Saturday

HADIDHI YA KINYAKYUSA , WATOTO WA KYUSA NA NAMNA MWANAMKE ANAVYO SAWIRIKA KATIKA HADIDHI

0 comments



MWANDISHI WA HADIDHI NA MAKALA HII

 MWAMSIKU JOCELYNE RICHARD 

                                 

              WATOTO WA KYUSA
Hapo kale katika mji wa Morogoro wilaya ya Kilombero, alipata kuwapo mwanamke mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina ka Kyusa. Mwanamke huyu alipata umaarufu kutokana na moyo wake wa ukarimu ambao alijaaliwa na Muumba pamoja na kipaji chake cha kutengeneza dawa za kienyeji zilizokuwa zikitibu magonjwa mbalimbali. Alitengeneza dawa hizo kwa kutumia majani na mizizi ya miti mbalimbali. Si hivyo tu lakini pia mwanamke huyu alikuwa mzuri wa sura na maumbile, mambo ambayo kwa ujumla yalimuongezea umaarufu. Pamoja na mambo yote mazuri ambayo Kyusa alijaaliwa, kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuolewa.  Katika kipindi cha kuwapo kwa Kyusa kulikuwa na shughuli za uhamiaji toka sehemu moja kwenda nyingine kwa lengo la kutafuta mahali ambapo pangefaa kwa shughuli mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji nakadhalika. Jamii za watu mbalimbali kutoka Morogoro zilifanya misafara yao kupitia Kilombero kijiji ambacho kimepakana na mji wa Iringa ulioko nyanda za juu kusini. Jamii ya kwanza kufanya msafara ilikuwa ni jamii ya wapogoro wanaopatikana eneo la Ifakara, katika msafara wao walifika katika kijiji alichokuwa akishi Kyusa na kwa bahati nzuri walifika nyumbani kwa Kyusa. Kutokana na ukarimu aliokuwa nao Kyusa aliwapokea wageni wale vizuri kwa kuwapa chakula, vinywaji na mahali pa kupumzika. Wageni wale walistaajabu kukutana na mwanamke ambaye aliweza kuwapokea vizuri kwani walikuwa hawafahamiani. Wageni wale walimshukuru sana Kyusa na kisha kuendelea na safari yao kuelekea Mbeya. Sifa za Kyusa zilienea mahala pote ikawa kila msafara uliokuwa ukielekea Mbeya ulifikia kwa Kyusa kwa ajili ya kupumzika na kujionea aina hiyo ya mwanamke aliye pata kujaaliwa moyo wa upendo na ukarimu kwa kiasi kikubwa. Wageni hao pia hawakwenda mikono mitupu, walibeba zawadi kedekede kwa ajili ya Kyusa. Na Kyusa naye hakuwaacha wageni waondoke hivihivi bali aliwafungashia chakula cha kutosha, maji na dawa mbalimbali za kienyeji alizokuwa akitengeneza mwenyewe ili wasitaabike kwa njaa, kiu na maradhi wakiwa njiani. 
Pamoja na mambo mengi mema aliyojaaliwa Kyusa, kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuolewa. Lakini alibahatika kupata watoto ambao alizaa na baadhi ya wanaume aliokuwa akiwapokea kutoka sehemu mbalimbali. Kutokana na uzuri aliokuwa nao wanaume wengi walimtamani na waliishia kuzaa naye tu paipo kumoua. Kyusa aliwalea watoto wake katika maadili mema na kuhakikisha kuwa wanaipendeza jamii, ingawa baadhi ya watoto wake walipokua wakubwa waliondoka kwa baba zao. Misafara ile kuelekea Mbeya ikiwamo wake kwa waume pamoja na watoto walipendezwa na tabia ya Kyusa ya ukarimu na upendo, na waliamua kuungana na kuwa kitu kimoja  hata kufikia hatua ya kujiita “bhana bha Kyusa” yaani “watoto wa Kyusa”. Na ndiyo maana hadi leo kuna kabila la Wanyakyusa linalopatikana mkoani Mbeya. Kabila hili asili yake ni mwanamke Kyusa ambaye alifanyika kama daraja la kuunganisha jamii mbalimbali na kuunda jamii moja yenye nguvu.  Wanyakyusa humuenzi kutokana na ukarimu na upendo aliowatendea walipokuwa katika misafara yao. Pia kuna sehemu katika mji wa Kilombero unaitwa “kwa Kyusa”, inaaminika kuwa mwanamke huyo alipata kuishi maeneo hayo.


