Friday

WASIFU WA EBRAHIM HUSSEIN MWANAFASIHI NGULI WA KISWAHILI

0 comments



Imeandikwa na Profesa M.M.Mulokozi

EBRAHIM HUSSEIN (alizaliwa 1943)
Ebahim Hussein (baadaye EH) ni mshairi, mwandishi na mtambaji wa hadithi, mtunzi na mwigizaji wa tamthilia, mfasiri, mtengenezaji wa filamu, na msomi mahiri kabisa.


Alizaliwa 1943. Alisomea Aga Khan Dar es Salaam. Mwaka 1966-69 alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD) akijikita katika Fasihi, Kifaransa, Sosiolojia na Thieta. Mwaka 1970-74 alisomea Chuo Kikuu cha Humboldt, Ujerumani, na kubobea katika taaluma ya Thieta. Mwaka 1975 alirejea Tanzania na kuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadaye alikuwa Profesa wa Thieta katika CKD hadi alipoamua kuacha kazi mwaka 1985.


Hussein alitunukiwa Tunzo ya Uandishi ya UWAVITA mwaka 1988. Mwaka 1999 alitunukiwa Tunzo ya Zeze ya Mfuko wa Utamaduni Tanzania.

Kazi ya Uandishi

EB alianza kuandika akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka ya 1960. Wanafunzi wengine wa kipindi hicho waliojipambanua katika fasihi ni E. Kezilahabi na Penina Muhando.

 Kazi zake za mwanzo zilijikita katika masuala ya utamaduni na utambulisho (Wakati Ukuta) na shairi la Ngoma na Vailini. Mgogoro changamani wa kitamaduni unajidhihirisha katika mvutano wa vizazi, mvutano kati ya walisoma na wasiosoma (elimu ya Kizungu), mvutano kati ya Pwani na Bara, na mvutano kati ya Uislamu na Ukristo, na kati ya usasa na ujadi. Ujumbe muhimu tunaoupata katika tamthilia hiyo ni kwamba mabadiliko ni lazima na hayaepukiki.


Mgogoro huo wa utambulisho unaakisiwa vizuri  katika shairi lake la mwaka 1968 la Ngoma na Vailini.

Ngoma na Vailini   Huo, huo mpwitopwito wa ngoma Unachemsa damu yangu na matamanio yaliyo ladha  Damu iliyopozwa na kubembelezwa Na vailini nyororo, vailini inayonita Kwa huzuni yenye furaha.

 Sasa nachemka na kupwitapwita Sasa nna furaha na kuburudika Mdundo wa maisha Raha ya nafsi Wapi niende?  Lazima ni-swali, lazima niabudu Nimuabudu Allah Lakini ataisikia sauti yenye panda Sauti inayotokana na mwenye kuvaa Kanzu na msalaba?
Mwaka 1969 Hussein aliandika tamthilia ya Kinjeketile ambayo ilihusu mapambano ya kupinga utawala wa kikoloni wa Kidachi kusini mwa Tanzania. Tamthilia hiyo haikusawiri hisia za uzalendo tu, bali pia ilichambua suala zima la maana ya ukombozi kifalsafa; itakuwaje iwapo nabii wa ukombozi atashindwa katika azima yake ya kuwakomboa watu wake; je, neno alilolizaa litakuwa halina maana tena? Kiistiara, tamthilia hiyo inaweza kuchukuliwa kuwa fumbo kuhusu Nyerere na Azimio la Arusha, na hivyo kuakisi mgogoro mkuu wa kihistoria wa wakati wa kutungwa kwake.

Hussein alichapisha Mashetani mwaka 1971. Tamthilia hiyo ililitazama suala la mgogoro wa kihistoria wa kitabaka baada ya Uhuru na Ujamaa. Tabaka tawala la awali (kiuchumi), likiwakilishwa na Juma, linajikuta katika mvutano na tabaka jipya la vibwanyeye wa Afrikanaizesheni linalowakilishwa na Kitaru. Hatimaye tabaka la awali inabidi liporomoke wakati tabaka jipya linaota mbawa.  Kwa kutumia mbinu ya mchezo ndani ya mchezo, Hussein anauweka sambamba mgogoro huo baina ya vibwanyenye wenyeji [binadamu] na mgogoro wa kitaifa baina yao na Mzungu [shetani] anayeondoka, akiwakilisha mkoloni na lugha na utamaduni wake. Je, binadamu na shetani ni maadui, au ni marafiki? Shetani kauawa kweli au tayari kamteka mno binadamu kiasi cha utawala wake kubakia katika akili ya mtawaliwa japo mkoloni mwenyewe hayupo kimwili?

