Friday

UHAKIKI RIWAYA YA SIKU YA WATENZI WOTE FANI NA MAUDHUI

0 comments
Katika  makala hii tumeligawa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambao umebeba usuli wa kitabu, sehemu ya pili ni kiini ambapo kutakuwa na uhakiki wa fani na maudhui ya riwaya ya Siku ya Watenzi Wote.


 Sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Siku ya Watenzi Wote ni riwaya iliyoandikwa na Shaaban Robert. Ni riwaya ya kufikirisha na inayotoa mwongozo kuhusu maisha na namna ya kuhusiana katika jamii.

Mwandishi ametoa picha halisi ya maisha na namna binadamu wanavyotakiwa kuishi. Wazo kuu katika riwaya hii ni maadili na suala la kufanya ibada katika kipindi cha ujenzi wa jamii mpya baada ya uhuru. Riwaya ilichapishwa mwaka 1968 baada ya uhuru ambapo anagusia maisha yalivyokuwa.

Mwandishi anagusia masuala kama vile ufisadi, umaskini, dhuluma na mapenzi.


Ufuatao ni uhakiki wa fani na maudhui ya riwaya ya Siku ya Watenzi Wote iliyoandikwa na Shaabani Robert. Kwa kuanza tutaanza na vipengele vya maudhui na kumalizia na fani. Katika maudhui tutaanza na dhamira.


Mosi ni suala la maisha baada ya kifo. Mwandishi anaeleza kuhusu ufufuo ambao wanadamu wanaungoja baada ya kifo. Anasisitiza juu ya kuwapo siku ya mwisho ambayo itakuwa ya hukumu na kuwa’ kila mwanadamu atahukumiwa kwa kuzingatia matendo yake aliyoyatenda akiwa duniani.

Mwandishi anadhihirisha hili kupitia mazungumzo ya Ayubu na mwajiri wa Bi Nunu. Mwandishi anasema;
“Watazamia majilio ya siku ya hukumu?...siku hiyo ya maisha mapya na utukufu, na haki na halali, na  malipo na mapendeleo, na mapenzi na furaha, imo katika kuja, nayo itakuja kwa kila hali. Wajibu na kazi yetu ni kuiandalia.” Uk 33
Imani hii juu ya maisha mapya na hukumu ya mwisho ndiyo iliyojengeka katika jamii zetu. Watu wa dini mbalimbali wanaamini kuwa ipo siku dunia itafikia mwisho na hapo maisha mapya yataanza ambayo ni tofauti na ya sasa.


Pili ni suala la dini. Mwandishi amejadili kuhusu dini kwa upana zaidi ambapo amejadili dini zote mbili yaani uislamu na ukristo. Ameonesha kuwa watu wote tunatakiwa kusali na kufanya ibada bila kujali Biblia na msahafu vinasema nini.

Kwake dini safi ni ile inayojali maslahi ya watu. Kwa mfano mwandishi anamuonesha Azizi akiwa anamsimulia Yusuffu kuhusu mafundisho ya Ayubu anasema,
“Atakwambia kwamba harudi katika mapokeo ya kanisa la Roma wala msikiti wa Qureshi. Huenda moja kwa moja katika maslahi kwa wote; haidhuru zimo au hazimo katika misahafu ijulikanayo.” Uk. 11.
Pia katika dini mwandishi anasisitiza kuhusu suala la sadaka.

Watu wanatakiwa kutoa sadaka iliyosafi. Ameonesha kuwa tunatakiwa tutoe sadaka kwa Mungu ikiwa ni njia ya kumshukuru na kumjaribu Mungu ili atubariki. Kwa mfano: Msimulizi anaelezea kuwa katika jengo la Adili kulikuwa na makasha matatu ya sadaka, anasema
“La kwanza lilipambanuliwa kwa alama, ‘Sehemu ya Mungu’ la pili ‘Sadaka’ la mwisho, ‘Maskini’. Uk. 10.
Anaonesha pia umuhimu wa sadaka anaposema;


“Mwenyezi Mungu husema kwamba leteni zake zote katika ghala, mmjaribu kama hatawamiminia baraka ambayo hamtaweza kupokea." Uk. 8.
Aidha katika dini anasisitiza kutokufanya ibada kwa unafiki.

