ajira” hiyo inamridhisha na kumnufaisha Mwandishi? Kama haimridhishi, nini kifanyike ili aweze kunufaika zaidi na matunda ya jasho lake? Hili ndilo suala kuu la wasilisho letu. Lengo la makala ni kuonesha kuwa ingawa hivi sasa uandishi wa vitabu nchini Tanzania, kwa Waandishi wengi, si ajira, shughuli hiyo huweza kuwa ajira endapo marekebisho ya kisera na kimtazamo yatafanyika ili kupanua soko la vitabu, hususani kwa kuichagiza sekta ya umma iweke utaratibu bora zaidi wa kununua na kusambaza vitabu vya ridhaa katika soko la shule na maktaba za umma. Utaratibu huo utamwezesha mwandishi kurejesha gharama za uandishi na kubakiwa na ziada, na hivyo kuubadilisha uandishi uwe ajira inayomwezesha kujikimu badala ya kuwa shughuli ya hiari tu ya kufanya “baada ya kazi muhimu” zinazompatia riziki. Ingawa wadau wa vitabu ni wengi, mjadala wetu utajikita kwa Mwandishi wa vitabu vya Kiswahili nchini Tanzania.
USULI
Katika makala tuliyoyawasilisha kwenye Kongamano la Arusha la BAKITA na TCDC mwaka 2018, tulitaja mambo yatuatayo kuwa msingi wa maendeleo ya uandishi na usomaji katika jamii yoyote ile. Mambo hayo ni:
Hali ya uchumi (ukwasi dhidi ya ufukara)
Mfumo wa elimu, pamoja na sera kuhusu lugha na usomaji
Kiwango cha kisomo kwa Umma
Kuwapo kwa lugha inayounganisha Taifa
Mambo haya bado ni ya msingi tunapojadili suala la uandishi kuwa ajira, japo hatukusudii kuyajadili tena hapa. Wasilisho hili fupi litajikita katika suala la uandishi kuwa fursa ya ajira, na namna ya kuliwezesha jambo hilo, na ni mwendelezo na ufafanuzi wa mapendekezo yetu tuliyoyatoa katika makala ya Arusha. Tutaanza kwa kueleza dhana ya uchapishaji, kisha tutaelezea hali ya tasnia ya uchapishaji wa vitabu nchini Tanzania, na katika sehemu ya mwisho tutapendekeza na kufafanua Mikakati ya kueneza vitabu na usomaji kwa Watanzania wote na kuwawezesha waandishi kunufaika na jasho lao.
DHANA YA UCHAPISHAJI
Uchapishaji ni mchakato wa uandaji, utoaji, ugharimiaji, utangazaji na usambazaji wa maandishi katika nakala nyingi ili yawafikie walengwa. Kutokana na maendeleo ya teknolojia, uchapishaji wa kisasa si lazima utoe nakala nyingi; unaweza ukafanywa pia kwa njia ya kidijitali mtandaoni.
HALI YA UCHAPISHAJI TANZANIA
Uchapishaji nchini Tanzania hivi leo ni wa aina tatu: Wa kibinafsi, kiserikali na kiasasi. Uchapishaji wa kiserikali na kiasasi hatutauzungumzia hapa kwa kuwa hautoi fursa ya ajira kwa Mwandishi anayejitegemea. Wachapishaji hai binafsi hivi sasa huenda hawazidi 15 (bila kuhusisha wachapishaji-waandishi ambao wanachapisha vitabu vyao wenyewe tu). Uchapishaji wa kibinafsi ni wa kibepari. Ubepari ni mfumo unaotegemea soko. Bidhaa hutengenezwa ili ziuzwe; pakiwa na soko kubwa la bidhaa fulani, bidhaa hiyo huzalishwa kwa wingi. Soko likipungua, bidhaa huzalishwa kidogo au haizalishwi kabisa. Katika muktadha wa vitabu, soko ni wasomaji. Kama hakuna wasomaji, na hakuna usomaji, uzalishaji wa vitabu utakuwa mdogo au hautakuwapo. Je, hali ya soko la vitabu (wasomaji) na usomaji ikoje nchi Tanzania?
