Saturday

HADITHI YENYE ASILI YA KABILA LA KIMAKONDE INAYOMZUNGUMZIA MWANAMKE NA JINSI AMBAVYO MWANAMKE ANASAWIRIWA.

0 comments


Mwandishi
Baraka Emmanuel Simon

Kwa mujibu wa Wamitila (2003) anafasili dhana ya hadithi kuwa ni masimulizi ambayo yanatumia lugha ya mjazo au nathari na mtiririko wake kuwa mwepesi au sahili.


 Katika fasili hii Wamitila anaweka mkazo kuwa hadithi haina budi kuwa na lugha ya mjazo hata mtiririko mwepesi na sahili wa hiyo hadithi. 

Pia, Mulokozi (2017) anafasili hadithi kuwa ni masimulizi, ni ganizi (kutokana na kugana = kusimulia), ni fani yenye kusimulia habari fulani. Anaendelea kueleza kuwa hadithi huweza kueleza matukio katika mpangilio fulani mahsusi, huwa na wahusika yaani watendaji au watendwaji katika matukio yanayosimuliwa. 
Sio hivyo tu, pia Mulokozi (keshatajwa) anaeleza kuwa vilevile hadithi hutumia lugha ya mjazo, lugha hiyo wakati mwingine huchanganywa na mazungumzo (dailojia) na hata ushairi au nyimbo. Huwa na maudhui ya kweli au ya kubuni, na yenye funzo au ujumbe fulani kwa jamii.

Wamitila (2016) anaelezea usawiri kuwa ni hali na mtindo wa uwasilishaji wa wahusika, mandhari na matukio katika kazi ya kifasihi. Aidha, Issa (2013) akimrejelea Wamitila (2002) anaeleza kuwa usawiri wa wahusika ni mbinu ya kisanaa inayotumiwa katika kazi ya fasihi ambayo kwayo mambo yanahusiana na wahusika hao huoneshwa. Mambo hayo ni pamoja na wasifu wao, tabia zao, lugha zao, itikadi zao, vionjo vyao na mitazamo yao.
Hivyo, kwa ujumla dhana ya usawiri wa mwanamke inaweza kufasiliwa kuwa ni mbinu ya kisanaa inayotumiwa katika kazi ya fasihi ambayo kwayo mambo yanahusiana na mwanamke. Mambo hayo ni pamoja na wasifu wake, tabia yake, lugha yake, itikadi yake, vionjo vyake na mitazamo yake.
Baada ya kuangalia fasili ya dhana mbalimbali zilizojitokeza, ifuatayo ni hadithi ambayo asili yake ni kabila la Kimakonde ambayo imeweza kumsawiri mwanamke kwa namna mbalimbali.

