FAFANUA
MAANA YA FASIHI SIMULIZI KWA KUREJELEA MAONI YA WATAALAMU TOFAUTI.
v Maana ya fasihi simulizi
Fasihi simulizi imeelezwa kwa namna tofauti
na wataalamu mbalimbali wa fasihi.
Finnegan (1970) anaeleza kuwa fasihi simulizi ni
sanaa ambayo hutegemea msanii ambaye huiumba kwa maneno katika tukio maalumu.
Katika fasili hii Finnegan hajagusia mambo muhimu katika fasihi simulizi kama
vile muktadha, namna ya uwasilishaji, uhifadhi na badala yake amejikita zaidi
katika ubunifu alionao msanii anayeiumba fasihi husika.
Kirumbi (1975:15) ameona kwamba, fasihi simulizi ni
masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa mdomo, si masimulizi yaliyoandikwa tangu
awali, kwa ajili hii basi, tutaona katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa
ulumbi (ufundi wa kusema).
Matteru
(1983:26) anatueleza kuwa fasihi simulizi ni
aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo kwa kuumbwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa
wasikilizaji na watumiaji wake. Aidha Matteru anaendelea kusema kwamba, fasihi
simulizi ikiwa ni sanaa itumiayo maneno katika kutoa dhana fulani, hutegemea
sana nyenzo mbalimbali za kuonekana na kusikika zitumiwazo na binadamu katika
kujieleza.
Msokile (1992:3) anasema kuwa fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia
lugha. Kazi hiyohuifadhiwa kwa kichwa na kusambazwa kwa njia ya masimulizi ya
mdomo. Anamalizia kwakusema kwamba,
fasihi simulizi imekuwa ikirithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Fasili hii ina ubora
wake kwa sababu ni kweli fasihi simulizi hurithishwa kutoka kizazi
hadi kizazi na pia njia kuu ya uwasilishaji wake ni masimuliizi ya mdomo,
lakini kwa upande mwingine
ina mapungufu kwa sababu inaonesha njia moja tu ya uifadhi wa fasihi simulizi kwa maana kwamba fasihi simulizi huhifadhiwa kichwani tu, haijazungumzia njia zingine za uhifadhi wa fasihi simulizi zilizotokana na
maendeleo endelevu ya sayansi na teknolojia kama vile vinasa sauti, kanda za kurekodi
na maandishi.
Mlacha (1995:16) ametueleza kwamba fasihi simulizi
ni nyanja katika maisha ya jamii am- bayo huchangia sana katika kuiendeleza na
kuidumisha historia ya jamii husika. Alipokuwa akifafanua zaidi juu ya fasihi
simulizi Mlacha alisema kuwa ‘fasihi simulizi huchangia katika kuelimisha jamii
kuhusu asili yake, chanzo na maendeleo ya utamaduni wake na maisha ya jamii
hiyo kuanzia zamani’.
Wamitila (2003:44) anatueleza kwamba, fasihi simulizi
ni dhana inayotumika kurejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya
masimulizi au kwa mdomo. Yeye kwa hakika hayuko mbali sana na msingi mkuu wa
fasihi simulizi uliosababisha kuwepo kwa tawi hili la fasihi. Kwa upande
mwingine Wamitila (2003:15) anatueleza kuwa tawi hili la fasihi linatu- miwa
katika jamii kama njia ya kupashana maarifa yanayohusu utamaduni fulani,
historia ya jamii, matamanio yao, mtazamo wao na historia yao. Kwa mtazamo wake
huo, tunaweza ku- jumuisha kuwa fasihi simulizi ndicho chombo muhimu cha jamii.
Mwanafasihi Kimani Njogu (2006: 2) anatueleza kuwa fasihi simulizi ina ubunifu
na uhai wa kipekee wenye kutoa fursa njema ya kuibua nadharia za kijamii,
kiuchumi na kisiasa. Pia a- naifananisha aina hii ya fasihi na uti wa mgongo wa
maendeleo ya binadamu, kwani ndani yake kuna masimulizi, maigizo, tathmini za
mazingira na mahusiano ya kijamii.
Kezilahabi (1989) anasema; fasihi simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhanna
ya fasihi itolewayo kwa mdomo bila kuandikwa. Istilahi hii ina dosari kwani
neno simulizi halina maana ya kinachosemwa –oral- bali ni kitu kinachosimuliwa
–narrative-.
TUKI (2004) inatoa fasili ya
fasihi simulizi kuwa ni fasihi inayo uhifadhiwa na
kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi
kizazi kingine kwa njia ya mdomo kama vile hadithi, ngoma, navitendawili.
fasili hii inamaana kuwa nyenzo kuu ya uwasilishwaji wa fasihi simulizi ni mdomona kwamba
fasihi simulizi hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine baada ya
kuhifadhiwa.Lakini fasili hii ina
mapungufu yake kwa mfano
haijaelezea hiyo fasihi simulizi
inahifadhiwawapi ili iweze kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
na kwa mujibu wao njia kuu yakuwasilisha fasihi
simulizi ni mdomo kwa maana kwamba hakuna njia
nyingine inayowezakutambulisha fasihi
simulizi zaidi ya njia ya mdomo pekee.
