Sephania Mungasyeghe Kyungu
sepahaniakyungu06@gmail.com
+225 624 373 371
Ikisiri
Makala hii ililenga kuchunguza mchango wa wasanii wa Bongo Fleva katika kutandawazisha Kiswahili, kwa kujikita kwa Diamond Platnumz. Hali hii ilichochewa na ukweli kwamba wasanii wa Bongo Fleva wana mchango mkubwa katika kutandawazisha Kiswahili, huku makundi mengine yakiwa; wasanii wa ushairi andishi, tamthiliya, riwaya na kadhalika. Hata hivyo, wasanii waliokuwa wameangaziwa zaidi na wataalamu katika kutandawazisha Kiswahili ni wasanii wa kazi andishi kama vile; ushairi andishi, tamthiliya na riwaya, ilhali wasanii wa Bongo Fleva walikuwa hawajaangaziwa. Hivyo, lengo mahususi la makala haya lilikuwa ni kuchunguza mchango wa wasanii wa Bongo Fleva katika kutandawazisha Kiswahili kwa kujikita kwa Diamond Platnumz ili kuziba pengo la maarifa lililokuwepo. Nadharia uliyoongoza uchambuzi wa data ni Nadharia ya Ushawishi wa Kijamii ya Friedkin (1998). Data za utafiti huu zilipatikana kwa njia ya mtandao wa Youtube ambapo mtafiti alichambua nyimbo mbalimbali za Diamond Platnumz na zile alizoshirikishwa ili kubaini mchango wake katika kutandawazisha Kiswahili. Imebainika kuwa Diambond Platnumz ana mchango mkubwa katika kutandawazisha Kiswahili ikiwa ni pamoja na kutumia lugha ya Kiswahili katika nyimbo zake, kutumia lugha ya Kiswahili katika nyimbo alizoshirikishwa na kuwafundisha Kiswahili wasanii wenzake.
1.0 Utangulizi
Kutandawazisha Kiswahili ni kitendo cha kukifanya Kiswahili kuvuka eneo la mwambao wa Afrika Mashariki kimatumizi. Hii ni kwa sababu eneo la mwambao wa Afrika Mashariki ndiyo eneo asili la lugha ya Kiswahili (taz. Chiraghdin na Mnyampala, 1977; Choge, 2008). Kiswahili ni lugha iliyo na majukumu mengi ndani na nje ya Afrika (Chabet-choge, 2020). Maelezo haya yanadokeza kwamba Kiswahili kimevuka mipaka ya eneo la mwambao wa Afrika Mashariki kimatumizi. Kwa kuwa nje ya eneo la Afrika Mashariki kuna lugha zingine ambazo zilikuwa zinatumika kabla ya Kiswahili kuanza kutumika ni wazi kwamba kuna juhudi za ushawishi zimefanyika kuhusu matumizi ya Kiswahili. Miongoni mwa watu muhimu katika mchakato huu wa kukitandawazisha Kiswahili ni wasanii. Makala hii imelenga kundi hilo la wadau kwa kujikita hasa kwa wasanii wa Bongo Fleva huku mjadala ukiegemezwa zaidi kwa Diamond Platnumz. Mjadala umeongozwa na Nadharia ya Ushawishi wa Kijamii Friedkin (1998). Makala hii imeanza kwa kueleza dhana ya ushawishi kwa kuwarejelea wataalamu anuwai miongoni mwa wale waliozungumzia dhana hiyo. Sehemu ya pili imeangazia ushawishi alionao Diamond Platnumz katika jamii. Sehemu ya tatu imeeleza methodolojia ya utafiti huu. Sehemu ya nne inatoa maelezo ya mchango wa Diamond Platnumz katika kutandawazisha Kiswahili. Mwisho, makala hii imetoa hitimisho.
