MBAYA WETU (
K. WALIBORA)NI TAMTHILIA INAYOSAWIRI MASUALA IBUKA. FAFANUA HUKU UKITOA MIFANO.
Maswala ibuka ni jumla ya mambo yanayoiathiri
jamii moja kwa moja. Maswala kama haya yamesawiriwa vilivyo katika tamthilia ya
Mbaya Wetu (2014).Masuala haya yanakusudia kutoa mafunzo maalumu kwa wasomaji
hususan vijana.
Tunaongozwa na nadharia ya uhalisia. Lukacs (1963) anaeleza kuwa
uhalisia sharti ujihusishe na mambo halisi yanayotokea katika mazingira halisi
kupitia kwa wahusika. Wahusika ni vielelezo yakini vya binadamu wa kawaida kwa
vile wao wanatumia lugha ya binadamu. Hali halisi ya wahusika na lugha
wanayoitumia humwezesha mwanadamu kujifafanulia uwezo wake wa kutenda mambo na
mtazamo wake kuhusu maisha.
Njogu (1997) anasema kuwa kazi ya msanii ni kiungo chake na jamii
anayoilenga. Walibora anaibua masuala yanayoiathiri jamii ya kisasa katika
ngazi zote za maisha. Masuala anayoyajadili yanalenga kumfanya binadamu awe
mwanajamii mwema anayewajali wenzake. Anagusia nyanja za kijamii, kisiasa,
kielimu, kitamaduni na kiuchumi. Nyanja hizi humsaidia binadamu kukuza hisia
zake, tabia zake na kuyaelewa mazingira yake. Masuala ibuka yanayoibuliwa ni pamoja na Ufisadi, Ufeministi(Haki za wanawake)
ukiukaji wa haki za binadamu(haki za wafungwa), matumizi ya dawa za kulevya na
mapenzi na ndoa.
v Ufisadi.
Ufisadi ni matumizi
mabaya ya mali au raslimali za chama, shirika, watu au nchi kupitia rushwa kwa
ajili ya kujinufaisha mwenyewe. Ufisadi umekuwa ni janga katika mataifa mengi.
Obara (2015) anaeleza kuwa ufisadi unafaa kutangazwa kama janga la kitaifa
nchini Kenya. Hii ni kutokana na kuongezeka kwa visa vya ufisadi. Kuna ufisadi
bungeni ambapo wanakamati wa kamati ya uhasibu wanapokea hongo na kuandaa
ripoti za kupotosha kisha majina ya watu wenye ushawishi wanaohusika na kashfa
hii yanaondolewa. Ufisadi mwingine unashuhudiwa katika tume ya kupambana na
ufisadi. Mwenyekiti anamsimamisha kazi naibu wa mkurugenzi kutokana na ukosefu
wa maadili na anarudishwa na mkurugenzi siku hiyo hiyo. Pia, mradi wa
vipakatalishi kwa watoto wa shule za msingi unasitishwa kwa kutofuatwa kwa
kanuni za kisheria. Hali hii inasikitisha kwa vile inabainika kuwa taifa la
Kenya linapoteza bilioni sitini na tisa kila mwaka kupitia kwa ufisadi.
Nalo shirika la AFP
(2014) linaeleza kuwa mahakama ya“Tel
Aviv, Israel” inamhukumu waziri wa zamani miaka sita gerezani na kumtoza
faini ya dola elfu mia mbili na tisini kwa kuhusika katika sakata ya ufisadi.
Anachukua hongo ya dola elfu mia moja na sitini anapokuwa mamlakani ili
kusitisha miradi ya umma.
Katika tamthilia ,
inatambulika kuwa usifadi ni swala
ambalo limekita mizizi katika ngazi mbalimbali za kijamii. Fiona ambaye ni mama
mwuza buzaa na chang’aa katika eneo hili,amewalisha rushwa ili kuendeleza
biashara yake haramu ya uuzaji Pombe haramu. Kwenye ukurasa wa 9 MTU II
anasema:
[Kwa Fiona] Na hata kama humjui huyu polisi kwani hicho ni kitu kwako wewe Fiona?... Ghalibu hukosi chochote
cha kumlainisha moyo wake yabisi. Askari wote lao moja...... yaani bora mkono
wende kinywani..... basi!
Hii ni ithibati kuwa
Fiona amewarambishwa askari hawa mlungula hivyo basi upo uwezekano kuwa kuja
kwao hakuna hofu yoyote ile kwa mwuzaji na wateja wake kwa kuwa dawa yao imo
katika himaya ya Fiona.
Swala hili
la ufisadi vile vile lajitokeza wazi katika wahusika wengine kama njia ya
kuuficha na kuuziba ukweli hasa katika misingi ya kifamilia. Jamii ya Mzee
Temba inajikita katika njia-panda wakati mwanao kitindamimba Matari anapotiwa
mbaronikwa kumwibia nduguye, Tonge ng’ombe wa maziwa na kumwuzia Jefule mwenye
bucha. Temba anaingiwa na wasiwasi kwa kukosa la kufanya. Anaamua kwenda kwa
Tonge ili amrai kukubali kuiondoa kesi kutoka mikononi mwa polisi hadi nyumbani
ili waelewana kama jamii.Kwenye ukurasa wa 32 Mzee Temba anasema:-
............ Ni kweli Matari kakowa manza, lakini yeye Tonge asikubali
polisi wampeleke nduduye mahakamani. Hiyo haihalisi......Hata kidogo
haihalisi.....Nitamnasihi Tonge anasihike, tuje pamoja naye kwenye kituo cha
polisi tuwambie polisi mambo haya tuyamalizie nyumbani....