Hali ya usomaji nchini Tanzania (na Afrika Mashariki kwa jumla) tumeijadili katika makala ya Arusha (Mulokozi 2018), hivyo hapa tutagusia tu mambo machache katika yale tuliyoyasema katika makala hayo (ambayo kwa kadiri ninavyofahamu, hayajachapishwa popote). Ili kurahisisha mjadala, tuvigawe vitabu vinavyochapishwa katika makundi makuu 2 (A na B):
KUNDI A
Vitabu vya kiada (vya shule na vyuo)
Vitabu vya ziada (vya shule na vyuo)
KUNDI B
Vitabu vya ridhaa (vya jumla, vya burudani, vya kujisomea kwa mapana)
Machapisho rasmi ya kiasasi (ya serikali, mashirika ya kijamii, mashirika ya dini, n.k.)
Kwa wakati huu, soko kubwa la vitabu vya Kundi A liko mashuleni na vyuoni; soko kubwa la vitabu vya Kundi B ni jamii pana, yaani watu binafsi pamoja na maktaba za umma. Kwa lugha rahisi, soko kubwa la vitabu vya Kundi A ni serikali. Hivyo maamuzi yoyote ya kisera au kivitendo ya serikali kuhusu kundi hilo la vitabu sharti yaathiri sekta nzima. Hii ni kwa kuwa tasnia ya vitabu Tanzania kwa sasa imejikita hapo (yumkini 90% ya biashara ya vitabu inahusu Kundi A). Ili kuibadilisha tasnia ya uchapishaji iwe chanzo cha ajira kwa wadau, sharti uwiano huu ubadilishwe: vitabu vya Kundi B vipewe fursa zaidi.
Kwa sera ya sasa, vitabu vya Kundi A vinadhibitiwa na serikali, kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) katika hatua zote kuanzia uandishi hadi utoaji, usambazaji na usomaji. Hivyo kwa kundi hili la machapisho suala la ajira kwa waandishi na biashara kwa wachapishaji halipo. Wadau wa vitabu wameilalamikia serikali kuhusu sera hii, lakini msimamo wa serikali haujabadilika. Hoja kuu ya wadau ni kwamba wakipewa fursa ya kushiriki katika utoaji wa vitabu vya Kundi A, ambavyo vina soko la hakika na vinaingiza mapato makubwa, ziada itakayopatikana itawawezesha kuchapisha na kusambaza vitabu vya Kundi B na hivyo kukuza usomaji. Serikali haijakubaliana nao labda kwa kuwa inaona ni nafuu zaidi kwa upande wa gharama kuandaa na kuchapisha vitabu hivyo yenyewe kupitia TET. Hoja yetu katika makala haya ni kwamba badala ya kung’ang’ania vitabu vya Kundi A, wachapishaji (isipokuwa TET) wajikite katika utoaji wa vitabu vya Kundi B ambavyo kwa hulka yake na wingi wake haviwezi kuandikwa na kutolewa na serikali peke yake.
Usomaji, ndani na nje ya shule na vyuo, na katika jamii pana, huendelezwa na hukuzwa na vitabu vya Kundi B (ambavyo kwa wakati huu nchini Tanzania huchapishwa kwa uchache sana, na mashuleni ni kama haviko kabisa). Kwa kuwa vitabu vya usomaji wa ridhaa vya kumvutia mtoto apende kusoma havipo, tunalea taifa la watoto wasiokuwa na tabia wala mazoea ya kusoma, na hivyo kuua juhudi za kuunda utamaduni wa usomaji, na hatimaye kuua elimu na soko la vitabu. Na soko la vitabu likiuliwa ni dhahiri kuwa hapatakuwa na “ajira” kwa waandishi na wachapishaji.
