Swali:
TUMIA NADHARIA YA KIUTANZU KUHAKIKI TAMTHILIA YA PANGO.
Hii ni nadharia ambayo inahusu ugawaji wa
tanzu mbalimbali za fasihi katika makundi yake mahsusi. Katika nadharia hii
huwa tunazama katika namna ya kujuana kufahamu utanzu ni nini? una sifa gani?
unaweza kutumika kivipi ili kueleza usemaji mbalimbali.
Miongoni mwa waasisi wa nadharia hii ni
Mgiriki Aristotle. Mgiriki huyu anatoa maoni kuwa utanzu huwa na sifa mahsusi
hasa alipotazama na kusikiliza aina mbalimbali za fasihi. Katika utafiti wake
huu, aligungua kuwa Wagiriki walikuwa na masimulizi maarufu ambayo waliyaita
Tendi au Tenzi.
Waaidha walikuwa na nyimbo ambazo
walipoziimba ziliambatana na firimbi, nzumari, zeze, kinubi, pembe n.k. Aliona
vile vile Wagiriki walikuwa na maagizo ambayo yapo mengine yaliyohuzunisha
mathalan msibahuku mengine yakichekesha yakimsawiri mwanadamu katika ubaradhuli
na uduni wake. Kisha kulikuwa na yale yaliyokuwa ya mseto wa msiba na
kuchekesha. Kwa Aristotle haya yalikuwa na sifa za kipeke zilizojitosheleza na
mtunzi asingewezakutoka utanzu mmoja hadi mwingine.
Hata hivyo kuwa wataalamu kama
Mikhail(Bakhtin) waligundua kwamba ni vigumu kwa utanzu kuwa na upekee usioingiliana na utanzu mwingine.
Tanzu zinaweza kuingiliana, kutaguzana na vile vile tanzu ni nyumbufu na
zinasheheni utelezi mkubwa.
Kwa mujibu wa maoni haya, mwandishi mmoja
anaweza kuandika tamtilia moja ikahusisha hadithi na ushairi lakini ikabaki
tamthilia tu. Vile vile utanzu kama riwaya huweza kuwa na hurafa,
nyimbo,visasili,vitendawili na tanzu nyingine nyingi.
Na wakati utanzu mkubwa unameza tanzu ndogo
ndogo, hizi tanzu ndogo ndogo hutumika kimtindo kufanikisha utanzu mkubwa. Kwa
mfano:-Methali katika riwaya inaelezza kazi kwa ujumla na vile vile wimbo
hufanya kazi hiyo ama utunzi huo kama simulio na kuhamisha wimbo.
Kuna mtaalamu David Cryig ambaye yeye
anashughulikia, kuzaliwa, kukua,kunawiri, kudididmia na kutokomea kwa tanzu za
fasihi. Anasema kuwa utanzu huzaliwa kutokana na tabaka la kuzalisha mali
katika jamii.
Kama utanzu wa riwaya kimagharibi ulizalishwa
na ubepari- mhusika mdogo anatupwa baharini kwa sababu amekuwa tajiri.
Katika tamthilia ya Pango iliyoandikwa na
K.W. Wamitila, swala la nadharia ya kiutanzu linadhihirika wazi kabisa. Mtuzi
huyu ameangazia tanzu aina ainati katika kazi yake ya fasihi licha ya kuwa
tamthilia.
Utanzu ambao unadhihirika wazi hapa ni ule wa
nyimbo ambao huwa mojawapo wa vipera vya fasihi simulizi. Kwa hakika nyimbo
huwa sehemu muhimu sana ya jamiina ambapo huwa na malengo na maudhui maalum.
katika Tamthilia ya Pango, utanzu huu umetumika katika muktadha aina ainati.
a) Kunao wimbo unaoongozwa na Kibwana (uk.
36-37). Wimbo huu unalilia hali ya wakombozi kukosa misimamo imara wa kupigania
haki yao ya uongozi.Hili bila shaka ni kundi ambalo linamwunga mkono Katango
kijana ambaye amejibwaga ulingoni kumenyana vikali na Ngwese. Kibwana anasema
hivi:
Kibwana: ……………………tulibeba
gogog hili la hatima yetu
tulipagaze mabegani kwa
kujitolea
tulipofika katikatiya mto
baadhi wakakimbia
wakakimbia
wakakimbia
wakakimbia…………
b) Wimbo
mwingine umejitokeza kwenye uk. 38 na ambao unaongozwa na Ngoi.Wimbo huu
ni wa kumsifu Ngwese kuwa ndiye afaaye
kuliongoza Pango. Kupitiakwa wimbo huu, tunaweza kuona kuwa wimbo huu umejawa
na majisifu na majigambo chungu nzima hasa unapomlinganisha Ngwese na vitu
mbalimbali.