Arusi ni tamthilia inayodhaniwa kuzungumzia siasa, hasa matatizo ya Ujamaa ikiendeleza pale Kinjeketile ilipoachia. Kadhalika Arusi inadhaniwa kuzungumzia muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa njia ya mafumbo.  Mwandishi anabashiri matatizo katika ndoa hiyo.

Tamthilia ya kwenye Ukingo wa Thim ina mandhari ya Nairobi na Kisumu nchini Kenya. Hii pia inarejelea migogoro  ya kitamaduni na kifalsafa.
Yawezekana Hussein ameandika miswada mingine tangu 1988, lakini hakutaka kuichapisha.

EB alihusika katika mgogoro wa ushairi wa miaka ya 1960 na 1970 alipoamua kutunga mashairi huru kama lile la Ngoma na Vailini tulilolidondoa hapo juu. Mgogoro huo ulifikia kilele miaka ya sabini ulipoibuka mjadala mkali kati ya walioitwa washairi wa Mlimani au wa kisasa wakiongozwa na E. Kezilahabi, na washairi wa kijadi wakiongozwana A. Andanenga, S. Gonga, na watunzi wengine.

Tathmini

Hussein ndiye mwandishi bora wa tamthilia katika Afrika Mashariki, na anaweza kuwekwa kwenye ulingo mmoja na Wole Soyinka wa Nijeria. Kazi zake zinahusu matatizo ya Afrika yote, na hata ulimwengu mzima, japo yanatazamwa kwa jicho la Kitanzania. Masuala ya ukombozi wa mwanadamu (si wa kisiasa tu), migongano ya kitamaduni na kitaifa, mgogoro wa vizazi, mivutano ya kitabaka, yanajitokeza katika kazi zake. Usaliti wa Uhuru, ambapo Mkombozi anageuka kuwa mkandamizaji, unsawiriwa katika tungo zake za Ngao ya Jadi na Jogoo Kijijini na nyinginezo.  Tanzia ya Mwafrika ambaye amekuwa mtumwa na kisha raia wa kikoloni na mateka wa mataifa mengine inaoneshwa vizuri katika kazi zake  Mwafrika anaendelea kuwa mateka kiroho, kinafsi na kitamaduni (achilia mbali kisiasa na kiuchumi) hata baada ya uhuru wa bendera: Hebu tuone vifungu vichache kutoka katika tamthilia ya Mashetani:



SHETANI:  Rafiki mpenzi, rafiki mwandani. Rafiki wa milele. Rafiki wa daima. Ninakupokea. Ninaifurahikia leo, siku ya uzao wako. Kutoka katika tumbo la giza jeusi, kuingia katika ulimwengu wa nuru nyeupe.  (msisitizo ni wangu)
BINADAMU:  Uko wapi?
SHETANI:  Hunioni. Huwezi kuniona. Nimejigeuza upepo. (Anacheka). Hunioni lakini unanihisi. Huna la kunifanya eh? (Anacheka).  Wewe huogopi kugombana na mtu usiyemwona na ambaye anakuona?
BINADAMU:  Na fadhila gani uliyonipa wewe?
SHETANI.  Umeshasahau mara? Sikuwa mimi rafiki yako mkubwa? Sikuwa mimi ndugu kipenzi?  Sikukutoa gizani nikakuonyesha mwangaza? Nikakufanya mwandani wangu, nikakupa siri yangu. Leo unaitumia siri hii kunidhuru mimi? (Msisitizo ni wangu).
BINADAMU:  Na wewe vilevile ulitaka siri hiyo kunidhuru mimi  kunikatakata maini, kunigawanya, kuutoa mwili wangu katika nafsi yangu. Ile haikuwa siri au hidaya; ile ilikuwa sumu. Ile ilikuwa nafsi na roho yako uliyotaka kuipuliza katika hali yangu.
(E. Hussein, 1971 Mashetani, uk. 1- 8)


Maneno haya yaliyosisitizwa yana maana kubwa. Binadamu (Mwafrika Mweusi) anatolewa katika weusi wake (giza jeusi) na kuingizwa katika Uzungu (nuru nyeupe). Baadaye Binadamu anapozindukana hamwoni Shetani.  Mkoloni hayupo kimwili tena, bali yuko katika hisia, imani, fikira, lugha na matendo ya watawaliwa. Mwafrika tayari amekwishatekwa kiakili.
Hapa tunauona mgogoro wa ki-“Prospero na Kaliban” (Shakespeare).