Hadithi ya Nachuli
Hapo zamani za kale, palikuwepo na mwanamke mmoja aliyekuwa akifahamika kwa jina la Nachuli, ambaye alipata kuishi katika kijiji kimoja kiitwacho Chiwonga. Nachuli alikuwa ni mama wa watoto watano ambapo alikuwa akiishi pamoja na mume wake. Nachuli alikuwa akiishi maisha ya tabu sana kutokana na mumewe kutojihusisha na shughuli za uzalishaji mali za kilimo. Nachuli alikuwa akitoka asubuhi na mapema kwenda mtoni kuchota maji na baada ya hapo alianza safari ya kwenda shambani kulima. Alikuwa na uwezo wa kulima hekali tatu peke yake bila ya mume wake.
Siku moja asubuhi na mapema wakati akielekea shambani na watoto wake alikutana na chatu mkubwa ambaye alitaka kummeza mtoto wake mmoja ambaye alitangulia mbele. Kwa ujasiri aliokuwa nao Nachuli aliweza kumkaribia yule chatu na kumpiga mundu kichwani, papo hapo yule chatu alikufa akakatwa kichwa chake na kuchimbiwa chini. Baada ya hapo ndipo waliendelea na safari   ya kwenda shambani. Ilipofika jioni waliweza kurejea nyumbani huku akiwa na mzigo wa kuni kichwani, mtoto mgongoni na mikononi akiwa amebeba dumu la maji na jembe.
Nachuli alifika nyumbani huku akiwa amechoka hoi bin taaban, ambapo pia ilimbidi atayarishe chakula ili waweze kula. Wakati akiandaa chakula mume wake alirejea nyumbani toka kilabuni akiwa amelewa chakali. Mume alianza kuporomosha matusi kwa mke wake kwa madai kuwa amechelewa kurudi shamba.
Giza lilipoingia, ukafika muda wa kwenda kulala wakati ambapo mume alimuomba mke wake washiriki tendo la ndoa lakini Nachuli aliweza kumuomba mume wake wasifanye hicho kitendo kwani alikuwa akidai kuwa amechoka kutokana na shughuli alizokuwa akizifanya kutwa nzima. Mume hakuweza kumuelewa mkewe na alianza kumpiga huku akimtishia kumfukuza hapo nyumbani usiku huohuo. Kutokana na uwoga wa kufukuzwa nyumbani usiku huo wa manane ilibidi tu amtimizie mume wake kile alichokawa anakitaka. Asubuhi ilipofika Nachuli aliendelea na shughuli zake za kila siku.
Msimu wa mavuno uliwadia ambapo pia shughuli zote hizo alizifanya Nachuli huku mume wake akiwa mtu wa kushinda katika vilabu vya pombe. Ulipofika msimu wa mauzo ya mazao hayo, mazao yaliuzwa lakini mwanamke  hakuweza kupata kiasi chochote cha pesa na badala yake pesa zote alizimiliki mwanaume. Nachuli alipokahitaji pesa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani alimfuata mume wake na kumuomba pesa za matumizi.
Kutokana na Nachuli kuchoshwa na tabia na mienendo ya mume wake aliamua kuanza kutoka nje ya ndoa kwa kukutana na wanaume mbalimbali ambao walikuwa wanampatia mahitaji yake binafsi. Hii ni kwa kuwa tu wakati mwingine Nachuli alikuwa akiomba pesa kwa mume wake lakini alikuwa ananyimwa.
Siku moja Nachuli alikutana na rafiki yake kipenzi Lupapi ambaye alipotezana nae miaka kadhaa iliyopoita. Lupapi alimshangaa sana Nachuli kwa kumuona vile alivyokonda. Nachuli aliweza kumueleza Lupapi mambo yote anayokumbana nayo katika ndoa yake hiyo, alimueleza mambo yote mabaya anayofanyiwa na mume wake. Lupapi alimshauri Nachuli kuwa amuendee kwa mganga huyo mume wake ili tu kuweza kumfanya apunguze mabavu katika ndoa yao hiyo. Nachuli alikubali ushauri huo ambapo waliongozana wote hadi kwa mganga wa kienyeji ili kuweza kupata suluhisho hilo.
Baada ya kufika kwa mganga, Nachuli aliweza kumueleza mganga matatizo yake yote yanayomsibu. Mganga alitimiza wajibu wake ambapo alimpatia dawa Nachuli na kwambia akamuwekee hiyo dawa mume wake kwenye chakula anachopendelea na alimsihihi asithubutu kuonja wala kula hicho chakula kilichowekwa dawa. Nachuli alirudi nyumbani na kufanya hivyo kama alivyoelekezwa. Ilipofika jioni mume wa Nachuli alirejea toka kilabuni, alipewa kile chakula kilichowekewa dawa na kukila huku akisifia kimepikwa vizuri. Mara tu baada ya kumaliza kile chakula mume alianza kutapika huku akitokwa na jasho mwili mzima mithili ya chemchem. Haikuchukua muda mrefu yule mume alifariki papo hapo. Nachuli alianza kuhangaika huku akiwa hajui la kufanya. 
Watu waliweza kufika pale nyumbani kwa ajili ya kumfariji Nachuli kwa matatizo yaliyompata. Ndugu na jamaa walipanga taratibu za mazishi na baada ya mazishi Nachuli alipaswa arejee kwao kwa wazazi wake. Nachuli hakuwa  anaruhusiwa kurithi mali kwa kuwa katika jamii hiyo mke hakuwa na mamlaka ya kupata mirathi. Baada ya Nachuli kurejea kwa wazazi wake aliweza kufanyiwa matambiko ili kuondoa mkosi katika familia yao na vizazi vijavyo, hatimaye baada ya hapo Nachuli aliweza kuishi kwa raha mustarehe.