Baada ya uandishi wa hadithi inayohusu asili ya kabila la Wanyakyusa, yafuatayo ni maelezo yanayoonesha mwanamke ni nani na  kwa namna gani hadithi hiyo imemsawiri mwanamke katika Nyanja mbalimbali. Kwa kuanza na dhana ya mwanamke kama ilivyofasiliwa na wataalamu mbalimbali.
Wamitila (2016) anafasili dhana ya mwanamke kama mtu mwenye uwezo wa kujifungua, yaani ni mtu wa jinsi ya kike. Nao TUKI (2004) wanamfaili mwanamke kama binadamu mwenye jinsia ya uke, nbeu ya kike ya binadamu. Wanaendelea kueleza kuwa binadamu huyu mwenye jinsia ya kike hushika ujauzito na kuweza kuzaa. Lakini pia katika mtazamo mwingine TUKI (Ishatajwa) wanaeleza kuwa mwanamke ni kiumbe anayekaa na mwanaume bila ya kuoana. Mfano “Asha ni mwanamke wa Juma”. Tukizichunguza fasili hizi mbili inaonesha ni kuwa mwanamke amepewa sifa kuu mbili ambazo ni kuwa na jinsia ya kike, na pili ni suala la kuweza kujifungua. Lakini TUKI wameongeza maelezo ya ziada kuwa mwanamke ni mtu mwenye jinsia ya kike anayekaa na mwanaume bila ya kuoana. Dai hili linaibua mjadala katika kumpambanua mwanamke, Je? yule mwenye jinsi ya kike, anauwezo wa kujifungua na ameolewa, yeye ataitwa nani?. Na yule mwenye jinsi ya kike ila hawezi kushika ujauzito ni nani. Hivyo tunaweza kufasili dhana ya mwanamke kama mtu mwenye jinsi ya kike, na anatofauti kubwa kimaumbile na mwanaume.
  
MWANAMKE ANAVYO SAWIRIKA KATIKA HADIDHI HII.


