Mwandishi
Baraka Emmanuel Simon
Ikisiri
Makala hii inaeleza Athari ya Uislamu na Uarabu katika Tendi za Kiswahili; Mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari.
Makala hii imeanza kwa kufafanua dhana ya tendi, Uislamu na Uarabu kwa lengo la kupanua mawanda ya kuelewa dhana hizi. Baada ya kufasili dhana hizo pia, makala hii itaeleza kwa ufupi kuhusu Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari. Makala hii imebainisha Athari ya Uislamu na Uarabu katika Tendi za Kiswahili; Mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari kama vile mianzo na miisho ya kifomula, mandhari, vina, maudhui ya dini ya Kiislamu na msamiati.
Utangulizi
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa utendi ni ni utungo wenye kusimulia matukio ya kishujaa yenye uzito wa kijamii au kitaifa. Aidha, Wamitila (2003) anaeleza kuwa utendi ni shairi refu la kimasimulizi linalozungumzia kwa mapana na mtindo wa hali ya juu matendo ya mashujaa au shujaa mmoja.
Wamitila (2016) anafasili Uislamu kuwa ni dini inayojengwa kwenye imani kuwa Mungu wa kuabudiwa ni mmoja tu na Mtume Muhammad (S.A.W) ni mjumbe wake.
Wamitila (keshatajwa) anafafanua Uarabu kuwa ni tabia na mwenendo unaohusishwa na maneno ya Uarabuni.
2.0 Muhtasari wa Utenzi wa Rasi’ lGhuli
Utenzi wa Rasi’ lGhuli ni utenzi ambao umetungwa na Mgeni Bin Faqihi mwaka 1979. Aidha, Utenzi wa Ras’ LGhuli unatokana na kisa cha Kiarabu kiitwacho Futuhu ‘lYamani ikiwa na maana kushindwa au kutiishwa kwa Yemeni. Kisa hicho cha Kiarabu husimulia jinsi nchi ya Yemeni ilivyoshindwa na kutekwa na majeshi ya Waislamu yakiiongozwa na Mtume Muhamadi mwenyewe, Seyyidna Ali bin Abi Talibu (kuanzia sasa Seyyidna Ali) na Seyyidna Umar bin Khatab kunako karne 6. Tafsiri ya utendi huu umepewa jina la Rasi ‘lGhuli linalotokana na jina la kebehi la mtawala wa makafiri wa Yemeni ambaye jina lake halisi aliitwa Mukhariki bin Shahabu. Jina hili la kebehi Ras ‘lGhuli lina maana ya Kichwa cha Nyoka. Kwa ujumla utendi huu una beti zipatazo 4584.
Muhtasari wa Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari
Utenzi wa Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari ni utenzi ambao umetungwa na Hemed Abdallah Bin Said mwaka 1972 ambao una jumla ya beti 405. Utenzi huu unahusu wanawake waovu na vitimbi vyao na namna wanavyoweza kumuingiza mtu katika maasi ambayo hakupata kuyawaza wala kuyatenda. Mtu huyo anayeingia katika vishawishi hivyo ni Kadhi Kassim Bin Jaafari na watu walioweza kumuingiza katika maasi hayo ya kumuasi Mwenyezi Mungu ni pamoja na mke wa mfalme Marwani, Bi. Kikongwe mmoja na msichana.
4.0 Nadharia ya Uchambuzi wa Data
Makala haya yameongozwa na nadharia ya Kiislamu (Taib, 2004) katika fasihi, ambayo mihimili yake kwanza, fasihi lazima iendeleze Uislamu ambao nguzo mama yake ni kukiri kwamba kuna Mungu mmoja naye ni Allah na Muhammad ni Mtume wake kama inavyokaririwa katika kitabu kitakatifu cha Quran. Pili, fasihi ilenge kukosoa makosa ya binadamu kwa misingi ya mafundisho ya dini ya Kiislamu ambayo yanachukua Quran Tukufu na Sunnah kama mwongozo wa maisha kamili ya mwanadamu. Nadharia hii ya Kiislamu ndiyo iliyowezesha kuangalia Athari ya Uislamu na Uarabu katika Tendi Za Kiswahili: Mifano kutoka katika Utenzi Wa Ras’ Lghuli na Utenzi Wa Kadhi Kassim Bin Jaafari.