Kwa
mawazo ya wataalamu hawa, twaweza kuhitimisha ya kuwa fasihi simulizi ni sanaa
ina- yotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana katika kufikisha ujumbe
uliokusudiwa kwa hadhira husika. Hii ni sanaa ambayo ujumbe wake upo katika
mfumo mzima wa pande mbili za mawasiliano kuwepo pamoja ana kwa ana hii ikimaanisha
fanani yaani mtu anayerithisha (msimuliaji) na Hadhira yaani mtu anayerithishwa
(msimuliwaji). Kwa njia hii fasihi simulizi hushirikisha au huwafikia watu
wengi na mawazo ambayo jamii iliyakubali, imeyakubali, ina- endelea kuyakubali
yatokeapo na inayapitisha na au kuyakabidhi kwa kuendelezwa kutoka kizazi
kimoja hadi kizazi kingine kwa njia ya mdomo. Kwa hali hiyo basi, kwa vile
taarifa zinazopatikana ni za mdomo, upo uwezekano wa utata, upotoshwaji na
upoteaji wa taarifa muhimu za kale ambazo kama zingeliandikwa zingelidhihirisha
ukweli wa mambo yalivyo- kuwa.
Haiyumkini
mapokeo ya fasihi simulizi yanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuiunda,
kuirekebisha, kuifundisha na kuiboresha jamii.
Vile
vile kutokana na fafahuzi hizo inaweza kueleweka kuwa fasihi simulizi ni sanaa
inayoitumia lugha ya kusemwa( masimulizi na utendaji) inayowasilishwa kwa
hadhira kwa njia ya ana kwa ana, mfano njia ya elekroniki kama vile CD, redio
na runinga. Fasihi simulizi hii huhifadhiwa kwa njia ya kichwa, maandishi au kurekodi
ili iweze kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi.
Fasihi
simulizi ndiyo fasihi ya awali. Aina hii ya fasihi imeanza wakati binadamu
alipoanza kutumia lugha kama moja ya chombo cha mawasiliano. Tangia hapo ndipo
mwanadamu alipoanza kuimba, kutumia methali, vitendawili, nahau, n.k.
Jinsi
dunia ilivyobadilika kimaendeleo, na fani za fasihi simulizi ziliendelea
kubadilika. Kuto- kana na mabadiliko hayo ya binadamu tangu alipomudu kutumia
lugha, uwepo wa maendeleo endelevu hadi kutokea kwa mapinduzi ya viwanda na
baadaye mwishoni kuingia kwa tekno- lojia mpya, haya yote yalisababisha
mabadiliko hadi katika fasihi simulizi.
Mabadiliko
haya yaliigawa fasihi simulizi katika fasihi simulizi ya zamani ambapo ilianza
sambamba na bina- damu kujua kutumia lugha. Baada hapo, kulipotokea maendeleo
ya mitambo na kutokea ma- pinduzi ya viwanda, pakatokea mabadiliko katika
fasihi simulizi na kukatokea fasihi simulizi ya kisasa.
Kuingia
kwa teknolojia mpya kuliibadili fasihi simulizi ya sasa, hivyo kuanzia sasa
twaweza kuipa jina la fasihi simulizi teknolojia mpya. Kwa nadharia hiyo basi,
makala haya yataangalia aina kuu mbili tu za fasihi simulizi yaani fasihi
simulizi ya zamani na ile ambayo kwa mapokeo ya kisasa ni ya fasihi simulizi
teknolojia mpya.
v Utata uliopo wa kufasiri fasili ya fasihi
simulizi
Hadi sasa kuna tafsiri nyingi juu ya
dhanna ya fasihi simulizi kutokana na kutoafikiana kwa wataalamu wa fasihi.
Kirumbi (1975) anasema: fasihi simulizi ni masimulizi tunayoyapokea mdomo kwa
mdomo. Katika fasihi simulizi kuna utumiaji wa ulumbi (ufundi wa kucheza na
lugha). Kwa maelezo ya Kirumbi ni kwamba chombo cha kutongolea fasihi simulizi
ni midomo na kwa hiyo katika fasihi simulizi tunakuwa na masimulizi.
Kuna baadhi ya wataalamu wanadai kuwa
fasihi simulizi ni masimulizi ya kale ambayo hurithishwa kizazi kimoja hadi
kingine. Kwa baadhi ya watu fasihi simulizi hufungamanishwa na masimulizi ya
mambo ya kale. Kwa jina la kashifa fasihi hii huitwa fasihi ya kimapokeo.
Baadhi ya wanafasihi hudai kuwa istilahi yenyewe ina mgogoro hivyo wanataka
Istilahi mbadala itumiwe badala ya Simulizi. Kezilahabi (1989) anasema; fasihi
simulizi ni istilahi inayotumiwa kuelezea dhanna ya fasihi itolewayo kwa mdomo
bila kuandikwa. Istilahi hii ina dosari kwani neno simulizi halina maana ya
kinachosemwa –oral- bali ni kitu kinachosimuliwa –narrative.