Baada ya kuangalia hadithi hapo juu, basi haina budi kuangali namna ambavyo mwanamke amesawiriwa katika hadithi hiyo na usawiri huo umeweza kuoneshwa kama ifuatavyo:
Mwanamke anasawiriwa kama mlezi, kwa mujibu wa TUKI (2012) wanaeleza kuwa mlezi ni mtu anayemtunza, kumhudumia na kumfundisha mpaka akue. Katika hadithi iliyotolewa hapo juu Nachuli anaonekana ni mtu ambaye amekuwa mlezi kwa watoto wake muda wote. Mwandishi anamuonesha Nachuli akichukua majuku yote ya malezi kwa watoto wake, amekuwa akiongozana nao kwenda shambani hadi wakati wa kurudi shamba. Mfano hadithi inasema;
“…………………akielekea shambani na watoto wake alikutana na chatu mkubwa ambaye alitaka kummeza mtoto wake mmoja ambaye alitangulia mbele.”
Maelezo haya yanadhihirisha namna gani Nachuli (mwanamke) anakuwa karibu na watoto wake lakini mume haonekani akijihusisha na wala haonekani kuwa karibu wa watoto wake kama mlezi. Sio katika hadithi hii tu, hata katika tafiti mbalimbali zilizopata kufanywa mwanamke ameweza kuonekana kama mlezi. Mfano Issa (2013) katika utafiti wake alioufanya kuhusiana na Usawiri wa Mhusika Mwanamke katika Ushairi wa Mathias Mnyampala: Mifano kutoka Diwani ya Mnyampala (1965) na Waadhi wa Ushairi (1965)  anaeleza kuwa jamii nyingi mwanamke anasawiriwa kama mlezi wa watoto na familia kwa amekuwa akibebeshwa majukumu ya malezi. Hivyo, kwa maelezo hayo yanadhihirisha wazi kuwa katika jamii nyingi kwa kiasi kikubwa mwanamke amekuwa akisawiriwa kama mlezi.
Mwanamke anasawiriwa kama mtumwa kwa mwanaume. Ndalu na wenzake (2014) wanaeleza kuwa mtumwa ni mtu ambaye humilikiwa na mtu mwingine akifanyishwa kazi bila malipo. Katika hadithi ya hapo juu inamsawiri mwanamke ambaye ni Nachuli anamilikiwa na mume wake huku akiwa anafanya kazi za shamba kwa juhudi kubwa lakini baada ya shughuli zote unapofika msimu wa mavuno na mauzo ya mazao hayo mume ndiye humiliki pesa zote. Mbali na hapo mwanamke ameonekana akitukanwa kwa sababu tu ya kuchelewa kurudi shambani
“Wakati akiandaa chakula mume wake alirejea nyumbani toka kilabuni akiwa amelewa chakali. Mume alianza kuporomosha matusi kwa mke wake kwa madai kuwa amechelewa kurudi shamba.”
Hii inaonesha ni kwa namna gani amekuwa akitumikishwa mithili ya mtumwa. Mbiu (2013) katika utafiti wake anaeleza kuwa katika jamii za Kiafrika mwanamke anaposhindwa kumuwajibikia mume wake basi anaweza kuadhibiwa ikiwa ni hata kupigwa. Maelezo hayo yanaonesha kuwa katika jamii bado inaonekana mfumo dume ukishika hatamu, hii inaonekana pale mwanamke anapomilikiwa na mume wake huku akifanyishwa kazi mbalimbali.
Mwanamke anasawiriwa kama mshirikina, kwa mujibu wa Wamitila (2016) anaeleza kuwa mshirikina ni mtu anayeongozwa na imani zisizokuwa na msingi wa kisayansi; anayependa ushirikina; anayefuata imani za jadi hasa kuhusu kutendeka kwa mambo. Katika hadithi ya hapo juu inaonesha Nachuli akiwa ni mtu ambaye anaongozwa imani za jadi. Hii inaonekana pale ambapo Lupapi na Nachuli wanashauriana kwenda kwa mganga ili kuweza kumdhibiti mume wa Nachuli. Mwandishi anasema;
“Lupapi alimshauri Nachuli kuwa amuendee kwa mganga huyo mume wake ili tu kuweza kumfanya apunguze mabavu katika ndoa yao hiyo. Nachuli alikubali ushauri huo ambapo waliongozana wote hadi kwa mganga wa kienyeji ili kuweza kupata suluhisho hilo.”
Maelezo haya yanathibitisha ni kwa namna gani Lupapi na Nachuli walikuwa wakiamini sana masuala ya ushirikina kwa kuona kuwa kufanya hivyo ndio itakuwa suluhisho la matatizo yao yanayowakabili.
Mwanamke anasawiriwa kama mzalishaji mali, pia katika hadithi hii inamsawiri Nachuli ambaye ndiye mwanamke kuwa ndiye mzalishaji mali katika familia yao huku mume wake akiwa ni mtu wa kushinda kwenye vilabu vya pombe kutwa nzima. Msimuliaji anasema;
“Msimu wa mavuno uliwadia ambapo pia shughuli zote hizo alizifanya Nachuli huku mume wake akiwa mtu wa kushinda katika vilabu vya pombe.”
Hivi ndivyo alivyosawiriwa mwanamke katika hadithi hii ya Kimakonde. Lakini mbali na hayo Mbiu (2013) katika utafiti wake wa Usawiri wa Mwanamke katika Ngano za Kisambaa anasema kuwa mwanamke ndiye mwajibikaji mkubwa katika shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya familia yake na jamii nzima kwa ujumla. Anaendelea kueleza kuwa pamoja na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali bado mwanamke anawajibika katika kufanya shughuli zote za nyumbani, shughuli hizo ni kama vile kuzaa, na kutunza watoto, kuuguza wagonjwa, kupika na kufua nguo kazi ambazo anazifanya bila malipo na pia hazihesabiki kama kazi za uzalishaji. 
Pia, katika hadithi hii mwanamke anasawiriwa kama ni mtu jasiri. Wamitila (2016) anaeleza kuwa jasiri ni mtu anayethubutu kufanya mambo ya hatari au magumu. Nachuli ameonekana kama jasiri katika hadithi hiyo hapo juu, na hii ni kutokana na tu vile alivyothubutu kukabiliana na chatu ambaye alitaka kummeza mtoto wake. Msimuliaji wa hadithi anasema;