Athari ya Uislamu na Uarabu katika tendi za Kiswahili; Mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari
Wamitila (2002), anaeleza kuwa, tenzi nyingi za Kiswahili zinafanana kidhamira na kifani. Asilimia kubwa ya tendi za Kiswahili, zina maudhui ya dini ya Kiislamu. Kimtindo zinafanana kwa kutumia fomula ya fasihi, fomula sawa za ufunguzi na ufungizi, kwa mfano, tendi zote za Kiswahili huanza kwa dua na kumaliza kwa dua, msuko na mgogoro wa msuko unaokaribiana. Uislamu na Uarabu umeonekana kuwa na athari kubwa sana katika tendi mbalimbali za Kiswahili na hii imekuja kuthibitishwa katika makala hii kama ifuatavyo:
5.1 Mianzo na Miisho ya Kifomula
Tenzi (tendi) nyingi zimekuwa zikitumia mianzo maalumu na kumalizia kwa miisho maalumu. Aghalabu tendi hizo huweza kuanza kwa dua na kumalizia kwa dua. Dua hiyo, anaombwa Mwenyezi Mungu mmoja, ambaye ndiye mwenye uwezo wa kila kitu. Kwa mfano, Utenzi wa Ras’ LGhuli, beti mbili za mwanzo zinaanza kwa duwa:
Awali bisumi ‘llahi
Jina la Mola Ilahi
Pweke asiye shabihi
ndiye wahidi Qahari
Arahamani Rahimi
ndiye hai ‘l Qayumi
mwenye ezi ya dauhni
alipendalo hujiri
Kutokana na beti hizi mbili za mwanzoni Utenzi wa Ras’ LGhuli mtunzi anaanza kwa dua tukufu. Hii ni dasturi ya waumini wa dini ya Kiislamu, ambapo kila jambo halina budi kuanzishwa kwa dua ya kumtaja Mwenyezi Mungu. Vilevile, katika Utenzi wa Ras’ LGhuli, mtunzi anamalizia kwa kumuomba Mwenyezi Mungu (S.W). katika ubeti wa ili akirimiwe, na AIlah (Mwenyezi Mungu). Mfano;
228. Rabi ndiwe muadhamu
nataka uwarahamu
wazee wangu timamu
walo bara na bahari
Katika mifano hiyo hapo juu, mtunzi ameonesha kuwa, Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo wa kila jambo kwa mja wake. Anamuomba Mwenyezi Mungu awarahamu wazee timamu walo bara na bahari.
5.2 Vina
Wamitila (2016) anasema vina ni dhana inayotumiwa katika taaluma ya ushairi kuelezea silabi zinazofanana katika sehemu sawa katika mpangilio wa ubeti wa shairi. Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari una vina vilivyofanana katika mistari mitatu ya mwanzo kutoka ubeti wa mwanzo hadi ubeti wa mwisho.
Mfano 1: - Utenzi wa Ras’ LGhuli
261. Akangia kwa haraka
babaye akamfika
kalala kajifunika
kwa libasi ya hariri
262. Akampiga ajili
kwa upanga wa sigali
kumuwanya pande mbili
na rasi kaitairi
Mfano 2: Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari
52. Kulia kwake imamu
Akaliya na Kasimu
Na jamii ya kaumu
Pasibake mmoya
213. Akamtaka Kasimu
Nilapo ndio haramu
Sijile kuvuta tamu
Nijile kukuombeya
Katika Utenzi wa Ras’ LGhuli ubeti wa 261 kuna kina kinachoishia na silabi “ka” na ubeti wa 262 kina chake kinaishia na silabi “li” lakini kwa upande wa Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari ubeti wa 52 na 213 umeweza kuishia na vina sawa ambavyo “mu”. Uwepo wa vina katika tenzi hizi mbili inadhihirisha jinsi ambavyo Uislamu na Uarabu umeathiri tendi za Kiswahili. Hii ni kwa sababu zipo aya mbalimbali za Qur’an Tukufu ambazo zina vina ndani yake, mfano Surat An-Nas, Surat Al-Ikhlas hata Surat Al-Falaq pia ni miongoni mwa aya ambazo zimekaa kwa mfumo wa vina. Hivyo basi, hapana shaka kuwa Uislamu na Uarabu umeathiri tendi za Kiswahili.