Kwa
yakini mzee Temba alifanya vivyo hivyo ingawa tarajio lake halikuwa swari tu
kama alivyotaka yeye. Tonge kwa upande wake alihitaji sheria ifuatwe ili Matari
na Jefule wawe mfano mwema kwa wale walio na tabia kama zao.Waaidha familia ya
Jefule kupitia kwa Bi. Mkubwa. Kwenye ukurasa wa 62 bibi huyu asema:-
[Baada ya kusalimiana mikononi]Mzee Temba, nimekujia kadha si kadha
wa kadha. Hebu sikiliza.Watu wa Jefule wamenituma nije niseme nanyi.Wako radhi
kulipa fidia kesi imalizikie papa hapa kijijini isiende mahakamani mjini.
Kupitia
kwake inadhihirika wazi kuwa jamii ya Jefule iko tayari kumhonga Tonge ng’ombe
mmoja ili kesi hiyo imalizikie nyumbani. Hata hivyo masharti ya Tonge yalikuwa
marudishe ng’ombe wote sita waliopata kuibwa.
Tonge
akiwa katika kituo cha polisi ili kuona kuwa walitiwa mbaroni wanakumbana
vilivyo na mkono wa sheria, anakutana ana kwa ana na kizingiti kingine kutoka
kwenye maafisa wa polisi.
Tume
ya huduma za maafisa wa polisi iliwafuta kazi maafisa hao baada ya kuwakagua
maafisa 1,300 kwa kipindi cha miezi 14.
Mbali
na msemaji wa kikosi cha polisi wa utawala Masoud Mwinyi,wengi wa wale
waliosimamishwa kazi walitoka katika idara ya trafiki.
Mwenyekiti
wa tume hiyo Johnston Kavuludi alisema kuwa wakati wa ukaguzi huo waligundua
kwamba maafisa wa vyeo vya chini wanaofanya kazi katika idara hiyo walikuwa
wakituma kiwango cha fedha wanachopata kwa maafisa wanaowasimamia kupitia simu
zao.
Lakini wakenya pia wamelaumiwa kwa
kuchanga kuongezeka ufisadi kwenye idara hiyo aidha kwa kutojua au kwa kupuuza
sheria. Naibu mkurugenzi wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi Michael
Mubea anasema wananchi wanapaswa kutokubali kutoa hongo na badala yake kutoa
bondi inavyohitajika kisheria kunapotokea makosa.
Kule Tanzania mambo ni yale yale.
Kupitia vile vile kwenye habari za BBC Januari 2,2015 ilitangazwa wazi kuwa
idara ya polisi ilikuwa ikiongoza katika visa vya ufisadi.Ripoti hiyo ilisema
kuwa idara ya polisi ndiyo
taasisi inayochukua hongo zaidi nchini Tanzania kulingana na ripoti ya ufisadi
katika jumuiya ya Afrika mashariki.
Ripoti
hiyo ilisema kuwa maafisa wa polisi walipokea asilimia 25 ya hongo zote
zilizotolewa kwa wafanyikazi wa taasisi za uma mwaka uliopita.
Ya
pili ni idara ya mahakama,ambayo wafanyikazi wake walitia mfukoni asilimia 18
ya hongo,huku mashirika yalio na majukumu ya usajili na utoaji wa leseni yakiwa
katika nafasi ya tatu kwa asilimia 10.
kwa
mujibu wa gazeti la The Citizen, Idara ya Polisi nchini Tanzania ilitajwa kuwa
ya tatu kwa ufisadi katika jumuiya ya Afrika Mashariki.
Polisi
wa Uganda wanaongoza wakifuatiwa na wale wa Kenya katika nafasi ya pili na wale
wa Burundi wakiwa katika nafasi ya nne.
Kulingana
na ripoti hiyo maafisa wa polisi wa Rwanda ndio wasiochukua hongo ya juu Afrika
Mashariki.
Utafiti
huo ulifanywa mwezi Julai na Agosti mwaka
wa 2014 na shirika la lenye na maslahi ya kimaendeleo barani afrika
ForDIA likishirikiana na Jukwaa la uwazi nchini tanzania Trafo.
Kwenye
tamthilia ya Mbaya Wetu, polisi vile vile wamejitokeza wazi kuwa wanyonyaji wa
wananchi. Hii inadhihirika wazi wakati Tonge anapoambiwa kuwa na ASKARI 1
kuwa:-
Nilikwambia
karandinga letu halina hata tone la mafuta.Sisini maaskari waaminifu, hatupendi
kuwarubuni watu.Mafuta yaliyomo ni ya kuwapeleka wanywaji wa Pombe haramu mjini
kushatakiwa mahakamani, Kwa hivi sasa hatuna washukiwa wa ulevi.....Wataka
nikuambie mara ngapi nawe? Labda nyie mtumie gari lenu.
Huu umekuwa msemo wa kawaida wakati
raia wanapohitaji huduma kutoka kwa polisi.Polisi hupenda sana kusingizia
kukosekana kwa mafuta ya gari. Ajabu ni kwamba ukiwaarifu kuwa wakubali upeleke
gari lao kwa mafuta halisi, hamtaelewana kabisa. Sarakasi ni kuwa ukijitolea
kuwapa hela za mafuta ya gari, karandinga huenda ulikotaka bila kupitia kwenye
kituo cha mafuta!Iwapo utakuwa mgumu basi utapewa vitisho vya kila namna.
Kwenye kituo cha polisi pamewekwa
kibao kipana kilichoandikwa ilani “HAPA SI MAHALI PA KITU KIDOGO”.Ilani hii ni
kinyume cha mambo. Hiiinadhihirika wazi wakati Tonge anaposhinikizwa kulipia
huduma kwa kuelekezwa kufafanua maana ya ilani hiyo na Askari II. Anapotoa noti
kadhaa na kumpa Askari II kisha kuuliza iwapo ametimiza masharti,madahalo
unadhihirisha wazi kuwa ilani hiyo si haramu bali halali kwani wanaiboronga
maana yake ili kuitumia kuwaibia raia.