Mosi, mwanamke ameonekana kama chombo cha starehe. Balisidya (1982) anasema, ukandamizaji wa mwanamke na mwanaume unategemea sana uhusiano wao wa kimapenzi. Anaendelea kueleza kuwa kazi nyingi za fasihi humchora mwanamke kama mlezi, kiumbe dhaifu na chombo cha starehe. Naye Samwel (2010) anaeleza kuwa karibu asilimia 90 ya nyimbo za bongo flea zina dhamira ya mapenzi kati ya mwanamke na mwanaume, na mwanamke huonekana kama kiumbe anayependa sana fedha na anasa na hivyo hutumiwa na wanaume kama chombo cha starehe, yaani kumburudisha na kumfurahisha mwanaume. Katika hadithi hii inaoneshwa kuwa mwanamke Kyusa alikuwa ni mwanamke mwenye mvuto ambaye wanaume wengi walimtamani kimapenzi, jambo ambalo lilimfanya aonekane  kama  chombo starehe kwa aijili ya kuwaburudisha baadhi ya wanaume waliokuwja wakifanya misafara yao kuelekea Mbeya. Aya ya pili (2) mstari wa kwanza
                     “alibahatika kupata watoto ambao alizaa na baadhi ya wanaume
                          aliokuwa akiwapokea kutoka sehemu mbalimbali.”
Vilevile katika hadithi hii mwanamke amesawiriwa kama mlezi wa familia na jamii kwa ujumla. Momanyi (2001) anasema kuwa jukumu la malezi ni la wazazi wote wawili (baba na mama). Lakini kutokana na mfumo dume mama ndiye aliyeachiwa jukumu hili, huku baba akijishughulisha na uzalishaji mali. Akinukuliwa na Kimaro (2016), Omari (2008) anaeleza kuwa mwanamke katika jamii anachorwa kama mtu muhimu katika kurithisha maadili toka kizazi kimoja hadi kingine. Anafafanua zaidi kuwa kwa kuwa mama ndiye anayeshinda nyumbani kwa muda mrefu, basi ananafasi kubwa katika malezi ya watoto na jamii kwa ujumla. Ni kweli kuwa katika jamii nyingi hasa za waswahili mwanamke ndiye aliyepewa jukumu kubwa katika kuhakikisha familia na jamii inapata malezi bora Tukiichunguza hadithi hii inaonekana kuwa kiasi kikubwa mwanamke Kyusa amechorwa kama mlezi wa familia pamoja na jamii. Alihakikisha wageni waliokuwa katika misafara ya kutafuta makazi wanapata malezi bora. Aya ya pili mstari wa 4
                               “Kyusa aliwalea watoto wake katika maadili mema na kuhakikisha
                                  kuwa wanaipendeza jamii”             
Pia mwanamke amesawiriwa kama chemchem ama asili ya jamii fulani. Katika hadithi hii inaoneshwa kuwa asili ya kabila la wanyakyusa ni kutokana na uwapo wa mwanamke Kyusa, mwamamke ambaye ana mchango mkubwa katika uanzishwaji wa kabila la Wanyakyusa.
                            “Misafara ile kuelekea Mbeya ikiwamo wake kwa waume 
                                 pamoja na watoto walipendezwa na tabia ya Kyusa 
                                 ya ukarimu na upendo, na waliamua kuungana n
                                 kuwa kitu kimoja  hata kufikia hatua ya kujiita
                              “bhana bha Kyusa” yaani “watoto wa Kyusa”. 
                                 Na ndiyo maana hadi leo kuna kabila la 
                                Wanyakyusa.
Lakini pia katika hadithi hii inaoneshwa kuwa suala la ndoa kwa mwanamke ni la lazima, na  endapo mwanamke wa Kiafrika asipoolewa huonekana kama ana mkosi katika jamii yake Suala hili la ndoa linachukuliwa katika mitazamo tofauti ndani jamii. Kuna wataalamu ambao huona ndoa kama jambo linalomgandamiza mwanamke, lakini pia wapo wataalamu ambao wanasisitiza ndoa kama falsafa ya Kiafrika. Temples (1945) anasema kuwa katika maisha ya waafrika suala la ndoa ni la msingi katika kudumisha na kuendeleza uhai. Katika mtazamo mwingine  tofauti naye  Wamitila (2002) anaiona ndoa kama asasi ya kitamaduni inayoendeleza ukandamizwaji wa mwanamke. Imejengwa katika msingi wa itikadi ya uwezo alionao mwanaume na mwanamke akichukuliwa kama chombo tu. Jamii pia ina ona kuwa suala la kuolewa kwa mwanamke ni lazima, na inaonekana kama ni mkosi kukosa mume. Mwanamke Kyusa anaonekana kuwa na kasoro kutokana na kukosa mume na kuishia kuzalishwa na wanaume tofauti, kama inavyothibitishwa katika aya ya pili mstari wa 1
                         “Pamoja na mambo mengi mema aliyojaaliwa Kyusa, kwa bahati
                             mbaya hakufanikiwa kuolewa. Lakini alibahatika kupata watoto
                             ambao alizaa na baadhi ya wanaume aliokuwa akiwapokea kutoka
                             sehemu mbalimbali”
Fauka na hayo mwanamke pia amesawiriwa kama kiumbe mwenye upendo na ukarimu, Inaoneshwa katika hadithi kuwa Kyusa alijipatia umaarufu kutokana na moyo wenye upendo na ukarimu kwa watu aliokuwa akiwafahamu na hata wale aliokuwa hawafahamu. Kitendo cha Kyusa kuwapokea watu waliokuwa wakitafuta makazi kwa kuwapa makazi na chakula, ni jambo linalodhihirisha kuwa mwanamke huyu alijawa upendo, ukarimu na huruma kwa jamii. Suala hili la ukarimu linaonekana katika kazi nyingine ya fasihi ambayo ni riwaya ya Bwana Myombekere na Bi Bugonoka iliyoandikwa na Kitereza (1980). Bugonoka ni mwanamke ambaye ana upendo kwa mumewe na kwa jamii pia, anaoneshwa kuwakirmu watu wa jamii yake kwa kuwapikia chakula, kuwapa malazi nakadhalika. Ni dhahiri kuwa wanawake wengi wanamioyo ya ukarimu ndani ya jamii kama anavyosawiriwa Kyusa ndani ya hadithi hii, aya ya kwanza mstari wa 
                              “kutokana na ukarimu aliokuwa nao Kyusa aliwapokea wageni wale
                                 vizuri kwa kuwapa chakula, vinywaji na mahali pa kupumzika”.
Mwanamke kama mfumbuzi wa tiba mbalimbali, katika hadithi hii Kyusa amechorwa kama mwanamke anayejishughulisha na utengenezaji wa dawa za kienyeji ambazo zilitumika kuwatibu watu aliokuwa akiishi nao ndani ya jamii yake na hata wale ambao walikuwa wakifanya misafara na kuweka kituo nyumbani kwake. Dawa hizo zilimsaidia kuingiza kipato kwa kiasi kikubwa kwani ndiyo shughuli ya kiuchumi aliyokuwa akiifanya
                                  “na kipaji chake cha kutengeneza dawa za kienyeji zilizokuwa
                                   zikitibu magonjwa mbalimbali. Alitengeneza dawa hizo kwa
                                   kutumia majani na mizizi ya miti mbalimbali”.
Kwa ujumla mwanamke amaechorwa katika sura mbalimbali katika kazi nyingi za fasihi, na kwa kiasi kikubwa ameonekana kubebeshwa majukumu makubwa kama vile uzazi na ulezi wa familia yake na jamii kwa ujumla. Lakini hadithi hii kwa kiasi kikubwa imeonesha mambo chanya kwa mwanamke na kwa kiasi kidogo imegusia masuala hasi upande wa mwanamke. Kutokana na ugandamizaji ambao mwanamke amekuwa akiupata ndani ya jamii baadhi ya wanawake ambao wamefanikiwa kuliona suala hili katika mtazamo hasi wameweza kuanzisha harakati za kumkomboa mwanamke. Hivyo jamii kwa ujumla iungane kupiga vita ugandamizwaji kwa wanawake.



