Monday

Nafasi ya mwanamke katika Jamii , Uislamu na mwanamke

0 comments
Nafasi ya mwanamke katika jamii
 
 Na Hawra Shamte @masshele



KATIKA jamii nyingi mwanamke anaonekana kama chombo cha kumstarehesha mwanaume. Kabla ya Uislamu hadhi ya mwanamke ilikuwa chini kuliko kitu chochote kile, mtu alikuwa akimthamini ngamia wake kuliko mwanamke.
Mwanamke alionekana kuwa ni duni na ni mchafu. Akiwa katika hedhi jamii nyingi zilikuwa zikimtenga kama mwenye ukoma.
Kuzaa mtoto wa kike lilikuwa ni jambo la aibu katika bara la Arabu na ndiko watoto wachanga walikozikwa wangali hai kwa baba kuhofia huzuni.
Bara Hindi nako kwa wale waliokuwa wakifuata mila ya Sati mwanamke anayefiwa na mumewe alizikwa na mumewe kwa kuwa Bwana wake kafa yeye hana budi kumsindikiza.
Mila hiyo pia ilipatikana katika baadhi ya jamii za Kiafrika ambako Machifu walikuwa hawazikwi peke yao ni lazima waambatane na msichana wa kati ya miaka 14 hadi 17 kwa imani ya kuwa atakwenda kumstarehesha Chifu huko aendako.
Hivyo mwanamke hakuhesabika kama kiumbe mwenye roho inayoweza kujitegemea, inayostahili heshima na kuenziwa. Alionekana kama ni kiumbe aliyeumbwa ili kumuondoshea upweke mwanaume na kumzalia watoto hivyo alikuwa sawa na kiwanda cha uzalishaji, kwani mbali na jukumu la kuzaa na kulea, katika jamii nyingi mwanamke ndiye mzalishaji mali mkuu.
Wakati mwanaume anafanya kazi masaa 8 hadi 10 kwa siku, mwanamke anafanya kazi kwa zaidi ya masaa 16 kuanzia usafi wa nyumba, ulezi wa watoto, upishi wa chakula, kutoa huduma kwa mwanaume na hata kutafuta chakula cha familia.
Uislamu ulipokuja kumuondolea mwanamke mzigo huo na kutamka bayana kuwa mwanaume na mwanamke ni mbeya mbili zilizoumbwa ili kusaidiana, kupendana na kuoneana huruma.
Na Allah akasisitiza tena kuwa hakuna mbora kati ya vile alivyoviumba, bali mbora kwake ni yule anayemcha Mungu tu na kwamba wafanyao vitendo vyema wakiwa wanaume ua wanawake watapata ujira wao kwa Mwenyezi Mungu.
Naye Mtume (s.a.w.) alisema kuwa mwanamke ni Malkia wa nyumba. Kazi za kupika, kufua, kupiga deki, kupiga pasi na kadhalika si zake na pindi anapozifanya huzifanya kwa huruma zake na mapenzi yake kwa mumewe.
Watoto wetu wanapopotoka lawama nzito humuelemea mama kuwa malezi yake hayakuwa mazuri, na hilo ni ukweli usiopingika kuwa mama ndiye chuo kikuu cha mafunzo kwa mtoto na ndiye mwalimu wa kwanza kabla ya mwingine yeyote yule. Na ndiyo maana lugha za asili tunazozingumza huitwa 'Mother Toung'.
Mafunzo ya mwanzo anayoyapata mtoto ndiyo anayoamua mwelelekeo wa mtoto huyo wanasaikolojia wanasema kuwa akili ya mtoto hunasa kama sumaku na kinachoingia akilini mwa mtoto hakitoki kama nakshi iliyonakshiwa katika jiwe. Ka nakshi fii hajar.Kwa maana ya kuwa nakshi hiyo haiwezi kufutika kamwe.
Hivyo ili mama awe mwalimu bora ni muhimu kwake apate elimu ambayo pia ni wajibu kwake kama ilivyo wajibu kwa mwanaume. Elimu ni amri iliyotiliwa mkazo na ilishuka mwanzo kabla ya amri nyingine zozote zile.
Hivyo ni lazima kwa mwanamke wa Kiislamu kuitafuta elimu popote pale na ni haki ya Muislamu kuinyakua popote pale atakapoikuta.
Kwa mantiki hiyo hakuna dharura yoyote anayoweza kuitoa Muislamu kwa kukosa elimu kwani kuitafuta ni faradhi kama kusali, kufunga na kufanya ibada nyingine yoyote ile hivyo Waislamu wanapaswa wafahamu kuwa eimu ni ibada ya faradhi kwao.
Elimu na wanawake wa Kiislamu nchini.
Ushiriki wa wanawake wa Kiislamu nchini Tanzania katika kutafuta elimu ni finyu sana na kati ya wanawake asilimia 20 wanaopata elimu, asilimia tano tu ni Waislamu na hali hiyo inatolewa sababu nyingi za kihistoria. Kubwa ya zote ni ile inayodai kuwa kumuelimisha mwanamke ni kupoteza wakati kwani hatimaye ataolewa na kubaki jikoni. Fikra hizo si za Kiislamu na zinapaswa kupigwa vita kwa nguvu zote.
Katika nchi zilizopiga hatua ya kusimamisha sheria ya Kiislamu kama vile Iran asilimia 72 ya wanafunzi walioko katika vyuo vikuu ni wanawake na tayari zaidi ya asilimia 50 ya wanawake wameelimika, si ajabu ukakuta asilimia 80 ya Maprofesa wa vyuo vikuu ni wanawake na kwa msingi huo ni rahisi pia kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi na hakuna suala la upendeleo kwa sababu uwezo wanao.
Mwanamke katika nchi kama hiyo siyo tena chombo cha starehe kwani hutamkuta katika matangazo ya biashara wala hutamkuta akiwa uchi kwa azma ya kumshawishi mwanaume kwa hali yoyote ile.
Wanavaa hijab kisheria na wala hawazuiliwi kushiriki katika harakati mbalimbali za kijamii, wanashirikiana na wanaume bega kwa bega huku wakichunga hijab zao.
Hivi leo hapa kwetu eti hijabu ni kikwazo katika kazi! Hiyo ni kujiendekeza na kutokuwa tayari kuingia Uislamu wote!
Namalizia kwa hadithi ya Mtume (s.a.w.) inayosema kuwa atakayenilelea vizuri vijakazi vyangu angalau watatu namwahidi pepo!