Takwimu za uchapishaji wa vitabu tulizozitoa mwaka 2018 bado zinatoa picha halisi ya hali ya uchapishaji na usomaji nchini kwa kulinganisha na mataifa mengine:
Jedwali Na. 1: Ulinganishi wa Uchapishaji Afrika na Sehemu nyingine Duniani (Mifano Teule)
NCHI
WAKAZI
MACHAPISHO
(MAPYA NA CHAPA MPYA)
UWIANO
UINGEREZA (UK)(2005)
68,000,000
206,000
1:330
UBELGIJI (1991)
12,000,000
13,913
1:863
MAREKANI (USA) (2010)
330,000,000
328,259
1:1005
KOREA KUSINI (2011)
52,000,000
44036
1:1181
ISRAEL (2006)
9,000,000
6866
1:1310
SWEDEN (2010)
10,000,000
4074
1:2455
CHINA (2013)
1,400,000,000
440,000
1:3181
CUBA (2003)
12,000,000
1488
1:8065
AFRIKA KUSINI (1995)
59,000,000
5418
1:10890
UGANDA (1996)
45,000,000
288
1:156250
KENYA (1994)
53,000,000
300
1:176667
BUKINI (MADAGASKA) (1996)
27,000,000
116
1:232959
TANZANIA (1990)
58,000,000
172
1:337209
MALI (1995)
20,000,000
14
1:1428571
Takwimu hizi, licha ya utata wake, zinadhihirisha kuwa kwa idadi ya watu tu Tanzania kuna uwezekano wa kuwa na soko kubwa la vitabu, lakini kiuhalisi hakuna soko kubwa na ndiyo maana vinachapishwa vitabu vichache mno. Hatuwezi kusema hakuna waandishi kwa sababu utafiti unaonesha kuwa waandishi wapo kwa wingi, na miswada mingi inaandikwa, lakini haichapishwi (Mulokozi 2018). Kwa kuwa hakuna soko, hata maduka ya vitabu hakuna au yanakufa.
Tukirejea kwenye dhana yetu ya awali kuwa katika mfumo tulio nao kitabu ni bidhaa, na kama hakiuziki hakiwezi kutoa ajira kwa wahusika, ni wazi kuwa mbinu za kuibadilisha hali hii lazima zianzie hapa kwenye suala la soko la vitabu.
MIKAKATI: NINI KIFANYIKE?
Vitabu vya Kundi A tayari vimewekewa ukiritimba wa dola hivyo haviwezi kutoa soko na ajira kwa wadau walio nje ya dola, ambao ndio tunaowalenga hapa. Hivyo soko la kutazama hapa ni lile la Kundi B, na mkazo sharti ukitwe hapo. Ili kukuza soko hilo, ni muhimu hatua zifuatazo zichukuliwe katika kuimarisha mitaala na maktaba shuleni; na kuimarisha na kuongeza maktaba za umma.
Mitaala na Maktaba za Shule
Yanahitajika mabadiliko ya kuhamasisha na kukuza usomaji katika mashule na vyuo; hili laweza kufanyika kwa kubadili mitaala ya elimu, hasa ya lugha, ili iweke mkazo zaidi katika kusoma kwa mapana (kwa ridhaa); na kuhakikisha kuwa kila mtoto wa shule ya msingi (kuanzia darasa la 3) anasoma kwa ridhaa angalao vitabu 30 kwa mwaka, na kila mwanafunzi wa sekondari anasoma angalao vitabu 50 kwa mwaka. Ili mkakati huu ufanikiwe, sharti serikali ihakikishe kuwa kila shule inakuwa na maktaba nzuri iliyosheheni vitabu na machapisho mengine ya ridhaa, hasa vitabu vya burudani kama riwaya, tamthilia na mashairi, vitabu vya maarifa, magazeti na magazini. Ili mkakati huu ufanikiwe, inabidi serikali ikubali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya maktaba za shule kila mwaka. Kimahesabu, kwa shule 10000 tu, kama serikali itanunua nakala mbilimbili za kila kitabu kinachofaa kinachochapishwa nchini, kwa ajili ya shule 10000 tu kila mwaka, na kama vinachapishwa vitabu 200, na kila kitabu kinauzwa kwa bei ya Sh. 10000/= tu, itahitajika bajeti ya 10000x200x20000 = 40,000,000,000 (sh. bilioni 40) kwa mwaka. Bajeti hii ndogo, mbali na kuwa chanzo cha ajira kwa waandishi na wachapishaji, inaweza kuibadilisha jamii ya Watanzania na kuifanya iwe jamii ya wasomaji badala ya wasemaji tu.