Ngoi: (Akiimba) Wa Ngwese yuko hapa, wa Ngwese
Wa Ngwese kimbunga, yu hapa, wa
Ngwese
Wa Ngwese shoka la kuikata miti
mikinda, wa Ngwese
Wa Ngwese mti uko tayari, wa Ngwese
Wa ngwese shoka tia mpini, wa
Ngwese
Wa ngwewe kelele kinapinda
majani
yakitutetemeshe
Wa ngwese…….. bingwa wa Pango.
c) Katika onyesho la tatu, Mama ambaye ni mkewe
Seki, anajikuta katika kuuimba wimbo(uk 55) Maudhui ya wimbo huu ni kumsuta
mumewe(Seki) kwa kutupilia mbali,majukumu yake katika nyumba.Twafahamu kuwa
nyimbo huweza kudhihirisha hisia alizo nazo Mwimbaji. Kwa kupitia wimbo huu,
tunapata taswira ya sononeko tupu la Mama kuhusu mienendo ya mume wake. Waaidha
anaonyesha kujuta mikononi mwa Seki kama mume wake. Anaimba hivi:
…………………. “uchungu huu uliokithiri
moyo una uchungu
siku hizi mumeamegeuka umande
jua lipigapo anajiweka upande
kazi hafanyi
lawama hakomi
kisha chakula adai………….”
Hapa tunapata kuwa Seki haachi pesa za
matumizi ingawa ajapo nyumbani ataka kula! Iwapo atakosa chakula, atapandwa na
wakwao hali ambayo imemkera na kumsononesha Mama pakubwa.
Wimbo huu vile vile unadhihirisha wazi kuwa
wanawake wamedharauliwa na jamii. Kwenye huo wimbo Mama aimba:
…………wake tumedhalilishwa na kuteseka
kuni
kutafuta na watoto juu migongoni
chakula
kutafuta na kuandaa jikoni
huku
wenzetu njia wanazishika
huku
sisi na wana tunasakimu…………(uk 55-56)
d) Utanzu huu vile vile unajitokeza kwenye onyesho
la nne uk.88. Huu ni wimbo wa ukomboziwa Pango hasa baada ya Ngwese kugunduliwa
hila zake. Kupitia kwenye wimbo huu, tunaweza kufahamu kuwa waliomwunga mkono
sasa wamebadili misimamo wa na sasa wamekubali kumwunga mkono Katango kuwa Kiongozi
wa Pango.Wimbo huu wasema:
sauti: Kimbunga cha uongo ngo ngo
Kimbunga
chaharibuPango ngo ngo
Kimbunga Kumbuka njia ya mwongo
kimbunga alisema yote Katango!
Kimbunga hata mlinzi hulindwa!
Wanapouimba
wimbo huu, tunawaona wote wakishikana mikono wakiwa na furaha kubwa huku
Katango akiinuliwa juu.
Ulumbi.
Hiki ni kipera cha fasihi simulizi
ambachokimezama katika mkumbo wa mazungumzo. Utanzu huu umejitokeza wazi katika
kazi hii.Hii inadhihirika wazi kwenye ukurasa wa 9 wakati Katango anapotoa
kauli yake ya kuwarai wakazi hawa kumchagua kuwa Kiongozi wao. Kauli hii
iliteka bakunja umati uliokuwa pale kabla ya Ngwese kupewa fursa ya kumwaga
shindo lake.
Kwa hakika sifa hii ya lumbi wa Katango imetambulika
na wengi katika tamthilia hii akiwemo Babu ambaye kwenye ukurasa wa 69 anasema
hivi kwa kumjibu Susa:-
Babu:
(Kwa mshangao mkubwa) Unasema nini sasa?
Iweje Katango asiongee na ni mlumbi maarufu
kijijini?
Iweje kuwa haongei
na ni bingwa wa kuyasanifu maneno? Iweje?
Hali hii ilitokea baada ya kugunduliwa kuwa
Katango ametiwa kitata asiweze kuongea tena.