5.3 Mandhari
BAKITA (2015) wanafasili dhana ya mandhari kuwa ni mwonekano wa mahali unaojumuisha ardhi, milima na mabonde. Mandhari ni moja wapo ya athari nyingi ya Uislamu na Uarabu inayoonekana katika tendi za Kiswahili. Katika mandhari hizo huoneka umeshamiri sana Uislamu au mahali ambapo Waislamu wamekuwa wakihudhuria mara kwa mara katika maeneo hayo. Aidha, mandhari hizo mara nyingi huchora maisha ya waislamu kwa ujumla wake. Aghalabu, mandhari hizo huwa ni halisi ambayo hata kwenye Qura’n Tukufu maeneo hayo yamepatwa kutajwa.
Mfano; Utenzi wa Ras’ LGhuli
26. Hadithi hiyo yuani
ina maneno bayani
ya vita vya ‘lYamani
zamani zake Bashiri
Mfano; Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari
165. Akenda kati ndiyani,
Yendayo msikitini,
Magharibi muwadhini,
Kadhi akamsikiya.
Mifano iliyoonyeshwa hapo juu inaonesha ni mandhari ambayo imeonekana katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari ambayo ni moja kati ya athari ya Uislamu na Uarabu katika tenzi hizi mbili. Mfano mandhari ya Yamani iliyotajwa katika Utenzi wa Ras’ LGhuli ni miongoni mwa maeneo ambayo yameweza kutajwa katika Qura’n Tukufu ambayo ndio mwongozo wa waumini wote wa dini ya Kiislamu, ambapo inaonesha kuwa eneo hilo palishawahi kutokea vita baina ya Waislamu wakiongozwa na Mtume Muhammad (S.A.W) dhidi makafiri huku lengo ikiwa ni kuilingania dini ya Mwenyezi Mungu (Allah) na kuhakikisha dini hiyo inasimama barabara. Aidha, kuhusu mandhari ya msikitini iliyotajwa katika Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari ni miongoni mwa sehemu tukufu kwa waislamu wote. Msikiti ni sehemu ambayo Waislamu hutumia kwa ajili ya kufanya maombi kwa Mwenyezi Mungu (Allah). Hivyo basi, kutokana na kutajwa kwa mandhari hizo inadhihirisha ni kwa namna gani tenzi hizi za Kiswahili zilivyoathiriwa na Uislamu na Uarabu.
5.4 Maudhui ya dini ya Kiislamu
Wamitila (2003) anaeleza kuwa maudhui ni jumla ya mambo yote yanayozungumziwa katika kazi ya fasihi. Anaendelea kueleza kuwa maudhui hutumika kwa upana kujumlisha dhamira, falsafa, itikiadi na msimamo. Aidha, maudhui ni moja kati ya athari nyingine ya Uislamu na Uarabu katika katika tendi za Kiswahili; mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari. Tenzi hizi mbili zimeonekana kubeba maudhui ya dini ya Kiislamu hususani vile ambavyo zinaonekana zikianza kwa dua na kumaliza kwa dua kwa kumuomba Mwenyezi Mungu kwani yeye ndiye muweza wa yote hapa duniani na huko akhera. Kwa mfano, Utenzi wa Ras’ LGhuli, beti mbili za mwanzo zinaanza kwa duwa:
Awali bisumi ‘llahi
Jina la Mola Ilahi
Pweke asiye shabihi
ndiye wahidi Qahari
Arahamani Rahimi
ndiye hai ‘l Qayumi
mwenye ezi ya dauhni
alipendalo hujiri
Mfano huu unaonesha jinsi ambavyo umeanza kwa dua, na huu ndio utaratibu wa jamii ya waislamu wote kwamba pale unapoanza jambo lolote huna budi ya kuanza na dua.