Kisomo na Elimu ya Kujiendeleza na Maktaba za Umma
Ili kukuza soko la vitabu, inatubidi kuhamasisha na kukuza usomaji katika jamii (nje ya shule). Mkakati huu sharti uambatane na:
a) Kueneza kisomo (literacy) na elimu ya kujiendeleza kwa watu wazima;
b) Kuimarisha na kupanua mfumo wa maktaba za umma. Suala la kisomo na elimu ya watu wazima halina mjadala, na linafahamika vizuri nchini Tanzania, nchi ambayo miaka ya 1970-1990 ilifanikiwa kufuta ujinga kwa zaidi ya 70% . Hapa tutajikita zaidi katika kipengele cha maktaba za umma.
Maktaba za Umma
Maktaba za Umma (Tanzania Bara) husimamiwa na kuratibiwa na Shirika la Huduma za Maktaba (TLS). Kutokana na uwekezaji mdogo, idadi ya maktaba za umma haijaongezeka tangu miaka ya 1970. Kwa hakika imepungua, kwani wakati huo kulikuwa na maktaba za vijiji ambazo leo hazipo tena. Hivi sasa (2018) kuna maktaba 21 za mkoa na 18 za wilaya nchini kote (Tanzania Bara). Wilaya zilizofikiwa ni asilimia kama 20 tu. Hivyo, ni sahihi kusema kuwa ukosefu wa maktaba za umma ni janga la kitaifa linalochangia katika kuua kisomo na kudumisha ujinga, na hatimaye kuua soko la vitabu na ajira kwa wadau, wakiwamo waandishi na wakutubi. Ni wazi kuwa, ili kukuza na kudumisha usomaji nchini Tanzania, uwekezaji katika huduma za maktaba ulioanza miaka ya 1960 na baadaye kufifia inabidi ufufuliwe, na mpango wa kuwa na maktaba kila wilaya utekelezwe. Na maktaba si majengo tu, ni vitabu. Mkakati tunaoupendekeza ni kama ule wa uimarishaji wa maktaba katika mashule. Hivyo, kimahesabu itahitajika bajeti ya takriban Sh. Bilioni 8 kama ifuatavyo:
-Tuseme, kama kielelezo tu, kuwa Tanzania – Bara na Zanzibar - ina maktaba za umma 200 (zikiwamo za wilaya, mikoa na nyinginezo).
-Kama nakala 10 tu za kila kitabu cha ridhaa kinachochapishwa Tanzania zitapelekwa katika kila maktaba ya wilaya/mkoa, na kama vitachapishwa vitabu tofauti 200 kila mwaka, zitanunuliwa nakala 2000 za kila kitabu. Kama bei ya kila kitabu ni Sh. 20,000/=, itahitajika bajeti ya Sh 20000x2000x200 = 8,000,000,000 tu (sawa na sh. bi. 8). Ingawa hizi zinaonekana kuwa fedha kidogo, lakini taathira yake kwa tasnia ya vitabu itakuwa kubwa. Hii ni kwa kuwa kwa wachapishaji wetu wengi ambao ni wadogo, zikinunuliwa kwa mpigo nakala 2000 za kila kitabu wanachotoa, wataweza kurejesha gharama zao za uzalishaji, kumlipa mwandishi mrabaha, na kubakiza ziada kidogo ili kuwekeza zaidi. Muhimu zaidi, vitabu vipya kama 200 vitakuwa vinachapishwa kila mwaka, na hivyo kuongeza idadi ya vitabu vya kujisomea vilivyopo na kuhuisha tasnia ya uchapishaji. Utaratibu huu sijaubuni mimi, unatumika (au ulikuwa ukitumika) katika baadhi ya nchi zenye wakazi wachache na hivyo idadi ndogo ya wanunuaji wa vitabu, kwa mfano nchi za Skandinavia. Utaratibu unaofanana na huu ulitumika pia katika Mradi wa Vitabu vya Watoto (CBP).