“Siku moja asubuhi na mapema wakati alielekea shambani na watoto wake alikutana na chatu mkubwa ambaye alitaka kummeza mtoto wake mmoja ambaye alitangulia mbele. Kwa ujasiri aliokuwa nao Nachuli aliweza kumkaribia yule chatu na kumpiga mundu kichwani, papo hapo yule chatu alikufa akakatwa kichwa chake na kuchimbiwa chini.”
Hivyo basi, hii inaonesha kuwa mwanamke anaweza kuliendea jambo lolote lile ambalo linaonekana kuwa jambo gumu na kuweza kufanikiwa.
Aidha, mwanamke pia anasawiriwa kama msaliti. Katika hadithi hii tunaona namna ambavyo Nachuli anamsaliti mume wake kwa kutoka nje ya ndoa kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu. Msimuliaji wa hadithi anasema;
“………….aliamua kuanza kutoka nje ya ndoa kwa kukutana na wanaume mbalimbali ambao walikuwa wanampatia mahitaji yake binafsi. Hii kwa kuwa tu wakati mwingine Nachuli alikuwa akiomba pesa kwa mume wake lakini alikuwa ananyimwa.”
Suala la mwanamke kuwa msaliti kwa mume wake halijazungumziwa katika hadithi hii tu yenye asili ya Kimakonde ila hata kazi nyingine za kisanaa mwanamke amekuwa akisawiriwa kama msaliti. Mfano, katika nyimbo mbalimbali za Bongo Fleva zimekuwa zikumchukulia mwanamke kama msaliti na tamaa ya pesa ndio imekuwa ikiwafanya wanawake kuwasaliti wanaume zao. Hii imeonekana hata katika wimbo wa Prof. Jay uitwao Nikusaidieje, sio wimbo huo tu hata wimbo wa Christian Bella – Msaliti, wimbo wa Bushoke akimshirikisha Jose Chameleon – Mama Roda. ni baadhi ya kazi nyingine za kisanaa ukiachana na hadithi ambazo zimemsawiri mwanamke kama msaliti. 
Fauka ya hayo, mwanamke anasawiriwa kama chombo cha starehe. Katika hadithi ya hapo juu inamuonesha jinsi ambavyo Nachuli alikuwa akilazimishwa na mume wake kushiriki tendo la ndoa bila kujali kuwa mke alikuwa amechoka kutokana na kazi alizokuwa akizifanya kutwa nzima. Msimuliaji wa hadithi inasema;
“Giza lilipoingia, ukafika muda wa kwenda kulala wakati ambapo mume alimuomba mke wake washiriki tendo la ndoa lakini Nachuli aliweza kumuomba mume wake wasifanye hicho kitendo kwani alikuwa amechoka kutokana na shughuli alizokuwa akizifanya kutwa nzima. Mume hakuweza kumuelewa mkewe na alianza kumpiga huku akimtishia kumfukuza hapo nyumbani usiku huohuo. Kutokana na uwoga wa kufukuzwa nyumbani usiku huo wa manane ilibidi tu amtimizie mume wake kile anachokitaka.”
Sio tu katika hadithi hii ya Kimakonde ambayo imemsawiri mwanamke kama chombo starehe ila hata watafiti wengine katika kazi zao wameweza kuliona hilo. Mfano, Abdalla (2015) katika utafiti wake wa Kutathmini Usawiri wa Mhusika Mwanamke katika Hadithi Simulizi za Wapemba anaeleza kuwa mwanamke katika jamii hutumika  kama chombo cha starehe ambapo wanaume  hutumia  na kuondoa  kiu zao za matamanio ya  kimwili. Hii ni dhahiri kwamba jamii zilizo nyingi humchukulia mwanamke kama chombo cha starehe.
Mwanamke anasawiriwa kama mtu ambaye hahusishwi kwenye suala la mirathi. Kwa mujibu wa BAKITA (2015) wanafasili mirathi kuwa ni mali zilizoachwa na mtu aliyefariki dunia ambazo hugawiwa kwa wanaostahili kwa mujibu wa sheria. Katika hadithi hiyo hapo juu inaonesha namna ambavyo Nachuli hakuweza kupewa mirathi baada ya kufariki mumewe na hii ni kutokana tu na mila na desturi kandamizi hususani kwa mwanamke ambapo huonekana kuwa mwanamke haruhusiwi kurithi mali zilizoachwa na mume wake wakati anapofariki. Msimuliaji anasema;
 Nachuli hakuwa anaruhusiwa kurithi mali kwa kuwa katika jamii hiyo mke hakuwa na mamlaka ya kupata mirathi.
Maelezo hayo ya msimuliaji yanaonesha ni kwa namna gani katika jamii hiyo ambavyo mwanamke amekuwa akinyimwa haki zake za kurithi mali zilizoachwa na mume wake. Suala la mwanamke kunyimwa mirathi halijazungumziwa katika hadithi hii tu bali hata katika baadhi ya kazi za fasihi andishi kama vile tamthiliya hata riwaya pia zimekuwa zikimuonesha mwanamke kama mtu ambaye amekuwa akikosa haki zake za msingi katika mirathi. Mfano, katika tamthiliya ya Hussein (1988)  Kwenye Ukingo wa Thim inamuonesha mhusika Martha jinsi ambavyo aliweza kukosa haki yake ya msingi ya kupata mirathi mara baada ya kufariki mume wake ambaye ni Herbert. Hii inadhihirisha kuwa katika baadhi ya jamii za Kiafrika bado kumekuwa na utamaduni ambao unamnyima mwanamke haki ya kurithi mali alizozichuma na mume wake enzi za uhai wake.
Kwa ujumla, hivi ndivyo ambavyo mwanamke ameweza kusawiriwa katika hadithi ambayo asili yake ni kabila la Wamakonde. Usawiri wa mwanamke ambao umeonekana katika hadithi hii umeweza pia kuonekana hata katika kazi nyingine za kifasihi kama vile tamthiliya, riwaya hata ushairi pia.