5.5 Msamiati
Kwa mujibu wa Massamba (2004) anafasili dhana ya msamiati kuwa ni jumla ya maneno yatumikayo katika. Katika tenzi hizi mbili zimeoneka kutawaliwa sana na msamiati ambao hupatikana katika dini ya Uislamu. Hii inadhihirisha kuwa ni mojawapo athari nyingine ya Uislamu na Uarabu katika katika tendi za Kiswahili; mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari.
Mfano: Utenzi wa Ras’ LGhuli
423. Akajibu shekhe Ali
Nimetumwa na Rasuli
Kwenda kwa Ras’ LGhuli
Sultani wa kufari
529. Baadaye akainuka
Akisema napulika
Kusifu wako Rabuka
Maneno yako mazuri
Mfano: Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari
92. Sultani kabaini,
Mwana nimekuidhini,
Nauipate yakini,
Ya kwamba atapoteya.
165. Akenda kati ndiyani,
Yendayo msikitini,
Magharibi muwadhini
Kadhi akamsikiya.
Katika mifano ya hapo juu imesheheni msamiati ambao kwa asili yake ni Uislamu na Uarabu. Mfano katika Utenzi wa Ras’ LGhuli neno Rasuli - humaanisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, Rabuka – bwana wako. Pia, maneno yaliyotumika katika Utenzi wa Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari kama vile Sultani - humaanisha kiongozi ambaye mara nyingi hupatikana katika jamii za Waarabu, Magharibi – ni wakati wa swala kwa waumini wa dini ya Kiislamu, muwadhini – huyu ni mtu anayewaita waumini wa Kiislamu pale unapowadia muda wa kwenda kuswali na Kadhi – ni kiongozi kwa ngazi ya mahakama ya Uislamu (Hakimu) ambaye hutoa hukumu.
Hitimisho
Kwa kuhitimisha, tunaweza kusema kuwa makala hii inayohusu Athari ya Uislamu na Uarabu katika katika tendi za Kiswahili; Mifano kutoka katika Utenzi wa Ras’ LGhuli na Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari imeweza kuonesha jinsi Uislamu na Uarabu ulivyoweza kuathiri tendi za Kiswahili. Aidha, kupitia makala hii inaweza kuwa mchango tosha katika nyanja ya kujifunza tendi za Kiswahili kwani itasaidia kujua mambo mbalimbali ambapo hapo awali wajifunzaji wa tendi za Kiswahili hawakuweza kuyajua. Mathalani suala vina, kupitia makala hii wajifunzaji wataweza kujua na kutambua kuwa asili na chanzo cha vina ni kutoka katika Quran Tukufu ambapo waandishi wengi hususani wale Waislamu na wale waloathiriwa na dini ya Kiislamu waliweza kuchukua maarifa hayo na kuhamishia katika kazi mbalimbali za ushairi ili tu kuleta mavuto katika kazi zao. Sio hivyo tu, bali hata katika suala zima la mianzo na miisho itambulike kuwa kazi nyingi za fasihi kuwa na mianzo na miisho ya dua ni moja ya athari kutoka katika uislamu kwani Waislamu wamekuwa na utamaduni wa kuanza jambo kwa dua na kumaliza kwa dua huku dua hizo zikielekezwa kwa Mwenyezi Mungu ambaye ndio muumba wa ardhi na mbingu.
MAREJELEO
BAKITA (2015), Kamusi Kuu ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.
Faqihi, M. (1979) Utenzi wa Ras’ LGhuli. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Massamba, D. P. B. (2004) Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: TUKI.
Mohamed, H. (1972) Utenzi wa Kadhi Kassim Bin Jaafari. Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili Dar es Salaam: DUP.
Mulokozi, M. M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Taib, A. H. (2004). ‘Mafundisho ya Uislamu katika kazi za Shaaban Bin Robert’. Tasnifu ya MA Kiswahili. Islamic University in Uganda. Haijachapishwa.
Wamitila, K. W. (2002), Uhakiki wa Fasihi: Misingi na Vipengele Vyake. Nairobi: Kenya Lithotho Ltd.
_______________ (2003) Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication Ltd.
________________(2016). Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide-Muwa Publishers.
Wasiliana na Mwandishi
Baraka Emmanuel Simon ( Baraka, Jr)
0654245488 / 0693300491
Baraka Emmanuel Simon ( Baraka, Jr)
0654245488 / 0693300491