Baadhi ya waajiri hutumia fursa hiyo kutimiza matakwa yao na kuwaacha waliojiunga na programu hizo wakihangaika.- Wadau wasema mtu anatakiwa kukaa katika programu hizo kwa miezi sita hadi 12, baada ya hapo aajiriwe.
- Wengine wasema internship ni makubaliano ya kijana na mwajiri, hawapaswi kuingiliwa.
Dar es Salaam. Mara baada ya kumaliza masomo ya elimu ya juu, ni ndoto ya vijana wengi kupata kazi katika makampuni mbalimbali kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Hata hivyo kutokana na ugumu wa kupata ajira unaosababishwa na nafasi chache za kazii, baadhi yao huamua kujiunga na makampuni kwa ajili ya program za mafunzo ya kuongeza ujuzi wa kufanya kazi (Internship) kupata maarifa yanayostahili.
Kwa baadhi ya makampuni, kipindi hiki hutumika kumuandaa mtu kwa nafasi iliyopo wazi au kumfundisha mtu ajipatie maarifa na ujuzi anaoustahili.
Mwongozo wa Taifa wa programu hizo (National Internship Guidelines) uliotolewa na wizara Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu mwaka 2017, unaeleza programu hizo zinapaswa kufanyika kati ya miezi sita hadi 12.
Hata hivyo, suala hilo limekuwa na maoni tofauti kutoka kwa wadau hasa ya muda ambao mtu anatakiwa kuutumia katika programu ya internship kabla ya kupata kazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni huduma za mawasiliano na mahusiano ya umma ya Serengeti Bytes, Kennedy Mmari amesema internship ni kipindi ambacho mwajiri anampima mtu kwa kumpatia mafunzo kivitendo ili kuufahamu ulimwengu wa kazi na kumuondoa kwenye hali ya unadharia kama alivyofundishwa chuoni.
Licha ya kuwa wapo vijana ambao hukaa katika programu hizo kwa zaidi ya mwaka mmoja, Mmari amesema “mwajiri akikaa na mtu zaidi ya miezi sita kama intern (mtu wa mafunzo) anatakiwa kumpatia mkataba wa kazi.”
Afisa Mwajiri wa kampuni ya kusambaza dawa za binadamu ya Kas medics, Gerald Kanza amesema muda wa mtu kuhudumu kama intern unategemea zaidi kasi ya mtu kujifunza na kuelewa maarifa anayopewa na uzito wa majukumu ya mwajiri.
“Kinaweza kuwa kipindi cha miezi sita ndiyo lakini zipo kazi ambazo mwajiri husafiri kwa zaidi ya hata miezi miwili ambayo anakuwa nje ya ofisi. Huyo Intern anawezaje kujifunza mwenyewe? Inabidi mwajiri aendelee kumsoma intern na kuhakikisha amejifunza kwa kiwango stahiki,” amesema Kanza.
Naye John Pascal ambaye ni mtaalam wa masuala ya vijana amesema maana ya internship itazidi kupotea baadae endapo wahusika wanaofanya kazi hizo watakosa muamko wa kuchukua hatua na kufanya sawasawa na sheria zilivyo katika makampuni na mashirika maalum.
“Kwaasilimia kubwa mtu unapokubali kukaa kwenye internship mpaka mwaka mzima, ina maana wewe umeridhika na hali hiyo. Hivyo ili kukemea hali hii ni wajibu wa wahusika kuamka.” Amesema John.

Internship ni takwa la kisheria?
Mwanasheria kutoka kampuni ya Uwakili ya Extent Corporate Advisory (ECA), Nabiry Jumanne amesema Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 haijaongelea kuhusiana na masuala ya internship lakini Serikali imeweka utaratibu wa kufuata.
Nabiry amesema sheria hiyo imejikita kuongelea juu ya mahusiano ya mwajiri na mtu ambaye ameajjiriwa.
Mtu anayefanya kazi kama intern siyo mwajiriwa na mara zote hufanya kazi kutokana na makubaliano aliyonayo na kampuni.
Wakili mwanafunzi wa Shule ya Sheria (Law School), Neema Nyanda amesema masuala yote yanayohusiana na internship yanafanywa ndani ya kampuni kwa sababu “hakuna mtu wa nje anayehusika.”
