
- Mwanamke mmoja kutoka jijini Nairobi ameingia kwenye gumzo kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuangua kilio na kuzimia mara baada ya uhusiano na aliyekuwa mpenzi wake kuvunjika ghafla siku ya wapendanao.
Kenya. Video iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha mwanamke kutoka nchini Kenya akiangua kilio baada ya kuachwa na mpenzi wake sikukuu ya wapendanao ‘Valentine’ iliyoadimishwa jana Februari 14.
Watu wengi walionekana wakimzingira dada huyo wakati wa tukio hilo huku wakimfariji naye aliendelea kulia kwa uchungu, huku akionekana kugulia maumivu baada ya uhusiano wake kuvunjika siku ya Valentine.
Licha ya maswahiba wake kujaribu kumtuliza, kumfariji na wengine wakimtia moyo dada huyo alikuwa hatulii kwani aliendelea kulia na kutomsikiliza mtu yeyote akiendelea kujigaragaza sakafuni huku akimlaani mwanaume huyo aliyemuacha.
Kwingineko Polisi nchini Kenya wanachunguza tukio la mwanamke mmoja aliyejirusha ghorofani na kufariki dunia sababu ikiwa ni wivu wa mapenzi.
Polisi wanasema mwanamke huyo alijiangusha kutoka ghorofa ya sita na kufariki dunia chanzo ikiwa ni pale mpenzi wake alipopigiwa simu na mwanamke mwingine mara baada ya kufika nyumbani wakitoka kwenye starehe.
Kwa mujibu wa Tovuti ya TUKO ya nchini Kenya imeripoti kuwa mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Christine Rayon Lantel alifanya uamuzi huo baada ya kutofautiana na mpenzi wake walipokuwa kwenye jumba la Amani House iliyoko karibu na Thika Road Mall (TRM) Drive katika Kaunti ya Nairobi.
Maafisa wapelelezi wanaochunguza kisa hicho wamesema, “Kulitokea tofauti wakati mpenzi alipopigiwa simu na mwanamke mwingine, alikasirika na kujitupa.”
Credit : Mwananchi