Mwandishi anakemea wafuasi wa dini ambao wanasali kwa unafiki na wakitoka katika nyumba za ibada wanakashifu dini zao. Hili linadhihirishwa kupitia nyimbo ambapo mwandishi anasema;
                                   “Kichaka hiki kizuri,
                                    Kwa marashi ya utuli;
                                     Harufu yake si nzito…

                                     Kichaka hiki kichafu,
                                     Kwa uvundo wa harufu…” Uk. 07.
Msisitizo wa mwandishi kuhusu dini ni ule ufunuo mpya ambao wanadamu wote wanautegemea.

Maudhui ya namna hii ndiyo yanayohubiriwa katika jamii hata hivi leo kuwa wanadamu wote wasifungwe katika mafundisho ya dini fulani bali wajiandae na siku ya hukumu na ufunuo.

Nafasi ya mwanamke katika jamii. Mwandishi amejadili nafasi ya mwanamke kwa kuonesha kuwa mwanamke anamchango katika jamii. Amaetumia wahusika wanawake kama vile Binti Akili, Sarah, Bi Soma na wengine wengi.


Mwanamke amechorwa kama mtetezi na anayesaidia wengine. Kwa mfano: Sarah na Zena walimsaidia Bi Lela kukomboa sufuria kutoka kwa Mla Riba. Zena alimtamka,
“Hatuna budi kwenda sasa tukakomboe sufuria.” Uk. 96.


Mwanamke anachorwa kama kiumbe anayeweza kujikomboa kiuchumi. Katika riwaya mwandishi amemsawiri Binti Akili kama mwanamke anayeweza kuweka akiba na kujitegemea kiuchumi. Pamoja na kutokuwa na mume Binti Akili alifanya kazi na kuweka akiba ambayo ilimsaidia uzeeni.

Pia Zena alikuwa binti mdogo lakini alifanya kazi ili kujikomboa kichumi. Kwa mfano: Sarah anamsimulia shangazi yake kuwa siku inayofuata kuna sehemu anaenda na Zena. Anasema,
“Atanichukua kwenda kunionyesha afanyako kazi.” Uk. 86.
Wanawake ambao wanajikomboa kiuchumi wapo hata katika jamii ya leo. Wanawake hawa wamekuwa mfano kwa wengine na kudhihirisha kuwa wanawake wanaweza.


Mwanamke ameoneshwa kama mlezi. Kwa mfano: mwandishi amemtumia mwanamke aliyekuwa na watoto watatu wenye umri chini ya miaka nane. Mama huyo alitorokwa na mume wake lakini mwanamke huyu alilea watoto wake pamoja na kipato kidogo alichokuwa anapata. Mwandishi anasema;


“Lakini mwanamke aliyekimbiwa na mume au mfarukwa, hana budi kuvumilia dhiki hizi, na kutenda kazi ya baba na mama, na kukubali ujira mdogo uamriwao na kazi ya mwanamke.” Uk 4
Mwandishi anaonesha hali halisi ya maisha katika jamii kwani mwanamke ndiye aliyebebeshwa jukumu la malezi bila kujali nafasi ya mwanaume katika malezi hayo.


