Friday

SEHEMU ZA MWISHO ZA KITABU

0 comments


MADA: *SEHEMU ZA MWISHO ZA KITABU*

Wapendwa, karibuni katika somo la leo. Somo la leo litahusu *sehemu za mwisho za kitabu na jalada.* Imani yangu ni kwamba sote tumeshasoma somo la Nne na la Tano na kuelewa sehemu ya kwanza na ya maandishi katika kitabu. Sasa leo, tutamalizia sehemu mbili zilizobaki.

*Kurasa za mwisho wa kitabu*
Kurasa za mwisho wa kitabu zina vipengele vidogo kadhaa kama *Marejeleo/Bibliografia, Faharasa (Index) na Sherehe/Ufafanuzi wa maneno mapya (Glossary).* Ili kuelewa vizuri, ni vyema tukaangalia vipengele hivyo vidogo vya mwisho wa kitabu kwa umahususi wake.

*Marejeleo/Bibliografia*
Kuna mambo mawili hapa ambayo tunapaswa kuyafahamu kabla ya kwenda mbali. Jambo la kwanza ni kwamba neno *Marejeleo* limezoeleka kama *Marejeo.* Katika mjadala wetu ninapendekeza tutumie neno Marejeleo kwa maana ya kurejelea vyanzo vya maarifa au taarifa, ukitamka neno marejeo kuna hali ya ukakasi fulani unaoonesha kurudi kwa mtu au kitu. Kwamba mtu fulani hakuwapo kwa muda fulani na sasa amerejea. Hata hivyo, huu ni ushauri tu. Kwa wale wanaopenda tuendelee kuandika kwa mazoea hawawezi kukubali hoja hii. Lakini, katika uandishi wa kisasa, vitabu kadhaa vimeanza kutumia neno *Marejeleo* badala ya *Marejeo.*

Jambo la pili ni uhusiano wa neno *Marejeleo* na *Bibliografia.* Maneno haya mawili yamekuwa yakikanganywa kwa muda mrefu. Katika Kamusi na vitabu vingine vingi, maneno hayo yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni visawe. Kwamba mwandishi anaweza kuandika marejeleo au bibliografia kwa sababu yote ni sawa. *Pamoja na hayo, sisi tujitofautishe kwa sababu tunataka kuandika kwa kufuata taratibu za uandishi na uchapishaji makini wa vitabu.* Kwanza tukiri kwamba maneno hayo yanahusiana na kufanana sana kwa kuwa yote yanamaanisha orodha ya vyanzo vya maarifa. Hata hivyo, tuweke mpaka ili tuone tofauti kidogo.

*Marejeleo (references)* Hii ni orodha ya vyanzo vyote vya maarifa ambavyo vimetumika katika kitabu au andiko. Hapa hatutarajii kuona chanzo cha maarifa ambacho hakijatajwa ndani ya kitabu.

*Bibliografia (Bibliography)*
Hivi ni vyanzo vya maarifa ambavyo vimetumika ndani ya kitabu na vingine ambavyo vinapendekezwa kwa ajili ya kupanua zaidi maarifa. Hivyo, hapa tunatarajia kuona orodha ya machapisho au vyanzo vyote vilivyorejelewa ndani ya kazi, pamoja na vyanzo vingine ambavyo msomaji anashauriwa kusoma zaidi ili kupanua maarifa yanayohusiana na mada ya kitabu. *Tukiweza kuelewa hapa, basi tutakubaliana kwamba Marejeleo na Bibliografia ni mambo mawili yanayohusiana, lakini yanayoachana kidogo mahala.* Elimu hii inapatikana katika uga wa uandishi na uchapishaji tu. Ukiangalia maana za Marejeleo na Bibliografia katika vyanzo vya kawaida kama Kamusi za Kiswahili na Kiingereza, si rahisi kuweza kutofautisha mambo haya mawili.

Nitoe mfano mdogo tu ili kuweka sawa tofauti kati ya Marejeleo na Bibliografia. Mwandishi anapoandika kitabu anatumia vyanzo mbalimbali. Katika kuandika kazi yake, kuna mahala mwandishi atalazimika kutaja chanzo kwa unahusi ndani ya kazi ili kutoa mfano, kusisitiza au kufafanua zaidi hoja zake. Anaweza kutaja chanzo kwa kunukuu maneno, sentensi au kutaja tu chanzo husika kwamba kina maarifa fulani. Aidha, kwa upande mwingine, mwandishi anapoandika kazi yake anakuwa amesoma vyanzo vingi sana vya maarifa. Vyanzo hivyo si vyote vitakavyooneshwa kwenye kazi hiyo kwa umahususi. Hivyo, mwandishi atakapoorodhesha vyanzo vyote vilivyotumika ndani ya kazi yake basi atumie neno *'Marejeleo'* na endapo mwandishi atataka kuonesha vyanzo vyote alivyovisoma wakati anaandaa kazi yake, hata kama vyanzo vingine hajavinukuliwi kwa umahususi ndani ya kazi yake, basi aandike *'Bibliografia.'*