Hivyo tafsiri ya fasihi simulizi katika
Kiingereza ni –narrative literature- sio –oral literature-.Pamoja na migogoro huu kikubwa kufahamu ni kuwa fasihi simulizi
ni utanzu mmoja wa fasihi. Na fasihi simulizi ni sanaa ya masimulizi na matendo
inayofikisha ujumbe kwa hadhira iwe ni kwa kuimba, kutenda au kuzungumza.
Fanani katika fasihi simulizi hufaulu kutoa picha halisi ya dhanna anayoikusudia
iwe ni huzuni, furaha, kuchekesha au kusononesha. Katika usimuliaji fanani
hujitathmini kama anafaulu au la kwa kuitazama hadhira yake. Hali hii humsaidia
kubadili mbinu za usimuliaji, vilevile fanani huweza kushirikisha hadhira yake
na kuleta uhai katika masimulizi yake.
v Usuli wa fasihi
simulizi
Nadharia
ya fasihi simulizi ni mawazo yanayotoa mwongozo kuhusu mwelekeo wa jambo fulani
katika fasihi simulizi.
Kwa
kufanya hivyo, nadharia hizo zimeweza kuleta mabadiliko katika nadharia asilia zilizokuwepo
kwa mfano utamaduni wetu wa asili kama vile ususi, ufinyanzi, uchongaji, jando
na unyago umeathiriwa na ujio wa wageni.
Watafiti
wa Kimagharibi na wa Kiafrika wameangalia mambo mengi yaliyoikabili fasihi
simulizi ya Kiafrika na mawazo yao ni kama yafuatavyo:
MSAMBAO
Waasisi
wa nadharia hii ni Grimms na Thompson. Wanamsambao wamepingana na
wanaubadilikaji taratibu ambao waliamini kuwa kufanana kwa fani mbili za
kifasihi kunatokana na jamii hizo kupitia hatua sawa za kimaendeleo.
Wanamsambao
wanaamini kuwa pale ambapo kufanana kwa namna hiyo kutatokea, sababu ya msingi
ya mfanano huo ni kuwa katika kipindi fulani hapo zamani, jamii hizo ziliwahi
kukutana kwa namna fulani na makutano hayo yalisababisha hali ya kuazimana
baadhi ya mila na desturi.
Wafuasi
wa nadharia hii wanaamini kuwa utamaduni unaweza kusambaa kutoka katika jamii
imara na maarufu tena yenye nguvu kuelekea katika utamaduni wa jamii iliyo
dhaifu. Hivyo basi kutokana na mawazo ya wataalamu hawa ni kuwa fasihi simulizi
ya Kiafrika ilisambaa kutoka katika sehemu moja iliyostaarabika (Ulaya) kwenda
sehemu nyingine ambayo haijastaarabika (Afrika). Kwa mfano ushairi simulizi wa
Kiswahili ulitoka Uarabuni na Uajemi kuja Afrika.
KISOSHOLOJIA
Nadharia
hii ina mihimili mitatu ambayo ni ule wa Umahususi, mkazo katika
utendaji na dhima ya fasihi simulizi katika jamii. Umahususi,
ulijikita zaidi katika jamii peke yake badala ya taaluma ya sanaa jadi kwa
ujumla kama walivyofanya wananadharia wa nadharia ya kiutandawazi.
Katika
Utendaji, Wanasosholojia waliweka msisitizo katika kuchunguza utendaji wa kazi
mbalimbali za fasihi simulizi.
Kutokana
na msisitizo huo imebainika kuwa fanani wa kazi ya fasihi wana ujuzi na ustadi
wa kiutendaji katika sanaa
husika
na jambo hili limetuwezesha kuelewa kuwa katika fasihi simulizi kuna kipengele
cha utendaji.
Katika
msisitizo kuhusu dhima ya fasihi simulizi katika jamii, wanaamini kuwa uamilifu
wa fasihi simulizi upo hai na haufi na kwamba unabadilika kulingana na
maendeleo ya jamii husika.
Kutokana
na mawazo ya wananadharia, hii ni wazi kwamba asili ya fasihi simulizi ya
Kiafrika ni ndani ya jamii za Kiafrika zenyewe na si vinginevyo.
UTAIFA
Nadharia
hii ilizuka kwenye vuguvugu la kudai Uhuru Barani Afrika. Wanautaifa wanadai
kuwa wananadharia wa utandawazi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu lugha za
Kiafrika.
Kwa
kiwango kikubwa waliathiriwa na dhana za kikoloni na upendeleo wa kibepari kuwa
Afrika ni bara la giza na la washenzi wasiokuwa na aina yoyote ya ustaarabu na
walistahili kustaarabishwa na Wazungu kupitia mlango wa ukoloni.
Utaifa
umeasisiwa na Adeboye, Babalola, Daniel Kunene na Clark. Katika nadharia hii
wamejaribu kuondoa dosari ambazo nadharia zilizopita zimeshindwa kuondoa
kutokana na kwamba wananadharia waliopita mara baada ya kutafiti hawakuwa
tayari kuchapisha matokeo yao halisi ya utafiti. Wanaona ni kosa kubwa kufanya
utafiti bila kuwahusisha wahusika wa eneo la utafiti.