Ni dhahiri shahiri kuwa Katango ameibuka
kidedea katika fani hii ya ulumbi kwa kuwa bingwa wa kuyasarifu maneno maneno
anapozungumza. Katango angemithilishwa na walumbi mahiri kama Martin Luther
King Jr.(1929-1968), Barack Obama, John F. Kennedy(1917-1963) au P.L.O Lumumba
hapa nchini Kenya hasa katika makala yake yenye mvuto kwa Uteuzi wa msamiati
wenye mvuto wa kipeke hasa makala ya, “The Tragedy of Africa.”
Katango anazidi kuonyesha umahiri wake katika
ulumbi anaposadiki na wanakijiji kwa kugunduliwa hila za Ngwese na sasa
wanakubali kumwunga mkono kwa kusema hivi:-
Katango: ………… sasa macho tumeyafungua
sasa
upofu tumeupofua
sasa
vinywa tumefungua
maovu
nayo tumeyafukua.
Kwa upande mwingine utanzu wa misemo na methali vile vile zi metumika pakubwa katika
tamthilia hii ya Pango. Methali huwa kielelezo cha jamii. Kupitia methali mmoja
anaweza kuifahamu historia na mapisi ya jamii husika. Ipo mifano chungu nzima
ya utanzu huu katika kazi hii.
Kunguru ni mwoga lakini hana kipara(uk
34)
Msemo huu umetumiwa na Mama ikishauri Katango
ukiwana maana kuwa ajiepushe na maswalaya siasa kwani hayana mwisho mwema.
Asionyeshe ubabe kilamahali hivyo awe kama kunguru ambaye licha ya uwoga wake
wote kunguru hana kasoro wala cha kujutia.
Hujui
mkia hauongozi kichwa.( uk 35)
Seki kwa upande wake naye anautumia msemo huu kwa
Katango. Hapa Seki ambaye ni baba yake Katango ana maana kuwa Katango hawezi
kupata fursa ya kuliongoza Pango kwa vyovyote kwani Pango liko mikononi mwa
Ngwese.
Kuteleza
sio kuanguka (uk 46)
Methali hii imetumiwa na Ngwese alipokuwa akijaribu
kuwarai wanakijiji kumpa fursa nyingine ya kumchagua kuliongoza Pango hata ingawa hakutekeleza
wajibu wake ipaswavyo.Anajitetea kuwa bado kuna uwezekano wa yeye kuia bidii na
kujitahidi akipewa awamu nyingine.
Ngwese anazisha kwa kutumia msemo:kibuyu hakivunjwi
kwa kukosa maziwa, akiwa na maana kuwa kukosa kutimiza wajibu kwake kusiwe
chanjo cha kumwangamiza kisiasa.
Uchngu
wa kujifungua hauwazuii wanawake kushika
mimba.(uk
58)
Msemo huu umetumiwa na Babu alikuwa akijaribu kumpa
Katango moyo na matumani kuwa hata baada ya Ngwese kuibuka mshindi katika Uchaguzi
wa kuwakilishwa Pango bado ana nafasi ya kutwaa uongozi wa Pango kwa hivyo
asife moyo hata kidogo.
Ngoma
ya wana haikeshi.(uk 84)
Methali hii imetumiwa na Jitu 1. Jitu 1 ana maana
kuwa wakati wa vijana kuongozwa bado na kwa hivyo swala ambalo vijana
wanalidhania lakuongoza Pango ni ndoto za alinacha tu. Anaendelea kwa kusema
kuwa , “Hujasikia mshairi maarufu aliyesema
Haile ngoma ya wana sijaona ikeshayo?”
Utanzu mwingine ambao unadhihirika hapa ni fasihi ya ngoma au ngomezi. Katika jamii za kiafrika, ngoma ilichukuliwa kuwa
nafasikubwa sana katika mawasiliano na burudani.
Katika tamthilia hii, ngoma zimetumika katika muktadha
mbalimbali. Katika sehemu ya pili onyesho la kwanza(uk.36) ngoma inasikika
ikipigwa na vijana wanaompigia debe Katango.
Kwa vijana ngoma hii ni ishara ya mabadiliko katika
ulimwengusasa ikizingatiwa kuwa katika jamii zetu za kiafrika masogora walikuwa
wale wakongwe waliobugia munyu si haba.
Katika onyesho la tatu sehemu ya tatu(uk 75), wapo
watu kadhaa ambao wanacheza ngoma karibu na pango.Huenda ikawa
wanasherehekeanna kufurahikia hali yao inavyowaendea vizuri hata kama wengi
wanasota kitango malele.Katika onyesho la nne(uk 82) vile vile kazi inaanza kwa
ngoma tele.
