Chimbuko ni istilahi yenye maana ya kitu fulani kilipoanzia. Ni dhahiri kuwa kuna mijadala ya wataalamu mbalimbali inayozungumzia chimbuko la lugha ya Kiswahili.
Baadhi ya wataalamu hao ni pamoja na Chami (1994), Massamba na wenzake (1992 mpaka 1996), Freeman Granville (1959) na wengineo. Ifuatayo ni mitazamo yao kukusu chimbuko la lugha ya Kiswahili.
Chami (1994), Massamba na wenzake (1992 hadi (1996) wanasema utafiti uliofanywa na wataalamu wanaosema kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni Kingozi kizungumzwacho Kenya na Kishomvu kizungumzwacho maeneo ya Bagamoyo na Dar es Salaam hauna mashiko, hivyo basi litakuwa ni jambo la busara kama watafanyia upya utafiti wao.
Nae Freeman Granville (1959) Katika kitabu chake alichokiita "The Medieval of Kiswahili Language" anasema Kilwa hata kabla ya karne ya 10 ilikuwa na umuhimu mkubwa kibiashara, hivyo basi kulingana na umuhimu huo wa kibiashara miongoni mwa Wabantu wa Kilwa na wageni (Waarabu) ilipelekea kuibuka kwa lugha moja ambayo ndiyo inasadikika ni Kiswahili cha leo.
Wapo wataalamu wengine wanaosema kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni huko Afrika ya Magharibi (Kamerun). Wao wanaseme kuwa kwa kuwa Afrika ya Magharibi ndiko chimbuko la Wabantu wa mwanzo yawezekana ndiko Kiswahili kilipoanzia.
Pia wataalamu wengine wanasema chimbuko la lugha ya Kiswahili ni huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hawa wanasema baada ya wale Wabantu wa mwanzo kutoka Afrika Magharibi kukaa kwa muda mrefu katika misitu minene ya Kongo walianza kutawanyika kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutafuta maeneo yenye uoto wa asili, hivyo walijikuta wakitokea kingo za Uganda na Kigoma hadi kufikia Ziwa Viktoria walikaa hapo kwa muda mrefu hadi walipoamua kuondoka maeneo hayo na kuelekea katika mabonde yenye rutuba ya mto Tana katika visiwa vya Shupate na Shungwaya.
Baadae mwaka 1999 Massamba na wenzake wakaja na kusema kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni upwa wa pwani ya Afrika Mashariki. Wao wanamalizia kwa kusema kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni matokeo ya muingiliano wa muda mrefu kati ya Wabantu waliokuwa wakizungumza lugha zao za asili (Kibantu). Hivyo basi ni ukweli kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili ni pwani ya Afrika Mashariki.
Hivyo, kuhusu asili ya lugha hiyo kuna nadharia mbalimbali, kama vile:
- Kiswahili ni Kikongo,
- Kiswahili ni Pijini au Krioli,
- Kiswahili ni Kiarabu,
- Kiswahili ni lugha ya vizalia, pamoja na
- Kiswahili ni Kibantu