MAREJELEO
Abdalla, H. A. (2015). “Kutathmini Usawiri wa Mhusika Mwanamke katika Hadithi Simulizi za Wapemba.” Tasnifu ya Umahili  Kitengo cha Kiswahili, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. (Haijachapishwa).
BAKITA (2015), Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.
Hussein, E. (1988). Kwenye Ukingo wa Thim. Indiana University: Oxford University Press.
Issa, I. (2013). “Usawiri wa Mhusika Mwanamke katika Ushairi wa Mathias Mnyampala: Mifano kutoka Diwani ya Mnyampala (1965) na Waadhi wa Ushairi (1965).” Tasnifu ya Umahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Haijachapishwa).
Mbiu, C. (2013). “Usawiri wa Mwanamke katika Ngano za Kisambaa.” Tasnifu ya Umahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. (Haijachapishwa).
Mulokozi, M. M. (2017). Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili Kozi za Fasihi Vyuoni na Vyuo Vikuu. Dar es Salaam: KAUTTU.
Ndalu, A. E, Babusa, H. na Mirikau (2014). Kamusi Teule ya Kiswahili Kilele cha Lugha. Nairobi: East African Educational Publishers Ltd.
TUKI (2012). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila, W. K. (2003). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi. Nairobi: Focus Publication.
Wamitila, W. K. (2016). Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide-Muwa Publishers.

Wasiliana na mwandishi
Baraka Emmanuel Simon ( Baraka, Jr)

0654245488 / 0693300491

No comments:

Post a Comment