Utanzu wa ushairi
nao pia haukuwachwa nyuma. katika uk 38
wimbo wa Ngoi unachukua muundo wa shairi laaina ya kikwamba. Hapa kila
mstari/mshororo umeanza kwa neno moja ambalo ni ‘WA NGWESE’
Ngoi: (Akiimba) Wa Ngwese yuko hapa, wa Ngwese
Wa Ngwese kimbunga, yu hapa, wa
Ngwese
Wa Ngwese shoka la kuikata miti
mikinda, wa Ngwese
Wa Ngwese mti uko tayari, wa Ngwese
Wa ngwese shoka tia mpini, wa
Ngwese
Wa ngwewe kelele kinapinda
majani
yakitutetemeshe
Wa ngwese…….. bingwa wa Pango.
Katika uk 79 kupitia kwenye sauti baada tu ya mtuo
sauti inadhihirisha utanzu wa ushairi kwa kuanza kwa neno moja kisha kuzingatia
vina vya kati ifaavyo(za)kunena
haya:
Sauti: kisha nitauza,nitauza nipate dola
kisha nitauza,nitauza
nipate doola
kisha nitauza,nitauza
nipate pa…..uni
kisha nitauza,nitauza
nipate yuro
kisha nitauza,nitauza
nipate yeeni!!!
Katika shairi hili inabainika wazi kuwa mwandishi
amezama zii katika Mashairi aina ya kikwamba ambayo yamedhihirika wazi katika
tamthilia hii.
Waaidha Kibwana anaidondosha mistari ya
muundo wa ushairi(uk 88) ambapo anasema:
Kibwana(Akimzomea Ngwese)
Weye kimbunga upigaye
Weye tufani ufagiaye
Weye dhoruba utakasaye
Umejua ni nani wa
kututangua?
Utanzu
mwingine ambao umetumika hapa ni hadithi. Aghalabu hadithi
huwa nafasi kubwa na kiburudisho chenye mafunzo na maadili chungu nzima. Katika tamthilia hii, mwandishi
ametumia utanzu hii kupitia wahusika mbalimbali .
Katango
kwenye uk.42 anatongoa hadithi aina ya khurafa ambapo anasimulia kuhusu wanyama
walioamua kukichimba kisima baada ya ukame kutawala eneo lao. Kupitia kwenye hadithi
hii inadhihirika wazi kuwa ukubwa si neno bali maarifa. Hii ni kwa sababu licha
ya ukubwa wa wanyama kama ndovu, simba, twiga mbogo hawakuweza kuchimbua maji
hadi akatokea sungura ambaye hakudhaniwa kufaulu kwa udogo wake.
Hadithi
hii ni taswira au kiangaza mbele kuwa licha ya Ngwese na ubabe wake, hataweza
kulikomboa pango bali ni Katango(sungura) ambaye hadhaniwi kwa kuwa mtoto na
mdogo wa Busara.
Ukweli
huu unadhihirika mwishoni mwa tanthilia wakati ambapo wakazi hawa wanaghairi misimamo
wao na Kuamua kumwunga mkono Katango kwa kugundua kuwa hawana mustakabali mwema
mikononi mwa Ngwese.
Maigizo
vile vile yameangaziwa na mwandishi wa tamthilia hii ya Pango. Katika uk 52
Ngwese alipokuwa akizozana na Sakina kuhusu kwenda kutekeleza wajibu wa kikazi
baada ya kuchaguliwa,anamwigiza Sakina namna alivyokuwa akimshauri.
Ngwese:(Akiigiza) Kipindi cha kazi!
Kipindi cha kazi! (Anatembea huku na huku) Ni kweli nilisema ni kipindi cha
kazi, lakini sikusema ni nani atakayeifanya hiyokazi, unasikia? Kimsingi wao
ndiyo wanaotaka kuichapa hiyo kazi………
Utanzu
mwingine ambao umetumika hapa ni ule wa mawaidha. Katika jamii zetu mawaidha
yalitolewa na wakongwe au mtu aliyekupiku kwaumri na maarifa ya kimaisha na
aliyeaminika kuwa na Busara.
Katika
tamthilia wapo wahusika mbalimbali ambao wanajitikeza wazi kuwausia wahusika
wengine. Kwa mfano katika uk. 57, Babu anamshauri Katango kwa kumpamatumaini ya
kuzidi kupigana na kuona kuwa ndoto yake ya kuongozwa pango inatimia.