Pia mwanamke amechorwa kama kiumbe duni ambaye anaonewa. Ingawa amemjadili mwanamke katika nafasi chanya pia amedunisha. Kwa mfano mwandishi anatoa kisa cha mwanamke aliyepigwa na mume wake na mume huyo kupewa adhabu ndogo. Wakati huo mwanamke alipewa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu na kazi ngumu kwa kosa la kutupa kirungu kwenye dirisha tu. Mwandishi anasema;
“..aliingia kumpura mwanamke kwa makonde hata akawa hajifahamu na taabani…mtu huyu alikamatwa akapelekwa gerezani; lakini kwa kuwa mwanamke hakuumia mno adhabu juu ya mume ilikuwa kifungo cha siku moja na nusu….” Uk 5
Suala la umaskini. Umaskini ni hali ya kukosa uwezo wa kujikimu kimaisha. Mwandishi anaweka wazi kuwa hata baada ya uhuru wa Tanganyika hali za wananchi bado ni duni. Wananchi wengi wanaishi katika nyumba mbovu na wengine hawana hata uwezo wa kujkimu kwa mahitaji muhimu ikiwemo chakula. Hili linadhhihirishwa pale Ayubu anaposema;
“Katika watu hawa, palikuwa na maskini wanaume na wanawake waliokuja kutafuta msaada.” Uk. 10
Hali ya umasikini ndiyo imetawala jamii nyingi za Watanzania ambao wengi wao wanaishi katika hali duni.  Mathalani wengi hawana makazi na wengine hawana pesa za kujikimu kwa mahitaji yao ya msingi.
Suala la ndoa. Katika riwaya suala la ndoa limejadiliwa, mwandishi anaonesha kuwa ndoa ni makubaliano ya watu wawili wanaopenda na wanaoendana na kufanana kitabia. Vilevile ndoa imeoneshwa kuwa ni chombo chenye nguvu ya kuwaleta watu pamoja katika kutimiza makusudi ambayo watu walipewa na Muumba wao. Mwandishi anaonesha hili kupitia ndoa ya Ayubu na Sarah anaposema;
“Palikuwa na ushirika mkubwa kabisa wa maana kati ya Ayubu na mkewe..Sarah binti Rashid alijithibitisha kuwa msaidizi bora na msiri mkubwa wa mumewe …na Ayubu akawa mume wajibu na sahibu.” Uk 106
Ndoa kama ilivyojitokeza katika kitabu, ndivyo inavyothaminiwa katika jamii kuwa kiunganishi cha mtu na mtu, familia na famila na jamii kwa ujumla
UJUMBE
Ujumbe ni funzo alilokusudia mwandishi wa kazi ya fasihi kufikisha kwa wasomaji. Katika riwaya tunapata mafunzo yafuatayo;
Kwanza, Ushirikiano ni jambo la msingi katika jamii. Katika riwaya tunaona mwandishi akisisitiza juu ya ushirikiano wa jamii kama njia ya kukabiliana na changamoto za maisha. Ushirikiano unasisitizwa katika kusaidiana na kufanya shughuli pamoja. Kwa mfano mwandishi anaonyesha jinsi watu walivyokuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana katika jumba la Adili; anasema;
“Wanawake kadha wa kadha walikuwa wanafanya kazi mhalimhali humo kushona, kufuma na kusuka. Walicheka wakainama mbele ya wageni hawa halafu walitoka kwenda zao jikoni…”  Uk 14
Ujumbe wa pili ni kuwa sadaka na ibada ni vitu muhimu katika maisha ya wanadamu. Mwandishi anatukumbusha kuwa kutoa sadaka huleta sihi na baraka katika maisha ya kila siku. Kwa mfano anasema;
“Mwenyezi Mungu husema kwamba leteni zaka zote katika ghala, mmjaribu kama hatawamiminia baraka ambayo hamtaweza kupokea." Uk. 8.
Tatu, dini iliyosafi ni ile inayosimamia masilahi na haki kwa kila mtu bila kujali mapokeo ya madhehebu. Kwa mfano anasema;
