Saturday

Wanafunzi zaidi ya 38,000 kukosa mkopo elimu juu 2020-21

0 comments

  • HESLB imesema imepokea na kusajili jumla ya maombi ya wanafunzi 92,947.
  • Wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza ndiyo watakaopata mikopo hiyo 2020/21. 
  • HESLB imesema kuanzia saa 6 usiku wa leo, mfumo wake hautoruhusu kupokea maombi mapya.

Dar es Salaam. Wakati Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikitangaza kufunga dirisha la maombi ya mikopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020/21, zaidi ya wanafunzi 38,000 waliowasilisha maombi huenda wakaukosa mkopo huo. 
HESLB katika taarifa yake iliyotolewa leo (Septemba10, 2020), imesema imefunga rasmi dirisa la maombi ya mkopo kwa njia ya mtandao kwa mwaka wa masomo 2020/21.  
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema mfumo wa maombi hautaweza kuruhusu usajili wa maombi mapya ya waombaji isipokuwa kwa waombaji 7,500 waliopo mtandaoni ambao hawajakamilisha maombi hayo.
“Leo Alhamisi (Septemba 10, 2020) saa 6:00 usiku dirisha la upokeaji wa maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2020/21 kwa njia ya mtandao, litafungwa rasmi. Baada ya muda huo, usajili kwa ajili ya maombi mapya hautaruhusiwa,’’ amesema Badru. 
Hadi kufikia leo Septemba 10, 2020 wakati dirisha la maombi litafungwa HESLB imepokea na kusajili jumla ya maombi ya wanafunzi 92,947.
Hata hivyo, Agosti 31 mwaka huu wakati bodi hiyo ikiongeza siku 10 za maombi, Badru alisema katika mwaka wa masomo 2020/21, wanafunzi 54,000 wa mwaka kwanza wanatarajia kupata mikopo. 
Hiyo ina maana kuwa wanafunzi 38,947 sawa na asilimia 41.9 ya waliowasilisha maombi mpaka leo hawatapa mikopo hiyo.

Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga Sh464 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 145,000 wa taasisi za elimu ya juu na kati yao, 54,000 wanatarajiwa kuwa ni wa mwaka wa kwanza.
Rais John Magufuli  alipokutana na wanafunzi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) mkoani Iringa Mei 3 2018 alisema Serikali haiwezi kutoa mikopo ya masomo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu licha ya kuwa  imekuwa ikiongeza fedha za mikopo na kuwakopesha wanafunzi wengi zaidi.
"Nataka niwahakikishie Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini lazima niwaambie ukweli Serikali haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi wote" alinukuliwa Rais

No comments:

Post a Comment