Kuimarisha mfumo wa maktaba za shule na vyuo, na mfumo wa maktaba za umma, ni njia nzuri na mwafaka ya kuhuisha tasnia ya uchapishaji na kuhakikisha kwamba vitabu vinaendelea kutolewa na waandishi na wachapishaji wanaendelea kuwa katika ajira, hata kama si kutajirika. Mikakati hii miwili inahusu mchango wa wananchi kwa pamoja kupitia dola au serikali yao; uhamasishaji huu ukifanikiwa hatimaye utasisimua na kupanua soko la wanunuzi binafsi ambao wamejengewa tabia ya usomaji, na hivyo kupanua soko la vitabu.
Soko la Kawaida: Maduka na Maktaba za Kidijitali
Maduka ya vitabu huibuka na kufa kutegemea mwelekeo wa upepo wa kisera. Sera ya ukiritimba wa dola kwa vitabu vya Kundi A ilipolegezwa miaka ya 1990 maduka mengi ya vitabu yalianzishwa. Sera ya ukiritimba iliporejeshwa maduka mengi yakafa. Hii ni kwa kuwa maduka hayo yalitegemea sana soko la shule. Upanuzi wa utoaji wa vitabu vya Kundi B tunaoupendekeza hatimaye utasaidia kufufua maduka ya vitabu, maana vitabu hivyo havitolewi na serikali bali makampuni binafsi na asasi nyinginezo.
Maktaba na maduka ya kidijitali ni jambo jipya na geni kwa Tanzania, lakini linashika kasi na baada ya muda si mrefu litakuwa jambo la kawaida. Kizazi kipya cha vijana tayari kimo katika ulimwengu wa kidijitali na kinatamani kupata maarifa, burudani, taarifa na vitabu kwa njia hiyo kwa kuwa ni sahili kiuzalishaji na kiusambazaji, na ni ya gharama nafuu. Wizara zinazohusika, shule, vyuo na asasi mbalimbali zingeweka mkazo katika eneo hili. Hii ni pamoja na kuhamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya kuunda au kuunganisha baadhi ya vifaa vya kidijitali kama vile simu “janja”, ipad na laptop. Kudijitisha taifa la watu milioni 60 kutahitaji viwanda vya aina hiyo, vinginevyo tutakuwa tunafanya mzaha tu.
Gharama za Mwandishi
Watu wengi wanapozungumzia gharama za uchapishaji humfikiria mchapishaji na labda mchapaji na muuza vitabu, lakini ni nadra sana kumfikiria mwandishi. Utadhani mwandishi ni mashine ya roboti inayofyatua mistari tu bila gharama yoyote (ingawa hata roboti inahitaji nishati ya umeme). Lakini Mwandishi ndiye chimbuko la tasnia ya uchapishaji, maana, tutake tusitake, bila yeye hakuna kitabu. Kwa kurahisisha, gharama za mwandishi tunaweza kuzikadiria, kwa kiwango cha chini kabisa, kama ifuatavyo:
Kitabu X kurasa 200 (riwaya).
Utafiti miezi 6: 300000x6 = 1,800,000: Utafiti huu unafanyika katika maisha halisi – mashambani, vijijini, mitaani, sehemu za starehe, sehemu za ibada, fukweni, baharini, viwandani, n.k. kulingana na matakwa ya riwaya inayoandikwa. Tumekadiria gharama za chini za Sh. 10000/= tu kwa siku kwa miezi 6.
Uandishi wa mswada, rasimu ya 1, kurasa 5 kwa siku, siku 40 mafichoni= sh. 50000 kwa siku = 2,000,000
Uandishi wa mswada, rasimu ya 2, kurasa 10 kwa siku mafichoni,Sh. 50000 = 1,000,000
Uhariri na upitiaji, na msaada wa watu wengine: 10000/ukurasa = 2,000,000
Uchapaji na usanifu 3000/ukurasa = 600,000
Mengineyo (simu, karatasi, pepe, umeme, kalamu): 300,000
JUMLA: 7,700,000
Gharama za Mwandishi za kuandaa kitabu hicho hadi kiwe mswada unaofaa kukabidhi kwa Mchapishaji ni Sh. Mi. 7.7. Ili Mwandishi arejeshe gharama hizo kutokana na mrabaha wa 10% ya bei, na kama kitabu chake kinauzwa kwa bei ya Sh. 20000/=, itabidi ziuzwe nakala 3850. Mrabaha huo wa kwanza utakuwa ni wa kurudisha gharama alizozitumia tu, si mapato. Mapato yataanza kuonekana baada ya kuuza idadi hiyo ya nakala. Kama Mwandishi haendi mafichoni na hafanyi utafiti ulio dhahiri, bado gharama zitakuwapo ila zitajificha katika gharama za kawaida za kuishi wakati wa kuandika, pamoja na muda anaoutumia kufanya kazi hiyo badala yakufanya kazi nyingine ya kumpatia kipato; gharama yake haipaswi kuwa chini ya Sh. 10000/= kwa saa.