Huenda moja kwa moja katika maslahi kwa wote; haidhuru zimo au hazimo katika misahafu ijulikanayo.” Uk. 11.
MIGORORO
Baadhi ya migogoro iliyojitokeza katika kazi ni kama ifuatayo
Mgogoro kati ya mwanamke na mumewe juu ya malezi ya watoto. Mgogoro huu unaibuka pale mwanaume anapoacha kuwajibika katika kulea familia yake. Mwandishi anasema
“Aliniambia nusura angeniua mimi, au watoto kama nilishikilia kumsumbua” Uk 4
Mgororo kati ya masikini na matajiri. Mgogoro huu unachochewa na hali ya maisha ambayo inawapendelea wenye navyo na kuwaacha masikini katika mahangaiko yasiyo mwisho. Mwandishi anasema;
“Shindano la wazimu kati ya matajiri na masikini linaangamiza maisha ya mataifa katika ulimwengu”. Uk 4
Mgogoro kati ya Bi Nunu na muajiri wake. Huu unaibuka kutokana na kazi ya tafsiri aliyoifanya Bi Nuna na pale muajiri anapokataa kumlipa Bi Nunu pesa yake ya tafsiri. Mwandishi anasema;
“Nakariri kwamba kazi yako ni mbaya, tena umeharibu Makala yote. Fedha hii hapa shilingi arobaini na tano, nusu ujira chukua au acha”. Uk 31
Mgogoro kati ya Ayubu na mwajiri wa Bi Nunu. Huu ulichochewa na dhuluma aliyokuwa amemfanyia Bi Nunu.
FALSAFA
Falsafa ni imani aliyonayo juu ya maisha na ulimwengu. Katika riwaya mwandishi anaamini kuwa kuna maisha baada ya kifo hivyo watu wanatakiwa kutenda mema siku zote. Mwandishi anaamini kuwa ibada ya kweli ni ile inayojali wenye uhitaji na kuzingatia maslahi ya watu katika jamii.
Baada ya uhakiki wa vipengele vya maudhui.vifuatavyo ni vipengele vya fani
MUUNDO
Muundo ni mpangilio wa visa na matukio katika kazi ya fasihi. Mwandishi ametumia muundo moja kwa moja ili kuleta mtiririko mzuri wa visa na matukio. Kisa kinaanza kumuelezea Ayubu na shughuli yake ya kusimamia jumuia ya Jumba la Adili. Visa vinaendelea kwa kuonesha baadhi ya shughuli na misaada anayotoa Ayubu kwa jamii yake. Kisa kinaisha kwa ndoa ya Ayubu na sarah. Visa katika riwaya hii vimepewa majina kulingana na mawazo makuu yanaojadiliwa katika kila sehemu. Sura za riwaya hii ni 14 zenye vichwa Mabadiliko, Jumuia, Sadaka, Tafsiri, Kisichobadilika, Kufu, Kweli, Mkutano, Mandari, Jumamosi, Urafiki, Mshtaki, Riba na Fungate.
MTINDO
Katika kuwasilisha kazi yake mwandishi ametumia mtindo wa masimulizi. Msimulizi katika riwaya hii ni mwandishi mwenyewe na hili linadhihirika kwa matumizi makubwa ya nafsi ya tatu umoja na wingi. Pia kwa kiasi kidogo mwandishi ametumia dayalojia.
 Mwandishi ametumia uchanganyaji tanzu, ambapo aliingiza utanza wa ushairi katika baadhi ya sura ilihali kazi hii ni ya kinathari.  Ushairi umejitokeza katika ukurasa wa 7, 106, 76. Kwa mfano
“Tamati natia mwisho,kuwahadithia shani,
Hadithi ya furahisho kwa jamii duniani,
Kuwa kama makumbusho ya mtunzi Shaaban.” Uk106
Vilevile mwandishi anamalizia kazi yake kwa ubeti wa shairi. Mwisho huu ni wa kipekee tofauti na kazi nyingine za kinathari. Kwa mfano mwandishi anasema;
“Tamati natia mwisho,kuwahadithia shani,
Hadithi ya furahisho kwa jamii duniani,
Kuwa kama makumbusho ya mtunzi Shaaban.” Uk106
MATUMIZI YA LUGHA