Tonge:
Sawa?
Askari II:Si sawa.
Tonge:
Kwa nini?
Askari
II:Wajua kusoma
Tonge:
Kwa nini?....Mimi mtu aliyesoma sijui kusoma?
Askari
II:Basi soma pale.[Anamwonyesha ilani “HAPA SI MAHALI PA KITU KIDOGO”
Tonge: Hapa si pahali pa kitu kidogo!
Askari
II: Inakuelea?
Tonge: Yaani hongo hairuhusiwi hapa.
Askari
II: Hata kidogo.Kumbe elimu mnayosoma
haiwasaidii kitu. Ilani kidogo tu, inakushindwa kuelewa. Maanake hasa ni kwamba
hatukubali sisi kitu kidogo; twakubali kitu kikubwa tu.......
Akiwa kwenye kituo cha polisi kumletea
Matari chakula(mkate na soda) Fiona anakosa kuelewana na Askari II ambaye nia
yake kwa Fiona ilikuwa potofu huku akikejeli Fiona kutokana na tuhuma zake
mwenyewe kuwa Fiona na Matari ni wapenzi. Fiona kwa upande wake anayapinga hayo
na kupitia kwake tunajifunza kuwa amekuwa katika mstari wa mbele kuwahonga
Askari polisi. Hii inadhihirika wazi anaposema kwenye ukurasa wa 53:
Lo! Mara
ngapi nikulipeni hongo?......Mara ngapi?....Eeh?....Mbona hata mwaweza kujenga
makasri kwa mapesa ninayowahonga kila uchao.
Askari I naye anakiri kwa kusema:
“Ahaa!
Hilosikatai.Nimekula pesa zako kilamwezi kidogo kidogo”.
Ni wazi kuwa idara hii ya polisi
imeamua kukejeli ilani za utendajikazi kwa kulazimisha umma kuzielewa kinyume.
v UKIUKAJI WA HAKI ZA
BINADAMU(HAKI ZA WAFUNGWA.)
Haki ni kiungo muhimu katika utawala wa kidemokrasia na
ndiyo msingi wa sera za kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Serikali ina wajibu wa
kutambua, kuheshimu na kulinda haki hizi. Haki za binadamu sharti zitiliwe
maanani ili kuiendeleza jamii. Njogu (2007) anafafanua haki za makundi mbalimbali
kama vile wafanyakazi, wafungwa, walemavu na watoto.
Wafungwa wana haki ya kupewa mahitaji msingi kama binadamu
wengine. Haki hizo ni: kuishi, kupata mahitaji msingi kama chakula, makazi na
mavazi, kuheshimiwa na kupewa uhuru wa kujieleza, kumiliki mali na kutangamana
na wenzake. Visa vya ukiukaji wa haki za wafungwa vinashuhudiwa katika jamii
yetu. Makala ya “Magereza yetu yasifurike,” 2014, ukurasa wa 11, yanaeleza kuwa
idadi ya wafungwa katika magereza nchini Kenya inafaa kupunguzwa. Wafungwa
hawapati chakula cha kutosha, mazingira ni duni na huduma za afya ni duni. Nalo
shirika la AFP (2014) lilieleza kuwa mfungwa mmoja Marekani alizuiliwa
kuhudhuria mazishi ya mama yake.
Kwenye tamthilia wafungwa au watuhumiwa hawapewi haki yao.
Mahali wanakowekwa hapafai hata kidogo.Hii inadhihirika wazi kupitia kwa Matari
ukurasa wa 50:
Matari:[ Kwa askari]........Nimeathirika
sana nina njaa kibao, sijala kitu tangu usiku wa kuamkia jana, sikwambii huku
kuliwa na chawa na viroboto kwenye seli hii.
Wakati Matari anapoomba idhini ya
kuenda msalani, jibu analopata ni ishara tosha kuwa afya ya wafungwa na
washtumiwa imo hatarini kabisa. Hii inadhihirika kupitia kwa mdahalo huu
ukurasa wa 51:
Matari:Afande nataka mwenda kujisaidia.
Askari I: Tumia ndoo iliyomo humo ndani.
Matari: Ndoo imejaa.
Askari I: Nani alikuambieni muijaze ndoo
haraka?Wacha kunitumia kama kopola msalani.Nitakutandika ugeuke rangi uwe
mweusi kama kunguru.
Hii ni pamoja na kutowapa chakula kwenye seli na iwapo
wataletewa basi Askari wanakila wao wenyewe. Fiona anapomletea Matari soda na
mkate, Askari I anaanza kuula mwenyewe pasipokujua kuwa mfungwa anafaa apewe
haki yake. Kwake Askari huyu ni kuwa mfungwa au mtuhumiwa hana haki yoyote ya
kula akiwa kituoni.(uk. 53-54).
v
HAKI ZA WANAWAKE
Wanawake na wanaume wana haki sawa. Hata hivyo kutokana na sababu mbalimbali wanawake hawakuweza kufaidi haki zao kama wanaume. Mikataba mbalimbali imepitishwa kuhakikisha wanawake wanafaidi haki sawa na wanaume. Pia kuna sheria mbalimbali za nchi zinazolinda haki za wanawake.
Ikumbukwe kuwa mikataba mikuu ya haki za binadamu imeweka kanuni kuu ya kutobaguliwa katika kufaidi haki za binadamu kwa misingi ya jinsi, dini, kabila, rangi, umri, utaifa, na kadhalika. Hii inamaanisha kuwa haki za binadamu zapaswa watu wote wazifaidi bila ubaguzi wa aina yoyote.