2.0 Ushawishi katika Jamii
Ushawishi ni kuathiri matendo ya wengine kwa kuwabembeleza (Mayhew, 1997). Hii ina maana kwamba ni kuathiri matendo ya watu wengine bila kutumia nguvu, vitisho au ahadi ya malipo. Uwezo wa kuathiri matendo ya watu wengine aghalabu hutegemea hadhi, uwezo, mali na nafasi ya mtu katika jamii. Kimsingi maelezo haya yanamaanisha kwamba matendo ya watu wenye hadhi, uwezo, mali na nafasi yana athari kwa watu wengine katika jamii. Naye Friedkin (1998) mwanasaikolojia jamii, anasema kando na tofauti zilizozoeleka kama jinsi, dini, kazi au taaluma binadamu hutofautiana kwa nafasi ama nyadhifa zao katika jamii. Katika muundo jamii ni kawaida kuwapo na tofauti mbalimbali. Kutokana na tofauti zilizopo katika muundo jamii, wanajamii huathiriana. Kuna wakati wanakubaliana na mtu fulani katika jamii na kuna wakati hawakubaliani. Hivyo, katika mtagusano wa watu katika nafasi tofauti za jamii, kuna mchakato wa kuathiriana na kushawishiana inayoibuka. Ni kawaida katika jamii watu kubadilisha ama kuchukua mielekeo ya wengine ambao wanahusiana kwa namna moja ama nyingine. Kupitia maelezo ya Friedkin yanatusaidia kumaizi kwamba katika jamii kuna hali ya kushawishi na kushawishiana. Aidha, Friedkin anaongeza kuwa ni kawaida watu katika jamii kubadili mielekeo na maoni ili kukubaliana na watu wanaowachukulia kuwa ni muhimu kwao. Katika mazingira kama haya suala la ushawishi wa watu muhimu katika jamii linakuwa la msingi. Kwa sababu huchangia mabadiliko ya misimamo tabia, hisia na mielekeo ya watu wengi kuhusu mambo kadhaa.
Kulingana na Nadharia ya Ushawishi wa Kijamii ya Friedkin inasema lazima tutambue mchango wa mtu binafsi katika mchakato wa ushawishi. Hii ni kwa sababu kila mhusika au wahusika wana maoni na msimamo wao kama kundi kuhusu jambo fulani. Maelezo haya yana maana kwamba mtu binafsi anaweza kuwashawishi watu wa jamii fulani waliokuwa na maoni, tabia, hisia au mielekeo fulani. Pia, Friedkin anataja misingi mitatu ya mtu mmoja kushawishi wengine ambayo ni: Mshikamano, ufanano na umuhimu.
Katika mazingira ambamo wahusika wana mshikamano, kuna mahusiano ya mara kwa mara kuna uwezekano mkubwa wa kuathiriana. Katika mazingira kama haya si ajabu kumsikia Y akisema mimi ni kama X. Kwa hiyo, nitaamini na kutenda kama X ama nataka kuwa kama X, na nitakuwa kama X na kuamini afanyacho X. Aidha, Friedkin akirejelea maoni ya Deurkheim, 1933; Dahrendarf, 1959 na Hechter, 1987, kuhusu msingi wa tatu, anasema wahusika wanaochukuliwa kuwa muhimu katika kundi wana nafasi kubwa zaidi ya kuwashawishi wenzao ukilinganisha na wanaochukuliwa kuwa wana umuhimu mdogo. Mawazo ya Friedkin kuhusu nafasi ya watu muhimu katika kushawishi wengine yanaungwa mkono na (Goldsmith, 2015). Wasanii wa Bongo Fleva ni miongoni mwa watu wenye umuhimu katika jamii. Katika kundi la wasanii kuna wenye umuhimu mkubwa na wenye umuhimu mdogo. Miongoni mwa wasanii wenye umuhimu mkubwa katika muziki wa Bongo Fleva ni Diamond Platnumz. Ni katika mazingira kama haya makala hii ililenga kuchunguza mchango wake katika kutandawazisha Kiswahili.