Ili
kufahamu vyema historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika ni lazima kuhusisha
wataalamu na wanachuo wa taifa au jamii hiyo kwa sababu wataalamu na wanazuoni
hao ndio wenye ujuzi wa lugha, utamaduni na historia ya jamii hiyo.
HULUTISHI
Nadharia
hii iliasisiwa na wanazuoni wa Kiafrika wenye mtazamo kuwa hata wageni
wamechangia sana katika kukuza taaluma ya fasihi ya Kiafrika. Wananadharia hawa
wanaona kuwa fasihi ya kigeni na ya kijadi zimeathiriana na kuingiliana.
Miongoni
mwa waasisi na wafuasi wa nadharia hii ni pamoja na Mulokozi, Johnson na Ngugi
wa Thiong’o. Hivyo basi historia ya fasihi simulizi ya Kiafrika inaweza
kujadiliwa kwa kuhusisha au kuchanganya mawazo ya wataalamu wote wa kigeni na
wa kijadi.
Hata
hivyo, fasihi simulizi ya Kiafrika ilikuwepo hata kabla ya ujio wa wageni
lakini ilianza kupata athari mara baada ya ujio wao. Athari na mwingiliano wa
fasihi simulizi hauonyeshi kuwa fasihi imeanzia sehemu gani kwa kuwa fasihi
yoyote lazima iathiriwe na iathiri fasihi nyingine.
Hivyo
basi kila jamii au taifa huwa na fasihi yake na utamaduni wake ambapo
maingiliano ya watu na tamaduni zao huweza kuathiriana na hivyo kuathiri pia
fasihi ya jamii husika.
v UAINISHAJI WA TANZU ZA FASIHI SIMULIZI
Uanishaji wa
tanzu za Fasihi simulizi unakumbwa na matatizo mbalimbali, jambo linalopelekea
wataalamu kutofautiana katika kuainisha tanzu hizo na kupelekea kuchanganya
watu mbalimbali hasa wanafunzi katika kujua
ni zipi hasa ndizo tanzu za fasihi simulizi. wataalamu wengiwametofautiana
katika kuainisha
tanzu za fasihi simulizi kwa
mfano:
Kutofautiana kwa uainishajiwa tanzu za fasihi simulizi miongoni mwa wataalamu hao kumetokana
na matatizo mbalimbali yanayoikumba fasihi simulizi
kama yafuatayo:
Utajiri wa tanzu za fasihi similizi miongoni mwa jamii za kiafrika. fasihi simulizi huumbwa
kutokana na mazingira ya jamii husika na hali ya shughuli zao, jamii hutofautiana sana kimazingira pamoja na shughuli zao hali
inayosababisha kuwepo kwa fasihi nyingi na za namnatofauti
tofauti miongoni mwa jamii mbalimabali, hali hii inasababisha kuwepo kwa tanzu
nyingi za fasihi simulizi yaani zikikusanywa
fasihi simulizi za kihaya, kilugulu, kinyiha,kinyakyusa,kigogo,Kikuyu, kikamba,
kichaga, kipare, na nyingine nyingi unaweza kubaini tanzu nyingi zisizo
na ukomo jambo ambalo si rahisi kwa mtaalamu yeyote
kuainisha tanzu na vipera vyote vya fasihi
simulizi, hivyo kila mtaalamu huainisha kulingana na ufinyu wa uwelewa wa jamii
mbalimbali na ukomo wa utafiti wa mtaalamu husika. Hivyo basi kila jamii
ina tanzu zake za fasihi simulizi ambapo zaweza kufanana na jamii nyingine
au kutofautiana kabisa kutokana na utofauti wa tamaduni
moja na nyingi.
Kutokuwepo kwa vigezo mahususi vitakavyokubalika na wataalamu wote vya uainishajiwa
tanzu za fasihi simulizi ni jambo jingine linalosababisha ugumu katika
uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi.
Ni wazi kwamba katika shughuli yoyote inayohusisha uelezeaji, uainishajiauubainishaji wa tanzu za fasihi simulizi haifungwi na mipaka mahususi jambo ambalo kilamtaalamu
anaamua kutumia vigezo au hatua azitakazo yeye na kwa kuwa vigezo ni tofauti
basi wataalam au wanafasihi huishia kutofautiana na kila mtaalamu kuona vigezo
vyake ni borakuliko vigezo vya mtaalamu mwingine. Hivyo basi kutokuwa na vigezo mahususi katikauainishaji wa tanzu za fashi simulizi ni tatizo. Mfano:
Mulokozi(1996) Kwa upande wake Mulokozi anaainisha tanzu za
fasihi simulizi katika makundi sita ambayo ni MAZUNGUMZO, MASIMULIZI, MAIGIZO, USHAIRI,
SEMI, na NGOMEZI.