Licha ya miongozo iliyowekwa kusimamia internship, bado baadhi ya waajiri wamekuwa wakitumia changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, kuwaingiza katika programu hizo pasipo kuwaajiri hata baada ya kukamilisha mafunzo hata kama nafasi zipo.
Baadhi yao, ambao wameongea na mtandao Huu, . ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamesema programu hizo zinawasaidia kupunguza gharama za uendeshaji kampuni kwa sababu wanaingia katika programu hizo hawalipwi au wanalipwa posho kidogo lakini ujuzi wao unatumika kuifaidisha kampuni.
Hata wakati dhana nzima ya internship ikichukua sura mpya, vijana bado wana nafasi nzuri ya kuchangamkia fursa hizi kwa sababu zina manufaa mengi.
Lakini wakati programu hizo, kuna mambo mengi ya kuzingatia kuhakikisha unapata maarifa sahihi yatakayokuwezesha kuwa na sifa za kuajiriwa:
Kuwa mvumilivu
Uvumilivu huja kwa sura nyingi, inaweza kuwa katika changamoto zinazomkabili kijana anapokuwa mahali pa kazi pamoja na uchu anaokuwa nao kijana kukua kiuchumi kwa maana ya kupata malipo katika mafunzo.
Kwa makampuni mengi interns wanapewa pesa ya kujikimu pekee ambapo kwa mujibu wa waajiri walisema hakuna kiasi maalumu.
Meneja Jamii na Programu wa kampuni ya Seedspace Dar es Salaam, Mohammed Shellimoh amesema waajiri hufanya hivyo kufidia nauli na pesa ya chakula kwa vijana wanaokuwa kwenye programu hizo.
Jifunze kila kitu
Wakati baadhi ya intern wakilalamika kufanya kazi nyingi wawapo kwenye ofisi, Chrisostom Bwemo ambaye ni Mbunifu wa Programu amesema kipindi chake cha internship ndicho kilichomjenga kufikia kwenye ubora alionao sasa.
“Nikiagizwa kwenda kuchapisha kablasha nitaenda kwani nitajifunza hata jinsi ya kufanya hilo. Huwezi jua ni wapi utahitaji kutumia maarifa hayo,” amesema Bwemo.
Zaidi, amesema kipindi hiki ni muhimu kwa kila kijana kwani atapata maarifa tofauti tofauti hivyo ni vyema vijana wautumie muda huu ipasavyo.
Ni dhahiri kwamba vijana huenda hawatumii rasilimali walizonazo kujiendeleza katika kujua matumizi sahihi ya teknolojia zitakazowasaidia maishani.
Ili kuepuka kubaki nyuma, wadau mbalimbali wameshauri vijana kuutumia muda huu kuhakikisha wanajifunza mambo haya ili waweze kushindana sokoni

Mikakati ya Serikali
Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kutengeneza mwongozo wa programu ya mafunzo ili kuhakikisha vijana wanapomaliza masomo yao waweze kupata maeneo ya kupata uzoefu katika taasisi na mashirika ya sekta binafsi.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Antony Mavunde amesema wanachukua hatua mbalimbali kuwasaidia wahitimu wa vyuo vikuu ili kukabiliana na changamoto za ajira kwa kuwaongezea ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.
“Kwa sasa Serikali inawachukua vijana wa elimu ya juu na vyuo vikuu tunakwenda kuwaweka katika makampuni na viwanda mbalimbali, wanajifunza kwa miezi sita hadi 12. Akitoka anapata certificate of recognition (cheti cha kumtambua) ambapo akienda kuomba kazi, hiyo inakuwa ni kigezo tayari anakuwa amepata uzoefu ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira,” amesema Mavunde jana (Februari 7, 2020) Bungeni jijini Dodoma.
Amesema kati mwaka 2016 hadi 2021 wizara yake inaendesha programu maalum ya ukuzaji wa ujuzi wa vijana yenye lengo ya kuwafikia vijana milioni 4.4 ifikapo 2021 ili vijana hawa wapate ujuzi waweze kujiajiri na kuwaajiri vijana wengine.
Ripoti hii imeandaliwa na waandishi wa habari: Rodgers George na Tulinagwe Malopa