Wednesday

SEHEMU YA KIINI CHA KITABU

0 comments
*SOMO LA TANO*

MADA: *SEHEMU YA KIINI CHA KITABU*

Wapendwa, karibuni katika somo letu la leo. Somo linahusu sehemu za kitabu na mpangilio taarifa. Nianze kwa kukumbusha kwamba, katika somo la Nne, tuliona kuwa kitabu kina sehemu kuu nne. Sehemu hizo ni *kurasa za mwanzo, kurasa za maandishi yenyewe, kurasa za mwisho na hatimaye jalada.* Sasa, tayari tumeshaona sehemu ya kwanza ambayo ni kurasa za utangulizi. *Katika somo la leo tutaendelea na sehemu ya maandishi yenyewe ya kitabu.*

*Sehemu ya pili: Maandishi ya kitabu*
Sehemu hii ni nyeti sana. Sehemu hii inapaswa kutendewa haki kwa umakini kwa sababu ndiyo uwanja ambao mwandishi anapaswa kuuchezea vyema. Sehemu ya mwanzo ilikuwa ni ya maandalizi tu ili sasa mwandishi aingie uwanjani na kucheza mchezo wake kwa watazamaji ambao ni wasomaji. Hapa kunahitaji umakini katika uteuzi wa lugha ya kutumia, kupangilia hoja vizuri na kimantiki ili wasomaji wafuatilie kile ambacho mwandishi anataka kukisema. Tukumbuke kwamba, wasomaji walikuwa wanasubiri sehemu hii kwa hamu kubwa. Sasa ni kazi yako mwandishi kupakua chakula chako kwa umakini na weledi wa hali ya juu ili msomaji akimaliza kusoma anufaike kimaarifa.

Katika kupangilia mawazo yake kimantiki, mwandishi lazima agawanye  mawazo yake matika mafungu ambayo tunayaita *Sura.*  Kimantiki, kila sura inapaswa kuwa na wazo ambalo linajisimamia lakini lisilopingana na sura zingine. Sura zinapaswa kujengwa kwa namna ya kupokezana. Tukumbuke kwamba msomaji anaposoma kuanzia sura ya kwanza na kuendelea ni kama mtu anayetembea kuelekea sehemu fulani huku akikanyaga tofari moja baada ya jingine. Hivyo, sura hizi ni kama matofari ambayo hupangwa vizuri ili kuwezesha safari ya msomaji kwenda vizuri zaidi. Hivyo, sura zinapaswa kujengwa kwa umakini ili zisipoteze welekeo wa wazo kuu la mwandishi. *Tunaposema wazo kuu tunamaanisha lengo la kitabu ambalo hudokezwa na jina la kitabu tangu mwanzo.* Sura zinapaswa kulisana wazo la mwandishi na kuwezesha wazo hilo kupokezanwa kutoka sura moja hadi nyingine.

Wazo kuu au jina la kitabu ninalifananisha na tunda ambalo linaonekana zuri sana ukiwa kwa mbali. Msomaji anapopita dukani au maktabani akaona kitabu chako, hupenda jina la kitabu na pengine hata picha au mwonekano wa nje. *Hapo tunaweza kusema kwamba msomaji ameliona tunda kwa mbali sana na kulipenda.* Baada ya kutamani kitabu chako, basi hukinunua na kuweka malengo ya kukisoma. *Swali ni je, atakapokisoma na kumaliza, atauona ule uzuri aliouona mwanzoni?* Mwandishi makini akiwa na wazo hili akilini, basi lazima aisane sehemu hii ya kitabu kwa umakini na ufundi wote. *Katika mazingira haya sura zako zitakuwa kama matofali ambayo msomaji atayakanyaga wakati akienda kuangua tunda.* Ukipanga matofali yako vizuri, basi msomaji ataifurahia sana safari yake. Ukiharibu hapa, huenda msomaji akaweka kitabu chako pembeni. *Hapa ni sawa na aliyekata tamaa na kuamua kurudi nyumbani na kuliacha tunda.*

Mwandishi anapoisana sehemu hii lazima afikiri kwamba msomaji ameacha kazi nyingine na kuanza kusoma kazi yake. Katika mazingira hayo, lazima kuwe na lugha ya ushawishi, lugha ya kuvutia na ya kumburudisha msomaji kwa maarifa, kiasi cha kumfanya asiache kufuatilia mtiririko wa mawazo ya kitabu. Hivyo, katika sura hii, tunatarajia kuona ubunifu wa mwandishi kwa kiwango cha juu.

Aidha, katika kueleza mawazo katika sura, tunatarajia kwamba mawazo hayo yatapangiliwa katika mafungumafungu ambayo huitwa *Aya.* Aya hizi zinapaswa kupokezana taarifa kama wakimbiaji wanaopokezana vijiti. Kila aya inapaswa kuwa na wazo tofauti na aya nyingine kabla na baada yake. Yote haya, yanategemea uwezo, umahiri na umakini wa mwandishi.

Nimalize sehemu hii kwa kusema kwamba mwandishi anapaswa kupakua chakula chake kwa umakini na weledi ili kumpatia msomaji chakula kifaacho.

*©L.H. Bakize (18.03.2020)*
Chini ya EWCP na Ushirikishanaji Maarifa.


KARIBUNI KWA MJADALA
==============

No comments:

Post a Comment