3.0 Athari za Diamond Platnumz katika Jamii
Wasanii wa Bongo Fleva wana athari na ushawishi mkubwa sana katika jamii. Ushawishi huu umetokana na nafasi ya nyimbo wanazoimba katika jamii ikiwa ni pamoja na kuburudisha, kuelimisha, kuhamasisha, kuunganisha jamii na kadhalika. Miongoni mwa wasanii wa Bongo Fleva wenye ushawishi mkubwa ndani ya Afrika Mashariki na nje ya Afrika Mashariki ni Diamond Platnumz.
Tarehe 2/10/1989 majira ya saa 11 za jioni katika hospitali ya Amana Jijini Dar es Salaam ndiyo siku aliyozaliwa Diamond Platnumz. Alizaliwa katika familia duni ya Nassibu Salum Idd Nyange na wazazi wakampa jina Nassibu wakiamini ni jina la bahati, na cheti chake kikaandikwa kwa jina la Nassibu Abdul Juma. Kwa hiyo, jina la Diamond Platnumz ni lakabu (jina ambalo mtu hujipa au kupewa kwa sababu fulani).
Jina la Diamond Platnumz limeanza kusikia kwa wengi mwaka 2010 baada ya kutoa wimbo wa Nenda Kamwambie ambao uligusa Watanzania wengi, hasa waliokuwa wanasumbuliwa na wapenzi wao. Ubunifu wake katika utunzi na ladha yake mpya katika muziki wa Bongo Fleva ikawa ndiyo ufunguo wa kupokelewa vyema na watu mbalimbali ndani ya nchi na hata nje. Kupitia wimbo wa Nenda Kamwambie alifanikiwa kupata tuzo tatu kwenye Tuzo za Muziki Tanzania, baadaye Diamond Platnumz alitoa albamu yake ya kwanza aliyoiita Kamwambie kama jina la wimbo wake. Tangu hapo Diamond Platnumz amejizolea umaarufu mkubwa kimataifa hasa barani Afrika, na hivyo kuwa na athari kubwa kwa wasanii wengine nchini Tanzania. Wimbo uliofahamisha zaidi kimataifa ni wimbo wa Number One (2013) ambao korasi yake imeimbwa kwa Kiingereza (Reuster-Jahn, 2014). Wimbo wa Number One ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika na kumfanya Diamond Platnumz kutajwa kuwania tuzo kadhaa za kifahari za muziki mwaka 2014 kama vile The MTV Africa Music Award na The MTV Europe Music Award na kushinda tuzo ya Channel O Music Video Award. Mwaka 2014 pia alifanikiwa kutoa remix ya wimbo wa Number One Remix ambao alimshirikisha Davido nyota wa Nigeria. Wimbo huu ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika katika nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Kameruni, Nigeria na kadhalika.
Kwa mujibu wa Jarida la Billboard mwaka (2020) Diamond Platnumz alivunja rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara kufikisha watazamaji bilioni moja kwenye mtandao wa Youtube. Pia, amevunja rekodi ya kuwa msanii wa kwanza barani Afrika kufikisha watazamaji milioni mbili kwa masaa 13. Kwa sasa Diamond Platnumz anatamba na EP yake inayofahamika kwa jina la First of All (FOA) ambayo inaendelea kupata umaarufu sehemu mbalimbali ulimwenguni. Maelezo haya kuhusu msanii Diamond Platnumz yanaonesha namna msanii huyu alivyo na nafasi kubwa ndani ya Afrika na nje.
Suala la ushawishi wa msanii huyu limeonekana kutumiwa na wafanyabiashara anuwai wakimuonesha Diamond Platnumz akitumia huduma na bidhaa zao. Kwa mfano, mtandao wa Airtel, Pepsi, Itel, Sabuni ya Nice One, Rangi aina ya Coral Paints, Airtel na kadhalika. Pia, Chama cha Mapinduzi (CCM) kilitumia nafasi aliyonayo Diamond Platnumz kushawishi wapiiga kura katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Pia, wana michezo kama vile Simba Sports Club walimtumia Diamond Platnumz kuwashawishi mashabiki kuhudhuria Siku ya Simba maarufu kama Simba Day mwaka 2020.