Babu: Sikiliza Katango wangu, mwewe anapomchukua
kuku wako, humrushii mayai;maana
ukifanya hivyo hutobaki na chochote. Ni muhimu uwe na matumaini……….. sote tuwe nayo(mtuo) Uovu na ubaya haufichiki
Katango; na una mwisho pia;tutamjua huyo Ngwese hivi karibuni. Watu husema kuwa
uyoga hutoa mahali sawa lakini sio uyoga wote uliwao; watu hutambua upi wa
kuliwa naupi usioliwa.
Majigambo
ni utanzu ambao kwa hakika umejitokeza katika tamthilia hii.Katika usanii huu,
kuna pande mbili na kila upande unajipigia debe kuwa ndio unaofaa Kuamua misimamo
wa kisiasa katika sehemu hii ya Pango. Pande hizi zinaongozwa na
Katanga(kijana) na Ngwese(mzee)
Katika
uk 42-45 kwenye ile hadithi ya Katango kuhusu wanyama tunaona kuwa kila Mnyama
ajaye kukichimba kisima kila mmoja alijigamba namna alivyo na uwezo mkubwa.
Hata hivyo Katango anatumia mfano huu wa kisa kujigamba kuwa udogo wake
usichukuliwe kuwa Udhaifu bali ano uwezo wa kuiongoza sehemu hii ya Pango swa
na sungura aliyewapiku wale wanyama wenye nguvu waliomtangulia kisha kushindwa
kukichimba kisima.
Anapopata
fursa kwa upande wake, Ngwese kwenye uk.48 anasema:
Ngwese: (Kwa kujishasha)
Ndimi kimbunga nipigaye,
Ndimi tufani nifagiaye,
Ndimi dhoruba nitakasaye,
nani wa kunitangua?
kijana?
Kupitia
kwa usemi huu inadhihirika wazi kuwa Ngwese ana wingi wa majigambo kwa kujiona
kuwa ni mtu mwenye nafasi akilinganishwa na Katanga ambaye bado hali yake ya
kiuchumi bado nyembamba.
Hitimisho
Imedhhirika
wazi kuwa katika Tamthilia hii ya Pango, mwandishi ameangazia nadharia ya
kiutanzu ifaavyo. Amevishughulikia vipera mabalimbali vya fasihi ambavyo kwamba
vina niaya kuikamilisha kiufundi kazi yake.
Ufundi
kama huu huzidisha hamu ya kutaka kukisoma kitabu hiki kwa kuwa mabadiliko ya
tanzu mbalimbali huondoa kutamaushwa unapoisoma tamthilia hii.
Marejeleo.
Wamitila
K.W. (2002), Uhakiki wa Fasihi Simulizi. Misingi na Vipengele Vyake.
Nairobi Phoenix Publishers Ltd.
____________________(2004),
Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Nairobi: Focus Publications
Ltd.
_____________ (2016) Pango. Nairobi :Focus Publishers Ltd,
,.
Topan
Farouk M. (1975), Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili. Dar es
Salaam: Oxford University Press.
TUKI
(1981), Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Dar
es Salaam: Oxford.
Njogu
K. na R.M Wafula (2007), Nadharia za Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: K.L.B
Ogechi
N. O et al (2008), Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na Lugha za
Kiafrika. Eldoret: Moi University Press.
Njogu, K & Rocha, C. (1999). Ufundishaji wa Fisihi:
Nadharia na Mbinu. Nairobi: Jomo Kenyatta Foundation.
Msokile, M. (1993). Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi:
East African Educational Publishers.
Abedi, A. (1954). Sheria za Kutungu Meshairi na Diwani
ya Amri. Nairobi: East African Literature Bureau.
Hussein, E. (1983). Hatua Mbalimbali za Kubuni na Kutunga
Tamthilia Kufuatana na Misingi ya KiAristotle, Fssibi. Dar es Salaam:
TUKI.
Kezilahabi, E. (1983). Uchunguzi katika Ushairi. Fesihi.
Dar es Salaam: TUKI.
Madumulla, J. s. (2009). Riwaya ya Kiswshili:
Nadharia, Historic na Misingi ya Uchambuzi. Nairobi: Phoenix.
Wamitila, K.W.
(2003). Kamusi ya Fasihi: Istilahi na
Nadharia. Nairobi: Focus Books