(1)MAZUNGUMZO
ü Hotuba
ü Malumbano ya
watani
ü Ulumbi
ü Soga
ü mawaidha
(2)MASIMULIZI
a) Hadithi -
Ngano (Istiara, Mbazi, Kisa)
b) Salua –
ü kisakale,
ü mapisi,
ü tarihi,
ü kumbukumbu,
ü kisasili
(3) MAIGIZO (tanzu zake hutegemea na shabaha na muktadha
(4)USHAIRI
a)
Nyimbo
ü Tumbuizo
ü Bembea
·
ü Za dini
·
ü Wawe
·
ü Tenzi /Tendi
·
ü Mbolezi
·
ü Kimai
·
ü Nyiso
·
ü Za vita
·
ü Za taifa
·
ü Za watoto
·
ü Za kazi
(b) Maghani (ya kawaida, ya sifo- kivugo na tondozi)
Ghani masimulizi – rara, ngano, sifo, tendi
(5)SEMI
ü methali
ü vitendawili
ü misimu
ü mafumbo
ü lakabu
(6)NGOMEZI
-
ü Za taarifa
ü Za tahadhali
ü Za mahusiano k.m mapenzi
semi
· masimulizi
· mazungumzo
· maagizo
· ushairi
· ngomezi
Okpehwo(1992) kwa upande wake anaziainisha katika makumbo yafuatayo:
· Nyimbo za maghani
· masimulizi
· semi
· ngomezi
Mwanafasihi huyu anatoa mchango wake ifuatavyo kuhusiana na
uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi.
v Okpewho
anaeleza kuwa uainishaji wa hadithi/ngano ni tatizo la muda mrefu. Hata hivyo
anaeleza kuwa kuna vigezo/njia nne mpaka sasa ambazo zimetumiwa kuainisha
hadithi/ngano.
o Kwanza, kigezo cha unguli (protagonist of the
tale), katika kigezo hiki kunajitokeza ngano zihusuzo wanadamu, ngano za
wanyama, ngano za vichimbakazi, na ngano za miungu. Hata hivyo kigezo hiki
kinaonyesha kuwa na matatizo
Matatizo hayo ni pamoja na kufanana kitabia kati ya jamii moja na
nyingine. Kwa mfano katika ngano za
wanyama, wanyama hupewa uwezo wa kuzungumza, kufikiri, na kutenda kama
wanadamu. ·
Pia kigezo hiki kinapuuza namna mbalimbali katika ngano ambazo
vichimbakazi, wanadamu na wanyama huhusiana.
o Pili, kigezo cha lengo la ngano husika (purpose
of the tale), katika kigezo hiki ngano zinaainishwa kwa kuzingatia lengo la
simulizi husika. Hapa panajitokeza ngano za kimaadili, ngano za kuhimiza kazi
n.k. Okpewho anaeleza kuwa katika kigezo hiki kundi kubwa la ngano ni zile za
kimaadili.
o Tatu, kigezo cha sifa ya ubora wa ngano
(characteristic quality of the tale), kigezo ambacho ndicho kinaonekana kubeba
kundi kubwa la ngano. Katika kigezo hiki kuna ngano ayari (trickster
tales)-hizi huambatana na uelevu au ulaghai wa wahusika; ngano za mtanziko
(dilemma tales) na ngano za kihistoria ambazo huhusu vita, vizazi, mashujaa,
usuli wa kitu/jambo fulani n.k.
o Nne ni Kigezo cha muktadha wa utendaji wa
ngano husika. Katika kigezo hiki kinachoangaliwa ni ngano inatendwa wakati gani
na katika mazingira gani. Kwa mfano, kwa kutumia kigezo hiki tunaweza kupata
ngano zinazotendwa wakati wa mbalamwezi (moonlight tales), ngano zinazotendwa
wakati wa ibada (divination tales), ngano zinazotendwa wakati wa mapumziko ya
wawindaji (hunters’ tales) na nyinginezo.
Kwa ujumla vigezo hivyo vina matatizo kwa
sababu kuna uwezakano wa aina moja ya ngano kujitokeza katika vigezo vyote.
Kutokana na utata huo, Okpewho anazianisha ngano katika makundi yafuatayo:
o Kundi
la kwanza ni hekaya
(legends). Kundi hili linaelezwa kuwa ndio kundi kubwa kabisa la hadithi na
hujumuisha tarihi, ngano za mashujaa, ngano za mapenzi n.k.
o Kundi
la pili ni ngano fafanuzi
(explanatory tales). Hizi hufafanua asili ya kitu au wazo kwa kuzingatia
mazingira na tajiriba za jamii. Kundi hili linajumuisha aina mbili kubwa: (1)
Ngano zinazoelezea asili ya kuumbwa kwa ulimwengu, (2) Ngano zinazosawiri sifa
na tabia za viumbe mbalimbali katika mazingira yao. Aina hii ya pili
hujumuisha visasili na visaviini.
o
Kundi la tatu ni ngano zisizo fafanuzi (fables). Kundi
hili hujumuisha hadithi zinazohusu tajiriba zihusuzo wanyama, viongozi wa dini
iwe katika ulimwengu au vinginevyo. Katika hadithi hizi msimulizi hatoi maelezo
maalumu ni namna gani hadhira iifasili hadithi hiyo.