Kwa ujumla historia ya Diamond Platnumz japo kuwa imeelezwa kwa kifupi inaonesha nafasi aliyonayo Tanzania, Afrika Mashariki, bara la Afrika na nje ya Afrika. Je, kulingana na nafasi ya Diamond Platnumz aliyonayo anatandawazisha Kiswahili? Swali hili linashughulikiwa katika sehemu inayofuata baada ya methodolojia ya utafiti.
4.0 Methodolojia ya Utafiti
Mtafiti alipitia kazi anuwai za Diamond Platnumz na kueleza mchango wa kazi hizo katika kutandawazisha Kiswahili nje ya Afrika Mashariki ambapo ndipo asili yake. Mtafiti alipata kazi hizo kupitia mtandao wa YouTube. Kazi zilizochambuliwa kuonesha mchango wa Diamond Platnumz katika kutandawazisha Kiswahili ni zile ambazo zilipata kuwania tuzo mbalimbali za nje ya Afrika Mashariki, kazi ambazo ameshirikisha wasanii wa nje ya Afrika Mashariki na kazi ambazo ameshirikishwa na wasanii wa nje ya Afrika Mashariki.
5.0 Mchango wa Diamond Platnumz katika Kutandawazisha Kiswahili
Imeelezwa katika kipengele cha 3.0 kwamba wafanyabiashara, wanamichezo na wanasiasa wametambua nguvu ya Diamond Platnumz katika ushawishi. Kwa hivyo, wanamtumia katika mambo kadhaa kushawishi jamii kulingana na vile watakavyo. Hii inadokeza kwamba kulingana na nafasi ya Diamond Platnumz kila analolifanya lina nguvu ya kushawishi jamii kubadili mwelekeo. Sehemu hii, inajibu swali ambalo mtafiti alikuwa anajiuliza ambalo ni; je Diamond Platnumz kulingana na nafasi yake Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika kwa ujumla na nje ya Afrika ana mchango wowote katika kutandawazisha Kiswahili? Swali hili linajibiwa katika sehemu hii kwa kuongozwa na Nadharia ya Ushawishi wa Kijamii.
5.1 Kutumia Lugha ya Kiswahili katika Nyimbo Zake
Diamond Platnumz ana kawaida ya kutumia lugha ya Kiswahili katika nyimbo zake nyingi. Mathalani, katika wimbo wa Number One (2013) ambao ulipata umaarufu barani Afrika, na kuwania tuzo mbalimbali za kifahari kama MTV Africa Music Award na MTV Europe Music Award na kushinda Tuzo ya Channel O Music Video Award umetumia lugha ya Kiswahili (Reuster-Jahn, 2014). Rejea ubeti ufuatao katika wimbo wa Number One:
Kwanza mapenzi safari,
Ujana ni maji ya moto walinenaga zamani,
Pili tumetoka mbali kwa matatizo,
Changamoto tu visa visa fulani,
Tatu kidonda changu kwako maradhi,
Ma tu usononekapo kwangu simanzi,
Kwa mahaba uliyonipa nimenogewa,
Vurugu patashika ahh punguza kidogo,
Na mengine kadhalika mtoto si unanielewa,
Hapo hapo uliposhika,
Ukiongeza kidogoo! mmmh mwenzako ntaumia.
