KATEREGGE: NIKICHEZA NA OKWI, KICHUYA, WATAKOMA
NA SAADA SALIM
MKENYA Allan Kateregge amesema iwapo atatua Simba na kufanikiwa kucheza pamoja na Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya, wapinzani wao watakiona cha moto msimu ujao.
Kateregge yupo katika rada za Simba ambapo klabu hiyo inaonekana kupania kumnasa kiungo huyo tayari kuwatumikia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF).
Akizungumza na masshele blog jijini Dar es Salaam juzi baada ya fainali ya michuano ya Sportpesa, Kateregge alikiri kutakiwa na Simba akisema iwapo atafanikiwa kusajiliwa na timu hiyo, atafurahi mno.
Alisema kinachomvutia kutua Simba ni kutokana na umaarufu wa timu hiyo, lakini pia kuvutiwa kwake na wachezaji wa Wekundu wa Msimbazi hao kama Kichuya na Okwi.
Alisema amekuwa akiifuatilia sana ligi ya Tanzania kupitia vyanzo mbalimbali na kuvutiwa na uwezo wa Kichuya na kikosi cha Simba kwa ujumla, hali iliyomfanya mara kadhaa kuwauliza rafiki zake, Okwi na Paul Kiongera waliopita Msimbazi juu ya timu hiyo.
“Mara ya mwisho nimeongea na Okwi na kunieleza anakuja kucheza Simba, nafahamu uwezo wake tangu tulipokuwa SC Villa kabla sijakwenda Kenya kusajiliwa na Tusker na sasa AFC Leopards.
“Simba wakipeleka ofa yao kwa meneja wangu na mazungumzo kwenda vizuri, naamini ushirikiano wangu, Kichuya na Okwi, itakuwa ni balaa,” alisema.
Aliongeza: “Ukiachilia Okwi niliyecheza naye klabu moja, pia tulikuwa pamoja na kikosi cha Uganda, akiwamo Jjuuko Murushid ambaye bado yupo katika kikosi cha Simba, hivyo haitakuwa tabu kwangu kuzoeana na wenzangu kupitia hawa jamaa (Okwi na Murushid).”
Masshele blog lilimtafuta wakala wa mchezaji huyo, Alicia Nickols, anayeishi nchini Marekani, ambapo alisema kwa upande wake anazisikia tu taarifa hizo kwamba kuna klabu Tanzania zinamhitaji mteja wake.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Marekani, Alicia alisema amezungumza na mteja wake ambaye amempa taarifa hizo hivyo kwa sasa anasubiri barua ya maandishi kutoka Simba.
“Hatuwezi kuzungumza chochote kwani sijapata taarifa yoyote ya maandishi kutoka klabu hiyo, wala nyingine ya Tanzania. Pia kuna klabu nyingine za nje zinamhitaji Allan,” alisema.
Juu ya dau la mchezaji wake huyo, Alicia alisema hawezi kuweka wazi hilo mpaka hapo atakapopokea ofa kutoka Simba au klabu nyingine yoyote.