Matumizi ya lugha ni kipengele cha mtindo kilichobeba nafasi kubwa katika kazi za fasihi. Katika riwaya mwandishi ametumia lugha kwa ustadi mkubwa huku akihusisha tamathali za semi, misemo, methali na maneno ambayo hayatumiki sana katika jamii.
Tamathali za semi zinazojitokeza katika kazi ni tashibiha, mubalagha na tashihisi.
Tashibiha ni tamathali ya semi inayotumia kiunganishi kufanananisha vitu. Kwa mfano;
“Mshupavu kama jiwe”. Uk. 30.
“Ayubu ana moyo mkavu kama vumbi na baridi kama jivu na si wingu.” Uk. 65
“Mwangaza mzuri kama ule wa jua katika wakati wa vuli.” Uk. 37.
“Meno ya mwanya yaliyokuwa sawa na safu mbili za lulu katika kinywa.” Uk. 40.
Tashihisi;        “Wakati ulimpokonya wembamba wake.” Uk. 18.
“Maji ya josho la tibata na miujiza ya pango yake yalipatukuza kuwa pahali pa mizimu.” Uk. 81
Matumizi ya methali na misemo. Baadhi ya methali na misemo iliyojitokeza katika kitabu ni
“Heri shari nusu kuliko shari kamili.” 38.
“Mkulima mmoja walaji wengi”. Uk 94.
“Maiti haikosi mzishi”. Uk. 100.
Kipengele kingine cha fani ni Wahusika. Mwandishi ametumia wahusika tofauti tofauti kuiumba kazi yake na kufikisha ujumbe kwa hadhira.  Wafuatao ni wahusika katika riwaya ya Siku ya Watenzi Wote.
Ayubu, Alikuwa kiongozi wa dini katika nyumba ya adili ambaye alikuwa akiwafundisha watu kuhusu maadili na kuisha maisha mema. Alikuwa mpwa wa Binti Akili, binamu wa Sarah na mwisho alimuoa Sarah.
Binti Akili ni mhusika mkuu ambaye amesawiriwa kama shangazi wa Ayubu na Sarah. Pia alikuwa rafiki wa mwanasheria Yusuff. Ni mwanamke aliyekuwa na elimu, kipenzi cha watu, mlezi kwa kuwa alimlea Sarah baada ya wazazi wa Sarah kufariki.
Sarah ni mhusika mkuu ambaye amesawiriwa kama msichana mwenye upeo mkubwa, alipenda kujifunza na kusaidia wasiojiweza. Rafiki wa Yusuff na Zena. Alilelewa katika misingi ya dini hata baada yakupokea mirathi alikubali kutoa nusu ya mali kuwapa maskini.
Yusuffu ni mwanasheria aliishi nchi za ugenini kwa muda wa miaka kumi. Alikuwa rafiki wa Bwana Azizi, Binti Akili, Bwana Zakaria, Sarah na Ayubu. Alikuwa na mali nyingi kama vile magari matatuya kifahari. Pia alipenda kujifunza kuhusu dini na kusaidia watu wenye uhitaji.
Mandhari ni sehemu na wakati ambao fanani anatumia kujenga matukio. Katika riwaya mwandishi ametumia mandhari ya Dar es salaam kuonesha maisha yalivyo. Ametaja maeneo kama kariakoo, Ilala, Mnazi mmoja, Maasai na Kichwele. Kwa mfano: Msimulizi anaanza kwa kusimulia,
"Watu wawili walikuwa wanapita Barabara ya Bagamoyo katika Dar es salaam kwenda Forodhani." Uk. 1.
Pia msimulizi ametumia mandhari ya nje ya Dar es salaam kwa kutaja mikoa kama vile Tanga ambapo ametaja pango la Amboni na visiwani Zanzibar.
Kuhusu wakati, riwaya hii imeandikwa miaka kipindi cha uhuru. Hili linadhihirishwa na kauli za baadhi ya wahusika. Kwa mfano Yussuf anasema
“Nilipokuwa hapa uhuru ulikuwa haujulikani. Na sasa tazama!”  Uk1
Jina la kitabu Siku ya Watenzi wote, linasawiri kile kilichopo katika kitabu kwani mwandishi anasisitiza wanadamu kujiandaa na siku ya ufunuo au siku ya hukumu. Maandalizi haya yanajumuisha kuaweka akiba ya wema na sadaka kwa Mungu na wahitaji, kusimamia utu na masilahi ya wengine.




No comments:

Post a Comment