Hata hivyo bado baadhi ya makundi ya watu katika jamii hasa wanawake, hawakuweza kupewa nafasi sawa kufaidi haki zao. Ndio maana juhudi zimefanyika na zinaendelea kufanyika katika ngazi ya kimataifa, barani Afrika na hata hapa nchini Tanzania kuhakikisha kwamba haki za wanawake zinalindwa.
Mikataba ya Kimataifa inayolinda Haki za Wanawake
Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi
dhidi ya Wanawake wa Mwaka 1979.
Mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake au kwa jina jingine unajulikana kama ‘Mkataba wa Wanawake’ ndio mkataba mkuu unaolinda haki za wanawake duniani. Mkataba huu ulikubaliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwaka 1979 na ulianza kazi tarehe 3 Septemba, 1981. Tanzania imesaini na kuukubali mkataba huu tarehe 19/09/1985.
Mkataba huu umelenga kuhakikisha kuwa wanaume na wanawake wanafaidika kwa usawa na fursa za kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kiraia na kisiasa kwa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake.
Mkataba nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika wa
mwaka 2003.
Mkataba huu umepitishwa na wakuu wa nchi na serikali za Afrika mwaka 2003 huko Maputo, Msumbiji. Hadi Agosti 2004, ni nchi nne (4) tu za Umoja Afrika zilizoridhia mkataba huu.
Kwa ujumla, mkataba huu ambao pia unajulikana kama “Mkataba wa Maputo” unalinda haki za wanawake wa barani Afrika.
Na mojawapo ya sifa yake kuu ni kutamka wazi kwa mara ya kwanza katika sheria za kimataifa haki za uzazi za wanawake ikiwemo kutoa mimba kama imepatikana kutokana na kubakwa au inamuweka hatarini mwanamke. Pia mkataba huu nyongeza unapiga marufuku ukeketaji wa wanawake. Kwa ujumla, mkataba wa nyongeza wa haki za wanawake wa Afrika unaweka majukumu kwa nchi na serikali za Afrika kulinda na kutekeleza haki za wanawake katika nchi zao. Ubaguzi wowote wa kijinsia ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Ubaguzi unaokatazwa na Katiba unaweza kuwa dhidi ya rangi, kabila, jinsi, utaifa, mahali mtu alipozaliwa au hali ya maisha ya mtu. Kwa maana nyingine, katiba ya nchi inatoa haki sawa kwa wanaume na wanawake nchini Kenya katika Nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Baadhi ya mikakati wanajamii wanaweza kuitumia kuhamasisha ulinzi wa haki za wanawake katika jamii ni kama ifuatayo:-
Ø Kutoa elimu kwa jamii (wanaume, wanawake, viongozi wa kimila,
viongozi wa dini, walemavu n.k) kuachana kabisa na mila na desturi
zinazomkandamiza, kumuumiza na kumbagua mwanamke.
Ø Kutoa elimu katika ngazi ya
familia na kaya juu ya haki za wanawake
Ø Elimu hii itolewe kwenye
mikutano ya vijiji, mashuleni, masokoni, gulioni, nyumbani, kwenye vikundi vya
kuweka na kukopa, vyama vya ushirika n.k
Ø Kutoa taarifa kwa vyombo
husika pale haki za wanawake zinapovunjwa. Vyombo hivi ni pamoja na serikali ya
mtaa, polisi, idara ya ustawi wa jamii, asasi za kiraia zinazopinga ukatili
dhidi ya wanawake n.k.
Ø Kushirikisha wanaume kwenye
ulinzi wa haki za wanawake
Kumbuka wanawake wanayo haki ya kufaidi matunda ya utu/ ubinadamu wao sawa kabisa na wanaume. Baadhi ya mifano ya haki za wanawake ni:
Ø haki ya kuishi, uhuru na usalama wa maisha yake
Ø haki ya kutobaguliwa katika jamii kwa sababu tu ya jinsi yake
Ø haki ya kutotendewa kinyama
au kikatili
Ø haki ya kumiliki ardhi na/au mali nyingine yeyote inayohamishika na
isiyohamishika
Ø haki ya uhuru wa kutoa na
kueleza maoni yake
Ø haki ya kushiriki katika kutoa maamuzi yahusuyo maisha yake, familia
yake na jamii yake
Ø haki ya kupata elimu.
Ø haki ya kupata fursa sawa ya ajira na kulipwa ujira unaostahiki
Ø Haki ya afya na afya ya uzazi
Ø haki ya kupumzika kwa likizo ya uzazi.
Katika tahthilia, mwanamke
amenyang’anywa haki yake katika hali mbalimbali. Mifano ya wanawake
walioathirika katika ukosaji wa haki yao
katika jamii husika ni pamoja na Fiona, Lila,Mamaye Matari.
Jamii hii inamwona mwanamke kama
chombo cha kumfurahisha tu mwanamume na hakuna cha mno.Matari anaamua kumchukua
Fiona kama chombo chake cha kumrithisha kimapenzi. Hali hii inadhihirika wazi
wakati Fiona anapenda kwenye kituo cha polisi akiwa na nia ya kumpelekea Matari
chakula Askari I anasema:
Nimesema
hapewi mkate na soda. Seli sio mahali pa watu walio ndani na walio nje
kuonyeshana mapenzi.(uk.52)
Anazidi kunadi kuwa:
Na mpenzi
wako nani? Tangu hapo nakuona mwanamke mzima nikitakacho hunipi. Kumbe
umezuzuzuliwa na hilijambazi hatari mburumatari liitwalo Matari.Hili jambazi
ndilo dawa ya moyo wako sio?(uk 53)
Kupitia kwa usemi wa Askari I ni
ishara tosha kuwa hata yeye humwona mwanamke tu kama chombo tu cha kutimiza
haja za wanaume hakuna jingine.
Askari I anazidi kwa kusema kuwa:-
...........................