Kadhalika, katika wimbo wa Number One Remix (2014) ambao Diamond Platnumz alimshirikisha Davido, msanii maarufu kutoka nchini Nigeria alitumia lugha ya Kiswahili. Wimbo wa Number One Remix nao ulipata umaarufu katika nchi mbalimbali za Afrika kama vile Ghana, Nigeria, Afrika Kusini na kadhalika. Kulingana na African Muzik Award, wimbo wa Number One Remix ulitajwa kuwania Tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka (Best Song of the Year) mwaka 2015. Tazama matumizi ya lugha ya Kiswahili katika wimbo wa Number One Remix, Diamond Platnumz anaimba hivi:
Tatu kidonda changu kwako maradhi,
Ma tu usononekapo kwangu simanzi,
Kwa mahaba uliyonipa nimenogewa,
Vurugu patashika ahh punguza kidogo,
Na mengine kadhalika mtoto si unanielewa,
Hapo hapo uliposhika,
Ukiongeza kidogoo! mmmh mwenzako ntaumia.
Pia, Diamond Platnumz katika wimbo wa Ntampata Wapi (2014) ametumia lugha ya Kiswahili katika wimbo mzima. Katika wimbo wa Ntampata Wapi anaimba:
Sura yake mtaratibu,
Mwenye macho ya aibu,
Kumsahau najaribu,
Ila namkumbuka sanaa.
Wimbo huu wa Ntampata Wapi ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika na kufanikiwa kuwania Tuzo ya Wimbo Bora (Best Song of the Year) Mwaka 2015.
Vilevile, katika wimbo wa Marry You (2017) ambao Diamond Platnumz alimshirikisha Ne-Yo ametumia lugha ya Kiswahili. Katika wimbo wa Marry You Diamond Platnumz anasema:
Oooh! baby,
Hadithi hadithi utamu kolea,
Oooh! baby,
Leo najihisi hamu kuongea,
Yaliyo ndani ya mtima,
Nikueleze how i feel.
Wimbo wa Marry You ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika na kushinda tuzo ya Wimbo Bora wa Afrika (Best Song of the Year) mwaka 2018 katika Tuzo za Muziki wa Hip Hop.
Vilevile, katika wimbo wa Inama (2018) ambao Diamond Platnumz amemshirikisha Fally Ipupa ametumia lugha ya Kiswahili. Katika beti alizoimba Diamond Platnumz ametumia lugha ya Kiswahili kama inavyooneshwa katika ubeti ufuatao:
Kukudekeza kama mtoto,
Furaha nafurahia,
Unapogeuka moto,
Machozi unalia.
Wimbo huu wa Diamond Platnumz aliomshirikisha Fally Ipupa ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika. Kutokana na umaarufu huo, wimbo wa Inama ulipata fursa ya kuwania tuzo mbalimbali za AFRIMA kama vile Wimbo Bora wa Mwaka (Song of the Year), Wimbo Bora wa Kushirikisha (Best Collaboration) na video bora ya AFRIMMA (AFRIMMA Video of the Year) kwa mwaka 2019.
Pia, katika wimbo wa Waah! (2020) ambao Diamond Platnumz alimshirikisha Koffi Olomide ametumia lugha ya Kiswahili. Katika wimbo wa Waah! Diamond Platnumz anaimba hivi:
Anachukua anaweka,
Waah!
Anachukua anaweka,
Waah!
Anachukua anaweka,
Waah!
Wimbo wa Waah! ulipata umaarufu mkubwa barani Afrika. Umarufu wa wimbo huu pia ulisaidia wimbo huu kuwania Tuzo za Muziki wa Afrika katika nafasi Video Bora ya Bara (Best African Video) mwaka 2021. Pia, kutokana na umaarufu wimbo wa Waah! zimetolewa Lyrics ambazo zimetafsiriwa katika lugha anuwai ilmradi watu waelewe kulingana na umaarufu wake.