E. Hussein anaisawiri tanzia hii ya Mwafrika kwa lugha nzuri na fasaha ya Kiswahili. Uamuzi wake wa kutumia Kiswahili (naweza kuzungumza na kuandika lugha 5: Kiswahili, Kiingereza, Kifaransa na Kidachi, na labda Kiarabu) unatoa ujmbe muhimu kuhusu utetezi wake wa utaifa na utambulisho wa Mwafrika.

Kwa upande wa sanaa na mtindo, E. Hussein anatajwa kuwa mwanzilishi wa mtindo mpya wa uandishi wa tamthilia na ushairi. Mbali na kuandika tungo-huru tangu miaka ya 1960, Hussein vilevile ameandika maigizo ya kimajaribio (Jogoo Kijijini na Ngao ya Jadi) ambayo ni tendi zinazotokana na ngano au hekaya na zilizokusudiwa kutendwa jukwaani.

Matumizi ya lugha katika kazi za Hussein ni ya kiwango cha juu sana; inabidi mtu afasiri ishara zilizotumika ili kupata maana iliyomo. Hali hii ndiyo inayowafanya baadhi ya watu waamini kuwa anatumia lugha ngumu japo kwa hakika lugha yake si ngumu, bali tamathali na ishara zake ndizo ngumu zenye kujikita katika utamaduni wake wa Kiswahili uliochanganya na usomi na falsafa za ki-Magharibi.

Pamoja na hayo, Hussein hana utaifa au ukabila finyu katika uandishi wake, bali ni Mwafrika Mashariki. Tamthilia ya Kinjeketile ina mandhari ya nyumbani kwao Lindi,  bali kazi zake nyingine zinatendeka katika miji mbalimbali ya Tanzania; Jogoo Kijijni na Ngao ya Jadi zina mandhari ya Uganda, japo maudhui yanahusu Afrika nzima; na mandhari ya Kwenye Ukingo wa Thim ni Kenya.
Baadhi ya kazi za kisanaa alizoziandika E. Hussein:
 Alikiona (1967)
Wakati Ukuta (1969)
 Kinjeketile (1969)
 Mashetani (1971)
 Arusi (1980)
 Kwenye Ukingo wa Thim (1988)
 Ngao ya Jadi (1976) (hadithi inayotendwa jukwaani)
 Jogoo Kijijini (1976)  (hadithi inayotendwa jukwaani)

Tafsiri

Jambo la Maana (H. C. Andersen)
10)Samaki Mdogo Mwusi, n.k.

Marejeleo Teule

Jamaliddini, A 2006/1910 Utenzi wa Vita vya Maji Maji. TUKI, Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M 1976 "Uhakiki wa Kinjeketile"  Kioo cha Lugha 4: Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu Dar es Salaam.


Mulokozi, M.M & Shani Kitogo Usawiri Na Taathira Ya Vita Vya Majimaji Katika Fasihi [Simulizi na Andishi]. Tanzania Zamani (Journal of Historical Assoc. of Tanzania), Vol. 6 No. 2: 1-25.


Mwaifuge,  E.S 2009 Art and History: Ebrahim Husseins Kinjeketile. Tanzania Zamani (Journal of Historical Assoc. of Tanzania), Vol. 6 No. 2: 26-46.


Mwaruka, R 1968 Utenzi wa Jamhuri ya Tanzania. EALB, Arusha: Beti 252-293.
Ricard, A. 2000. Ebrahim Hussein, Swahili theater and Individualism. Dar es Salaam: Mkuki na Nyota.


Sengo, T.S.Y 1973 Ebrahim Hussein: Mwandishi wa Michezo ya Kuigiza. Katika Sengo, T.S.Y na Saifu D. Kiango 1973 Hisi Zetu. TUKI, Dar es Salaam: 58-95.

No comments:

Post a Comment