Nitapeleka salamu kwa dadako bila shaka kama yeye ni mzuri wa kugawa tenda na
kufungasha vilivyo kama mwanamke halisi wa Kiafrika. Sivipendi visichana vya
kisasa vinavyowaiga Wazungu na kujikondesha vikabaki kama shingo za
flamingo.Namtaka mwanamke aliyeunga Sawasawa.....aliyekula
akashiba......Nikipata nafasi nitamtafuta huyu dadako. Akinisikiza utapata
mkate na soda.
Hata Matari kwa upande wake anamwona
Vero, shemegiye kama chombo cha kujifurahisha. Hali hii ndiyo iliyopelekea Vero
kupata uja uzito kutoka kwa Matari ambaye ni shemeji yake. Katika ukurasa wa 56
Matari anakiri haya kwa kusema:
Afande
umeskia?Ee?Shemeji asimwambie mtu kwamba mimindiye niliyemtunga mimba.
Tabia zake Matari zinamwelekeza
kumbaka Fiona pindi alipotoka seli baada ya kuachiliwa akaenda moja kwa moja
kwa Fiona ambapo alimtaka amrudishie zile pesa alizomwibia Lila kabla ya
kushikwa. Fiona alimwarifu kuwa hazikuwa jambo ambalo Matari hakulikubali.
Matari akiwa na Fiona chemba
kunasikika sauti ya Fiona ikilia:
Uwiiiiii!
Uwiiiiii!Wacha kunibaka. Wacha kunibaka. Wacha kuniibia. Nduli wewe....Kama
wataka kuniua niue.
Kitendo hiki ndicho kilichomrudisha
Matari kwenye mikono ya sheria baada ya umati kutaka kumpiga kitutu.
Inasemekana kuwa Fiona ndiye aliyetoa mafuta ya gari la polisi.
Mwananamke pia amechorwa kama kiumbe
ambacho hakiwezi kukubalika kutoa ushairi na kufanya maamuzi katika
jamii.Kupitia kwa MAMA inaonyesha kuwa Temba hampi sikio hata kidogo katika
mijadala yake. Hii inadhihirika kupitia usemezano huu(uk 60):
Temba:[Anapuuza mikemeo ya
Mama. Anaketi Mkabala na mtoto wa meza]. Lila
Lila: Naam baba.
Temba:Nenda ukamwambie
Mjakazi aniletee chakula.Nina njaa.[Lila anaondoka]
Mama: Nauliza mwanangu yu
wapi?
Temba:[Anaita] Lila!
Lila: [Kutoka nje ya
jukwaa] Labeka!Baba.
Temba: Mwambie Mjakazi
asitie chumvi nyingi kwenye chakula. Kazoea vibaya sana huyu.
Lila: Ndiyo baba.
Temba: [Kwa Lila] Na
chsakula apashe moto vya kutosha
Mazungumzo haya yanamweka Mama katika
wingi wa wasiwasi ikibainika wazi kuwa mwanawe kitindamimba yumo hatarini. Hata
hivyo kupitia kwa Temba tunabaini wazi kuwa jamii haiku tayari kumkubali
mwanamke kikamilifu katika utoaji wa mielekeo.
Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa haki
za wanawake ni haki za binadamu. Kwani mwanamke anastahili kulindwa na
kuheshimiwa utu wake na kufaidi fursa zote zilizoko katika jamii yake kiuchumi,
kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
v MAPENZI
NA NDOA
Burke (1999) anaeleza kuwa baadhi ya watu hujiingiza katika
uhusiano kutokana na msukumo wa ubinafsi na unafiki. Kuna ukosefu wa mapenzi ya
dhati miongoni mwa wanajamii. Katika tamthilia , tunaelezwa kuwa mapenzi baina
ya Matari na Fiona ni karubandika tu .Hii ni kwa sababu Fiona anafaidika tu kwa kuwa baada ya Matari
kuwaibia watu basi yeye yu tayari kuzipokea zile pesa ambpo Matari na walevi
wenziwe huzipunguza kidogo kidogo tu. Hii inadhihirika wazi kwa kubainika wazi
kuwa babada ya Matari kumwibia dada yake Lila bunda lake la noti anazibeba hela
zote hizo kwa Fiona ambaye alizimenya zote baabda ya Matari kutowa mbaroni
mwanzo. Ugomvi wao kuhusu akiba ya pesa hizo ndio uliokuwa sababu ya Matari
kurudi mikononi mwa polisi.
Vilevile mapenzi yaliyojitokeza kati ya Matari na Vero
yanaelekea kuisambaratisha jamii ya Temba hasa ile ya mwanawe , Tonge. Hii ni kwa
sababu licha ya Matari na Vero kuwa mashemeji wameenda hatua ya kuwa wapenzi
kisha mimba ikapatikana.
Mapenzi na ndoa huambatana sako kwa bako. Ndoa ni kiungo
muhimu katika jamii. Hii ni kwa sababu huchukuliwa kama kilele cha ukuaji wa
mtu. Al- Farsy (1969) anafafanua kuwa ndoa inastahili kupewa umuhimu na udhati
na wahusika kwani huwaweka pamoja milele; mume na mke ni washirika wa milele na
sharti wawe tayari kwa majukumu yanayoandamana na ndoa. Ongachi (2014) anaeleza
kuwa ni vyema kuweka wazi matarajio kabla ya kufunga ndoa ili kupunguza
misukosuko. Katika jamii, tuanashuhudia visa vya ukatili katika ndoa
vinavyotokana na ukosefu wa mapenzi ya dhati. Matheka (2014) anasimulia kisa
cha mwanamke mmoja anayemdunga mume wake kisu baada ya ugomvi baina yao. Ugomvi
huo unatokana na mwanamume huyo kukosa kuwajibika katika kuilisha familia yake.