Kwa ujumla, matumizi ya Kiswahili katika nyimbo zilizobainihswa hapo juu kama vile Number Number One, Number One Remix, Ntampata Wapi, Inama na Waah! ambazo zimepata umaarufu mkubwa nje ya Afrika Mashariki yamesaidia kutandawazisha Kiswahili. Kwa sababu kulingana na nafasi ya Diamond Platnumz katika bara la Afrika kila anachotumia au kukifanya kina athari na ushawishi. Kwa hiyo, kitendo cha Diamond Platnumz kutumia Kiswahili katika nyimbo zake pamoja na umaarufu wake barani Afrika unasaidia kukitangaza Kiswahili kimataifa zaidi. Hii ni kwa sababu ni kawaida watu kupenda kujinasibisha na watu maarufu kwa vitendo.
5.2 Kutumia Lugha ya Kiswahili kwenye Nyimbo Alizoshirikishwa
Diamond Platnumz amekuwa balozi mzuri wa lugha ya Kiswahili nje ya Afrika. Hii inajidhihirisha kupitia nyimbo alizoshirikishwa na wasanii ambao hawatoki Afrika Mashariki na hawakijui Kiswahili. Sehemu hii inabainisha baadhi ya nyimbo ambazo Diamond Platnumz ameshirikishwa na wasanii kutoka nje ya Afrika Mashariki. Kwa mfano, Diamond Platnumz katika wimbo wa Time to Party (2018) alioshirikishwa na Flavour msanii nyota kutoka nchini Nigeria ametumia lugha ya Kiswahili. Rejea beti zifuatazo ambapo Flavour ameimba kwa lugha yake na Diamond Platnumz ameimba kwa Kiswahili:
No time to check time,
Every body shekelebe,
Shekere,
Oya mama eh eh shekere,
Oya sister eeh eeh shekere.
(Flavour)
Mayoyo (oh ma) changu cha ngama,
Moyoyo, (oh ma) wasije kudanganya.
(Diamond Platnumz)
Katika wimbo huo licha ya kwamba Diamond Platnumz ameshirikishwa, bado haachi kuwa balozi wa lugha ya Kiswahili. Kitendo cha Diamond Platnumz kutumia lugha ya Kiswahili katika wimbo wa Flavour ambaye ni msanii kutoka Nigeria kinasaidia kukitandawazisha Kiswahili katika nchi hiyo. Hii ni kwa sababu Flavour ni msanii maarufu nchini Nigeria na kitendo cha kumruhusu Diamond Platnumz atumie Kiswahili katika wimbo wake inaongeza ushawishi juu ya kujifunza Kiswahili.
Pia, katika wimbo wa Watora Mari (2016) ambao Diamond Platnumz ameshirikishwa na Jah Prayzah ameimba kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Ingawa katika wimbo huo kuna sehemu Diamond Platnumz ameimba kwa kutumia lugha anayotumia Jah Prayzah, kwa kiwango kikubwa ametumia lugha ya Kiswahili. Rejea beti za zifuatazo kwa ufafanuzi zaidi.
Ah darlie, kudhadhanuka kunge dhandi,
Zuma,
Inini handichagone, usaome moyo kunge nyanji,
Zuma,
Inini handichagone, usaome moyo kunge njanji”
(Jah Prayzah)
Eh siku hizi kidigitali unapata ambacho unakiona,
Yanini hospitali wakati kwako napona,
Mapenzi si surauli useme ikichanwa nitaishona
Hivyo, chonde tafadhali usiniekee miba ikanichoma
Wakaja wa magari
(Waiteke)
Na nyumba za kifahari
(Waiteke)
Wakalamba asali ah wakaniacha doro
Ah we paja me kidali
(Unitekee)
Chips kachumbari
(Uniteke)
Wanini sa ugali, sijazoea viporo
(Diamond Platnumz)
Wimbo huu wa Watora Mari katika akaunti ya Youtube ya Jah Prayzah ndio unaongoza kuwa na watazamaji wengi. Hii ina maana lugha ya Kiswahili iliyotumika katika nyimbo hiyo na Diamond Platnumz imesambaa kupitia wimbo huo nchini Zimbabwe na maeneo mengine yaliyotazama video hiyo.