Wasia wa kushika
"TAIFA ambalo wanawake wako nyuma kielimu ni wazi kwamba Taifa hilo halina maendeleo".
Hayo ni maneno aliyowahi kuyasema hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Maneno hayo aliyasema hayati Mwalimu Nyerere mwaka 1984 alipokuwa akifungua mkutano mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) uliofanyika Arusha.
Ni miaka 15 imepita tokea Mwalimu atoe tamko hilo lenye ukweli katika kila hali. Lakini je tamko hili lilishawahi kufanyiwa kazi kwa makusudi?
Maneno ya kuwapa wanawake kipaumbele ni propaganda tu za kisiasa ambazo Tanzania ni magwiji wa kuzieneza lakini kutekeleza sera kwao ni mwiko.
Ingelikuwa agizo hilo limetekelezwa angalau kwa asilimia 30 tu basi tungeweza kusema kuwa tumepiga hatua. Lakini leo hii bado wasomi wanawake waliopata shahada za juu kama vileMasters na PhD unaweza kuwaingiza kwenye kiganja cha mkono.
Hilo ni moja, la pili hata wale chipukizi wanamageuzi wa masomo nao hawapati nafasi tosha ya kupata elimu stahili.
Kwa hilo Watanzania tunapaswa kujiuliza ni wapi tunapokosea? Je, bado wazazi wana fikra za kuwa wanawake ni bidhaa mbovu? Au bado nafasi ya mwanamke ni jikoni na hawezi kutoa mchango mwingine wowote katika kuliendeleza Taifa kiuchumi, kisiasa na hata kijamii?
Bado kuna swali la kujiuliza, je, ni kitu gani kinachosababisha watoto wa kike walio wengi wasipate nafasi ya kujiendeleza kimasomo?
Je, ni hali ya kiuchumi ni mimba za utotoni ni kukosa akili au ni vipi!
Hali ya kiuchumi:
Kwa kiasi kikubwa watu wenye hali duni ya maisha hususan wale wanaopata kima cha chini cha mshahara au wafanyabiashara wa kijungu jiko hawamudu kuwasomesha watoto wao sio tu wa kike hata wale wa kiume.
Matokeo yake ni kuwa watoto wanapomaliza elimu ya msingi (na hata hivyo kuikamilisha ni bahati) huwa hawana la kufanya na kulazimika kufanya biashara ndogondogo kama vile kuuza karanga na kadhalika kwa ajili ya kuchangia pato la familia.
Katika wakati huo aghalabu stahamala ya watoto wa kike kuzidiwa na tamaa na huwa ni rahisi kwao kushiriki katika vitendo vya uasherati.
Kadhalika watoto wa kiume ni muda huo ambao hujikuta wamejiingiza katika vitendo vya uhuni kama vile uvutaji bangi, kuwa na magenge na hatimaye kujifunza wizi.
Katika hali kama hiyo mara nyingine ni vigumu mzigo wa lawama kuwatupia wazazi na ndipo Taifa linapopaswa kuubeba msalaba huo.
Katika mweleleo huo anayeathrika zaidi ni mtoto wa kike kwa sababu mustakbali wa maisha yake ya baadaye unakuwa umeshavurugika kabisa hasa pale anapojiingiza katika vitendo vya anasa na kubahatisha kupata mimba, kwani hapo hulazimika kuwa mama, mtafutaji na mhudumiaji na kupoteza kabisa matumaini ya kujiendeleza kielimu.