*Faharasa/Faharisi*: Faharasa au Faharisi ni orodha ya mada, maneno au majina yaliyotumika ndani ya kitabu inayooneshwa mwishoni mwa kitabu husika. Faharasa pia inaonesha kurasa ambazo majina, maneno au mada tajwa hupatikana ndani ya kitabu. Kitaalamu, *Faharasa* ni kama kipengele cha *Yaliyomo* ambacho kimepanuliwa zaidi. Kipengele hiki huwa kinatarajiwa kiandaliwe kwa Kompyuta. Si rahisi kwa mwandishi kuandaa kipengele hiki kwa kuandika majina, maneno au mada zilizotumika kitabuni kwa kutumia njia ya kawaida. Aidha, kipengele hiki ya Faharasa huwa kinaandaliwa baada ya mswada kusetiwa kwa ajili ya kuprintiwa. Hapo ndipo mtu anayeandaa Faharasa anaweza kujiridhisha kwamba majina, maneno au mada husika vitaweza kuoneshwa vinapatikana kwenye kurasa zipi kwa usahihi. Inashauriwa kuandaa Faharasa katika hatua za mwisho ili kipengele hicho kioneshe uhalisia. Majina na mada zinazooneshwa kwenye Faharasa huandikwa katika mtiririko wa alfabeti ili kumrahisishia msomaji kupata majina, maneno au mada hizo kwa urahisi. Ikiwa umakini hautatumika vyema, kuna uwezekano majina, maneno au mada zinazooneshwa kwenye Faharasa zikapishana na kurasa halisi kitabuni. Nia hasa ya Faharasa ni kumwezesha mtu anayetaka kutafuta jina, neno au  mada kitabuni, kuvipata haraka na kwa urahisi. Aidha, Faharasa inaweza kuwasaidia watafiti ili wafahamu kwamba neno au jina fulani limejirudia mara ngapi ndani ya kazi.
 *Kwa njia ya kupitia Faharasa, ndiyo maana mtu anaweza kukuambia kwamba jina Maria, Yesu, Yosefu au jina jingine, kwamba limetajwa mara ngapi kwenye Biblia Takatifu.* Aidha, ikumbukwe kwamba vitabu vingi havina Faharasa. Huenda ni kwa sababu waandishi wengi hawajui umuhimu wa kipengele hiki au pengine bado hatuna wataalamu wa kututengenezea kipengele hiki kwa kompyuta.

*Sherehe (Glossary)*
Hii ni orodha ya maneno na ufafanuzi wake ambayo huandikwa mwishoni mwa kitabu. Nia ya kipengele hiki ni kumpa msomaji maana za maneno magumu au ufafanuzi zaidi wa maneno yaliyotumika kitabuni. Hii itamsaidia msomaji kupata maana iliyokusudiwa anapokutana na neno hilo kitabuni. Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kwamba *Sherehe* ni kama *Kamusi* ndogo ya maneno yaliyotumika kitabuni na ambayo mwandishi anadhani yasipofafanuliwa maana zake, yanaweza kuathiri ujumbe wa mwandishi kwa msomaji.

*Jalada la kitabu*
Jalada la kitabu si geni kwa waandishi na wasomaji. Hii ni kwa sababu jalada ni kitu kinachoonekana kirahisi hata kabla mtu hajafungua na kuanza kusoma kitabu chochote. Katika hali ya kawaida, tunaweza kusema kwamba jalada la kitabu ni kama mlango wa kuingilia kwenye kitabu. Pia, kwa waandishi makini, jalada linatengenezwa kwa unadhifu na hivyo kuwa kama chambo cha kumnasa msomaji ili achague kitabu husika awapo sokoni au maktabani. Hivyo, jalada linapaswa kuandaliwa kwa umakini ili liwe la kuvutia hata kwa kutazama. Jalada linapaswa walau kudokeza kile kinachopatikana ndani ya kitabu husika.

Kwa kawaida, jalada lina mwonekano wa mbele na wa nyuma. Katika mwonekano wa mbele, jalada linapaswa kuwa na jina la kitabu, mwandishi (waandishi) wa kitabu (au mhariri/wahariri), mchapishaji, namba za mtiririko iwapo kitabu kinafuata mtiririko na taarifa za toleo husika la kitabu kama zipo. Kwa upande wa nyuma ya jalada, tunatarajia kupata maelezo kidogo na picha ya mwandishi kama ni muhimu. Taarifa na picha ya mwandishi vinapaswa kubadilishwa kutoka kitabu kimoja  hadi kingine ili kuepuka kuwachosha wasomaji. Aidha, uso wa nyuma wa jalada wengine huuita *Blabu.* Blabu ni maelezo mafupi kuhusu kitabu yanayoandikwa nyuma ya jalada. Hapa pia, kunaweza kuwa na nukuu fupifupi za wasomaji wa mswada zenye nia ya kukipigia upatu kitabu. Nukuu hizi zinatarajiwa kuwa zile zinazokisemea vizuri kitabu ili kuwavutia masomaji. Nukuu hizi mara nyingi hutarajiwa zitolewe na wasomaji wa mswada ambao wanafahamika zaidi katika eneo aliloliandikia mwandishi. Nukuu hizo huwahakikishia wasomaji kwamba kitabu hicho ni kizuri na hata wabobevu wa eneo husika nao wamesoma na kukubali kwamba ni kitabu kizuri.

*© L.H. Bakize (20.03.2020)*

==========

KARIBUNI KWA MJADALA

No comments:

Post a Comment