Tuesday

WHO: Janga la Uviko-19 bado lipo, virusi vipya kujitokeza zaidi

0 comments


  • WHO yasema ulimwengu bado haujafikia mwisho wa janga la Uviko-19.
  • Virusi hivyo vitaendelea kujitokeza kwa aina tofauti tofauti.
  • Yawataka watu kutopuuza tahadhari.

Dar es Salaam. Kama umeacha kuchukua tahadhari dhidi ya Corona (Uviko-19) kwa kisingizio kuwa ugonjwa huo umeisha, basi fahamu kuwa ndiyo kwanza kazi inaanza kwa sababu bado upo upo sana.

Hivyo jukumu la kupata chanjo na tahadhari za kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko bado ni lako ili kulinda afya yako.

Mwanasayansi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Soumya Swaminathan, amesema ulimwengu bado haujafikia mwisho wa janga la Uviko-19 wa sababu virusi hivyo vitaendelea kujitokeza kwa aina tofauti tofauti.

Swaminathan ametoa angalizo hilo jana Februari 13, 2022 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari nchini Afrika Kusini, ambako alikuwa ametembelea viwanda vya kutengeneza chanjo. 

"Kwa hivyo tunajua kutakuwa na anuwai zaidi, anuwai zaidi ya wasiwasi, kwa hivyo hatuko mwisho wa janga," Swaminathan alinukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Mwanasayansi huyo mkuu aliandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus. 

Jukumu la kupata chanjo na tahadhari za kunawa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko bado ni lako ili kulinda afya yako. Picha| BBC.


Swaminathan amesema hakuna mtu anayeweza kutabiri ni lini janga hilo litaisha. 

"Tusitangaze janga hili kama watu wengine wanavyofanya sasa. Itakuwa upumbavu kuacha tahadhari zote ambazo tumekuwa tukichukua wakati huu wote. 

“Tunahitaji kuendelea na tunatumai hadi mwisho wa 2022, tutakuwa tumeingia nafasi bora zaidi. Bado tunahitaji kuwa waangalifu," amesema.

Mwanasayansi mkuu huyo wa WHO amesema ulimwengu utajifunza jinsi ya kuishi na virusi vya Uviko-19 kama ilivyo kwa virusi vingine vya kupumua.

"Tutakuwa na mifumo bora zaidi ya uchunguzi ulimwenguni. Tunajua kuwa hata kama una maambukizi ya kawaida ya mfumo wa upumuaji au mafua, ni vizuri kuvaa barakoa yako,” amesema.

Wakati huo huo uamuzi wa Marekani kuhusu chanjo za Pfizer na BioNTech  kwa ajili ya watoto wadogo kuanzia miezi 6 hadi miaka 4 umeahirishwa kwa takriban miezi miwili baada ya idara inayosimamia Chakula na Dawa (FDA) nchini Marekani kusema inahitaji data zaidi. 

Serikali ya nchi hiyo ilipanga kuzindua chanjo kwa watoto wadogo mnamo Februari 21 kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Omicron miongoni mwa watoto.

No comments:

Post a Comment