Mke wake analamika kuwa anamwachia majukumu ya kuwalea watoto wao. Mwanamume
huyo anapata majeraha mabaya. Naye Muiruri (2015) anaeleza kisa cha mwanamume
anayechomwa na mke wake kwa sababu ya kukosa kuleta unga mjini Kirinyaga,
Kenya. Mwanamume huyo anazama katika ulevi na kuisahau familia yake. Mke wake
anasema kuwa anaamua kumchoma ili kumshurutishe ayatekeleze majukumu yake kama
mume na baba ya watoto wake. Katika tamthilia tunabainisha kuwa ndoa kati ya
Tonge na Vero inakosa Uaminifu. Tonge yuko mjini kusaka tonge huku mkewe, Vero
kuwa na jicho la nje hadi kupachikwa mimba na Matari ambaye ni shemeji yake.
Waaidha ushirikino ni swala muhimu sana katika ndoa. Hata hivyo
jamii nyingi hukosa kufahamu hili. Katika tamthilia inaonekana wazi kuwa Temba
hana nafasi ya kumpa mkewe sikio ili atoe mapendekezo katika jamii. Ameona kuwa
mawaidha ya Mama hayana msingi wowote pasipokujua kuwa pasi mchango wa kila
mmoja jamii haina nguvu.
v HAKI YA MALEZI KWA WATOTO
Watoto wana hadhi maalumu katika jamii na ni jukumu la
familia na serikali kuwaelimisha na kuwalinda. Haki za watoto kama vile malezi
bora, kulindwa dhidi ya dhiki, kupewa elimu, kutofanyishwa kazi nzito na kupewa
matibabu.
Mama na baba mtoto wana haki sawa katika kulinda na
kuyakidhi mahitaji ya mtoto. Kila mtoto ana haki ya kulelewa na wazazi halisi
au wazazi mbadala iwapo wazazi wake halisi hawajimudu kihali, kiafya au
wameaga. Hakuna mzazi anayefaa kujitenga kwa vile mtoto ni wa wote.
Katika tamthilia inathibitika wazi kuwa mzigo mkubwa wa
kumlea Matari uliachiwa Mama huku Temba akijitenga kabisa. Hii inajitokeza
kupitia semi mbalimbali wakati Matari anapotiwa mbaroni kwa kosa la kumwibia
Tonge ng’ombe wake. Tonge kwenye ukurasa wa 62 anasema:
Mama hii
leo mwanilaumu lakini ukweli ni kwamba matendo ya Matari ni tokeo la
kutendekezwa. Ni kosa lenu.Si langu.
Kupitia dondoo hili ni wazi kuwa
Matari hakuweza kuipata haki yake ya kupewa malezi ifaavyo ndipo awe mkamilifu
kimaandili. Kudekezwa huku kunapita mipaka kiasi kuwa hata anapokosea
hadharani, Mama yupo katika mstari wa mbele kulikana hilo waziwazi.
Temba kwenye ukurasa wa 66
anathibitisha kuwa kukosekana kwa juhudi za wote wawili katika malezi ya mtoto
ndiko kunakoleta balaa. Anaamini kuwa Matari amedekezwa pakubwa na Mama ndio
maana hakui na kuwa mwanajamii bora. Anasema hivi:-
Basi
endelea kumdekeza adekezwe. Yatakuja kukutokea puani.Wacha nende zangu.........
Hii ni wazi kuwa swala la malezi ya
Matari liliingia mchanga kwa kukosa maafikiano kati ya Wazazi kuhusu namna ya
kuwalea wanao. Huenda ikawa ndio sababu Ndugu zake wakubwa(Tonge na Lila)
waliweza kusoma kuliko Matari.
Suala la watoto kuzaliwa nje ya ndoa linashuhudiwa katika
jamii ya kisasa. Sheria inaeleza kuwa watoto wanaozaliwa katika ndoa au nje ya
ndoa wana haki sawa. Kila jamii ina mitazamo tofauti kuhusu watoto wanaozaliwa
nje ya ndoa. Kakah (2014) anasimulia kisa cha kiongozi mmoja nchini Kenya,
anayemtelekeza mtoto anayemzaa nje ya ndoa. Hili ni dhihirisho kuwa kumzaa
mtoto nje ya ndoa katika jamii kunachukuliwa kuwa ni haramu. Baadhi ya wanaume
hawataki kuhusihwa na watoto hao kwa sababu wanawaona kama si halali. Jukumu la
kumlea linawachiwa mwanamke.
Kwenye tamthilia upo uwezekano mkubwa kuwa ulezi wa mtoto
atakayezaliwa na Vero utaleta kizungumkuti. Hii ni mimba iliyotungwa na Matari
ikizingatiwa kuwa Tonge, nduguye hana habari. Tunakisia kuwa iwapo habari hizi
zitamkaa akilini Tonge ambapo upo uwezekano mkubwa kwa kuwa wanakijiji wameanza
kuyasoma chini ya maji, basi hatari ipo njiani. Uwezekano mkubwa upo wa Vero
kutafuta namna ya kumlea huyo mtoto pindi tu atakapozaliwa.
v
MATUMIZI
YA DAWA ZA KULEVYA.
Katika tamthilia hii Pombe imetawala pakubwa. Mwanzoni tu
mwa tamthilia inapoanza inadhihirika wazi kuwa Pombe imewaathiri watu wengi
mno.Tunakumbana moja kwa moja na Fiona ambaye ni mama mwuzaji wa Pombe haramu,
buzaa na chang’aa.
Makao yake hushona walevi kucha kutwa wakiwa na ari ya
kuburudika kwa kileo chao wakipendacho.