Kama kitabu kitanunuliwa nakala 2 kwa kila shule kwa ajili ya maktaba za shule 10000 kwa mpango uliopendekezwa hapo juu kwa ajili ya usomaji wa ridhaa, zitanunuliwa nakala 20000 ambazo zitampatia Mwandishi mrabaha wa Sh. Mi. 40 kama ifuatavyo:
20000x20000 = 400,000,000/10 = 40,000,000.
Kodi ya serikali: 15% = 6,000,000
Baki: 34,000,000/=
Hivyo kama Mwandishi hatatapeliwa, atalipwa Sh. 34,000,000/= baada ya kukatwa kodi. Hiki si kipato kidogo kwa Mtanzania wa kawaida wa leo. Kwa Mwandishi huyu uandishi utakuwa ni ajira ya kutosha, maana atakuwa anapata wastani wa Sh. 2,833,333/= kwa mwezi. Kama kitabu kitaendelea kuuzwa miaka inayofuata, mapato ya Mwandishi yataongezeka kulingana na ongezeko la mauzo. Bila shaka Mchapishaji atapata zaidi, na ataweza kutoa ajira kwa wahariri, wachoraji na wasanifu; lakini hayo ni mahesabu tofauti na hayatuhusu hapa. Ni wazi kuwa kwa Mwandishi huyu uandishi unaweza kuwa ajira endapo ataandika angalao kitabu kimoja kila mwaka.
Hakishiriki na Hakiambatani
Mapato mengine anayoweza kuyapata mwandishi ni yale yanayotokana na hakishiriki na hakiambatani za hakimiliki yake.
Hakishiriki (neighboring rights) ni zile haki zinazoshirikisha watu wengine, kwa mfano wimbo hutungwa na mtunzi na kuimbwa na mtu mwingine (mwimbaji), na wote wawili wana haki fulani katika wimbo huo. Halikadhalika, tamthilia huweza hutungwa na mtu tofauti na wale wanaoiigiza. Haki ambatani (subsidiary rights) ni haki za nyongeza, kwa mfano za tafsiri, utoaji katika matoleo au maumbo maalumu, k.m. toleo lililofupishwa, toleo kwa ajili ya klabu ya usomaji, tafsiri, toleo kwa ajili ya soko maalum kijiografia, n.k. Haki hizi pia hufafanuliwa katika mkataba kati ya Mwandishi na Mchapishaji. Katika mikataba mingi mapato ya haki ambatani hugawanywa kwa uwiano wa 50-50 kati ya Mwandishi na Mchapishaji; mikataba mingine humpa Mwandishi haki zaidi – hadi 80%.
Katika nchi zilizoendelea, mapato haya wakati mwingine huzidi mrabaha. Kwa mfano, riwaya za watu kama Ian Fleming (James Bond) zinapotengenezwa filamu waandishi hulipwa mamilioni ya dola. Katika Tanzania, ni waandishi wachache wanaolipwa haki hizi, hata kama kazi zao zimetumika kwa njia hiyo. Hili ni suala linalohitaji kushughulikiwa kisheria kati ya vyama vya waandishi na maprodyuza wa aina nyinginezo za sanaa zinazotumia kazi za waandishi hao.