                                                                      MAREJELEO
Balisidya, M. L (1982). The Image of the Women in Tanzania Oral Literature. Katika Kiswahili
                         Juz. Na 49/2, Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi Kiswahili (TUKI)
Kimaro, A. F (2016) Kuchunguza Taswira ya Mwanamke na Mbinu za Kifani Katika Mashairi:
                       Mfano wa Diwani ya Midulu. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria  cha Tanzania
Kitereza, A. (1980). Bwana Myombekere na Bi. Bugonoka Ntulanalo na Buliwhali.
                        Dar es Salaam: Tanzania Publishing 
Momanyi, C (2001). “Suala la Uana katika Utafiti wa Fasihi. Katika Utafiti wa Kiswahili.”
                        Makala za Kongamano la Chama cha Kiswahili Taifa – Kenya (2002). Nairobi
                        Moi University Press
Samwel, M. (2010) Masuala ya Kisasa katika Mashairi ya Mapenzi ya Muziki wa Bongo Fleva. 
                       Katika Mulika, Na 29&30. Dar es Salaam: TATAKI
Temples, P. (1945) Bantu Philosophy. Paris: Presence Africaine Publishers
TUKI      (2004) Kamusi ya Kiswaahili Sanifu. Dar es Salaam: Taasisi ya Uchunguzi Kiswahili
Wamitila, K. W. (2002) Uhakiki wa Fasihi, Misingi na Vipengele vyake.
                        Nairobi: Phoenix Publishers
Wamitila, K. W. (2016) Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide - Muwa Publishers

No comments:

Post a Comment