Hata hivyo Pombe hii imekuwa na madhara mbalimbali kwao
kwenye ndoa zao. Kwenye ukurasa wa 2 Mtu I anasema haya:-
Hapana........Uache
kumsifu Fiona bure bwana.Mgema akisifiwa tembo hulitia maji.Ama hujasikia wewe
watu siku hizi wanapofuka wanywapo Pombe?
Dondoo hili litakupa mwanya na mwangaza wa kufahamu kuwa
Pombe haramu ina uharamu wake kwenye afya za watumizi hasa viungo vyao ambapo
wengine hujikuta kuwa macho yao hayafanyi kazi kabisa. Hali kama hii
ilishuhudiwa na inazidi kushuhudiwa nchini Kenya ambapo walevi huathiriwa
pakubwa na Pombe haramu wanayoitumia.
Waaidha walevi wengi hasa wanaume
hutelekeza majukumu yao ya kindoa kwa wake zao.Hali kama hii hufanya familia
nyingi kuvunjika kwa kuwa mke huonakuwa haipo haja kuishi na mume ambaye tayari
ameyarudisha majembe ghalani mapema. Wengi wa wanawake huingilia ukahaba au
mipango ya kando kama inavyoshamiri kucha kutwa katika jamii zetu.
Wanawake wengi katika kaunti
zinazoathirika kwa Pombe wameonekana wakiandamana kuililia serikali iingilie
kati na kuona kuwa Pombe haramu imepigwa marufuku katika eneo lao na iwapo hilo
halitafanyika basi wanatishia kuhamia kwingineko waliko wanaume kamili!
Walevi wengi wanapokosa pesa za
kununua Pombe, wengi wao hujikuta wakiiba ili waweze kugharamia kileo. Katika
tamthilia tunaona kuwa Matari anaashinikizwa na raghba yake ya Pombe na kuwa
mwizi sugu na asiye na haya wala soni. Anamwibia dada yake, Lila waziwazi pesa
zake na kumpelekea kahaba wake muuzaji Pombe ambapo anaonekana akiwaburudisha
walevi wenzake.
Matari anakiri wazi kuwa ndiye
aliyeziiba pesa za dadaye kwa kuwema haya kwenye ukurasa wa 18:-
Fedha
zako nitakulipa.Saa hii sina, Nipemuda tu.Lakini la kumwambia Mama
usimwambie.....
Kwa hivyo ulevi na wizi ni pacha kiasi kwamba hutegemeana ilimtumizi aweze kutimiza ari yake ya kulewa. Hayo hayakukomea hapo.Matari vile vile ndiye aliyekuwa akiving’oavipuri kutoka kwenye trekta lao usiku na kuviuza ili aweze kupata pesa za ulevini.
Katika ukurasa wa 19 Mama anasema haya kwa Matari:-
Wajua.
Usiniambie hujui kwamba yupomtu wa mkono aliyeviiba vitu kwenye trekta na kuuza
kimojabaada ya kingine.......Trekta inaegeshwa usiku ikiwa na kila kitu. Hapa
kwtu usiku mbwa wakali sana hathubutu mtu ajinabi kuingia. Asubui ikifika vitu
kadhaa havipo...Sharti awe mmoja wetu..Mwizi wa vipuri labda ni babako
mwenyewe,mimiau wewe mwanangu.Mmoja wetu ana mkono.
Anapoachiliwa huru kutoka kwenye kituo cha polisi, Matari
anazidi kuonyesha kuwa ameathiriwa na wizi kisingizio kikiwa uchu wa
Pombe.Anaamua kukwapua nguo za Askari na kuzitia kwenye gunia. Aliziuza na
kuenda ulevini kwa Fiona kuwaburudisha walevi wenziwe. Haya yanajitokeza wazi
alipokuwa akihojiwa na walevi wenzake alikozipata hela za kuwalevya ilhali
amekuwa kwenye kituo cha polisi. Matari anakiri kwa kusema (uk 72)kuwa:-
Nilipotoka
ndani nilipita kwenye makazi ya maaskari polisi.Nikaona nguo kadhaa
zimeanikwanje.Wapuuzi hawa,wanaandika nguo nje, hawajui zinaweza kupeperushwa
na upepo wa arijojo..........
Uk 72-73 anaendelea kusema:-
...............Nikaangalia mbele na nyuma hakuna
mtu.Nikatazama kushoto na kulia,hamna mtu.Nitaangalia juu sikumwonaMungu
na chini sikumwona shetani.Nikaona gunia
......
Kwake Matari ulevi na wizi vimekuwa ngozi kiasi kwamba
vimemwandama kama kupe kumbanduka si rahisi. Waaidha inathibitishwa wazi kuwa
ana uhusianomkubwa sana katika kupoteakwa ng’ombe wa Tonge.Hii ilidhihirika
wazi kupitia kutiwa nguvuni kwake ambapo Askari waliandamana na Jefule hadi kwa
kina Matari na kumtia pingu kwa kushirikiana na Jefule kwenye huo wizi.
v UASHERATI.
Hiki ni kitendo cha kupenda kuzini.
Hali hii inadhihirika wazi kupitia wahusika mbalimbali katika tamthilia
hii.Kwanza kabisa Fiona amejitokeza wazi kuwa kahaba wa Matari. Huyu ndiye
mhisani wake wa uasherati. Hii ni kuwa uasherati wao huu umempelekea Matari
kutumia mbinu zozote za kupalilia mwingiliano huo kwa kutumia hela za wizi.
Matari ameonekana mara nyingi pindi anapoiba huelekea kiyuoni kwa kahaba wake
muuza pombe Fiona.
Mbali na Fiona, Vero pia amenaswa
katika mtegohuowa Matari.Licha ya Vero kuwa shemegi yakeMatari, wawilihawa
wanaingilia uasherati kiasi kwamba matendo yao yanasababisha uja uzito wa Vero.
