Monday

Mhalifu wa mtandaoni akamatwa Tanzania

0 comments

 

Thabo Bester, ni raia wa Afrika Kusini aliyekuwa akisakwa kwa udi na uvumba kutokana na tuhuma nzito za ubakaji, wizi na mauaji, alizozifanya na baadaye kutoroka gerezani alikokuwa akitumikia kifungo cha maisha, huku watu wote wakiamini kwamba amekufa.

Taarifa mpya ni kwamba, mtuhumiwa huyo amekamatwa na Jeshi la Polisi nchini Tanzania na sasa taratibu za kumrudisha nyumbani kwao, Afrika Kusini kwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea huku ikielezwa kwamba amekamatiwa jijini Arusha.

Taarifa za kipolisi, zinaeleza kwamba Thabo alikuwa na mchezo wa kuwatongoza wanawake Facebook, akiwaahidi kuwatafutia kazi au kuwaunganisha na kampuni za kimataifa za mitindo na kuishia kuwabaka na kuwaibia huku wengine akiwaua.

Ni tuhuma hizo ndizo zilizosababisha akakamatwa nchini Afrika Kusini na baada ya kukutwa na hatia, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani katika Gereza la Hloko jijini Bloemfontein, Mei 2022.

Hata hivyo, katika mazingira yaliyojawa na utata, ilikuja kuelezwa kwamba jamaa huyo amefia gerezani baada ya moto mkubwa kuzuka kwenye gereza hilo ukianzia kwenye selo aliyokuwa amefungwa.

Uchunguzi wa kidaktari, ukaonesha kwamba mwili uliokutwa kwenye selo hilo,ukiwa umeungua vibaya na moto, haukuwa wa Thabo, utata mkubwa ukaibuka.

Siku zikawa zinasonga mbele na baadaye, zikaanza tetesi za kuonekana kwa Thabo mitaani, akiwa amejibadilisha mwonekano na tetesi hizo zimefikia ukomo baada ya jamaa kukamatwa na makachero wa polisi nchini Tanzania.

Thabo amekamatwa akiwa sambamba na mwanamke aliyetambulika kwa jina la Dk. Nandipa Magumana ambaye ni mpenzi wake, anayetajwa kwamba ndiye aliyefanikisha mchezo wa kumtorosha gerezani.

No comments:

Post a Comment