HITIMISHO
Wasilisho hili limejadili suala la uandishi (na uchapishaji) kama chanzo cha ajira kwa waandishi wa Kiswahili na wadau wengine. Tumeonesha kuwa kwa wakati huu tasnia hiyo haijawa chanzo cha ajira kwa waandishi wengi kwa sababu mapato ya Mwandishi ni kidogo kuliko gharama anazozitumia. Tumependekeza namna bora ya kuufanya uandishi uwe ajira kwa kupanua soko la vitabu, kueneza usomaji mashuleni na katika maktaba za umma, na kuweka utaratibu wa serikali kununua idadi fulani ya vitabu vya ridhaa ili kukidhi soko hilo. Tukifanya hivyo tutapanua soko la vitabu vya ridhaa na hatimaye kujenga taifa la wasomaji ambao watakuwa soko la kudumu la vitabu vya aina zote.
MAREJELEO TEULE
Altbach, P and Teferra, D (eds) 1999 Publishing in African Languages: Problems and Possibilities. Bellagio Publishing Network, Boston.
Bgoya, W (2017) “Publishers, Authors and Africa’s Cultural Development: Do
the African intelligentsia and the African States care?” http://www.readafricanbooks.com/ opinions/publishers-authors-and-africa-s-cultural-development], imesomwa 5/9/2019.
Gibbs, J and J. Mapanje (eds) 1999 The African Writers Handbook. ABC, Oxford.
Hirji, K (2019) Under-education in Africa: From Colonialism to Neo-Liberalism. Montreal (Canada): Daraja Press.
Mcharazo, A and A. Olden (2016) “Fifty years of Tanzania’s national/public library service” accessed at https://journals.sagepub.com/doi/abs/10.1177/095574901664910725 on September 5, 2019,
Mlambo, A (2007) African Scholarly Publishing Essays.ABC Collective, Oxford.
Mcharazo, A and A. Olden (2016) “Fifty Years of Tanzania's National/Public Library Service”
https://journals.sagepub.com/doi/abs/10.1177/095574901664910725 May 2016 (imechapishwa pia katika jarida la Alexandria: the Journal of national and International Library and Informattion Issues. Kur. 136-144. Imesomwa 3/9/2019.
Mulokozi, M.M (1999) “The Experience of Being a Writer in Tanzania,” in Gibbs and Mapanje, which see: pp. 22-27.
Mulokozi, M.M (1999) “Publishing Kiswahili Books – A Writer's Perspective,” in Altbach, P and Teferra, D (eds) Publishing in African Languages: Problems and Possibilities. Bellagio Publishing Network, Boston, pp. 11-42.
Mulokozi, M.M and Sengo, T.Y.S 1995 History of Kiswahili Poetry A.D. 100-2000. Dar es Salaam: TUKI.
Mulokozi, M.M (2018) “Kiswahili na Uandishi, Uchapishaji na Usomaji Katika Afrika Mashariki” makala yaliyowasilisha katika Kongamano la BAKITA na TCDC, Arusha,………,
Tanzania (1997) Sera ya Utamaduni (Cultural Policy). Ministry Responsible for Culture, Dar es Salaam.
Tanzania (1999) Copyright and Neighbouring Rights (No. 7) Act (with Ammendments titled Written Laws (Miscellaneous Amendments) No. 3 Bill of 2019, and raising the fines for infringement of copyright from 5,000,000 to 20-30,000,000). Dar es Salaam: Government Printer.
UNESCO (1999) Statistical Yearbook 1999
Zell, Hans (2014) “How many Books are Published in Africa? The Need for More Reliable Statistics.” The African Book publishing Record Vol. 40, No. 1
VIFUPISHO
CBO: Children’s Book Organization (jina jipya la CBP)
CBP: Children’s Book Project(sawa na CBO)
EABDA: East African Book Development Association
EALB: East African Literature Bureau
EAPH: East African Publishing House
FEMRITE: Uganda Women Writers Asociation
TATAKI: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (zamani TUKI)
TEHAMA: Teknolojia ya habari na Mawasiliano
TLS(B): Tanzania Library Services (Board)
TPH: Tanzania Publishing House
TUKI: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Institute of Kiswahili Research)
UKUTA: Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania
UWAVITA: Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (Tanzania Writers Association)