Idara ya polisi pia imeathirika na
uasherati. Kupitia kwa usemi wa Askari I ni ishara tosha kuwa hata yeye ni
mwasherati mkubwa kwani anfikiria tu mwanamke upande wake ni wa mapenzi tu
hakuna jingine la mno.
Askari I anasema kuwa:-
...........................
Nitapeleka salamu kwa dadako bila shaka kama yeye ni mzuri wa kugawa tenda na
kufungasha vilivyo kama mwanamke halisi wa Kiafrika. Sivipendi visichana vya
kisasa vinavyowaiga Wazungu na kujikondesha vikabaki kama shingo za
flamingo.Namtaka mwanamke aliyeunga Sawasawa.....aliyekula
akashiba......Nikipata nafasi nitamtafuta huyu dadako................
Isitoshe kupitia kwa mazungumzo kati ya MTU I na MTU II ni
kuwa Lila ni changudoa tu mjini ila hakuna cha mno anachokifanya huko.
MTU
II:Tena anavuta bangi, sikuambii kuvuta sigara. Fikiri mwanamke kuvuta sigara
na bangi?Kajifanya kwenda mjini kufanya ajira ya usekritari kwenyeofisi ya
mawakili sijui nini.Wapi bwana! Changudoa yule. Watu waliokwenda mjini
wamemwona usiku akigombania waume.(uk 37)
v
Hitimisho
Makala
haya yameangazia masuala ibuka katika
Tamtilia ya Mbaya Wetu. Masuala ambayo yamejadiliwa ni :, mapenzi na ndoa,
malezi, ufisadi,matumizi ya dawa za kulevya,Uasherati na ukiukaji wa haki za
kibinadamu. Masuala haya yanatokea katika jamii tunamoishi. Hili linadhihirika
kutokana na habari zinazoripotiwa katika vyombo vya habari kama vile
magazeti.Visa vya ubaguzi wa wanawake vinashuhudiwa katika jamii. Watu wengi huwaona wanawake kuwa viumbe ambao
hawajakamilika wakupewa sikio katika maamuziya jamii.Wengine huwaona wanawake
kuwa vyombo vya kuwaridhisha wanaume tu. Hii inatokana na dhana potovu kuwa
mwanamke mahali pake ni jikoni tu. Mapenzi na ndoa ni suala linalochukua nafasi
kubwa katika jamii yetu. Hii ni kwa sababu inajenga msingi wa familia na
kuifunganisha jamii. Hata hivyo, asasi hii muhimu inakumbwa na changamoto tele
zinazotokana na ukosefu wa mapenzi ya dhati. Tunashuhudia visa vya ukatili,
ulevi, usaliti, uasherati, kutowajibika na talaka katika ndoa nyingi.
Suala
la ufisadi ni janga katika mataifa mengi. Tunasoma magazetini
kuhusu kashfa za ufisadi miongoni mwa viongozi kama vile: Goldernberg,
Chickenigate na Angloleasing. Visa hivi vinatekelezwa na watui wenye
tamaa na ubinafsi. Jamii haitaki hawa
kuwajibiki katika kazi zao na hawayajali maslahi ya wananchi wao huweka hongo.
Hasa hili limepelekea kuzukakwa visa vingi vya uporaji mali ya umma kwa kuamini
kuwa hongo ndiye mkombozi wao hasa kwenyeidara husika ambayo ni polisi. Hivyo
basi ni ombi la kila mmoja kulivalia njuga swala hilina kuona kuwa maozo yote
yanatiwa katika kaburi la sahau kwa kuwa pasi kufanya hayo jamii itazidi
kuathirika pakubwa.
v
Marejeleo.
ü
Al Farsy,
A. S. (1969) Kurani Tukufu. Nairobi: Paulines’ Publications Africa.
ü
Drabble, M.
(1995) The Oxford Companion to English Literature. New York: Oxford
University Presss.
ü
Farouk,
M.T. (1974) Uchambuzi wa Maandishi ya Kiswahili. Nairobi: Oxford
university press.
ü
Githinji,
E. (2014) ‘Watoto Watatu Walioteswa Waokolewa’. Taifa Leo, Aprili 3, uk.
4
ü
Kalama, M.
(2013) ‘Mienendo ya Dada Zetu Yazidi Kukang’anya’. Taifa Leo, Juni 13,
uk. 10
ü
Kamusi
ya Karne ya 21 (2013). Nairobi:
Longhorn Publishers Karanja, D. (2008) “Masuala Ibuka katika Fasihi ya
Watoto’’. Tasnifu ya uzamili, Chuo kikuu cha Kenyatta.
ü
Kavuri, P.
(2008) “Dhuluma za Watoto katika Riwaya za Kiswahili.” Tasnifu ya
uzamili, Chuo Kikuu Cha Kenyatta.
ü
Masinjila,
M. (1994) Teaching Oral Literature. Nairobi: Kenya Literature Oral
Association.
ü
Njogu, K na
Chimera, R. (1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation.
ü
Onchong’a,
E. (2013) ‘Malezi ya Wana ni Ushirika’. Taifa leo, Juni 17, uk. 11
ü
Shirika la
AFP (2014) ‘Wamtetea Mfungwa’. Taifa Leo, Juni 20, uk. 13
ü
__________(2014)
‘Vita Vimeathiri Watoto Milioni Tano Syria’. Taifa Leo, Machi 12, uk. 13
ü
___________(2014)
‘Wanahabari Waanza Mgomo Australia’. Taifa Leo, Mei 8, uk. 14
ü
__________(2015)
‘Albino Matatani’. Taifa Leo, Aprili 8 , uk. 13
ü
___________(2015)
‘Kanisa Kupitisha Ndoa za Jinsia Moja’. Taifa Leo, Machi 19, uk. 13
ü Walibora,K(2014) Mbaya wetu,Nairobi,Moran East
Africa Publishers