Monday

FASIHI INAVYO MKOMBOA MWANAMKE KIJINSIA

0 comments
  • Namna fasihi inavyo weza kumkombona na kumkandamiza mwanamke.
  • Kumekuwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na asasi katika jamii kwa ajili ya kuleta ukombozi kwa wanawake.
Jitihada hizo hufanywa kutokana na kuwapo kwa ukandamizaji dhidi ya mwanamke, katika masuala anuwai ya uhusiano wa kijinsia.
Suala la kukosekana kwa usawa kati ya wanawake na wanaume katika jamii si la Tanzania au bara la Afrika pekee, bali limekuwako duniani kote. Suala hili limekuwa likihusishwa na utamaduni wa jamii husika.
Tofauti baina ya nchi zetu na pahali penginepo duniani ni kwamba, katika nchi kama Ufaransa, Marekani na Uingereza; harakati za kuleta usawa zilianza kufanyika mapema kupitia dhana ya Ufeministi ambayo baadaye ilisambaa sehemu mbalimbali duniani.
Mary Wollstonecraft aliyeishi nchini Uingereza, alitoa kitabu mwaka 1792 kilichoitwa “A Vindication of the Rights of Woman”. Yeye hakuwa mtu wa kwanza kupata elimu ya ukombozi huo na haki za wanawake, lakini alikuwa wa kwanza kuwa mshenga na kichocheo cha ukombozi kwa wanawake kwa kutia hamasa na chachu.
Tukirejelea katika muktadha wa nchi yetu ya Tanzania, kwa upande wa fasihi suala hilo linasawiriwa na wasanii mbalimbali.
Katika makala haya, tatapitia tamthiliya ya “Nguzo Mama” iliyoandikwa na Penina Muhando na kuchapishwa mwaka 1982. Dhamira kuu katika “Nguzo Mama” inayoibuliwa na mwandishi ni ukombozi wa mwanamke. Muhando anawachora wanawake wakifurukuta kuinua ‘nguzo mama’ yaani kujiletea ukombozi.
Hata hivyo, katika kufanya hivyo, hawawashirikishi wanajamii wengine kama vile wanaume na watoto. Pamoja na jitihada zote wanazofanya, mwishoni wanakutana na vikwazo mbalimbali na kwa sababu hiyo kutopiga hatua yoyote mbele.
Mpaka mwishoni mwa igizo, hakuna mafanikio. Kuna migogoro mingi inatawala kati ya wanawake wenyewe. Aidha, wanaume wamechorwa kuwa kikwazo cha mafanikio ya wanawake.
Mtazamo hasi dhidi ya wanawake na ukandamizaji katika muktadha wetu ni suala la kiutamaduni zaidi. Suala hilo linahitaji hatua madhubuti na ya dhati katika utekelezaji wake ili kuleta ukombozi wa kweli.
Baadhi ya masuala ambayo huchukuliwa kuwa ya kikandamizaji, kwa sababu ya athari za mila na desturi za jamii zetu, kwa baadhi yetu huonekana ni sehemu ya maisha.
Mathalani, suala la kupigwa kwa wanawake katika baadhi ya makabila huashiria mapenzi mazito. Katika jamii kama hizo, mwanamke asipopigwa na mumewe huona kwamba hapendwi. Katika muktadha huo, kuleta mabadiliko kunahitaji kuchimbua mizizi ya kiutamaduni iliyokita katika akili za wanajamii na kuwaathiri kisaikolojia.
Tukirejelea tamthiliya ya “Nguzo Mama”, mwandishi anataka kutuzindua akili katika yafuatayo:
Mosi, kuna hitaji kubwa la wanajamii, wanawake kwa wanaume kuelimishwa juu ya ukombozi wa mwanamke. Pili, ukombozi wa wanawake utafanikiwa tu ikiwa wanajamii wote watashirikishwa katika kumkomboa mwanamke.
Kwa kuwa mwanamke ni sehemu ya jamii na jamii hiyo huundwa na mchanganyiko wa wanajamii, kila mwanajamii ana jukumu la kutimiza ili kuleta ukombozi huo. Aidha, mwandishi anaelekea kutueleza kuwa, ili kulifanikisha suala la ukombozi wa mwanamke, ni lazima kuung’oa mfumo mbaya uliojengeka katika jamii ambao umejikita katika utamaduni wa jamii ambao ndio humkandamiza mwanamke kupitia mawakala wake kama vile wanaume na taasisi mbalimbali. Ili kufanikisha ukombozi wa mwanamke, jamii yote ielimishwe kwanza mijini na zaidi vijijini ambapo desturi potofu zimetamalaki.


No comments:

Post a Comment