Balisidya (Matteru) (1987) Anagawanya fasihi simulizi
katika tanzu tatu ambazo ni:
·
Nathari,
·
Ushairi
·
Semi
(1) NATHARI
A. Ngano
ü Istiara ·
ü Hekaya ·
ü Kwa nini na kwa namna gani ·
ü kharafa
B. Tarihi
·
ü Kumbukumbu ·
ü Shajara
ü Hadithi za historia ·
ü epiki
C. Visasili
·
ü Kumbukumbu
·
ü Tenzi
·
ü Kwa nini na kwa namna gani
(2) USHAIRI
A. Nyimbo
ü Tahlili
ü Bembea
ü Tumbuizo
ü Ngoma
ü Mwiga
ü Watoto
ü kwaya
B.Maghani
ü Majigambo
ü Vijighani
ü Shajara
ü tenzi
(3) SEMI
A. Vitendawili
ü Kitendawili
ü Mizimu
ü mafumbo
B. Methali
ü Msemo
ü nahau
C. Misimu
ü Utani
ü Masaguo
ü soga
Upungufu wa uainishaji huu
Katika uainishaji wake, baadhi ya tanzu hazionekani ama tunaweza
kusema zimeachwa kabisa. Mfano visakale, ngomezi, Balisidya anauweka utenzi
kuwa ni kipera cha visasili katika kundi la nathari.
Hapa anaibua mjadala kwani kama tujuavyo kuwa utenzi katika fasihi
simulizi huhusisha uimbaji pia. Hivyo swali la kujiuliza ni je utenzi ni
nathari?
Vilevile kuna kuingiliana kwa tanzu. Mfano kumbukumbu na kwanini
na kwa namna gani ni tanzu ambazo zinajitokeza katika kundi zaidi ya moja.
Ngure(2007) yeye anaainisha
kama ifuatavyo:
· usimulizi
· tanzu fupi
· ushairi simulizi
Wamitila(2010) ameainisha tanzu zifuatazo:
· hadithi
· maagizo
· ushairi
· semi
· ngomezi
Simiyu (2013)
ameainisha tanzu hizi nne kama ifuatavyo:
· semi bunifu
· ushairi
· maagizo
· hadithi.
Kwa mujibu wa Mulokozi katika
Mulika namba 21(1989). Pamoja na kwamba Fasihi ni kongwe lakini kitaaluma bado
ni changa kwa sababu ilianza kuchungunzwa hivi karibuni. Hivyo imepelekea
kutokuwepo kwa nadharia, marejeo, wala istilahi zenye kutosheleza mahitaji ya
taaluma hiyo. Tatizo hili linadhihirika pale tunapoangalia kazi za wataalamu
mbalimbali kuhusu tanzu za Fasihi Simulizi.
Kwa upande wa nadharia kitabu
pekee kinachozijadili tanzu za Fasihi Simulizi kwa urefu ni kitabu cha Ruth
Fennegan kinachoitwa Oral Literature in Africa (1970)
. Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za Fasihi
Simulizi. Badala yake kuna miongozo michache kwa ajili ya shule za sekondari
kama vile Balisidya, N (1975)
na Taasisi ya Elimu (1987)
Kule nchini Tanzania Mulika
namba 21 ni jarida la kitaaluma linalotoa fursa kwa wataalamu, waalimu na
wanafunzi katika kujadili mada mbalimbali za kiswahili. Jarida hili
lililoandikwa mwaka 1989 ndani yake kuna makala ya Fasihi Simulizi inayohusu
tanzu za Fasihi Simulizi na vipera vyake iliyoandikwa na M.M.Mulokozi.
Hivyo basi kutokana na
kukosekana kwa nadharia zinazoongoza ugawaji wa tanzu za Fasihi Simulizi ya
Kiswahili wataalamu wengi wamekuwa wakitumia vigezo mbalimbali ambavyo ni
maudhui, fani, matukio, idadi ya waimbaji, vifaa vinavyotumika na namna ya
uimbaji.
Hivyo basi utata umekuwa ukijitokeza katika uanishaji na ugawaji
wa tanzu na vipera vya fasihi simulizi. Utata huu unatokea kutokana na
kutofautiana kwa vigezo vinavyotumiwa na wataalamu mbalimbali katika ugawaji
huu, kwani kila mtaalamu hutumia vigezo vyake kulingana na matakwa ama mtazamo
wake. Hebu sasa tuwatazame baadhi ya wataalamu ambao wameainisha tanzu za
fasihi simulizi, tukiangalia pia udhaifu na ubora wa vigezo walivyotumia.
Kuingiliana kwa tanzu na vipera vya fasihi simulizi kiuwasilishwaji ni moja ya
matatizo ya uainishaji wa tanzu za
fasihi simulizi. wanafasihi wanakubali kwamba katika uainishaji wa tanzu
za fasihi simulizi kuna ugumu kutokana na kwamba tanzu hizo huingiliana katika
uwasilishwaji.kwa mfano muziki huweza
kuuwasilishwa kama sanaa ya maonesho na semi kuuwasilishwa kama
mazungumzo au masimulizi. Hivyo kutokana mwingiliano huo si rahisi kuainisha
tanzu zafashi simulizi. Ambapo katika vipera upo ugumu katika utanzu wa ushairi
hasa kati ya kipera cha nyimbo na
maghani mfano: kazi za kifasihi alizoshiriki Mrisho Mpoto kama vile“Gongo
lamboto” Jomba”, “Adela”
na nyingine kama hizo ni
kazi kuhitimisha kama ni maghani au ni nyimbo kwani kuna sifa za
kuitwa nyimbo na zipo sifa pia za kazi hizo kuitwa maghani.