Mimba za utotoni:
Hili ni tatizo ambalo halistahili kufumbiwa macho, na tatizo hilo linaonekana kwa wingi sana katika jamii zilizo duni.
Hata hivyo uchambuzi huo haukusudii kuhalalisha upatikanaji wa mimba kiholela kwa watoto wa walalahoi bali ninachotaka kuainisha ni wapi tatizo liliko lala.
Katika hilo nathubutu kusema kwamba tatizo kubwa liko katika malezi.
Malezi ya wakati huu yamekuwa magumu kwa wazazi takriban wote na hapo ndipo jamii inapopaswa kujiuliza ni wapi ilipokwenda upogo?
Wachunguzi wa masuala ya kijamii wanasema kuwa kuna aina ya mafunzo ambayo wazazi hawana tena nafasi ya kuwapa watoto wao.
Mafunzo hayo yapo katika mtindo wa vitendo na ushauri.
Kivitendo watoto wana tabia ya kuiga kutokea kwa wazazi wao lakini endapo wazazi hawatengi muda wa kukaa nawatoto wao, watoto wataiga saa ngapi? Matokeo yake watoto huiga vitendo vya watoto wenzao na mara nyingi huwa si vitendo sahihi kwa jamii staarabu.
Zamani kulikuwepo na muundo maalum wa kutoa ushauri nasaha ambao kila jamii ilikuwa na utaratibu wake na walitumiwa watu kama bibi, babu, shangazi, mjomba na kadhalika na ushauri huo mara nyingi ulikuwa ukitolewa kwa mifano, mafumbo, methali na hadithi.
Katika utaratibu huo, watoto walikuwa na desturi ya kusikiliza mawaidha ya wakubwa na kuyatekeleza na ndipo methali ya asiyesikia la mguu huvunjika guu ilipochukua nafasi yake na kuthaminiwa na wanajamii wote. Lakini za paukwa pakawa utamu njoo, uongo kolea!
Hivyo ndivyo vito vya thamani vilivyoing'arisha jamii, lakini sasa tunategemea nini iwapo mwalimu mkubwa wa watoto wetu ni Runinga , mapenzi yao ni kuangalia Egoli na Sunset Beach na filamu nyinginezo ambazo mtoto anaweza kumkaripia baba yake bila kisisi!
Je, watoto wa kike hawaendelei na masomo kwa kukosa akili?
Inaelezwa kuwa wasichana hupenda masomo laini laini ya sanaa kuliko yale magumu ya sayansi kutokana na kutopenda kujifunza au kuwa na akili finyu.
Hili ni gumu kidogo kuliunga mkono kwa sababu katika nchi ambazo kuna mfumo mzuri wa elimu na vitendea kazi vya kutosha wanawake wana uwezo sawa na wanaume katika kutafakari katika masomo na wengi wao wamefanikiwa kuingia vyuo vikuu na kupata ajira bora.
Hilo ni wazi kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa mwanamke anapokuwa makini humshinda mwanaume katika tafakuri na hata utendaji kazi.
Ninachotaka kusema ni kuwa taifa la Tanzania bado halijawapa wanawake nafasi maridhawa ya kuonesha vipaji vyoa na umahiri wao katika mambo mbalimbali ya kitaaluma.
Tunapaswa kuufanyia kazi wasia wa marehemu Mwalimu Nyerere wa kuwa hakuna maendeleo kwa Taifa ambalo wanawake wako nyuma kielimu

No comments:

Post a Comment