Kwa ujumla nyimbo nyingi ambazo Diamond Platnumz ameshirikishwa hata kama ametumia lugha nyingine kama vile Kiingereza hakuacha kutumia lugha ya Kiswahili. Hii inaonesha Diamond Platnumz amaekuwa balozi mzuri wa Kiswahili kimataifa katika kutandawazisha lugha ya Kiswahili. Jambo hili ni la mfano kwa watu wengine wenye nafasi kutumia fursa hiyo katika kutandawazisha lugha ya Kiswahili barani Afrika na nje.
5.3 Kuwafundisha Kiswahili Wasanii Wenzake
Diamond Platnumz amekuwa akiwafundisha wasanii anuwai lugha ya Kiswahili pindi anapoimba nao ili kuleta vionjo kwenye wimbo. Mathalani, katika wimbo wa Number One Remix (2014) wa Diamond Platnumz ambao alimshirikisha Davido kutoka Nigeria alimfundisha Davido aimbe baadhi ya mishororo kwa Kiswahili. Katika wimbo wa Number One Remix Davido anasema:
Your body de shake, my money de wait for you baby,
No time de waste, make you go de place,
For real, oh sweety,
Tupate ubaridi kidogo,
(Lets get a little refreshment)
Kwa mama ukale ugali wa mhogo,
(And you can eat ugali made from cassava flour at my mothers place)
Baby we can do it your way,
Anything you want it’s okay,
Tanzania to Lagos, i go make you famous,
Even if they mad at us.
Katika beti hii ambayo anaimba Davido katika wimbo wa Number One Remix, kuna mishororo inaimbwa kwa Kiswahili ambayo ni Tupate ubaridi kidogo na kwa mama ukale ugali wa mwogo. Kwa mujibu wa Reuster-Jahn (2014) anasema Kiswahili alichotumia Davido katika mistari hiyo alifundishwa akiwa studio. Kitendo cha Diamond Platnumz kumfundisha Kiswahili Davido kinachangia kutandawazisha Kiswahili. Kwa sababu baada ya Davido kutoka Studio na kurudi kwao atakuwa amejifunza lugha ya Kiswahili. Matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa wasanii wasiojua Kiswahili katika nyimbo za Diamond Platnumz ni ishara kwamba huwa anawafundisha wakiwa studio.
Pia, Ne-Yo kutoka Marekani katika wimbo wa Marry You (2017) anatumia Kiswahili katika beti la kwanza mshororo wa mwisho. Wimbo wa Marry You ni wa Diamond Platnumz ambao amemshirikisha Ne-Yo. Kwa hiyo, kitendo cha Ne-Yo ambaye hajui Kiswahili lakini tunaona kwenye wimbo huo alitumia lugha hiyo ni ishara kwamba alifundishwa na Diamond Platnumz. Ne-Yo katika wimbo wa Marry You anaimba hivi:
When i look at you,
I see the ever very air breath,
I see the sun girl how you shine on me,
Niko mzima kwa sababu ya wewe tu.
(Im grown up because of you)
Katika mshororo wa mwisho Ne-Yo anatumia lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha anayoitumia. Hii inaonesha kwamba Diamond Platnumz alimfundisha Ne-Yo Kiswahili wakiwa studio. Kitendo cha kufundisha Kiswahili kwa wasanii wa kigeni kunachangia kutandawazisha Kiswahili.
Matumizi ya Kiswahili kwa wasanii wageni walioshirikishwa na Diamond Platnumz yanajitokeza pia kwenye wimbo wa Iyo (2021). Katika wimbo huo Focalistics kutoka Afrika Kusini anaimba baadhi ya mishororo kwa Kiswahili. Katika wimbo wa Iyo Focalistic anaimba hivi:
We kijana mdogo,
We kijana mdogo,
Ke tla ho bontsha spokko.