Mabadiliko yanayoikumba fasihi simulizi ni moja ya tatizo katika uainishaji wa tanzu zake.Fasihi simulizi sio tuli kwa maana ya kwamba hupokea mabadiliko
kulingana na mfumo wamaisha ya watu na kwasababu si tuli basi tanzu zake huweza
kuongezeka kutokana na mfumohalisiwa maisha kwani maendeleo endelevu ya sayansi
na teknolojia yamepanua uwanja wakimaingiliano wa kifasihi katika nyanjaya maisha, mwingiliano huo
husababisha uchanganyaji wa tanzu za fasihi simulizi wa jamii zinazokutana jambo ambalo
kimsingi ni endelevu hivyohuleta ugumu
katika kuainisha tanzu za fasihi simulizi.
Kutokuwepo kwa nadharia zinazoongoza uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi ya Kiswahili.1japokuwa fasihi simulizi ni kongwe lakini kitaaluma fasihi
simulizi ni changa kwa sababu imeanza kuchunguzwa hivi karibuni. Hivyo
inapelekea mahitaji ya taaluma hiyo, kwa upande huu wa nadharia kitabu pekee kinachozijadili tanzu za fasihi simulizi kwa undani ni kitabu chaRuth Fennegana kinaChoitwa (Oral
Literature in Africa, 1970). Kwa upande wa Kiswahili hakuna kitabu kinachojadili uwanja wa tanzu za fasihi simulizi na
badala yake kuna miongozomichache kwa ajili ya shule za sekondari mfano:(
Taasisi ya Elimu 1987 ) Hivyo kutokana na kukosekana
kwa nadharia zinazoongoza uanishaji wa tanzu za fasihi simulizi, wataalamu
wengiwemekuwa wakitumia vigezo mbalimbali
kama vile fani na maudhi na kuleta utofauti katika kuainisha
kwao.
Kutokana na kuwepo kwa ugumu katika uainishaji wa tanzu za fasihi
simulizi kama kikundi tunapendekeza
njia ambayo itakuwa ni msingi wa uainishaji wa tanzu za fasihi
simulizi.
Kama
inavyofahamika kuwa utendaji ndio msingi mkubwa wa fasihi simulizi. hivyo basi
kama utendaji ndio msingi wa fasihi simulizi
si ngumu kukubali kuwa tanzu zote za fasihi simulizi zijulikanazo na
zisizojulikana labda kwa sababu ya ufinyu wa mazingira tunayoyafahamu au mipaka ya
tafiti zina utendaji.
Kwa hiyo, njia bora ya uanishaji wa tanzu za fasihi simulizi ni
utendekaji wa tanzuya fasihisimulizi
husika, hii inamaana kuwa kwa kila utafiti utakaofanywa katika kubaini uwepo
wa tanzufulani ya fasihi simulizi ni lazima zihusianishwe na utendekaji wa
tanzu hizo.
v Sifa bainifu za fasihi simulizi
Fasihi simulizi ina sifa zake mbalimbali ambazo ni
pamoja na zifuatazo:
o Husambazwa kikalima
o Huwa na hadhira mahususi iliyo hai
o Huwa na wakati na mahali maalumu pa
uwasilishaji
o Huwa na fomula ya kiada ya kuanza na kumaliza
o Hulenga utendaji kunaoifanya hai
o Mtunzi asiyejulikana bali ni mali ya jamii
o Hubadilika kulingana na wakati
o Wahusika wa aina mbalimbali
o Huwa na vipera vingi
o Hutungwa kila wakati
o Msimuliza ndiye mhusika wa kati
o Ala zake kuu ni sauti, mdomo na ishara za
mwili
v Majukumu yake/dhima katika jamii.
o Kukuza, kueneza, kuboresha na kuhifadhi
utamaduni.
o Kukuza, kueneza, kupanua na kuhifadhi lugha.
o Kuitumbuiza jamii.
o Kuhifadhi historia ya jamii.
o Kuwahamasisha wanajamii kujikomboa kisiasa na
kitamaduni.
o Kusifia viongozi au asasi za kijamii zilizo
bora.
o Kukosoa na kuelekeza uongozi na asasi za
kijamii.
o Kuelimisha jamii kuhusu mazingira yake.
o Kuhamasisha wanajamii kudumisha na kuimarisha
utu na utanmaduni wao.
o Kuhifadhi amali, maarifa na mmmsingi wa
jamii.
v Vikwazovinavyoikabili fasihi simulizi.
o Uvumbuzi wa maandishi. Awali Fasihi Simulizi ndiyo iliyokuwa sanaa
ya pekee ya lugha. Kupitia kwayo wanajamii walijifurahisha na kuhifadhi mila na
tamaduni zao. Mengi sasa huhifadhiwa katika maandishi
o Washindani badala. Awali, watoto walijumuika kusimuliwa hadithi
au vitendawili. Siku hizi pumbao la watoto halitokani na masimulizi kwa sababu
wametekwa na vitumeme vya kila nui. Fasihi Andishi, redio, runinga,
tarakilishi, mtandao, pataninga na vifaa vinginevyo hutumiwa siku hizi kama
njia badala za kujipumbaza.
o Mapisi. Watoto wa sasa hushughulika mno na elimu ya
vitabu kuliko ya Mapokeo
o Mwingiliano na mtagusano wa jamii mbalimbali. Mtagusano wa watu wa jamii mbalimbali
umepunguza uhalisia wa Fasihi Simulizi. Vijana hawawezi kujieleza kwa lugha
moja. Kumeibuka jamii isiyo na lugha wala utamaduni imara. Wamerithi
mchanganyiko wa mawazo kadhaa. Labda tuuite utamaduni mseto au chotara.
o Uhakiki wa Fasihi Simulizi. Ulinganishi wa Fasihi Simulizi za jamii
mbalimbali hudumaza tanzu hizi. Tamasha za muziki na maigizo shuleni na vyuo
huwa zimetengwa na hali halisi ya utendaji wa tanzu hizi.
o Mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu hutilia mkazo masomo mengine
huku Fasihi Simulizi ikipuuzwa
v Ya kuzingatia ili fasihi simulizi iendelee kuwepo
o Kusisitiza utafiti wa tanzu na vipera vya
Fasihi Simulizi
o Kuifundisha Fasihi Simulizi shuleni na
taasisi nyinginezo
o Kuhimiza uhifadhi wa Fasihi Simulizi
o
Kuhakikisha
lugha za kienyeji hazifi
o Kupambana na lugha za kikoloni ili wanajamii
wasidharau Fasihi Simulizi
v Hitimisho.
Kwa kuzingatia yaliyajadiliwa katika makala haya ni dhahiri shairi
kuwa fasihi simulizi ina nafasi kubwa
kabisa katika jamii kwani huindama na kuifinyanga jamii katika kila pembe.
Waadha ni wazi kuwa umri wake nimkongwe zaidi kwani usuli wake ni tangu jadi
binadamu alipopata tu uwezo wa kuzungumza.
Tukitazama kwenye ufafanuzi wake ni kuwa wanafasihi wengi
wameinukia na maana na maelezo mbalimbali kuhusiana na fasihi simulizi ingawa
kipengee kinachowaunganisha ni kuwa ni aina ya fasihi ambayo ni ya ana kwa ana
kupitia mdomo huku hifadhi zake zikiwa kichwani mwa binadamu.
Uainishaji wa tanzu za fasihi vile vile una changamoto zake kwa
kuwa kila mwanafasihi huzichanganua kama anavyozidhania kibinafsi kwa kuwana
ufinyu wa nadharia zinazochanganua tanzu hizi.
Waaidha fasihi simulizi inazo dhima zake pamoja na sifa zake
bainifu katika jamii bila kusahau kuwa vipo Vikwazo mbalimbali ambavyo
vinaikumba fasihi simulizi.
Hivyo basi fasihi simulizi ni mihimili katika jamii yoyote ile.
o Balisidya,
M. L, (1983), Tanzu na Fani za Fasihi Simulizi, kutoka kwa Mulika
namba 19 (1987), Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu Dar
es Salaam.
o Mulokozi,
M.M (1996), Fasihi ya Kiswahili, Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria
cha Tanzania.
o Mwanbusye,
D (2012), Lugha, Utamaduni na Fasihi simulizi ya Kinyakyusa, Dar es
Salaam.
o Ngure,
A (2003), Fasihi Simulizi kwa Shule za Sekondari, Nairobi,
Phoenix Publishers Ltd.
o Finnegan,
R. (1970), Oral Literature in Africa, Open Book Publishers,
Cambridge.
o TUKI,
(1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Nairobi, Oxford University
Press Ltd.
o TUKI,
(2004), Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Dar es Salaam, Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
o Knappert,
J. (1979). Four centuries of Swahili Verse. Heinemann. London.
o Mayoka,
J.K. (1993). Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka. Ndanda Mission
Press.Tanzania.
o Senkoro, F.E.M.K. (1987). Ushairi,
Nadharia na Tahakiki. DUP. Dar-es-Salaam.
o F. E. M. K. Senkoro (1982) Fasihi.
Press and Publicity Centre. Dar es Salaam.
o K. W. Wamitila
(2004) Kichocheo cha Fasihi, Simulizi na Andishi. Focus
Publications Limited: Nairobi
o M.M. Mulokozi (1989) Tanzu za fasihi
simulizi. Katika Mulika. Na 21
o M. MsM. MSokile (
1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. E.A.E.P. Nairobi
o P.Mhando na N.Balisidya (1976) Fasihi
na sanaa za maonyesho. T.P.H. Dar es Salaam
o S. OSS. Okpewho (1992) African Oral
Literature. Backgrounds, Character, and Continuity. Indiana University
Press. U.S.A