We kijana mdogo,
We kijana mdogo,
Kijana mdogo,
Kijana mdogo.
Katika mfano huo, unaonesha Focalistic anaimba baadhi ya mishororo kadhaa kwa Kiswahili. Mishororo hiyo ambayo Focalistic aliimba kwa Kiswahili hapana shaka alifundishwa na Diamond Platnumz ili kuongeza vionjo kwenye wimbo wake. Kitendo cha kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wasanii anaowashirikisha kunachangia kutandawazisha Kiswahili.
6.0 Hitimisho
Makala hii imeshughulikia mchango wa wasanii wa Bongo Fleva katika kutandawazisha Kiswahili kwa kujikita kwa Diamond Platnumz. Sehemu ya kwanza ya makala hii imeeleza dhana ya ushawishi ambapo imeelezwa kwamba katika maisha yetu ya kila siku watu wenye nafasi kubwa katika jamii wana nafasi kubwa ya kuwaathiri na kushawishi wengine kuhusu mambo anuwai. Imeelezwa kwamba wasanii ni miongoni mwa watu wenye nafasi kubwa katika jamii, hivyo wana nafasi kubwa ya kuathiri na kushawishi watu wengine kuhusu mambo mbalimbali. Miongoni mwa wasanii wa muziki wa Bongo Fleva wenye nafasi kubwa ni Diamond Platnumz. Imeelezwa kwamba sekta zingine kama vile michezo, siasa, biashara na kadhalika zimetambua nafasi ya msanii huyu katika ushawishi kwa watu wengine. Hivyo, makala hii ililenga kushughulikia mchango wake katika kutandawazisha Kiswahili kulingana na nafasi yake. Imebainika kwamba Diamond Platnumz anachangia kwa kiasi kikubwa kutandawazisha Kiswahili. Mchango wa Diamond Platnumz katika kutandawazisha Kiswahili ni pamoja na kutumia lugha ya Kiswahili kwenye nyimbo zake, kutumia lugha ya Kiswahili kwenye nyimbo alizoshirikishwa na kuwafundisha Kiswahili wasanii wenzake.
Marejeleo
Chebet-choge, S. (2020) “Uenezi wa Kiswahili baada ya Uhuru wa Afrika Mashariki kwa Mtazamo wa Nadharia ya Mfumo Changamano. Kioo cha Lugha, Juz. 18: 1-21.
Chiraghdin, S. na Mnyampala, M. (1977) Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.
Chobe, S.C. (2008) Role of [a] in Swahili. Research in African Language & Lingusitics, Juz. 8: 19-43.
Friedkin, N.E. (1998) A Structural Theory of Social Influence. Cambridge: Cambridge University Press.
Goldsmith, E.B. (2015) Social Influence Sustainable Consumption. New York: Springer Publishers.
Mayhew, L.H. (1997) The New Public Professional Communications and the Means of Social Influence. Cambridge: Cambridge University Press.
Reuster-Jahn, U. (2014) “English Versus Swahili: Language Choice in Bongo Fleva as Expression of Cultural and Economic Changes in Tanzania. Swahili Forum, Juz. 21: 1-25.
Diskografia
Diamond Platnumz. (2013) Number One. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamond Platnumz na Davido. (2014) Number One Remix. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamond Platnumz. (2014) Ntampata wapi. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamond Platnumz. (2017) Marry You. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamnond Platnumz na Fally Ipupa. (2018) Inama. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamond Platnumz na Koffi Olomide. (2020) Waah! Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Diamond Platnumz na Focalistic, Mapara, A Jazz na Ntosh Gazz. (2021) Iyo. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).
Flavour na Diamond Platnumz. (2018) Time to Party. Dar es Salaam: Ma-ma-mastercraft on the Beat Wasafi.
Jah Prayzah na Diamond Platnumz. (2016) Watora Mari. Dar es Salaam: Wasafi Classic Baby (WCB).

0 Comments